Fransisko wa Asizi

Fransisko wa Asizi (kwa Kiitalia Francesco d'Assisi; tangu utotoni jina la ubatizo Giovanni, yaani Yohane (Mbatizaji), liliachwa kutumika; pia ubini mwana wa Petro Bernardone ulikuja kuachwa baada ya wao kushindana; Assisi, Italia, 1181 au 1182 - Assisi, 3 Oktoba 1226) alikuwa mtawa shemasi wa Kanisa Katoliki.

Mchoro wa zamani wa Fransisko wa Asizi unaoaminiwa kufanana naye kuliko yote

Baada ya kuishi ujana wenye raha, aliongokea maisha ya Kiinjili ili kumtumikia Yesu Kristo aliyekutana naye hasa katika watu maskini na walalahoi, akijifanya fukara vilevile, na hatimaye alitaka kufa uchi ardhini.

Akizungukazunguka huko na huko, hadi Nchi takatifu, aliwahubiria watu wa kila aina upendo wa Mungu akilenga kuiga kikamilifu kila siku mfano wa Yesu kwa maneno na matendo[1].

Alianzisha jumuiya ya kitawa yenye matawi mbalimbali ambayo leo ni utawa wenye wafuasi wengi kuliko yote wakikadiriwa kukaribia milioni moja duniani kote.

Alitangazwa na Papa Gregori IX kuwa mtakatifu tarehe 16 Julai 1228.

Anaheshimiwa na wengi hata nje ya Kanisa lake, ambalo limemtangaza [msimamizi]] wa wanaoshughulikia hifadhi ya mazingira.

Sikukuu yake inaadhimishwa tarehe 4 Oktoba[2].

Maisha na karama yake

hariri

Ulaya na Kanisa mwishoni mwa karne XII

hariri

Fransisko alipozaliwa, Ulaya na Kanisa vilikuwa na hali ya kutatanisha kuliko kawaida, kutokana na mvutano kati ya mapya na ya kale.

Mambo ya kale ni yale ya utawala wa ngazi mbalimbali ulioenea kutoka Ufaransa kuanzia karne IX: kila mtawala aliweza kugawa eneo lake na kuwakabidhi watawala wa chini akiwadai sehemu ya mapato na hasa msaada wakati wa vita, kufuatana na ahadi yao ya kuwa waaminifu kwake moja kwa moja. Utawala huo ulikuwa ukirithiwa na watoto ambao waliheshimiwa kama masharifu yaani watu wa ukoo bora na kutakiwa wawe hodari vitani. Ili watawale vizuri na kulinda maeneo yao walikuwa wakiishi katika ngome pamoja na watumishi wao. Watu wa kawaida waliishi mashambani katika hali ngumu sana hata wakaitwa watumwa wa ardhi. Hivyo Ulaya ilikuwa na askari na wakulima tu, mbali ya viongozi wa Kanisa na watawa.

Kwa hali ya maisha watawa, ambao walikuwa aina ya wamonaki tu, na makleri wa juu walilingana na masharifu, ila makleri wa chini hawakuwa na elimu wala mali nyingi. Utajiri wa Kanisa, ambalo lilifikia kumiliki karibu nusu ya ardhi ya Ulaya nzima, uliwapotosha wengi na kuvuta miito ya bandia. Wengi walitambua haja ya urekebisho ndani ya Kanisa, na juhudi za pekee zilifanywa na wamonaki kama vile Hildebrando (ambaye akawa Papa Gregori VII) na Mt. Petro Damiani katika karne XI, halafu na Mt. Bernardo wa Clairvaux katika karne XII akihimiza kupambana na maovu ya viongozi wa Kanisa hata kwa kutohudhuria ibada za wale wanaoishi vibaya. Jitihada hizo zilifanikiwa kidogo tu, kwa sababu ni vigumu kurekebisha mitindo mibaya iliyoenea, hasa katika mazingira ya dini.

Hali hiyo ilichangia uenezi wa Waislamu na hasa wa Wakatari (maana yake Watu Safi); wazushi hao, baada ya kupata wafuasi kwa kushambulia maovu ya viongozi wa Kanisa, walikuwa wakifundisha njia ya roho zao kukombolewa. Kwa kuwa eti, ulimwengu huu ni mbaya, si kazi ya Mungu wetu, ni lazima kujitenga nao kwa kukataa vitendo na vyakula vinavyohusika na uzazi. Viongozi wa Kanisa walichelewa kuona hatari hizo, mpaka zilipokwishaenea mno: ndipo walipoanza kuzikabili hata kwa silaha wakishirikiana na baadhi ya watawala. Hata hivyo uzushi ukaendelea kustawi, kwa kuwa wengi walipenda maisha magumu ya watu hao kuliko yale ya viongozi wa Kanisa; hivyo waliwasaidia wasikamatwe.

Uzushi wa aina nyingine ulianza muda mfupi baadaye (karne XI hiyohiyo) huko Lyon (Ufaransa Kusini). Mchochezi wake ni Valdo, ambaye alikuwa mfanyabiashara, akaguswa na Injili, akawapeleka mabinti wake kuishi monasterini, akauza mali zake, akawagawia maskini, akaanza kuhubiri huko na huko kama walivyofanya wengine kabla yake wakisisitiza ufukara kama njia bora ya wokovu. Wengi waliguswa wakajitahidi kushika masharti ya Injili, hata baadhi yao wakaanza kuwashambulia makleri wabaya, kususia ibada zao na kuwapiga pia. Msimamo huo ulipingwa vikali kama kiburi na unafiki. Basi Valdo na wengine walipokatazwa na maaskofu wasihubiri tena wakafikia hatua ya kuwakataa.

Huko Italia Kaskazini walitokea wengine wakisisitiza kazi kuliko ufukara (Mafukara wa Lombardia na Wahumiliati, maana yake Walionyenyekea) ambao walikuwa wote watengenezaji wa vitambaa duni vya sufu kwa ajili ya maskini na ambao walichanga mali na mapato wakiishi kishirika.

Mifumo hiyo yote ilionyesha uhai wa dini, na juhudi za walei wengi kwa urekebisho wa Kanisa. Jambo hilo jipya lilitokana na udhaifu wa makleri, pia na umbali wa wamonaki na maisha ya umati. Wamonaki pia walianza kushambuliwa kwa kufuata ufukara bandia na kula jasho la wengine, tena kwa kutoshughulikia uchungaji. Hivyo walei wakaaanza kujiongoza hata katika mambo ya kiroho.

Msingi wa matukio hayo ni miji kupanuka haraka sana. Baada ya mwaka 1000, kitovu cha Ulaya si tena vijijini na mashambani. Waliomiminika mijini walianza kukataa utawala wa ngazi wa zamani na kujichagulia viongozi ambao wadumu muda fulani tu, demokrasi ikaenea. Miji hiyo huru ikaanza kuvamia maeneo ya jirani ili kuyatawala, ukaweka watawala wa zamani chini yake. Mijini utengano wa matabaka matatu ya zamani ukawa unapungua: watu wadogo waliojiimarisha kiuchumi (hasa waliofanya biashara ya bidhaa kutoka nchi za mbali) wakazidi kupata nguvu hata kulingana na masharifu. Pamoja na utajiri watu hao walipaswa kujipatia elimu walau kidogo (ndio mwanzo wa kazi ya walimu wa watoto), hata wakatamani walingane kabisa na masharifu kwa kuiga mitindo yao ya Cortesia (maana yake Ustaarabu) ambayo ilidai kumheshimu mwanamke fulani kama mtawala wa binafsi, na kwa ajili ya huyo kujifanya wakarimu, wapendevu, wachangamfu, na kutunga nyimbo na mashairi. Mitindo hiyo ilienea kutoka ngome za masharifu hadi barabara na vichochoro vya mijini, ambapo vikosi vya wavulana vilikuwa vikiwaimbia wasichana.

 
Makazi ya Fransisko alipokuwa mdogo.

Asizi katika karne XII

hariri

Kwa asili Asizi ni mji wa Kirumi ambao ulipata umuhimu kwa sababu unatawala barabara kuu ya mkoa wa Umbria kutoka Spoleto (makao ya mfalme mdogo aliyekuwa chini ya mfalme mkuu wa Ujerumani) hadi Perugia mji uliokuwa chini ya utawala wa Papa. Wakati huo kulikuwa na ushindani mkubwa kati ya Asizi uliokuwa chini ya mfalme mkuu na jirani yake Perugia uliosimama upande wa Papa.

Mbali ya hayo ndani ya mji wenyewe yalianza mapigano kati ya mayores (wakubwa, yaani masharifu) na minores (wadogo) yaliyosababisha masharifu wengi kukimbilia Perugia na hivyo kuzidisha chuki kati ya miji hiyo. Matokeo yake ni mapambano ya mwaka 1202 ambayo Fransisko pia aliyashiriki akashikwa mateka kwa mwaka mzima.

Mbali ya hao watu wadogo waliotajirika (hasa kwa biashara), Asizi ulikuwa na mafukara, lakini tofauti na wale wa zamani (watumwa wa ardhi) ambao pamoja na kuwa na maisha magumu hawakukosa chakula (pia kutokana na mshikamano wao). Kumbe ufukara wa mijini haukuwa na dawa, uwe umetokana na kukosa kazi au kulipwa kidogo au kuugua. Ngazi ya mwisho ilikuwa ya watu waliotengwa na jamaa kama vile wakoma.

Ili tuelewe mazingira hayo ni lazima tukumbuke kwamba “sifa ya kijamii” (yaani jinsi mtu au neno wanavyotazamwa na jamii yote) ilikuwa na nguvu sana hata kuwabana wote waseme na kutenda ilivyotarajiwa. Hata hivyo mtu aliweza pia kuchangia au kubadilisha mitazamo ya umati, na Fransisko anajulikana kwa kipawa cha kuelewa, kugusa na kujivutia jamii nzima.

Mfanyabiashara

hariri

Maandishi yote yanayomhusu yanasisitiza utajiri mkubwa aliozaliwa nao. Hatuwezi kumuelewa tusipozingatia sana jambo hilo lililomfanya alelewe namna ambayo inatokana na utajiri, inasisitiza umuhimu wa utajiri na kulenga ongezeko la utajiri. Baba yake hakuwa na kiwanda, ila aliweza kutajirika ajabu kwa kusafirisha vitambaa vya thamani kutoka Ufaransa. Ingawa hatuna habari nyingi za hakika kuhusu wazazi na malezi yake, hiyo inaweza kutosha.

Mwaka wake wa kuzaliwa umehesabiwa kuanzia tarehe ya kufa, kwa kupunguza miaka iliyosemekana aliishi. Habari nyingine kuhusu kuzaliwa kwake ziliweza zikatungwa ili kumfananisha na Kristo. Jina lake la ubatizo Yohane lilibadilishwa na baba yake ili kukumbusha moja kwa moja nchi ya Ufaransa, asili ya utajiri wake (Fransisko = Mfaransa).

Elimu yake ilikuwa ya wastani: alijua kidogo Kilatini, Kifaransa, mashairi na Biblia. Malezi yake yalimfanya hodari hasa katika biashara ili aweze kuendesha shughuli zote za baba yake. Na kweli kabla hajaongoka aliiweza sana kazi hiyo. Kama kawaida ya zamani zile, akiwa na umri wa miaka 20 alianza kuhesabiwa mtu mzima na kujihusisha na siasa na vita pia ili kushika nafasi ya juu zaidi kama sharifu. Ndicho kipeo alichojiwekea. Unakumbukwa ukarimu wake kwa maskini, lakini hata ukarimu huo aliuzingatia ili kutimiza wajibu wa ustaarabu kuliko kwa kumpendeza Mungu. Kwa lengo hilohilo la kujitafutia usharifu akawa askari, na akiwa kifungoni Perugia akazidi kuwachangamkia wote, hata sharifu fulani mkorofi. Kuhusu hali iliyotangulia uongofu wake hatujui zaidi, ila mwenyewe aliona kwamba kuishi kwa kufuata mitindo ya ulimwengu kunamchukiza Mungu.

Uongofu

hariri
 
Giotto, Fransisko anavua hadharani, Basilika la juu la Asizi

Jinsi gani neema ya Mungu ilileta ndani ya mtu huyo mapinduzi yanayotushangaza hata leo? Hatujui vizuri mabadiliko hayo yalichukua muda gani, wala asili yake ni nini, ila kwamba Fransisko alianza kuguswa na huruma halisi kwa maskini. Mwenyewe alipousimulia uongofu wake katika wasia alisisitiza hatua ya kushinda hofu ya wakoma aliyokuwa nayo sana. Basi baada ya kumbusu mmojawao, alichagua kuwa nao badala ya kuwa sharifu, yaani ashuke badala ya kupanda daraja katika jamii. Baada ya uteuzi huo akasita bado kidogo kabla hajaacha ulimwengu na kujitoa kwa Mungu. Kutokana na hatua hiyo muhimu alianza kufurahia machungu badala ya matamu: ndiyo maisha ya toba (utawa).

