Elia Bombarone

(Elekezwa kutoka Elia wa Cortona)

Elia Bombarone wa Cortona (labda Bevilia karibu Assisi, 1180 hivi; Cortona, 22 Aprili 1253) alikuwa mfuasi wa Fransisko wa Asizi ambaye alimteua kuwa makamu wake. Baada ya uongozi wa Yohane Parenti, Elia alichaguliwa kuongoza tena utawa wa Ndugu Wadogo.

Kanisa la Mt. Fransisko huko (Cortona), lililojengwa na Elia.

Maisha

hariri

Elia alijiunga na Fransisko baada ya masomo ya sheria, akapewa naye kazi mbalimbali alizozitimiza kwa nguvu kubwa.

Fransisko alimteua kushika nafasi yake baada ya kuona jamaa ya kwanza imegeuka shirika halisi, hivyo alihitajika kiongozi mwenye msimamo na pengine ukali pia. Fransisko alijieleza kwamba hapendi kutesa wenzake, ingawa anaweza. Basi, akamuachia Elia ambaye, mwanzilishi akiwa bado hai, alifuata maelekezo yake, ingawa alimueleza maoni yake pia kuhusu utungaji wa kanuni, hasa kwa lengo la kufanya iwezekane kwa kiongozi yeyote kudai watawa utekelezaji wake.

Katikati ya vipindi viwili vya uongozi wake (1221-1227, halafu 1232-1239) alimjengea Fransisko kanisa zuri sana, halafu jirani nalo konventi kubwa mno, ili kushindana na abasia za Wabenedikto. Pia alionyesha ushindani fulani na Yohane Parenti, hata akahamisha masalia ya Fransisko bila ya kibali chake, akasababisha vurugu kutoka kwa watu wa Assisi.

Ulijitokeza hivyo mvutano kati ya asili ya utawa huko mjini na hali yake mpya ya kimataifa. Kwa kumchagua tena bradha huyo, shirika lililenga kuleta usuluhisho kati ya pande hizo mbili: si kurudia maisha ya awali, bali kuokoa usawa kati ya makleri na mabradha.

Elia alimgeuza mwanzilishi kuwa fahari ya shirika kuliko kielelezo cha kufuatwa. Mwenye vipawa na elimu, aliathiri sana viongozi wa dini (Papa Gregori IX) na wa siasa (kaisari Federiko II), alistawisha misheni huko Mashariki na kukuza nyumba za masomo, lakini pia alidhulumu vikali watetezi wa kanuni.

Bila ya kuweza kutembelea kanda za shirika, alishika uongozi wote mikononi mwake, akichagua Watumishi na walinzi, akihamisha ndugu, akituma wawakilishi wake huko na huko wasimamie (pengine bila ya busara) kazi ya Watumishi, na akikataa kuwasikiliza na kuitisha mkutano mkuu.

Pamoja na hayo, fahari zake binafsi, ushuru aliowatoza mfululizo Watumishi (kwa ajili ya ujenzi n.k.), msisitizo wa kwamba kila ndugu ajishughulikie badala ya kusaidiwa na mabradha, vilisababisha hatimaye njama dhidi yake, hadi Gregori IX akaitisha na kuendesha mkutano mkuu ambao ulimuondoa madarakani na kutunga sheria za kupunguza mamlaka ya Mtumishi mkuu.

Badala yake alichaguliwa Alberto wa Pisa (1239-1240), Mtumishi wa Uingereza, kanda ambayo kuliko zote ilikua mbali na Fransisko na kujali elimu. Ingawa alikufa baada ya miezi michache tu, uchaguzi wake ulionyesha kwamba maendeleo ya shirika, yaliyotakiwa na viongozi wa Kanisa na ndugu walio wengi, yataanza tena kusonga mbele moja kwa moja.

Kwamba maendeleo hayo yalikuwa kinyume cha nia asili ya mwanzilishi (walivyosisitiza wenzake na wengineo waliomfahamu vizuri) haikuwa kizuio kwa umati walioridhika kutekeleza amri za kanuni, kuwa mafukara kuliko watawa wengine na kuheshimiwa na waamini pia kwa niaba ya mzee wao aliyezidi kutazamwa mkuu ajabu.

Elia, baada ya kuacha uongozi, aliingia siasa akijitahidi kupatanisha Papa na Kaisari, ambao wote wawili walikuwa wanamheshimu sana.

Mwaka 1239 alitengwa na Kanisa Katoliki akahamia kwenye ikulu ya Federiko II kama mshauri wake. Baada ya kifo cha Kaisari huyo (1250) alipatana tena na Kanisa akafariki huko Cortona.