Eratosthenes
'
Eratosthenes | |
---|---|
Amezaliwa | 276 KK |
Amefariki | 194 KK |
Kazi yake | mtaalamu wa hisabati, jiografia |
Eratosthenes wa Kirene (kwa Kigiriki Ερατοσθένης ο Κυρηναίος; 276 KK - 194 KK) alikuwa mtaalamu wa hisabati, jiografia, historia na lugha tena mkurugenzi wa maktaba ya Aleksandria katika Misri. Anakumbukwa hasa kama mtu wa kwanza aliyekadiria mzingo wa dunia. Anasemekana aliibuni neno "jiografia".
Maisha
haririEratosthenes alizaliwa mnamo mwaka 276 KK mjini Kirene wa Libya. Kirene ulikuwa mmoja kati ya miji iliyoundwa na Wagiriki wa Kale huko Afrika Kaskazini.
Alikwenda Athens kwa masomo yake alipofundishwa na wanafalsafa na wataalamu mashuhuri. Mnamo mwaka 255 KK alihamia Aleksandria iliyokuwa mji mkuu wa Misri. Akawa mwalimu wa mwana wa mfalme na mwaka 236 KK alikuwa mkurugenzi wa tatu wa maktaba ya Aleksandria iliyokuwa kitovu cha kimataifa cha elimu kwa sababu ya mkusanyiko mkubwa wa vitabu.
Maktaba ya Aleksandria
haririKama mkuu wa maktaba ya Aleksandria aliweza kuchungulia ujuzi wa wakati wake akaendelea kuitumia na kuendeleza mafundisho mbalimbali. Maktaba hii ilikuwa kitu cha ajabu kwa sababu wakati ule vitabu vyote vilinakiliwa kwa mkono na kuwa na thamani kubwa. Erastothenes alikuwa juu ya vitabu lakhi kadhaa.
Jiografia
haririAlichora ramani ya dunia isiyohifadhiwa lakini ilitajwa mara nyingi katika maandiko ya watu wa kale. Eratosthenes alijua bara 3 za Ulaya, Libya (Afrika) na Asia. Asia ilijulikana kwake hadi Uhindi, nchi iliyofikiwa na Aleksander Mkuu. Alijua ya kwamba Afrika, iliyojulikana kwa jina la Libya wakati ule, ilizungukwa kwa maji kutokana na taarifa ya msafara wa Wamisri miaka 300, kabla yake lakini hakujua ya kwamba inaenea pia kusini kwa ikweta.
Kwa ramani yake alibuni utaratibu wa longitudo na latitudo ingawa ulikuwa tofauti na ule wa sasa.
Mzingo wa dunia
haririWazo la kuwa dunia ina umbo la tufe lilijulikana kabla ya Eratosthenes. Yeye anajulikana kama mtu wa kwanza aliyeweza kukadiria mzingo wake kwa njia ya upimaji[1][2].
Alitumia pembe jinsi gani jua linavyoonekana kutoka mahali pawili duniani pamoja na hisabati ya duara.
- Kwanza alihisi ya kwamba umbo la mzingo wa dunia litakuwa kama duara.
- Wakati wa safari moja alitazama jinsi gani jua liliakisiwa na maji ya kisima kirefu mjini Siene katika Misri ya kusini kwenye saa ya mchana tarehe 21 Juni. Alielewa maana yake ni kwamba mji huu ulikuwa kwenye tropiki ya kansa ya dunia na jua lilikaa kwenye kilele cha anga kabisa siku ile wakati wa mchana. Kwa hiyo alichukua pembe ya jua kuwa nyuzi 90. Alijua pia ya kwamba hali hii itarudia kila mwaka tarehe ileile.
- aliweza kupima pembe jinsi jua lilivyoonekana kwake Aleksandria tarehe ileile saa ya mchana.
- alijua umbali kati ya Aleksandria na Siene[3].
Nyingine ilikuwa hisabati ya duara ya kawaida. Kwa njia hiyo alikadiria mzingo wa dunia kuwa "stadia" 252,000. Hii ni tokeo nzuri sana. Hakuna uhakika alitumia stadia gani; kama alikadiria stadia ya Kigiriki yenye urefu wa mita 185 ingemaanisha mzingo wa kilomita 46,620 ambayo ni kubwa zaidi kwa asilimia 16. Kama alitumia stadia ya Misri za mita 157.5 ingemaanisha kilomita 39,690 ambayo ni karibu sawa na upimaji wa leo.
Hisabati
haririKatika hisabati anajulikana jinsi alivyobuni "Kichujio cha Erastosthenes" ambacho ni mbinu wa kugundua namba tasa.
Aliandika namba asilia zote kuanzia mbili hadi namba aliyotaka kuifanyia utafiti kama ni namba tasa au la.
- Alianza na 2.
- alifuta vizidisho vyote vya namba tasa unazojua au kugundua
- alianza na 2 na vizidisho vyake kama 4, 6, 8, 10 na kadhalika.
- aliendelea kwa kufuta 3 (namba tasa inayofuata) na vizidisho vyake kama 6, 9, 12 na kadhalika.
- sasa alirudia kuangalia chanzo cha orodha. Namba inayofuata isiyofutwa ni namba tasa tena. Katika mfano huu alikuwa ni 5. Aliendelea kufuta vizidisho vyake.
- Kwa njia hii alirudia kuangalia orodha upya na kugundua namba tasa zote zilizomo.
Marejeo
hariri- ↑ Astronomy 101 Specials: Eratosthenes and the Size of the Earth, tovuti ya Chuo Kikuu cha Bucknell, iliangaliwa Novemba 2020
- ↑ Carl Sagan: The measure of Eratosthenes,
- ↑ Dennis Rawlings (1982): The Eratosthenes-Strabo Nile Map. Is it the earliest surviving instance of spherical cartography? Did it supply the 5000 stades arc for Eratosthenes' experiment?, Archive for History of Exact Sciences volume 26, pages 211–219 (1982)