Alipotambua kwamba ukoma wa roho yake ulitisha kuliko ule wa ngozi ya wagonjwa alianza kuwakaribia kwa upendo si tu kwa kuwagawia mali, bali hata kwa kuhatarisha afya yake: akiwa tayari kuambukizwa nao alikuwa pia tayari kutengwa na jamii moja kwa moja kama vile hao. Hivyo kwake neno kuu halikuwa ufukara kama juhudi za kujinyima, bali kama kushiriki kabisa hali ya watu wa mwisho, kwa kuwa hao ni wenzetu kwelikweli na kielelezo cha Kristo. Baadaye, Utawa wa Ndugu Wadogo ulipoimarika kwa kupata miundo ya shirika, ulisisitizwa ufukara wenyewe, kiasi kwamba kanuni ya kudumu haitaji wakoma wala huduma kwa maskini. Basi, kwa wasia wake Mt. Fransisko kabla hajafa alisisitiza tena karama halisi ya uongofu wake pamoja na mengine yaliyoanza kusahaulika, kama vile kazi za mikono.

Jambo la kwanza linaloonyesha wazi neema ya Mungu ikimfanyia kazi ni ile ndoto iliyomrudisha nyumbani wakati wa kwenda vitani akiwa na miaka 23. Tangu hapo hakuweza kuridhika tena na maisha ya zamani, akawa anafuata mawazo yake mapya badala ya kupiga kelele na wenzake baada ya kuwagharimia karamu kama mfalme wao. Alijaribu kuishi pangoni na kusali tu, akishinda vishawishi vikali vya kiroho. Siku moja katika kanisa la Mt. Damiano akasikia sauti ya Msulubiwa ikimuagiza arekebishe Kanisa lake. Ingawa alielewa maneno hayo kama kwamba yanahusu jengo, muhimu ni kwamba akawa amekutana na Msulubiwa ambaye mateso yake yanajumlisha na kuyatia maana mateso yote ya binadamu. Kuanzia hapo akaambatana na Yesu moja kwa moja katika ukweli wa maisha yake duniani: ndivyo unavyoeleweka ugumu wote wa maisha ya Fransisko.

Matendo yake yakazidi kumchukiza baba yake aliyeweza kuvumilia ubadhirifu wake ulipolenga usharifu, lakini si uliposaidia maskini tu. Hivyo baba akamshtaki mahakamani, akimpatia hatimaye nafasi ya kujitambulisha mbele ya wote kama askari wa Kristo moja kwa moja: ni kwa sababu alikataa kuhukumiwa na serikali kwa kujidai ni mtumishi wa Mungu, na hivyo ni mtu anayeweza kuhukumiwa na Askofu tu. Baba alipodai mali zake mbele ya huyo, Fransisko akakubali mara moja akimrudishia pamoja na pesa, nguo zote na hata jina, akitamka hadhara ya watu kwamba kuanzia hapo atamuita Baba Mungu tu, si Petro Bernardone tena. Uamuzi huo wa kishujaa uliowagusa sana wote ulimfanya asiweze kurudi nyuma: amejitoa kwa Mungu moja kwa moja na kuacha hakika ya riziki. Kubaki uchi mbele ya wote kulikuwa na maana nyingine pia, kwa sababu kulikuwa ni malipizi ya hadharani yaliyoweza kutolewa na Kanisa kadiri ya sheria. Hivyo Fransisko alionyesha nia yake ya kuanza na moja, akitubu anasa za zamani alizozifuata kwa nguo maridadi. Tena wakati huo lilizingatiwa sana neno la Mt. Jeromu la “kumfuata uchi Kristo uchi” kuwa ndiyo namna bora ya toba. Basi, kuanzia hapo alishiriki kabisa hali ya wasio na kitu, akisikitikia tu kutozaliwa katika hali hiyo, maana yake ufukara wake ulikuwa wa hiari na wenye kustahili, hivyo ni utajiri fulani kwa Mungu.

Kufuata mtindo wa Injili

hariri
 
Porsyunkula huko Asizi

Baada ya Fransisko kujitangaza mtawa ilimbidi atambue atakuwa wa namna gani. Alikataa upadri, lakini si kwa sababu ya kuudharau kama walivyofanya wazushi; kinyume chake, toka mwanzo alijaliwa imani ya pekee kwa ekaristi na kwa wanaohusika nayo. Aliuona upadri kuwa ni cheo kikubwa mbele ya Mungu na hata mbele ya watu, naye hakupenda kuheshimiwa wala kuwa na hakika kuhusu riziki. Kwa sababu hiyohiyo hakupenda kuwa mmonaki, ingawa aliwaheshimu Wabenedikto na kushirikiana nao vizuri. Tena akitaka kuwa kweli mtu wa mwisho na kuwaheshimu wote, hakukubali kushambulia mapadri na wamonaki kwa maovu yao.

Baada ya kukataa hali hizo mbili ndani ya Kanisa, alianza kujitafutia maisha asiyoyajua bado na asiyoweza kuelekezwa na mtu yeyote. Basi, akavaa kanzu ya mkaapweke, lakini alikuwa akirudi mjini kila siku ili kuombaomba mawe ya kutengenezea makanisa na chakula pia. Kwa hiyo hakusogea mbali na watu, bali alizidi kuhusika na maisha ya Asizi, ingawa kwa namna yake, akipokea hasa dharau alivyokusudia. Maisha yake yote hakuvunja uhusiano na jamii kama walivyofanya watawa wengi, bali akaendelea kuwa ndugu wa wote na kushiriki maisha yao ya kila siku.

Miaka miwili aliyotumia kuyarekebisha makanisa ilikuwa migumu sana kimwili na kiroho tukizingatia pia mahangaiko yake kuhusu wito. Lakini Mungu akapokea malipizi na sala yake akamuangazia sehemu ya Injili aliyoisikia wakati wa Misa. Enzi hizo walei wengi walivutiwa na maneno ya Injili ambayo waliyaelewa namna yao, bila ya ufafanuzi wa kitaalamu. Fransisko alifanya vilevile, ndiyo maana maisha yake yakaja kuwapendeza wengi na kuenea kasi ajabu. Dondoo ambalo lilimgusa na kumuangaza hasa ni lile la Yesu kuwatuma mitume wake kwa mara ya kwanza. Tangu hapo alikusudia kufuata Injili hiyo, hata ufukara wake ukapata sura nyingine, yenye kulenga utume. Kutokana na mwanga huo akabadili kanzu yake na kutupa viatu vyake na kujifungia kamba, ambayo ilikuwa ishara ya toba, tena haikuweza kuficha pesa (tofauti na mshipi wa ngozi). Halafu akaanza kuhubiri toba kwa unyofu uliowagusa wengi. Ndipo Waasizi walipoanza kumuelewa si kichaa, na ndipo alipoanza kupata wafuasi. Wa kwanza alikuwa Bernardo wa Quintavalle, mtu maarufu tena tajiri, wa pili Petro Cattani, padri. Ndio mwanzo wa jamaa iliyokuja kumhangaisha sana, kwa sababu hakuwa na wazo la kuanzisha chochote wala hakupata mtu wa kumuelekeza. Tena wakati huo haikuwa rahisi kukubali padri aongozwe na mlei.

Katika wasia wake Fransisko akikumbuka hatua hiyo muhimu alisisitiza kuwa ndipo Mungu mwenyewe alipomfunulia afuate mtindo wa Injili takatifu, yaani hasa madondoo yale aliyoyakuta katika kufungua mara tatu kitabu cha Misa kilichokuwa juu ya altare: 1) “Ukitaka kuwa mkamilifu, nenda ukauze…” 2) “Msichukue chochote kwa safari…” 3) “Anayetaka kunifuata, ajikane…” Baada ya kusoma hayo, aliwaambia wenzake ndiyo kanuni na maisha ya wale wote watakaowafuata. Ufukara wa Kifransisko ukifuata madondoo hayo ya Injili ni wa moja kwa moja kwa mtawa binafsi na kwa shirika zima. Kwa kuchagua mtindo huo wa Injili takatifu alitofautiana na watawa wale waliofuata tangu karne nyingi mtindo wa Kanisa la mwanzoni wa kuwa na mali zote shirika. Ndivyo walivyofanya wamonaki ambao hawakuwa na chochote chao binafsi, lakini monasteri zao zilikuwa tajiri, kiasi kwamba wakaanza kushambuliwa kama wanafiki wanaokula jasho la wengine na kukosa ufukara halisi.

Waamini wengi kama Bernardo na padri Petro walitamani mtindo mwingine, pamoja na uadilifu wa makleri, uchungaji wenye bidii na ujirani na watu, hasa wenye shida. Mungu aliwachagua watakatifu Fransisko na Dominiko Guzman ili kuridhisha Wakristo hao. Wote wawili walishika ufukara wa kijumuia pia, ingawa Mt. Fransisko aliusisitiza zaidi akiudai pia kama msimamo katika jamii ili kupigania ujamaa na usawa wa binadamu. Hata baada ya wengine kujiunga naye hakushughulikia suala la nyumba: waliishi kwenye pagale za makanisa, huku wakizungumziwa sana mjini kwao. Halafu wakaanza kusafiri wakihubiri huko na huko, si kama kawaida ya mapadri, bali kwa kutoa mfano wa ufukara na unyenyekevu, halafu kwa kujibu maswali ya watu waliowashangaa. Polepole waliweza pia kuhimiza toba na msamaha ili kueneza amani: muhtasari wa mawaidha yao ni salamu ile ambayo Fransisko alidai kufunuliwa na Mungu, “Bwana akujalie amani”.

Baada ya jaribio la kwanza la namna hiyo wakaongezeka, naye akawatuma tena wawiliwawili sehemu mbalimbali kisha kuwashirikisha mang’amuzi yake, kwamba wasikate tamaa kwa kuona ugumu wa baadhi ya watu, wamtegemee Mungu, wahubiri toba kwa nguvu ili kuokoa watu, wadumu watulivu katika dharau. Walipoulizwa waitwaje walijibu tu kuwa ni watu wa toba kutoka Asizi, yaani hawakujiona kuwa shirika maalumu, bali kundi mojawapo la wale wengi ambao toka zamani walijifunga kufanya toba kwa namna maalumu hadharani.

Mwaka huo 1209 walipofikia idadi ya 12 walichukua hatua ya kuelekea Roma ili kuthibitishwa na Papa katika maisha yao na kuruhusiwa naye katika utume wao, ili kushinda upinzani uliojitokeza na hasa kujihakikishia njia yao ni njema. Kwa ajili hiyo walipaswa kupanga kikamilifu zaidi wanataka kufanya nini.

Kanuni ya awali

hariri
 
Kanzu iliyotumiwa na Fransisko mwaka 1215 hivi.

Kanuni hiyo ilihitajika ili kujipendekeza kwa Papa na kupata kibali chake. Fransisko katika wasia akashuhudia kwamba aliandikisha “kwa maneno machache na kwa unyofu, naye bwana Papa akaniimarisha”. Leo hatuna tena kanuni hiyo kwa sababu iliendelea kurekebishwarekebishwa mpaka mwaka 1221 ilipotolewa kanuni ndefu ambayo tunayo, tena mpaka mwaka 1223 Papa alipothibitisha kwa maandishi toleo la kudumu linalofuatwa na Utawa wa Kwanza mpaka leo.

Ni kwamba miaka yote Fransisko alizidi kung’ang’ania azimio lake la kushika kikamilifu mtindo wa Injili takatifu, lakini pia maisha yalimlazimisha kung’amua haja ya kuulinganisha na hali halisi mbalimbali. Ugumu mwingine wa kazi hiyo kwake ulitokana na kukosa utaalamu wa sheria uliolitawala Kanisa la zamani zake kwa namna ya pekee. Hivyo hata alipomuachia mwingine uongozi akazidi kudai ndugu wamtii ingawa hana tena mamlaka juu yao. Alitamani kuwa daima mtu wa mwisho hata shirikani, lakini hakuweza kuachana na wajibu wake kwa shirika lililoanza kwa njia yake. Hata katika safari ya kwenda Roma alimteua Bernardo kuwa kiongozi, lakini mbele ya Inosenti III aliyejitokeza ni Fransisko. Papa huyo alikuwa anakabiliana na matatizo mengi ya Kikanisa na ya kisiasa, lakini yeye, kwa kupitia ngazi mbalimbali (hasa Askofu Guido wa Asizi na Kardinali Yohane wa Mt. Paulo), alifaulu kuongea naye na kukubaliwa.

Viongozi hao walijitahidi kwanza kuelekeza mifumo mipya ya kiroho kwenye umonaki, na pili iliposhindikana wakairuhusu mradi isifuate uzushi bali ikubali kuongozwa na makleri kusudi isivuruge maisha ya Kanisa. Hivyo Mt. Fransisko na wenzake walipokataa kanuni za kitawa zilizokwishakubaliwa, wakaruhusiwa kwa sauti tu wafuate azimio lake na kuhubiri toba.

Maisha ya Ndugu Wadogo huko Asizi

hariri

Kisha kurudi kwa furaha Asizi walibanana katika kibanda fulani huko Rivotorto, halafu wakahamia Porsyunkula. Mahali penyewe panatusaidia sana kuelewa karama ya Kifransisko: si maisha ya kimonaki yanayohitaji kujitegemea kwa mashamba makubwa na mifugo, wala ya wakaapweke wanaohitaji kuishi mbali na watu, bali ni utawa unaohitaji utulivu na upweke kwa ajili ya sala, lakini pia unadai uhusiano mkubwa na watu wa nje ili kupata riziki na hasa kuwajenga kwa mifano na maneno. Hivyo si kati ya watu, wala si mbali nao.

Mchana ndugu walikuwa wakienda mjini kufanya kazi mbalimbali ndogondogo na kuwahimiza watu waishi kwa uadilifu. Muda uliobaki, hasa usiku, ulikuwa kwa ajili ya sala upwekeni. Maelezo mengine kuhusu maisha ya wakati huo tunayapata tena katika wasia ambamo Fransisko ametuachia ukumbusho wa kudumu.

Jambo la kwanza ni ufukara mkuu ambao uliwadai ndugu wote wawaachie maskini mali zao. Hivyo jumuia haikuwa na kitu, ikaishi kwa shidashida pembeni mwa jamii kama watu waliotupwa, wakiridhika na kanzu moja tu, tena duni sana, wakiiongezea sanasana viraka ndani na nje ili kupunguza baridi, halafu kamba na kaptura. Mavazi ya namna hiyo yalikusudiwa kudhihirisha hali ya chini ya ndugu wadogo katika Kanisa na jamii kwa hiyo yalitakiwa kusababisha dharau, si heshima.

Jambo la pili ni maisha ya sala, ambayo yalikuwa tofauti kwa ndugu wakleri na kwa mabradha kutokana na elimu yao: wa kwanza walijua Kilatini, lugha ya liturujia; wa pili kwa kawaida hawakujua hata kusoma. Hivyo Fransisko na wakleri wengine walitumia Sala ya Kanisa, wakati mabradha walipangiwa kurudiarudia Sala ya Bwana mara kadhaa. Kwa njia ya liturujia Fransisko akazidi kupata ujuzi wa kidini, ila aliendelea kuchukia jambo moja la elimu ya wakleri, yaani kwamba mara nyingi ujuzi wao waliutumia kuipotosha maana halisi ya maneno ya sheria na hata ya ujumbe wa Mungu. Aliona kwamba elimu hiyo haitoshi kuwafanya watu watambue na kushika kama yeye uhusiano uliopo kati ya mateso ya walio wengi na yale ya Yesu. Ukweli huo unajulikana na watu wenye upendo, si wenye elimu tu. Ndiyo sababu Fransisko katika malezi hakusisitiza mafundisho na ujuzi kwa jumla, bali mang’amuzi na mifano inayogusa mioyo.

Upande wao mabradha, kama vile katika mifumo mingine ya wakati huo, walitumia Sala ya Bwana ambayo kwao ilikuwa na uzito wa pekee, kutokana na jinsi Fransisko alivyoongoka kwa kumkataa mzazi wake na kumchagua Mungu tu kuwa baba yake: ndiye tegemeo pekee na ndiye anayewafanya watu wote kuwa ndugu.

Juu ya msingi huo wa udugu, tofauti ya sala haikuleta ubaguzi kazi ya wakleri na mabradha: wote walikuwa wakijiona wajinga na kujiweka chini ya yeyote, unavyosisitiza wasia baada ya kukumbuka namna yao ya kusali. Alipouandikisha ameshamruhusu Mt. Antoni wa Padua awafundishe wanashirika mambo ya dini, lakini anaendelea kuogopa elimu hiyo pia itawavimbisha na kuwasogeza mbali na wito wao wa udogo, kumbe ujinga unaleta dharau aliyotamani daima.

Hivyo tena katika wasia akataja mara kazi ya mikono, akieleza inavyowapasa wote, hata yeye mwenye madonda ya Yesu! Katika kusisitiza kazi ndogondogo kama za mwanzoni alitoa sababu mbili: moja ni kufukuza uvivu, kama ilivyofundishwa na wamonaki toka zamani; lakini inayotajwa kwanza ni maalumu kwa kazi hizo za watu wadogo, yaani kutoa mfano mzuri kwa wanaowaona.

Wafransisko wa kwanza walifanya kazi hivyo, pasipo kulenga malipo moja kwa moja. Ndiyo sababu mara nyingine hawakulipwa chochote kwa kazi waliyoifanya. Hapo wakaikimbilia “meza ya Bwana” kwa kuombaomba nyumbani kwa watu. Zamani hizo katika Kanisa ilieleweka wazi kuwa fukara ana haki ya kuishi na kuwa Mungu anamkaribisha chakula kwa njia ya watu wakarimu.

Hata hivyo daima kuombaomba kuna ugumu wake, hasa aibu na dharau za watu. Lakini hizo zinachangia ustawi wa unyenyekevu na udogo kwa kuweka kweli katika ngazi ya mwisho ya jamii. Pamoja na malengo hayo, ni wazi kwamba kwa Fransisko njia ya kawaida ya kujipatia riziki ni kufanya kazi wenyewe, si kutegemea tu kazi ya wengine kama walivyotafsiri baadaye shirikani.

Jambo lingine la pekee ambalo Fransisko alilikumbuka katika wasia ni salamu ya amani aliyofunuliwa na Bwana. Amani hiyo ilihitajika sana, hasa wakati huo wa vitavita, lakini yeye alilenga pia amani ya rohoni, yaani amani ya Kimungu inayoondoa dhambi. Hivyo salamu yake ya Kiinjili ilikuwa kama muhtasari wa mahubiri yake.

Baada ya kukumbusha hayo yote, wasia unasisitiza ufukara wa majengo (nyumba na vikanisa) ya wafuasi wake, pamoja na msimamo ambao wawe nao, yaani wa kuishi huko kama wageni na wasafiri tu, tayari kuondoka siku yoyote kama walivyofanya huko Rivotorto walipomuachia nafasi punda wa mkulima mkorofi.

Kwa msingi huohuo wa udogo wasia unaongeza katazo la kwamba watawa wasimkimbilie Papa wala ofisi zake ili kupewa fadhili, yaani idhini ya kutenda tofauti na watu wengine. Katazo hilo kali lilikusudiwa tena kulinda udogo wa jamaa yake. Fransisko toka mwanzo alijichagulia nafasi ya mwisho asipende kushindana wala kujilinda na mtu yeyote. Katika kufafanua katazo hilo alitamka wazi kuwa ndugu wadogo wasiombe fadhili hata kama ni kwa ajili ya kuhubiri. Aliutaka utume, lakini hakupenda uharibu udogo: aliona ni afadhali kuacha utume sehemu fulani kuliko kuacha udogo.

Hivyo ni wazi tofauti iliyopo kati yake na Mt. Dominiko. Mwanzilishi huyo wa Utawa wa Wahubiri alilenga uenezaji wa ukweli, akatafuta njia za kufikia lengo hilo, yaani ubora wa mapadri wake kuhusu elimu na utakatifu; kwake ufukara ulikusudiwa kuwafanya wahubiri wapokewe katika mazingira yale tuliyoyaeleza. Ili kufikia lengo hilo alijipatia fadhili nyingi toka kwa Papa, uenezaji wa ukweli usije ukazuiwa na mamlaka nyingine yoyote. Kumbe Fransisko alifanya tofauti, kadiri ya chaguo lake: alipotambua kuwa Bwana amewaita yeye na wafuasi wake wakaokoe watu, alijitahidi kufanya hivyo lakini bila ya kuacha nafasi ya mwisho aliyojichagulia. Aliona si rahisi kubaki pembeni mwa jamii na mwa Kanisa (kama vile wakoma na wengineo), na papo hapo kujihusisha kikamilifu na maisha ya jamii (ili kuleta amani) na ya Kanisa (kama shirika kubwa ajabu), lakini kabla hajafa alisisitiza tena katika wasia chaguo la mwanzoni, ambalo ni la maana kwa karne zote kwa vile daima watakuwepo watu wa mwisho wenye kudharauliwa.

Msanii wa Bwana

hariri

Hatuwezi kuelewa vizuri maisha hayo ya mwanzoni tusipozingatia jambo lake lingine ambalo ni la pekee katika Kanisa la Magharibi, yaani tabia ya kupenda viigizo na kuchekesha watu ambayo ilichangia kwa kiasi kikubwa uenezi wa Ufransisko na mafanikio ya utume wake. Fransisko alikuwa mfurahivu si kwa silika tu wala si kutokana na muungano wake na Mungu tu. Alipenda kufanya mambo ya ajabuajabu kwa makusudi mazima ili kuwashangaza watu na kuwafanya watafute majibu ya maswali yaliyojitokeza ndani mwao. Kwa maana hiyo alipenda kujiita “ioculator” (= mtu wa viigizo na vichekesho, msanii) wa Bwana.

Zamani hizo “msanii” alikuwa mtu anayepata riziki kwa kuchekesha watu akitenda mambo ya ajabuajabu popote pale anapopita: tena haogopi kutoa ujumbe mzito katika vichekesho vyake, kwa kuwa amejiweka pembeni mwa jamii. Basi, Fransisko aliamua kuwa mtu wa namna hiyo kwa ajili ya Bwana, yaani kwa lengo la kuwavuta watu na kuwapasha ujumbe wa toba. Ndiyo njia yake ya kufanya utume.

Akiwa kwanza mfanyabiashara hodari alijua vizuri namna ya kuwavuta watu wanunue bidhaa zake; baadaye akatumia kipawa hicho ili watu wapokee ujumbe wake. Kwa namna za kuvaa na kutenda, pamoja na kuvumilia dharau, yeye na wenzake waliteka roho za watu, hata walipoacha utani na kuhimiza toba wakasikilizwa kuliko wahubiri wa kawaida makanisani. Hivyo walitangaza Injili mitaani katika mazingira ya watu wa kawaida na kwa mitindo na lugha vinavyotumika mitaani.

Basi, baada ya kumaliza kuikarabati Porsyunkula, walishughulika zaidi mjini wakitoa mfano wao na kuhimiza toba; halafu usiku hasa walikazania sala katika utulivu wa porini. Hivyo polepole Waasizi wakabadili mtazamo wao juu yao na kuanza kuwaheshimu. Ushindi huo ulipatikana kwa gharama kubwa (dharau, mateso n.k.), lakini ushindi muhimu zaidi ni ule walioupata juu yao wenyewe wakijipatia hivyo furaha na uhuru wa wana wa Mungu.

Mt. Klara na Dada Wadogo

hariri

Kuanzia karne XI wanawake wa Ulaya walishika nafasi za maana kuliko kawaida katika jamii na Kanisa, wakijitokeza pia kwa wingi kufuata tapo lolote la kiroho la Kikatoliki au la kizushi. Kumbe Fransisko hakupata mwanamke yeyote wa kumfuata kwa walau miaka sita tangu aongoke, na hata baada ya kumpata Mt. Klara, hakuwapata tena wengi. Sababu ni kwamba hakuwa mchungaji wa roho bali mtu mwenye kutafuta njia yake, wala hakuwa na mpango wa kuanzisha lolote, bali alitaka kushiriki tu hali ya watu wa mwisho. Basi, kwa wanawake nafasi ya mwisho haikuwa tu ile ya wakoma, bali pia ya makahaba na ya wachawi. Hivyo kwao chaguo la nafasi ya mwisho lilikuwa gumu zaidi, si tu upande wa mateso bali pia upande wa dharau, mbali ya kwamba lingesababisha masingizio juu ya uhusiano wao na ndugu wa kiume.

Klara alizaliwa mwaka 1193 au 1194, hivyo alikuwa na miaka 12-13 Fransisko alipovua utu wa kale mbele ya mji mzima katika uwanda ule ambako iko nyumba ya Klara. Kwa hakika huyo akaendelea kusikia habari mbalimbali juu ya Fransisko: alivyopata wafuasi, mmojawao Rufino binamu wa Klara; alivyokubaliwa na Papa n.k. Hatujui kama ni kwa sababu hizo kwamba alikataa ndoa mbalimbali mpaka akafikia umri wa miaka 18, wala hatujui kama walikutana mara nyingi kwa mashauri ya kiroho. Ila tunajua kwa hakika kuwa baada ya Klara kukimbia nyumbani usiku na kujiunga na jamaa ya ndugu wadogo, akifuatwa na mdogo wake Mt. Agnesi baada ya wiki mbili tu, Fransisko alitimiza wajibu wa kumlisha kiroho kwa mahubiri, mifano na hata maandishi.

Kwa ushahidi wa Klara tunajua kwamba hata kwake himizo kuu la Fransisko lilikuwa kuambatana moja kwa moja na ufukara wa Mwana wa Mungu. Mapema sana (kabla ya mwanzo wa mwaka 1213) Fransisko aliwaahidia akina Klara kuwashughulikia sawa na ndugu wa kiume, akafanya hivyo mpaka kufa, ingawa kipindi fulani alijizuia asiwatembelee kusudi ndugu wengine wasipate kisingizio cha kufanya hivyo.

Klara aliitikia kwa namna bora ya upendo na uaminifu, akamsaidia kuelewa vizuri zaidi wito wake wa kitume. Kufika kwake kwenyewe kulimfanya Fransisko afikirie sana na kushauriana naye juu ya maisha atakayoyashika. Mara wakatambua njia ya wanawake iwe tofauti na ile ya wanaume: kwa hiyo Klara akawa mmonaki na baadaye abesi, ingawa kwa kushika kikamilifu ufukara mkuu na kuhusiana kidugu na wenzake.

Tofauti na ndugu wadogo, ambao Fransisko aliwaelekeza wafuate “mtindo wa Injili takatifu”, yaani Yesu alivyowaagiza mitume waende (Math.10:5-15), aliwaelekeza Waklara kwenye “ukamilifu wa Injili takatifu”, unaoonyeshwa hasa na heri nane na hotuba nzima ya mlimani (Math. 5:1-7:27), bila ya kuwabana kwa mtindo huo wenye vipengele vingi vya pekee. Tofauti inaonekana wazi katika ushahidi wa Askofu Yakobo wa Vitry ulioandikwa mwaka 1216 ukieleza maisha ya Wafransisko yalivyokuwa bado mwanzoni: wote walikuwa wanakula jasho lao, ila ndugu wa kiume kwa kufanya kazi hasa mjini au vijijini, kumbe akina dada kwa kubaki katika makao yao.

Fransisko aliwahurumia daima wanawake hao waliokubali dharau na magumu ya kila aina. Yeye, ambaye hakusita hata kidogo kufuata tu mtindo wa Injili, katika kuwaongoza alizingatia sana udhaifu wa jinsia yao, na kama kwa kulazimishwa tu na Klara alimruhusu kushika magumu mengi: kila mara huruma ya Fransisko na msimamo imara wa Klara vilikutana katika kumpendeza Mungu. Ni baada tu ya kung’amua msimamo huo, kwamba Fransisko alimuahidia atawatunza sawa na ndugu wa kiume. Mwongozo wake wa uso kwa uso ukawa muhimu kuliko kuwaandikia kanuni fulani: badala yake mwenyewe alichukua jukumu la kudumisha ufukara mkuu na udugu katika monasteri ya kike.

Mkutano mkuu

hariri

Huyo Yakobo wa Vitry, pamoja na “Ngano za Wenzi Watatu”, wanashuhudia jambo lingine muhimu katika Ufransisko, yaani mkutano mkuu ambao ulikuwa ukifanyika kwanza mara mbili kwa mwaka kwenye sikukuu ya Pentekoste na ya malaika Mikaeli, halafu kwenye Pentekoste tu ya kila mwaka, halafu tena kila baada ya miaka mitatu. Kuhusu wahudhuriaji, kwanza walikuwa ndugu wote, lakini walipoongezeka mno na kuenea mpaka mbali wakaruhusiwa kuhudhuria tu wahudumu wa jamaa. Mahali pa kukutana palikuwa Porsyunkula.

Kwa muundo huo Fransisko alitaka kudumisha umoja kati ya wafuasi wake, kwa kuamua pamoja juu ya sheria na mipango ya shirika, lakini hasa kwa kustawisha upendo wao wa kidugu na kwa kuwarudisha pale walipoanzia, wasije wakasogea mbali mno na wito wao wa asili.

Mpaka alipoishi, mwenyewe alikuwa moyo wa mikutano, awe anasikilizwa au kupingwa katika juhudi zake za kuokoa mambo makuu ya karama yake mbele ya marekebisho yaliyodaiwa ili kulingana na viongozi wa Kanisa, na wingi wa ndugu wa kila aina na mazingira mapya. Marekebisho hayo yalikuwa yanabadilisha polepole sura ya jamaa, isiwe tena kundi dogo la marafiki wanaodharauliwa, bali shirika linaloeleweka na kuheshimika.

Fransisko alikubali marekebisho kadhaa ya lazima, lakini akikumbuka siku za nyuma alikuwa na hamu ya kuzirudia: ndio utatanishi ambao ulimfadhaisha mpaka mwisho ukaendelea kuvuruga umoja wa utawa wake. Upande mmoja ndugu mdogo anapaswa awe mtu wa mwisho katika Kanisa na jamii, kupenda adharauliwe na wote na kukabili magumu kama ya waliotupwa na wenzao. Upande mwingine anapaswa awe mwanakanisa akishirikiana na wachungaji na kueneza toba kwa maneno yake pia, ambayo yapokewe kama muhimu kwa wokovu wa watu. Kushika hayo mawili bila ya moja kumponyoka, ndilo jaribio la Fransisko.

Zaidi ya hayo alikuwa akihimiza mkutano mkuu, ila pengine alikataza wasipite kiasi katika malipizi, kama alivyomkataza Klara. Mwishoni, baada ya kuwabariki wote, alikuwa akichunguza na kuruhusu wahubiri wapya kwa kuzingatia walivyo katika ujuzi wa dini, uwezo wa kusema na hasa ubora wa maisha, kwa kuwa alitaka wafundishe kwa matendo kuliko kwa maneno.

Uenezi wa shirika na kujihusisha kwa Kanisa la Roma

hariri

Yakobo wa Vitry alieleza furaha yake na mshangao akiona urahisi wa ndugu wadogo kupenya aina zote za watu, tofauti na wamonaki na wakleri. Ustawi wa shirika ulifanya lipate nguvu katika Kanisa na kuenea kwa kasi mahali pengi. Watawa hao wapya wakaja kuwavutia pia wanabaraza wa Papa, hata makardinali wakataka kuwa nao nyumbani mwao, na uhusiano na Papa ukawa mkubwa zaidi na zaidi.

Wakati huohuo nyumba za Kifransisko zikaanza kuwa za kudumu zaidi, ingawa si mali ya shirika, mpaka zikapata kila moja ndugu ambaye awe mlinzi wa wanajumuia wenzake.

Kwanza aliwashughulikia Kardinali Yohane wa Mt. Paulo, lakini bila ya kujihusisha mno. Baada ya kifo chake Fransisko akaona umuhimu wa kuwa na mwingine kama mwakilishi wa Papa, akamuomba awe Hugolino, Kardinali askofu wa Ostia, aliyemtabiria atakuwa Papa (akaja kuitwa Gregori IX). Huyo alikuwa na mang’amuzi mengi ya kisiasa na ya Kikanisa alipokutana naye huko Florence; Fransisko vilevile alikuwa ameng’amua mengi kuhusu uongozi wa shirika, tena kwa uchungu, hasa kuwa hataweza kuliongoza peke yake. Ndiyo sababu ukaanzishwa muundo wa provinsya, yaani kanda zilizokuwa kila moja chini ya ndugu fulani kama mtumishi.

Ugawaji wa shirika kikanda ulihitajika hasa baada ya kuvuka milima ya Italia Kaskazini (Alps) kati ya mwaka 1215 na 1217. Mwaka huo iliamuliwa pia kuvuka Bahari ya Kati ili kuendea Nchi Takatifu. Katika mkutano mkuu ulioamua hivyo, Fransisko aliwaeleza washiriki kuwa mwenyewe hawezi kubaki nyuma kisha kuwatuma ndugu zake wakabiliane na matatizo mengi, hivyo akajichagulia Ufaransa akaondoka. Alipofika Florence ndipo alikutana na Hugolino, wakafunga urafiki wa kudumu wakaheshimiana mpaka kufa. Mazungumzo yao ya awali ni kama picha ya yale yatakayofuata: Kardinali akimshauri Fransisko afuate busara, Mt. Fransisko akieleza motomoto sababu za imani zinazomuongoza, hatimaye Kardinali akinyamaza kwa kutambua Mt. Fransisko anaongozwa na Roho Mtakatifu. Hugolino alifaulu kumzuia asiende Ufaransa, shirika lisije likashambuliwa mno na wapinzani wake mbalimbali, lakini Fransisko hakukubali kuacha mpango wa kutuma ndugu kwenye nchi nyingine za Kikristo na hata za Kiislamu, akieleza kuwa Mungu aliyewatuma kwa wokovu wa watu wote atawatunza kokote alivyoahidi. Vivyo hivyo baadaye akakubali kiasi tu mashauri ya Hugolino, asiachane na mambo makuu ya wito wake.

Mbali na dhana ya kwamba Kardinali alipotosha mfumo wa Kifransisko kwa manufaa ya uongozi wa Kanisa, ukweli ni kwamba Fransisko alikubali marekebisho kadhaa akitambua madai yenye msingi ya ndugu wapya (hasa wa nchi za mbali na wasomi); zaidi tena wema wake ulimfanya ayakubali ili kukwepa kikwazo kinachoweza kusababishwa na mabishano kati ya ndugu. Ndiyo mateso ya miaka kumi ya mwisho ya maisha yake: alizidi kuona njia bora ya kuelekea utakatifu wa Kiinjili, kumbe wafuasi wake wengi wanashindwa kuikubali au wanakataa kuelekezwa, hata kwa kumpinga na kumdharau waziwazi.

Hivyo miaka ya ushindi na uenezi wa shirika, ndiyo miaka michungu zaidi kwake, kiasi kwamba akajaribiwa kukata tamaa na kujiona amedanganyika. Lakini akadumu kutegemea maongozi ya Mungu kwa shirika lake, akapokea mateso hayo pamoja na ya mwili kama namna nyingine ya kushiriki hali ya watu wa mwisho, na hasa ya Yesu msulubiwa aliyesalitiwa na wanafunzi wake.

Kuhusu uenezi wa shirika nje ya Italia tuna vitabu viwili muhimu kwa kuwa viliandikwa na wahusika, Jordano wa Giano kuhusu Ujerumani, na Thomas wa Eccleston kuhusu Uingereza. Hasa huyo wa pili bila ya kukusudia alionyesha wazi jinsi shirika lilivyozidi kusogea mbali na nia ya Fransisko kadiri mahali palipokuwa mbali na Italia na kadiri miaka ilivyozidi kupita.

Kwa vyovyote mwanzoni mwa uenezi huo hali ilikuwa ngumu, hasa kwa sababu hayakufanyika maandalizi yoyote, tena Fransisko alikataa katakata kuwaombea waliotumwa hati ya utambulisho toka kwa Papa. Hivyo sehemu nyingine walifukuzwa kama wachawi au wazushi, kwa sababu Papa Inosenti III alikubali shirika na kanuni lakini kwa sauti tu. Makubwa zaidi yaliwapata akina Berardo waliouawa na Waislamu huko Moroko (1220): ndio wafiadini wa kwanza wa shirika.

Matukio hayo yalichangia wazo la kuhitajika maandishi yenye kuthibitisha shirika, kwa kuwa Ndugu Wadogo walikuwa hawaeleweki: si wakaapweke, wala wamonaki, wala wakanoniki, wala mapadri wanajimbo, ila walidai kuwa shirika la kitawa bila ya kufuata mojawapo kati ya kanuni nne zilizokubalika kwa watawa.

Ni kwamba Fransisko aliogopa kanuni inayofuata mtindo wa kisheria badala ya mtindo wa Kiinjili: msimamo huo ulikuwa kinyume cha mazoea ya Kanisa la Roma hasa wakati huo. Mt. Fransisko aliona Injili inazidi kutudai kadiri tunavyoendelea Kiroho, kumbe sheria zinaweza kutekelezwa na kumfanya mtu ajipongeze na kuridhika asijitahidi zaidi. Hasa alijua ujanja wa binadamu katika kufafanua sheria ili wakwepe mizigo yake. Hata hivyo Kanisa likamdai kanuni maalumu ili kuondoa wasiwasi juu ya shirika hilo jipya. Upinzani huo pia, uliochochewa na wamonaki na mapadri walioshikilia mapokeo yao, ulionyesha haja ya kuthibitisha shirika kwa kanuni maalumu. Basi, kazi ilikuwa kuitunga: Fransisko aliziandika zaidi ya moja na kuzijaribu mpaka akatoa ile ya kudumu, akisisitiza hasa ufukara mkuu na kutaka pesa iepukike.

Katika kazi hiyo alisaidiwa na ndugu wataalamu wa sheria, mbali ya mapendekezo ya mikutano mikuu na ya Kardinali Hugolino. Juhudi za Fransisko zililenga kuhakikisha kanuni haitazimisha roho, yaani hamu ya ukamilifu wa Kiinjili.

Lakini kabla hajakabili moja kwa moja kazi hiyo aliamua kwenda ng’ambo ya Bahari ya Kati kwa jaribio kuu la maisha yake: kumshuhudia Yesu mbele ya sultani na ikiwezekana kuuawa kama ndugu mdogo halisi. Akaondoka fukara tena mpole, silaha zake zikiwa ni imani na upendo tu, tofauti na askari wa msalaba waliokuwa wakiuana na Waislamu.

Hamu ya kufia dini na ugonjwa wa Mt. Fransisko

hariri
 
Fransisko mbele ya Sultani al-Kamil (karne ya 15).

Hata kabla ya mwaka 1219 Fransisko alifunga safari aende kumshuhudia Yesu kwa Waislamu: katika mwaka wa sita tangu aongoke (1211) alipanda meli ambayo ikaishia Korasya; halafu mwaka 1214 hivi akaelekea Hispania ili kuvukia Moroko lakini akaugua ikambidi arudi nyuma.

Ni kwamba kuanzia karne XI, kama matokeo ya vita vya msalaba, Wakristo walipata tena hamu kubwa ya kufia dini, wasiridhike na ile namna ya kumfia Yesu siku hadi siku kwa maisha ya kimonaki. Fransisko pia alitamani kumrudishia Yesu ule upendo mkuu wa kutoa uhai kwa rafiki yake, lakini hakujitafutia mateso kwa kuwashambulia Waislamu kwa silaha wala kwa matusi, bali alijitahidi kuwaokoa kwa mahubiri yake motomoto lakini yenye upole pia. Kama vile alivyokuwa mstaarabu kwa wote kabla hajaongoka, akaendelea kuwa hivyo hata kwa Waislamu wakati wa vita vikali kati yao na Wakristo, kwa kuwa alisema, “Mungu ni ustaarabu”.

Alikwenda kwenye kambi lao kama mwanakondoo kati ya mbwamwitu, bila ya ulinzi wala hati ya kumtetea. Mbele ya sultani alibishana na shehe wake, akaheshimiwa kwa ujasiri wake wa kuhatarisha uhai wake ili kuokoa watu, na kwa ufukara wake uliomfanya akatae zawadi yoyote. Ni wazi alikuwa na karama ya kuvutia watu wowote, hata wasio Wakristo (mpaka leo anayo, ilivyoonekana siku ya kuombea amani iliyokusanya viongozi wa dini zote huko Asizi mwaka 1986). Fransisko alibaki Mashariki ya Kati (Siria, Misri na Israeli) zaidi ya mwaka mmoja.

Kabla hajaondoka Italia, akijitambua kuwa mkuu wa shirika kubwa, aliacha ndugu wawili kama makamu wake (Mathayo wa Narni na Gregori wa Napoli) akiwagawia madaraka. Lakini kazi iliyokuwa ngumu kwa mwanzilishi mwenyewe ikawashinda, na juhudi zao hazikufaa: k.mf. walitunga sheria mpya kuhusu mfungo ili zilingane na zile kali za mashirika mengine. Kumbe Fransisko hakuzipenda, akitaka zaidi kufuata Injili inayoruhusu kula vyovyote vilivyoandaliwa kwa watu wa Mungu. Kwake ilikuwa muhimu kuwa fukara kweli, na hivyo kukosa hakika ya kupata kila siku vyakula mbalimbali ambayo ingemdai mtu ajipangie mipaka asije akawa mlafi. Mfungo wa Kifransisko hasa si wa kujichagulia, bali unatokana na maisha yenyewe. Vilevile juhudi za ndugu wengine zilileta vurugu zikienda kinyume cha nia ya Fransisko ya kutoomba hati za utetezi kutoka kwa Papa na kuhusu namna ya kuhudumia wakoma.

Hali ya shirika ikawa ngumu kiasi kwamba bradha Stefano akavuka bahari bila ya ruhusa akamuarifu Fransisko, ambaye, kisha kushauriana na Petro Cattani, na kufunuliwa na Mungu la kufanya, akarudi haraka Italia akarudisha hali ya kwanza. Lakini aliona pia umuhimu wa kuwa na Kardinali mmojawapo ambaye alishughulikie shirika akamuomba kwa Papa kama tulivyokwishaeleza.

Ndipo pia alipokabili moja kwa moja kazi ya kutunga kanuni ya kudumu. Kwa ajili hiyo alimuomba msaada ndugu Kaisari wa Speyer, mtaalamu wa Biblia, apambe maagizo ya Kanuni kwa maneno hasa ya Injili ili sheria zisizimishe hamu ya ukamilifu: madondoo hayo yanachukua thuluthi moja ya Kanuni ya mwaka 1221.

Lakini tarehe 29 Septemba 1220 katika mkutano mkuu Fransisko akachukua hatua nyingine ya kushangaza, alijiuzulu katika wadhifa wa mkuu wa shirika. Sababu ni mbalimbali: hali mbaya ya afya, matatizo ya shirika, hamu ya kurudi chini na kutii badala ya kuwa kiongozi anayeheshimiwa na Kanisa lote. Pamoja na kuacha uongozi rasmi, hakuacha kuwajibika kama kielelezo kwa wote na mtungasheria mkuu.

Toka mwanzo waliomfuata hawakuzingatia sheria fulani, bali walikusudia kufanana naye; upande wake hakukubali kuwadanganya kwa kuwaonyesha utakatifu nusunusu au kuridhika na sifa yake bila ya kulingana nayo siku kwa siku. Hasa miaka ya mwisho akakazana asije akawa mtu wa kuheshimiwa badala ya mfano wa kufuatwa. Ndiyo sababu aliacha uongozi rasmi wa shirika ili aweze kuwa kielelezo wazi zaidi cha Ndugu Mdogo hasa katika kutii.

Ni vema tujiulize namna gani mfano wake uliweza kuwagusa watu wote. Upande mmoja ni kwamba wanahitajika watu wa Mungu, lakini hasa wasio mbali na jamii bali ni wenye kushiriki mang’amuzi ya watu wa kawaida, na wenye kupatwa na magumu ya maisha ya kila siku, hasa ya maskini. Upande wa pili nafsi yenyewe ya Fransisko ilivutia wote hata kabla hajaongoka, na mvuto huo wa kimaumbile ukaja kuzidishwa na utakatifu aliojaliwa.

Uamuzi wake wa moja kwa moja wa kushika nafasi ya mwisho ulisababisha kwanza dharau, lakini baadaye heshima kwa kuwa unagusa mioyo ya wote, ukionyesha tena njia ya Mwana wa Mungu aliyeshiriki kabisa hali ya binadamu jinsi ilivyo kimaisha. Maneno yake mepesi, matendo yake ya kueleweka, mwenendo wake wa kupendeza, salamu yake ya amani, kipawa chake cha kushirikisha furaha na uchungu, na mengineyo yalichangia ushindi wake. Lakini mwenyewe alilenga zaidi ushindi mwingine, yaani ule wa kuona furaha kamili katika majaribu ya kila aina, hata kutoka kwa wafuasi wake.

Kati ya mateso yaliyomuathiri hatuwezi kusahau yale ya mwili. Wote wanashuhudia kwamba tangu ujana wake alikuwa dhaifu, lakini baada ya kuongoka akatesa mwili wake kiasi cha kulazimika baadaye auombe umsamehe. Halafu alipokwenda ng’ambo ya bahari alipatwa na maradhi mawili ya kudumu, malaria (ambayo haikuwa na tiba wakati huo) na trakoma (inayosababisha upofu wa hatua kwa hatua).

Mbali ya mateso ya maradhi yenyewe, labda ni makali zaidi yale ya matibabu ambayo aliagizwa na ndugu Elia na Kardinali, akayavumilia kishujaa kabisa, k.mf. alipochomwa mishipa yote ya damu kati ya sikio na jicho kwa kutumia chuma cha moto. Ili ashiriki zaidi mateso ya wakoma na wengineo, na hasa ya Mwana wa Mungu, hakujihurumia kama wagonjwa wengi, bali alizidi kuwahurumia wengine, kama vile ndugu waliomuuguza, wenyeji wake waliosumbuliwa na wageni waliomtembelea, na wagonjwa fukara. Tena hakuacha ukali wa malipizi yake kwa lengo la kuwa mfano bora kwa wanashirika. Nguvu zake za kiroho tu zilimfanya azidi kulishughulikia shirika na kulitungia kanuni katika hali hiyo ya ugonjwa, pamoja na kuandika barua kwa watu mbalimbali na kudai atembezwe juu ya punda ili atoe ujumbe wa Mungu walau hivyo akishindwa kuhubiri.

Uandishi wa Kanuni

hariri
 
Kanuni ya kudumu iliyothibitishwa na Papa Honori III tarehe 29 Novemba 1223.

Kama alivyokubali jamaa yake igeuke kuwa shirika, tena kubwa, Fransisko alipaswa kukubali linahitaji miundo ya kufaa, kama vile mwaka wa unovisi (ulioagizwa na Papa Honori III mwaka 1220) na hasa kanuni. Ni vigumu leo kutambua mabadiliko yote yaliyofanyika katika yale maneno machache ya Injili yaliyokubaliwa na Inosenti III kwa sauti tu (1209) mpaka ikathibitishwa kanuni ya kudumu (1223). Miaka hiyo yote Fransisko alishughulikia ufumbuzi wa suala hilo zito, akisaidiwa au kupingwa na watu wengine, hasa wanashirika.

Kama kumbukumbu ya kazi hiyo inabaki sanasana kanuni isiyothibitishwa, ambayo inashuhudia hatua iliyofikiwa mwaka 1221, na ambayo iliongoza utungaji wa kanuni ya kudumu. Kwa jumla katika ile isiyothibitishwa, sura 17 za kwanza ni za zamani kuliko zile zinazofuata. Sura ya mwisho (24) ni sala tu ambayo ilitungwa na Fransisko na kubandikwa kama nyongeza.

Kwa nini kanuni hiyo haikuthibitishwa? Nani hakuridhika nayo? Mwenyewe au wafuasi wake au viongozi wa Kanisa? Hakika yeye alipendezwa nayo sana kwa jinsi inavyohimiza kuishi Kiinjili: ndiyo sababu mwishoni aliandika ndugu hawaruhusiwi kuongeza wala kupunguza wala kubadili hiyo kanuni.

Kumbe Kanisa lilidai kanuni iwe na sura ya kisheria zaidi. Hivyo kazi ya Fransisko ikaendelea, alivyoshuhudia hasa ndugu Leo ambaye alikuwa karani wake na kufuatana naye na ndugu Bonisyo kwenye mlima wa Fonte Colombo ili kukamilisha kanuni majira ya baridi kali kati ya mwaka 1222 na 1223. Leo ametueleza upinzani wa akina Elia na uchungu wa Fransisko aliokuwa anautoa katika sala, hasa kutokana na hakika aliyokuwanayo juu ya matakwa ya Mungu kwa shirika lake: alikuwa akitulia tu katika nia yake ya kuzidi kuonyesha kwa matendo yake yale ambayo Yesu alimfunulia.

Hata hivyo, ndugu wengi hawakukubali kuyapokea kama sheria kwao. Ilimbidi akubali baadhi ya madai yao, pamoja na mashauri mbalimbali ya Kardinali na labda ya Papa mwenyewe. Lakini, pamoja na kutimiza hivyo udogo wake, hakukubali kuacha yaangushwe mambo makuu ya wito wake. Hivyo kanuni ya kudumu kwa jumla inafuata ile isiyothibitishwa, tena inaonyesha wazi kuwa mwandishi mkuu ni Fransisko, pia mengine yamesisitizwa naye hata kuliko alivyofanya katika kanuni ya muda. Pamoja na hayo, shida kubwa aliyoiona ni kwamba kanuni ya kudumu kwa mtindo wake wa kisheria inaeleweka zaidi, lakini pia inawaruhusu wanasheria kuitafsiri kwa namna inayoiondolea umotomoto wake.

Ingawa hakuweza kukwepa maendeleo hayo, mpaka mwisho wa maisha yake alitafuta mbinu nyingine, kama vile kufanya Porsyunkula iwe kielelezo cha kudumu, ndugu Bernardo awe mfano bora wa ndugu mdogo baada ya mwanzilishi kufa, na hasa wasia wake mfupi na mrefu ambao karne zilizofuata ukazidi kuchochea uaminifu wa wafuasi wake na kusababisha marekebisho mengi ya shirika.

Tarehe 29 Novemba 1223 kanuni ilithibitishwa na Honori III ikawa sheria ya Kanisa ambayo Fransisko mwenyewe hakuweza kuibadilisha tena. Kwake na kwa Kanisa haukuwepo wasiwasi kuhusu kanuni kuwa ileile ingawa imerekebishwarekebishwa. Kama vile tangu mwaka 1209 hadi 1223, hata baadaye alidai kuwa ndiyo Injili yenyewe, yaani kiini chake.

Kwa njia ya kanuni hiyo Kanisa lilipokea aina mpya ya utawa isiyofuata sheria za kawaida. Katika kanuni zimeingia kwa pamoja karama ya Fransisko na mamlaka ya Kanisa linalopokea toka kwa Bwana wake zawadi ya maisha yaliyowekwa wakfu likiifafanua na kuiratibu na kuipa miundo ya kudumu. Fransisko aliufurahia uthibitisho wa Kanisa akazidi kuwahimiza ndugu zake waifuate hiyo kanuni akiwabariki kwa kila namna. Lakini katika kuielewa tunapaswa kuzingatia pia msimamo wa Kanisa lililoithibitisha. Lenyewe linadai mpaka leo ufafanuzi wake rasmi ubaki mikononi mwake, kama ulivyotolewa na Gregori IX (1230), Nikola III (1279), Klementi V (1312) na Inosenti XI (1679).

Upande wa Fransisko tukumbuke hakika yake ya kuwa ameangazwa na Mungu aonyeshe upya mtindo wa Injili takatifu kama njia bora ya ukamilifu. Kwa msingi huo aliita kanuni kitabu cha uzima, tumaini la wokovu, uti wa Injili, njia ya ukamilifu, ufunguo wa paradiso, sharti la agano la milele. Kwa njia yake ndugu wanaweza kupata utulivu wa kweli na kuonja utamu na wepesi wa nira ya Kristo. Kwa wokovu wao alitaka wajifunze maneno ya kanuni na maana yake, na kuitafakari ili washinde ulegevu na kutimiza ahadi zao. Alitaka watumishi wajitahidi kufanya itekelezwe kikamilifu kama alivyojitahidi mwenyewe aliyeandika kuwa wanaoivunja hawahesabu tena kama Wakatoliki wala ndugu zake wala hataki kuwaona mpaka watubu. Mwishowe alitaka kila ndugu mdogo afe akishika kanuni mikononi.

Katika wasia aliwakataza pia ndugu wote wasifafanue kanuni wasije wakaipotosha katika unyofu na usafi wake. Bila ya shaka hakuweza kumkataza Papa asitoe ufafanuzi, wala hakuwa na nia ya kuzuia maelezo manyofu yenye kulenga utekelezaji wake mtakatifu. Historia ya shirika ikaja kushuhudia kuwa unyofu huo mbele ya kanuni ndio uliostawisha utakatifu wa ndugu na utume wao: marekebisho ya mfululizo ya shirika ni kazi ya Roho Mtakatifu anayehuisha shirika la Ndugu Wadogo katika njia ya Injili wasipoachana na unyofu huo.

Maandishi mengine ya Mt. Fransisko

hariri
 
Baraka kwa ndugu Leo, iliyoandikwa na Fransisko kwa mkono wake mwaka 1224
 
Toleo la zamani kuliko yote yanayojulikana ya Utenzi wa viumbe, linalotunzwa katika maktaba ya Konventi takatifu ya Mt. Fransisko, huko Asizi.

Kanuni ndiyo maandishi yaliyojenga zaidi utawa wa Ndugu Wadogo na Kanisa pia. Tunasema ni ya Fransisko ingawa alisaidiwa kuitunga: kwa kiasi fulani ni vilevile kuhusu maandishi yake mengine ya Kilatini na ya Kiitalia. Kati yake tunaanza kuona mawili yanayotusaidia sana kuelewa historia ya shirika iliyofuata. Ya kwanza ni kanuni fupi kwa makao ya upwekeni, ambayo ni muhimu ili kuelewa mwelekeo huo wa Fransisko na wenzake ambao ukawa mwelekeo wa wale wote waliotamani kurudia ufukara na unyofu wa mwanzoni. Ya pili ni barua kwa Mt. Antoni wa Padua, ambayo ni muhimu ili kuelewa msimamo wa mwisho wa Fransisko kuhusu masomo yaliyokuja kushika nafasi kubwa katika shirika na kuchangia tukio la ndugu wengi kuishi mijini katika konventi kubwa (ndiyo asili ya jina “Wakonventuali”).

Kanuni hiyo fupi iliandikwa kati ya mwaka 1217 na 1221, yaani wakati kanuni ya muda ilipokomaa kutokana na mang’amuzi ya shirika. Mtindo wa maisha ulikuwa umebadilika: ndugu wengi, badala ya kuishi karibu na miji au vijiji wakifanya kazi na watu mchana na kukesha kwa Mungu usiku, wamekuwa wanapendelea kuishi mbali na watu ili kusali tu. Kwa ajili hiyo yaliongezeka makao maalumu ya upwekeni ambamo ndugu wanaishi kwa muda fulani wakishika desturi mbalimbali za wamonaki. Fransisko aliona umuhimu wa kuuratibu mwelekeo huo ulingane na karama ya Ndugu Wadogo, kama vile alivyofanya pamoja na Klara kwa wamonaki wake wa kike. Hivyo kanuni hiyo inasisitiza udugu na upendo kati ya wakaapweke, pamoja na udogo. Katika roho hiyo ya Kifransisko zinakubalika desturi zifuatazo za kimonaki: kuwa na ugo, chumba cha binafsi, ratiba inayofuata vipindi vyote vya Sala ya Kanisa, pamoja na kuamka usiku wa manane kwa Kipindi cha Masomo, na kimya kikuu hadi Sala ya Kabla ya Adhuhuri.

Fransisko alivutiwa sana na maisha hayo, kwa sababu yalimwezesha kushika ufukara wa pekee, akiishi mapangoni kati ya miamba na katika vibanda vya fito. Sababu nyingine ilikuwa kukwepa usumbufu wa watu waliomtafuta ili kumuona na kumheshimu. Hatujui kanuni hiyo fupi iliendelea kufuatwa mpaka lini, lakini mfumo wa upwekeni ukabaki na kuchochea juhudi katika shirika hadi leo, mbali ya kwamba desturi hizo zilienea mapema katika konventi zote.

Barua kwa Mt. Antoni iliandikwa baada ya kanuni kuthibitishwa, yaani mwaka 1224 au 1225. Hiyo mistari michache yenye sura ya kisheria ilikuwa jibu rasmi kwa ombi la kuruhusiwa awafundishe teolojia Ndugu Wadogo. Labda Antoni mwenyewe aliombwa afanye kazi hiyo akiwa msomi wa kwanza katika shirika. Kwa vyovyote hakupenda kuleta jambo jipya utawani pasipo ruhusa ya mzee wake. Huyo akimjibu aliheshimu elimu yake kwa kumuita “Askofu wangu”, halafu akamkubalia akitambua ni hatua isiyoepukika, lakini akaweka sharti lilelile linalohusu kazi yoyote, yaani kwamba roho ya sala na ibada isizimishwe nayo.

Ufupi wa barua, pamoja na utovu wa mapambo, unadokeza hali ya ndani ya mwandishi, kwamba aliamua kukubali kama kwa kulazimishwa na maendeleo ya shirika, ingawa anatambua hatari za kibali chake kwa siku za mbele. Basi, akamuachia Antoni jukumu la kuhakikisha masomo yasizimishe roho ya sala, akimuamini huyo mfuasi bora aliyeficha usomi wake kusudi awe ndugu mdogo halisi.

Hivyo ni wazi kwamba Fransisko hakuiogopa teolojia yenyewe: hivyo, ingawa alijiita mjinga kwa kutokuwa na elimu ya juu, alijiongezea mwaka hadi mwaka ujuzi wa Maandiko Matakatifu kwa njia ya liturujia akajitafutia msaada wa ndugu Kaisari wa Speyer ili kupamba kanuni ya muda kwa madondoo ya Biblia. Aliyoyaogopa ni kiburi cha wasomi, majivuno ya wahubiri, na hasa ujanja wa wanasheria, akijua kwamba hayo yote yanazuia Neno la Mungu lisizae matunda. Alitaka neno lipokewe kwa unyofu jinsi lilivyo na kutekelezwa; basi, njia pekee ya kuweza kufanya hivyo ni sala ya kudumu.

Bila ya shaka, Antoni katika kufundisha alitimiza sharti alilowekewa, kama walivyokuja kufanya baada yake walimu kadhaa, hasa Mt. Bonaventura. Lakini mwaka wa kifo cha Antoni (1231) waliingia shirikani walimu wa chuo kikuu cha Paris, ambao wakaendelea kufuata mitindo walioizoea nje ya Ufransisko. Hapo ndugu wadogo kama mwenye heri Egidi wa Asizi walilaani mji huo wakisema umeharibu kabisa Asizi, yaani karama ya mwanzoni.

Basi, barua hiyo inathibitisha tena busara ya Fransisko katika kukubali mabadiliko kadhaa asiache kupigania kiini cha karama yake, kuambatana na Yesu aliyeshika nafasi ya mwisho hapa duniani, akishikamana na watu wadogo, si kwa lengo la kuwapatia maendeleo ya kidunia tu, bali hasa kuwarudishia hakika ya kuwa ni wa maana kwa Mungu, kama si kwa watu wenye uwezo. Historia ya karne zilizofuata ikathibitisha ushindi wa Fransisko, yaani uhai wa karama hiyo katika Kanisa.

Kuhusu maandishi mengine aliyotuachia, tukumbuke kwamba maradhi yalikuja kumzuia kwa kiasi fulani asiendelee kusafiri sana kwa ajili ya utume. Hasa baada ya kutiwa madonda matakatifu akaja kuhitaji mfululizo ndugu wauguzi ambao wakawa hivyo mashahidi wa mambo mengi waliyoyaandika hapo baadaye. Walishuhudia mateso yaliyompata upande wa mwili na wa roho, yaliyomhusu binafsi na yaliyolihusu shirika na upinzani ndani yake. Hata katika hali hiyo hakukubali kulegeza maisha yake, akitaka azidi kuwa kielelezo cha ndugu mdogo kwa wote. Vilevile alipopunguza utume wake, hakuacha kuwashughulikia watu walau kwa maandishi. Basi, tutayachambua kidogo kama njia bora ya kumfahamu mwenyewe na mang’amuzi yake.

Jambo ambalo linarudiarudia daima ni umuhimu mkuu wa Mwili na Damu ya Kristo. Fransisko katika maandishi anaonekana mwenezaji wa pekee wa heshima kwa sakramenti hiyo. Katika hilo alifuata maagizo ya Mtaguso IV wa Laterano, lakini alipanga heshima hiyo katika ibada yake kwa Yesu. Kwake ni ajabu upendo uliomfanya awe mwanadamu hata akakubali kufa, na ni ajabu zaidi kwamba baada ya kurudi mbinguni anazidi kuitikia padri anapomuita katika maumbo ya mkate na divai. Kutokana na hayo alidai padri aheshimiwe na kujiheshimu kwa kuishi kitakatifu pamoja na kuadhimisha na kutunza vema Mwili wa Kristo.

Kuhusu barua halisi kwa mtu maalumu zimebaki chache sana; zilizo nyingi zilitumwa kwa viongozi wa shirika, kwa wakuu wa serikali, kwa wakleri na kwa waamini wengine wote kwa jumla. Lengo lilikuwa kusisitiza mawazo yake makuu yashikwe na kufanyiwa kazi.

Barua kwa shirika lote ilikusudiwa kukumbusha wajibu wa kila ndugu kama alivyokuja kufanya katika wasia.

Kwa waamini jumla aliandika mapema barua nyingine ambayo wengi wanaamini kuwa ndio mtindo wa maisha ambayo aliwapendekezea watu wa toba ambao walivutiwa na mfano wake wakaja kuitwa Utawa wa Tatu. Ndiyo sababu tunaikuta mwanzoni mwa kanuni ya Papa Paulo VI kwa Wafransisko wa Ulimwenguni, na nusu yake ya kwanza imo pia mwanzoni mwa kanuni ya Papa Yohane Paulo II kwa mashirika ya Utawa wa Tatu. Toleo la kwanza la barua hiyo lina sura mbili, kuhusu wanaofanya toba, halafu kuhusu wasiofanya toba. Kwa Fransisko toba ni kumpenda na kumuabudu Mungu kwa nguvu zote na kuzitii amri zake. Toleo la pili likaongeza mambo mbalimbali, hasa ukurasa juu ya Neno wa Baba ambamo alijumlisha fumbo la wokovu ili wote waishi kulingana nalo.

Tofauti na vijitabu hivyo vyenye sura ya barua ya wazi, kipo kingine cha pekee kilichosababisha wataalamu wabishane sana: ni mawaidha ishirini na manne ambayo ni kama muhtasari wa mafundisho ya Kibiblia ambayo Fransisko aliyasisitiza zaidi. Hatujui nani aliyakusanya wala lini. Si ajabu kwamba sura ya kwanza inahusu ekaristi na kueleza kwa undani imani kutokana na maisha ya sala hasa. Sura nyingine karibu zote zinahusu njia ya ufukara mkuu na unyenyekevu wa moyo. Kuanzia XIII mawaidha yana mtindo wa Heri, yakichimba zile za hotuba ya mlimani], isipokuwa XXVII inamchora mtumishi wa Mungu ambaye maadili yake yamekomaa na kulingana yote, yakishinda vilema.

Aina ya mwisho ya maandishi ya Mt. Fransisko ni sala ambazo alizitunga na kuzitumia na ambazo zinatuwezesha kupenya siri ya roho yake katika uhusiano na Mungu ambao ulifikia vilele visivyoelezeka. Katika maandishi ya aina hiyo hakulenga kuwaelekeza watu wafuate karama yake wala kuwahimiza wamtumikie Mungu, bali ni yeye na Mungu tu, hivyo tunafikia chanzo cha maandishi mengine na cha maisha yote ya Fransisko.

Kati ya sala hizo tunaweza kutia maanani Sifa za Mungu alizoziandika kwa mikono yake kwa faida ya ndugu Leo, huko mlimani Alverna, mara baada ya kung’amua mateso na upendo wa Yesu msalabani. Ni tunda la moto la kumtazama Mungu na kumuitia kwa majina na sifa mbalimbali kutokana na Biblia, liturujia au moyo wenyewe wa Mt. Fransisko: ndivyo alivyozama ndani ya Mungu akirudia kumuelekea na kusema, “Wewe…”

 
Bonde la Umbria likiwa na Mlima Subasio kwa nyuma: upande wa kushoto inaonekana Assisi katikati ya mlima.

Sala nyingine ya pekee aliitunga si kwa Kilatini, bali kwa lugha yake mwenyewe akiweza hivyo kutokeza kwa urahisi mkubwa zaidi yale aliyokuwanayo moyoni. Ni Utenzi wa Viumbe Vyote, shairi la kwanza la Kiitalia, ambalo alilitunga baada ya usiku wa mateso na majaribu ya kukatisha tamaa mnamo Aprili au Mei 1225, ambapo mwishoni aliahidiwa na Mungu uzima wa milele. Katika furaha isiyoelezeka ya kuwa na hakika hiyo akiwa bado duniani, Fransisko alianza kumsifu Mungu kwa viumbe vyake ambavyo yeye kuliko watakatifu wote alijaliwa kuona vinavyohusiana na Muumba. Tusisahau hali ya afya yake wakati huo, ambapo hakuweza kuona kitu wala kuvumilia mwanga, ila alikumbuka kwa shukrani mazuri yote aliyoyaona hasa katika bonde la Spoleto, ambalo alisema hajaona mahali pazuri zaidi.

Katika utenzi huo hataji viumbe hai isipokuwa binadamu, ambaye anapaswa kumsifu Mungu hasa kwa njia ya msamaha na uvumilivu. Basi, alianza akimtukuza Mungu kama alivyozoea, kwa maneno mbalimbali, lakini mara tu akakiri kuwa binadamu hastahili hata kumtaja. Baada ya kutamka wazi jinsi Mungu alivyo Mkuu mno kuliko mtu, akaanza kumsifu kwa ndugu jua: ndicho kiumbe kilichomuuma zaidi kwa wakati huo, lakini linammaanisha Mungu kwa namna ya pekee. Halafu akamsifu kwa mwezi, nyota, upepo, majira, maji, moto na ardhi inayotuzalia matunda, maua na majani. Hatimaye akafunga utenzi akiwahimiza watu kumsifu, kumtukuza, kumshukuru na kumtumikia Mungu kwa unyenyekevu mkubwa.

Utenzi huo unapinga uzushi ambao wakati huo uliambukiza wengi na kuwafanya waone ulimwengu ni mbaya na unatawaliwa na shetani. Fransisko hakubishana nao katika mihadhara ya dini walivyofanya Wadominiko, ila aliimba kwa lugha ya watu wadogo na kwa namna inayovutia juu ya uzuri na faida ya viumbe vinavyotangaza wema wa Muumba. Kwa kupokea ujumbe huo watu walikingiwa uzushi huo. Ndiyo njia ya Ndugu Wadogo katika utume: kuwaelekea watu wadogo kwa namna rahisi inayowasaidia kumgeukia Mungu kwa moyo wote. Usomi uliwazuia wengi wasione njia hiyo wala kuwafikia watu wa kawaida. Kumbe huyo mtu mnyofu, aliyejiita mjinga, aliwaelewa na kuwafikishia ujumbe wa imani.

Mtazamo mfurahivu uliomwezesha kuviona vyote kuwa ni ndugu zake, kwa kuwa vimeumbwa na Mungu yuleyule kwa faida ya mtu, ulimfanya asichoke kumshukuru na kuwaalika wote wafanye vilevile. Kuhusu mabaya yanayotokea pia hakuwalaumu mashetani, kwa kusema ndio walioharibu ulimwengu, bali aliwaona kama askari wa Bwana waliopewa kazi ya kuadhibu makosa ya binadamu. Huyo ndiye mkuu wa viumbe vinavyoonekana, na ndiye aliyeharibu ulimwengu wote kuanzia dhambi ya asili.

Katika maandishi yake Fransisko anatukumbusha kuwa yaliyotupata ni matokeo ya dhambi zetu, na kuwa tunapaswa kutubu kwa kushiriki kazi ya Mkombozi. Mwenyewe alizingatia sana fumbo la msalaba: toka mwanzo wa uongofu wake alimzingatia Yesu katika ukweli wa mateso yake ambayo yalianza pangoni yakaendelea maisha yake yote kabla hayajafikia kilele chake huko Kalivari. Kwa njia yake ukweli huo pia ukaja kuenea ukifuta uzushi uliomuona Yesu kama malaika tu. Ukweli huo unadai si imani tu, bali upendo na mshikamano naye. Kwa misingi hiyo Fransisko hakuweza kushindwa na uchungu wote wa miaka ya mwisho ya maisha yake, bali aliugeuza kuwa furaha kamili. Ndio ushindi wake pamoja na Kristo, uliothibitisha mafundisho yake. Ndivyo alivyoweza kuongeza baadaye mistari mingine katika utenzi huo ili kumsifu Mungu hata kwa ndugu kifo.

Miaka ya mwisho

hariri
 
Kaburi la Fransisko huko Asizi.

Baada ya kanuni kuthibitishwa, Fransisko alikwenda Greccio kujitafutia kimya na upweke. Ndipo alipopata wazo la kuadhimisha Noeli kwa namna mpya ili kuitia maanani zaidi. Kwa msaada wa mtawala wa kijiji hicho, kwa ushirikiano wa wananchi na kwa mahudhurio ya ndugu wengi, liliandaliwa pango lenye majani makavu, ng’ombe na punda, halafu ikaadhimishwa Misa ambapo Fransisko, akiwa shemasi, alisoma Injili na kuhubiri kwa utamu mkubwa. Lengo lilikuwa kuwafanya Wakatoliki wote wakumbuke jinsi Mwana wa Mungu alivyojishusha duniani, si tu kwa kujifanya mtu, bali pia kwa namna alivyozaliwa na alivyoishi. Chaguo lake la ufukara lilitegemea ukweli wa maisha ya Yesu kama mtu wa mwisho na mtu wa mateso. Baada ya miezi michache ufuasi huo wa moja kwa moja ukaja kuthibitishwa na madonda matano aliyotiwa juu ya La Verna.

Kati ya Greccio na mlima huo, Fransisko alipitia maisha ya Yesu na kuyafanya yawe mang’amuzi yake matamu na ya kutisha pamoja. Ndivyo alivyozidi kutambua ubora wa mifano: kwa kuwa Yesu ametufundisha kwa matendo kuliko kwa maneno; upendo tu unaweza kupenya mafumbo yake na kupokea kikamilifu ujumbe uliofichika humo.

Kwa upendo wa namna hiyo Fransisko alipanda mlimani ili kuishi na ndugu wachache msituni. Katikati ya mwezi Septemba 1224 alifikiwa na njozi ya pekee ambayo ilimuachia mwilini madonda ya Yesu. Kwa kuwa yeye aliyaficha akaagiza wenzake pia watunze siri; baada ya kufa tu watu wengi wakaja kujionea katika maiti yake ajabu hilo, ambalo liligusa zaidi mioyo kwa sababu ilikuwa mara ya kwanza kutukia duniani.

Mbali ya mateso hayo aliyojaliwa Kimungu, miaka ya mwisho ya Fransisko iliendelea kujaa yale ya kibinadamu pia. Kwanza maradhi ambayo matibabu aliyoagizwa kuyapata hayakuleta nafuu, bali yalizidi kuharibu na kumtesa: inatosha tukumbuke alivyochomwa kwa chuma cha moto kuanzia jicho hadi sikio. Halafu juhudi zake za kuendelea kuwa kielelezo cha toba kwa wafuasi wake, ambao upande wao walizidi kumtia uchungu hata katika kumtumikia na kumheshimu. Bila kusahau majaribu ya usiku wa roho yaliyoendelea mpaka katikati ya mwaka 1225, alipoahidiwa uzima wa milele.

Miaka hiyo ina mashahidi wa pekee, yaani ndugu wanne waliomuuguza mfululizo: Anjelo Tancredi, Leo, Rufino na Yohane wa Masifu. Wa kwanza kati yao wanajulikana sana kwa jina la Wenzi Watatu: baadaye wakaja kuandika kwa utiifu mambo waliyoyaona na kuyasikia. Kwa njia yao tunaweza kufuata hatua kwa hatua maendeleo ya malaria, iliyomsumbua Fransisko miaka sita mfululizo hata mwisho ikamuua, tena ya trakoma, iliyosababisha upofu karibu kamili, pamoja na maumivu ya mfululizo yanayofanana na yale ya macho kuwekwa juu ya miiba na kutokwa machozi.

Ndugu Elia na Kardinali Hugolino walimshughulikia sana, lakini bure. Pamoja na kutambua jambo hilo, katikati ya mwaka 1224 ndugu Elia alipata njozi na kufunuliwa kuwa Fransisko ataishi bado miaka miwili tu. Safari za mgonjwa zilizidi kupungua kwa wingi na kwa umbali, zikifanyika hasa kwa kujaribu matibabu na kurudi kila mara kwenye Porsyunkula.

Hata katika hali hiyo Fransisko hakuacha kulihangaikia shirika lake kadiri alivyoona linasogea mbali na karama yake. Ili awe kielelezo kwa wote alizidi kujinyima mahitaji ya mwili, na kutamani arudie maisha yaliyodharauliwa ya mwanzoni na kutumikia wakoma. Ndipo alipowaambia wenzake, “Ndugu, tuanze kumtumikia Bwana Mungu, kwa kuwa mpaka sasa hatujapiga hatua au ni ndogo sana”.

Aliogopa shirika lake litalegea kama mengine mengi, hivyo akatafuta mbinu za kuliokoa, kusudi kanuni isiwe mwisho wa juhudi za ndugu, bali kichocheo kwa kutafuta ukamilifu. Mbinu mojawapo ni wasia wa Kiroho aliouandika zaidi ya mara moja. Muhimu zaidi ni ule mrefu aliouandika katika wiki za mwisho za maisha yake. Haukukusudiwa kuwa kanuni mpya, ila kusaidia ile iliyoahidiwa kwa Bwana: ni kumbukumbu, onyo na shauri.

Kwanza ni kumbukumbu za uongofu wa Fransisko na za maisha asili ya shirika ambayo ndugu wote wafananishe nayo maisha yao. Katika kumbukumbu hizo hakutaja mateso yote aliyojaliwa na Mungu, bali alifafanua chaguo lake la kumfuata Yesu fukara kama utajiri pekee anaowaachia watoto wake. Hivyo wasia, ukiunganisha maagizo ya kanuni na mang’amuzi ya mwanzilishi, ukabaki katika shirika kama mwiba mwilini mwa wanaopenda kulegeza kamba, na kama changamoto kwa wote kadiri walivyompenda Fransisko, kwa kuwa ndiyo maneno yake ya mwisho aliyoyatoa kwa upendo mkuu akiwa amefanana na Yesu msulubiwa hata mwilini mwake. Ndiyo sababu toka mwanzo wasia ulisababisha shirikani mabishano yaliyohitaji kuingiliwa kati na Mapapa. Upande wa wasia walisimama ndugu waaminifu, ingawa kipindi fulani baadhi yao (Fraticelli) walipita kiasi hata kujitenga na Kanisa ili kupigania ufukara; baada yao kosa hilo halijarudiwa tena. Baadhi ya marekebisho ya shirika (k. mf. Wakapuchini) yalijifunga kushika wasia pamoja na kanuni, na hivyo wakafaulu kurudia maisha asili.

Pamoja na kumbukumbu, katika wasia tunakuta maonyo ya mwisho ya Fransisko kuhusu kuheshimu mapadri, kufanya kazi za mikono, kuishi kama wakimbizi katika nyumba duni, na kutoomba fadhili yoyote kutoka ofisi za Papa.

Polepole maonyo yakawa mashauri, na hasa shauri kuu lililo lengo la yote yaliyotangulia, kiasi kwamba ni katazo kali. Linahusu ujanja wa wanasheria katika kupotosha maana halisi ya maneno ya kanuni na wasia. Kuyaelewa kunahitaji unyofu uleule wa Fransisko pamoja na nia ya kuyatekeleza. Watakaofanya hivyo watapata baraka pana kabisa ya Mungu na ya kwake. Kivutio hicho kimejaa upendo wa mzee kwa watoto wake ambao ulijitokeza mara nyingi miaka ya mwisho katika maneno, maandishi na matendo.

Mfano mmojawapo ni Takwa la Mwisho alilomuandikia Klara ili kuwahimiza mabibi fukara wadumu mpaka mwisho katika maisha na ufukara wa Yesu. Ni kama wasia mfupi kwa wafuasi wake wa kike, ambao hakuwa na wasiwasi juu ya uaminifu wao, lakini aliwaogopea watashauriwa sana na watu wengine (viongozi wa Kanisa na wanashirika) walegeze masharti ya ufukara. Ndiyo sababu aliwaachia maneno hayo kwa maandishi ili wadumu imara katika nia yao. Historia iliyofuata ikaonyesha Fransisko alitabiri vizuri kuhusu Klara na wenzake, waliopaswa kupambana mfululizo na kishawishi hicho toka kwa viongozi waliowapenda. Ushindi wa Klara katika kutetea kwa uaminifu ufukara mkuu ulipatikana siku ya mwisho kabla hajafa, alipoletewa kanuni yake imethibitishwa na Papa Inosenti IV. Katika kanuni hiyo, ambayo katika Kanisa ilikuwa ya kwanza kuandikwa na mwanamke, Klara alifuata kwa kiasi kikubwa ile ya Fransisko kama thibitisho la umoja wa Kiroho katika tofauti za mitindo yao ya maisha; pia alinakili humo wasia huo mfupi alioutumia kama silaha katika mapambano.

