Wingu

(Elekezwa kutoka Cloud)

Wingu ni matone madogo ya maji yanayoelea pamoja katika angahewa juu ya ardhi. Mawingu ni mahali ambako mvua na theluji hutoka.

Mawingu angani

Kutokea kwa mawingu

hariri

Asili yake ni mvuke wa maji unaotokea wakati jua linabadilisha maji kuwa gesi ya H²O; mvuke unapanda juu kwa sababu ni nyepesi kuliko hewa. Baada ya kupanda kiasi cha kutosha hufikia umbali penye baridi na mvuke unatonesha kuwa matone madogo ya maji. Kama wingu ni juu sana baridi inasababisha mvuke kuwa fuwele za barafu au theluji.

Mvuke unahitaji viini kwa kutonesha. Viini hivi ni aina zote za vumbi iliyoko hewani. Mvuke uliopo hewani unaanza kutonesha kwenye vipande hivi vidogo sawa na mvuke katika chumba cha jikoni au bafuni unaotonesha kwenye kioo cha dirisha au ukutani.

Kuelea kwa mawingu na kunyesha kwa mvua

hariri

Matone ndani ya wingu yanaweza kuelea angani kwa muda mrefu kama ni madogo. Mara nyingi matone madogo huwa na kipenyo cha milimita 0.001 hadi 0.015 hivyo ni nyepesi na mwendo wa kuanguka ni polepole. Hali halisi hayaanguki kwa sababu mawingu hutokea sehemu penye upepo wa kupanda juu na mwendo wa upepo huzidi au kulingana na mwendo wa kuanguka kutokana na graviti.

Lakini matone yana mwelekeo wa kuungana na kuwa makubwa zaidi. Yanaweza kufikia kipenyo cha milimita 1-3 na kuwa mazito zaidi. Sasa uvutano wa graviti unapita mwendo wa upepo na matone yanaanza kuanguka chini kama usimbishaji.

 
WikiMedia Commons
Wikimedia Commons ina media kuhusu: