Mapacha (kundinyota)

(Elekezwa kutoka Jauza (kundinyota))

Mapacha (pia Jauza, kwa Kilatini na Kiingereza Gemini) [1] ni jina la kundinyota kwenye angakaskazi.

Nyota za kundinyota Mapacha (Gemini) katika sehemu yao ya angani
Ramani ya Mapacha - Gemini jinsi inavyoonekana kwa mtazamaji kwenye nusutufe ya kaskazini
Gemini iliyochorwa na msanii wa Uingereza mnamo mwaka 1825
Namna ya kuunganisha nyota kuu za Mapacha kwa kuonyesha mapacha wanaoshikana kwa mikono
Sanamu ya Castor na Pollux kufuatana na mitholojia ya Kigiriki

Mahali pake

Mapacha iko angani kwenye mstari wa Zodiaki kati ya Kaa (pia Saratani, lat. Cancer) upande wa mashariki na Ng’ombe (Taurus) upande wa magharibi.

Inapakana na kundinyota jirani la Kaa (Cancer), Pakamwitu (Lynx), Hudhi (Auriga), Ng'ombe (Taurus), Jabari (Orion), Munukero (Monoceros) na Mbwa Mdogo (Canis Minor).

Mapacha - Gemini ni sehemu ya zodiaki maana yake mstari wa ekliptiki unapita humo. Ilhali miendo ya Mwezi na sayari inafuatana karibu na ekliptiki magimba haya huonekana katika eneo la Mapacha kwa wakati fulani kwenye mwaka.

Jina

Mabaharia Waswahili walijua nyota hizi kwa jina la Jauza tangu miaka mingi wakifuata njia yao baharini wakati wa usiku kwa msaada wa nyota. Walipokea jina hili kutoka kwa Waarabu waliosema جوزاء jawzaaʾ ambalo linamaanisha mapacha[2]. Waarabu walitafsiri hapa jina la Ptolemaio aliyetaja nyota hizi vile kwa jina la Δίδυμοι didimoi yaani mapacha katika orodha yake ya Almagesti[3].

Wagiriki wa Kale waliwahi kupokea kundinyota hili likiangaliwa kama mapacha kutoka utamaduni wa Babeli. Hapa ni hasa nyota mbili angavu zaidi za Castor na Pollux zilizotazamamiwa kama vichwa vya watoto mapacha wawili. Katika mitholojia ya Wagiriki kuna hadithi ya malkia Leda aliyekuwa maridadi kiasi cha kumvuta mungu mkuu Zeus kwake. Zeus alimtembelea Leda katika umbo la bata maji (tazama pia Dajaja) akampa mimba. Leda alilala siku ileile kwa mume wake na kupokea mimba kutoka kwake pia. Wavulana wawili walizaliwa pamoja kama mapacha lakini Pollux alikuwa mwana wa mungu Zeus ilhali Castor alikuwa mwana wa mfalme. Walipendana na kusafiri pamoja kwenye Merikebu ya Argo na mashujaa wakubwa. Castor aliuawa katika mapigano; Pollux ambaye hakuweza kufa kutokana na na kuwa nusu-mungu akikuwa na huzuni akamwomba baba Zeus kumwunganisha na kakaye. Hivyo Zeus aliwaweka wote wawili angani kama nyota. Katika unajimu wa kisasa katika Afrika ya Mashariki jina "Jauza" limesahauliwa ikiwa kundinyota linaitwa kwa tafsiri tu "Mapacha".

Gemini - Mapacha ni kati ya makundinyota 48 yaliyotajwa tayari na Klaudio Ptolemaio katika kitabu cha Almagesti wakati wa karne ya 2 BK. Iko pia katika orodha ya makundinyota 88 ya Umoja wa Kimataifa wa Astronomia [4] kwa jina la Gemini. Kifupi chake rasmi kufuatana na UKIA ni 'Gem'.[5]

Nyota

Nyota za Mapacha huwa haziko pamoja kihalisi lakini zinaonekana tu vile kutoka duniani. Kwa uhalisi kuna umbali mkubwa kati yao, kama ziko mbali au jirani nasi. Kwa hiyo kundinyota "Mapacha" inaonyesha eneo la angani jinsi tunavyoiona kutoka Duniani.

Kuna nyota 85 katika eneo la kundinyota hili [6] na kuna mbili hasa zinazoonekaka vizuri kwa macho matupu zikikaa karibu na kuwa msingi wa jina la kundi ambazo zinaitwa Castor na Pollux kwa majina ya Kigiriki zilizotazamiwa na watu wa kale kama mapacha mawili. Nyota angavu zaidi ni Pollux inayofuatwa na Castor. Johann Bayer aliziona kwa kosa kinyume hivyo aliandikisha majina ya Alfa Gemininis kwa Castor na Beta Geminis kwa Pollux katika orodha yake.

  • Castor (Alfa Geminis) inaonekana kwa darubini kama mfumo wa nyota 6 zinazoonekana kwa macho kama nyota 1 tu. Ina umbali wa miakanuru 52 kutoka dunia. Uangavu unaoonekana ni 1.6.
  • Pollux (Beta Geminis) ni nyota jitu jekundu yenye mwangaza unaonekana wa 1.2 ikiwa umbali wa miakanuru 34 kutoka dunia. Pollux imegunduliwa kuwa na sayari ya nje inayoizunguka.
Jina la
Bayer
Namba ya
Flamsteed
Jina
(Ukia)
Mwangaza
unaoonekana
Umbali
(miakanuru)
Aina ya spektra
β 78 Pollux 1,16m 34 K0 III
α 66 Castor 1,58m 50 A1 V
γ 24 Alhena (Hanaa ya Jauza) 1,93m 105 A0 IV
μ 13 Tejat 2,94 bis 3,00m 250 M3 III
ε 27 Mebsuta 3,06m 900 G8 Ib
η 7 Tejat 3,24 bis 3,96m 250 M3 III
ξ 31 3,4m 64 F5 III
δ 55 Wasat 3,50m 60 F2 IV
θ 34 3,6m 150 A3 III
κ 77 3,57m 150 G8 III
λ 54 3,58m 80 A3 V
ζ 43 Mekbuda 3,7 bis 4,2m 1200 G0 + G1
ι 60 3,78m 150 K0 III
Habari za mwangaza na umbali vinaweza kubadilika kutokana na vipimo vipya

Tanbihi

  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya "Gemini" katika lugha ya Kilatini ni "Geminorum" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota ya kundi hili kama vile Alfa Geminorum, nk.
  2. ling. Knappert 1993
  3. PAL - Glossary "Gemini", tovuti ya mradi wa "Ptolemaeus Arabus et Latinus (PAL)" wa Bavarian Academy of Sciences and Humanities, iliangaliwa Oktoba 2017; Waarabu walitafsiri mapacha pia kama توأمان tawa-aman na neno hili latumiwa leo zaidi kwa kundinyota hili
  4. The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Julai 2017
  5. Russell, Henry Norris (1922). "The New International Symbols for the Constellations". Popular Astronomy. 30: 469–71. Bibcode:1922PA.....30..469R.
  6. The geography of the heavens and class book of astronomy by Elijah H. Burritt kupitia google books, iliangaliwa Julai 2017

Marejeo

  • Levy, David H. (2005). Deep Sky Objects. Prometheus Books. ISBN 1-59102-361-0. {{cite book}}: Invalid |ref=harv (help)
  • H. A. Rey, The Stars — A New Way To See Them. Enlarged World-Wide Edition. Houghton Mifflin, Boston, 1997. ISBN 0-395-24830-2.
  • Ridpath, Ian; Tirion, Wil (2001), Stars and Planets Guide, Princeton University Press, ISBN 0-691-08913-2
  • Ian Ridpath and Wil Tirion (2007). Stars and Planets Guide, Collins, London. ISBN 978-0-00-725120-9. Princeton University Press, Princeton. ISBN 978-0-691-13556-4.
  • Richard Hinckley Allen: Star-Names and their Meanings; kwa G. E. Stechert New York, Leipzig, London, Paris 1899, ukurasa 222 ff (online kwenye archive.org)
  • Jan Knappert, 1993: The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations; The Indian Ocean Review September 1993 Volume 6 No. 3 September 1993, kurasa 6-7, ISSN 1031-2331

Viungo vya Nje

 
WikiMedia Commons
  1. A Spring Sky Over Hirsau Abbey
  2. The Eskimo Nebula from Hubble
  3. The Medusa Nebula
  4. Open Star Clusters M35 and NGC 2158
  5. NGC 2266: Old Cluster in the NGC
  Makundinyota ya Zodiaki
Majina ya kisasa yanafuatwa kwa mabano na jina la mabaharia na jina la Kilatini (la kimataifa)
 

Kaa (Saratani – Cancer  )Kondoo (Hamali – Aries  )Mapacha (Jauza – Gemini  )Mashuke (Nadhifa – Virgo  )Mbuzi (Jadi – Capricornus  )MizaniLibra  )Mshale (Kausi – Sagittarius  )Ndoo (Dalu – Aquarius  )Nge (Akarabu – Scorpius  )Ng'ombe (Tauri – Taurus  )Samaki (Hutu – Pisces  )Simba (Asadi – Leo  )