Mbali ya maandishi yake, Fransisko alitafuta mbinu nyingine ili kudumisha shirika katika karama yake. Mojawapo ni kuwaagiza watumishi wa shirika watunze Porsyunkula kama kielelezo cha ufukara, kimya na sala ili ndugu wote wakumbuke wanavyopaswa kuishi. Kwa ajili hiyo alitaka wapangwe huko ndugu bora ambao mmojawao akifa, nafasi yake ishikwe na mwingine. Hivyo alisisitiza tena umuhimu wa mifano, ambayo isiwe ya mtu mmojammoja tu, bali ya jumuia nzima pia. Jambo hilo halikutekelezwa mahali pale, lakini katika historia ya shirika tunaona daima ndugu wakiomba ruhusa ya kutekeleza kikamilifu kanuni pamoja na wengine, hasa katika makao ya upwekeni; tunaona pia mchango mkubwa wa jumuia hizo katika kurekebisha kwa mfano wao hali ya utawa mzima. Mfransisko ni ndugu hasa, na maisha yake yanategemea sana jumuia: hawezi kuridhika ashike kanuni kibinafsi katika jumuia iliyolegea; ndiyo sababu ya maombi hayo. Pengine viongozi wenyewe wa shirika walipoona limelegea mno wakaja kuhamasisha wenye nia waunde jumuia za pekee. Namna zote mbili zikazaa matunda tele.

Fransisko, baaada ya kuuguzwa katika jumba la Askofu wa Asizi kwa siku kadhaa, aliomba ahamishiwe Porsyunkula ili afie pale alipoanzia maisha mapya. Alikuwa amebaki mifupa na ngozi tu, isipokuwa tumbo na miguu vimevimba kama kwa safura. Ndipo alipotunga ubeti wa mwisho wa Utenzi wa Viumbe Vyote. Mwaka mmoja kabla ya hapo alikwishaongeza ubeti mwingine juu ya msamaha ili kuwapatanisha Askofu na Meya wa Asizi. Basi ubeti juu ya kifo ukaja kukamilisha utenzi mzima kwa kuchungulia uzima wa milele, ambapo sifa za Mungu zinaimbwa bila ya mwisho. Ndivyo alivyojiandaa kufa katika mapenzi ya Mungu.

Siku za mwisho zilijaa ishara za upendo kwa marafiki wake: njiani alibariki Asizi na kuuombea, akamtabiria Klara kuwa atamuona na kufarijika, akawaita ndugu waliokuwa mbali (hata “kaka” Yakopa wa Settesoli kutoka Roma), akawagawia vipande vya mkate akifuata mfano wa Yesu. Katika yote alilenga ustawi wa roho zao na wa shirika, tunavyoona hasa katika baraka zake za mwisho alizozitoa kwa kufuata mfano wa mababu wa Israeli na Musa. Aliwabariki waliokuwepo na kwa njia yao alikusudia kuwabariki wale wote watakaoingia shirikani mpaka mwisho wa dunia.

Kati ya wote ndugu Bernardo alipata baraka ya pekee akaandikiwa maneno yafuatayo yawe kumbukumbu kwa wote siku za mbele: “Ndugu wa kwanza aliyenipa Bwana ni ndugu Bernardo, naye ndiye wa kwanza kutekeleza kikamilifu kabisa Injili takatifu akiwagawia maskini mali zake zote. Kwa hiyo na kwa sifa nyingine nyingi napaswa kumpendelea kuliko ndugu mwingine yeyote katika shirika zima. Ndiyo sababu nataka na kuagiza kadiri ninavyoweza kwamba yeyote atakayekuwa mtumishi mkuu ampende na kumheshimu kama nafsi yangu, na vilevile watumishi wengine wa kanda na ndugu wa shirika lote wamjali kama ni mimi mwenyewe”. Ndiyo mbinu ya mwisho ya Fransisko ili kuzuia utawa wake usipotoke: kumuacha mtu ambaye awe kielelezo kwa viongozi na kwa ndugu wengine badala ya mwanzilishi. Kisha kumuacha huyo mwandamizi (si katika uongozi bali katika kazi muhimu zaidi ya kuwa kielelezo), Fransisko hatimaye aliweza kuaga dunia amemaliza kazi yake na kulazwa uchi ardhini, usiku kati ya tarehe 3 na 4 Oktoba 1226.

Maandishi asili kuhusu Fransisko

hariri

Baada ya kupitia maisha na maandishi ya Fransisko, ni vema kujua jinsi habari zake zilivyotufikia kwa njia ya maandishi ya watu wengine pia. Baadhi yaliandikwa mapema kabla hajafa. Baadhi ni hati za Kanisa. Baadhi ni mafupi sana na yanamtaja tu katika kusimulia mambo mengine. Baadhi ni kazi ya watu ambao si Wafransisko, tena pengine hawakupenda huo mtindo mpya wa kitawa. Lakini bila ya shaka habari nyingi zaidi zinapatikana katika maandishi ya wafuasi wake. Kati yao ana nafasi ya pekee Klara kwa sababu ya utakatifu wake, ya uhusiano wa ndani na wa muda mrefu na Mt. Fransisko, na ya uaminifu wake katika kumfuata.

Maandishi mengine ya Wafransisko yanatofautiana si tu kwa urefu, kwa mtindo, kwa mpangilio au kwa ufasaha, bali pia kwa malengo na mitazamo. Hasa mabishano katika shirika yalifanya kila mmoja akusanye habari zilizompendeza ili kumchora Fransisko kulingana na msimamo wa kikundi chake: ndiyo sababu ni lazima tulinganishe maandishi yote ili kupata ukweli.

Thoma wa Celano ndiye wa kwanza kuandika kitabu cha maisha ya Fransisko. Alifanya kazi hiyo kwa agizo la Papa Gregori IX akikusanya shuhuda zilizotolewa katika kesi ya kumtangaza Fransisko kuwa mtakatifu (16 Julai 1228) pamoja na kumbukumbu zake mwenyewe za miaka sita aliyoishi karibu naye. Mwaka 1229 akamkabidhi Papa kitabu hicho ambacho aliipa uzito hasa miaka miwili ya mwisho ya Fransisko, ambapo utakatifu wake uling’aa kwa namna ya pekee. Pamoja na kufuata mtindo wa wasifu wa watakatifu wa zamani, Thoma alisisitiza mambo mapya ya Fransisko: ufukara, unyofu, unyenyekevu, wema kwa maskini, upendo kwa viumbe, mahubiri yasiyo na mapambo, hata madonda ya Msulubiwa. Kitabu hicho rasmi kilikusudiwa hasa kueneza heshima kwa Fransisko, lakini pia kulitetea shirika lake dhidi ya upinzani wa nje.

Kwa kila shirika, heshima inayotolewa kwa mwanzilishi inaliletea heshima na nguvu katika maisha ya Kanisa, na mara nyingi hata misaada na faida upande wa uchumi. Hivyo tunaelewa mafanikio ya haraka ya ndugu Elia katika kujenga kanisa kubwa la Mt. Fransisko huko Asizi. Kwa kumtukuza, shirika lilijitukuza. Ukweli huo ni wazi katika mwendelezo wa maandishi juu yake pia.

Miaka iliyofuata (1230-1234) zilitungwa sala na nyimbo za liturujia kwa heshima ya mtakatifu huyo mpya. Kati ya watunzi, Julian wa Speyer aliandika pia maisha yake (1232-1235), hasa kwa ajili ya Wafransisko na ya malezi yao. Wakati huohuo (1232-1239) Henri wa Avranches alitunga maisha ya Fransisko kwa mtindo wa shairi.

Katika miaka 1237-1239 sura yake nyingine ilichorwa na kuenezwa na kitabu kidogo, jina lake “Agano Takatifu la Mt. Fransisko na Bibi Ufukara”. Kichwa chenyewe kinaonyesha wazi kuwa kitabu kinasisitiza upendo wake kwa Ufukara kama mchumba wake. Humo yeye anaonekana kama fukara mdogo ambaye alimtafuta sana Ufukara, akamuona katika kilele cha mlima anapokaa, hapo wakasimuliana maisha yao na kufunga agano la upendo na uaminifu. Picha hiyo ikazingatiwa sana mpaka leo.

Hiyo ilikuwa miaka ya mwisho ya uongozi wa ndugu Elia, ambayo ilizidi kuwa na mabishano kati ya Ndugu Wadogo. Hata baada ya kumuondoa madarakani, mabadiliko ya maisha yakaendelea kufanyika na kusababisha maswali juu ya nia halisi ya mwanzilishi. Ndipo (1240-1241) Yohane wa Perugia alipoandika kitabu juu ya asili ya shirika ili kuamsha ule moto uliowaka mwanzoni kati ya wenzi wa Fransisko. Habari zake ni mpya kwa asilimia 60 na kutegemea hasa ushahidi wa mwenye heri Egidi. Kwa kuwa Yohane hakujitaja kitabu hicho kinaitwa “Kitabu Kisicho na Jina cha Perugia”.

Miaka ishirini baada ya kifo cha Fransisko hamu ya kujua habari zake ilikuwa imeongezeka ndani na nje ya shirika. Ndiyo sababu wakati wa mkutano mkuu wa mwaka 1244 mtumishi mkuu mpya aliagiza ndugu wote walete kwa maandishi kumbukumbu yoyote waliyonayo juu yake. Kutokana na agizo hilo vikapatikana vitabu viwili tulivyonavyo hata leo: cha kwanza kilitungwa katika miaka 1241-1247 kikaitwa “Ngano za Wenzi Watatu”. Kinategemea sana kitabu cha Yohane wa Perugia lakini kinatia mkazo zaidi juu ya Fransisko mwenyewe na kuonyesha njia ya kuongoka na kufanana na Kristo ambayo aliifuata na ambayo inawafaa wote. Cha pili kinaitwa “Mtungo wa Asizi” (1244-1260) kwa kuwa kinakusanya shuhuda za ndugu mbalimbali walioishi naye, pamoja na kuchukua msimamo dhidi ya mabadiliko shirikani.

Lakini kazi ya kuandika upya maisha rasmi ya Fransisko ilikabidhiwa tena kwa Thoma wa Celano, naye akaimaliza mwaka 1247. Kitabu hicho hakikukusudiwa kushika nafasi ya kile alichotangulia kukiandika, bali kukitimiliza kutokana na ushahidi wa wengi, hasa wenzi watatu, waliotuma kumbukumbu zao na za wenzao wa kwanza pamoja na barua kutoka Greccio (11 Agosti 1246). Kitabu cha pili cha Thoma kilisisitiza utakatifu wa Fransisko kama mkuu kuliko ule wa waanzilishi wengine wote, kwa hiyo ujana wake haukulaumiwa kama mara ya kwanza, Mt. Dominiko anaonyeshwa akimuinamia Fransisko n.k. Vimeongezwa: maneno ya Msulubiwa kwa Fransisko, njozi ya Papa Inosenti III kuhusu kazi yake ya kulitegemeza Kanisa n.k. Fransisko alizidi kulinganishwa na Kristo kama ilivyotarajiwa na wanashirika. Pamoja na hayo kitabu hicho kinatuletea kwa wingi habari za maadili yake, misemo yake na nia zake.

Hata hivyo shirika kwa jumla halikuridhika sana; ndiyo sababu katika miaka 1250-1252 Thoma akaandika kitabu chake cha tatu ambacho kinakusanya miujiza tu ya Fransisko ili kuzidi kumtukuza yeye pamoja na shirika lake.

Lakini hivyo vitabu vitatu vya Thoma vilionekana kukosa umoja na kuwa virefu mno hasa kwa kuvinakili kwa mikono. Ndicho kisingizio cha kudai maisha ya Fransisko yaandikwe upya katika kitabu kimoja tu. Lengo lingine la ombi hilo lilikuwa kulikinga shirika dhidi ya mashambulizi makali ya walimu wa chuo kikuu cha Paris waliopinga mambo mapya yaliyoletwa na Ndugu Wadogo, ambao baadhi yao wameambukizwa pia na matabiri ya kizushi ya abati Yohakimu wa Fiore. Huyo alipanga historia ya wokovu kwa namna yake akisema mwaka 1260 utakuwa mwanzo wa wakati wa Roho Mtakatifu ambapo Kanisa litafanywa upya na karama zake. Ndipo Wafransisko hao walipochota mawazo mbalimbali ili kuthibitisha umuhimu wa Fransisko katika hatua hiyo na katika historia ya wokovu jumla.

Basi mwaka huo mkutano mkuu ulimuagiza Bonaventura wa Bagnoregio, mtumishi wa shirika lote, aandike kitabu kipya. Hicho hakina habari mpya ila kinatumia zile za Thoma wa Celano. Tofauti kubwa ni namna alivyozitumia ili kumuonyesha Fransisko kuwa si serafi tu (alivyosema Celano) bali ni yule malaika wa mhuri wa sita mwenye alama ya Mungu aliye hai aliyetabiriwa na Ufu 7:2 kuwa atapanda toka Mashariki kufungua wakati mpya. Kwake Mungu aliye hai ndiye Kristo Msulubiwa, na alama yake ndiyo madonda matano aliyomtia Fransisko. Basi, kama ni hivyo, huyo si mtakatifu mmojawapo tu, bali ana nafasi ya pekee katika historia ya wokovu.

Mchoro huo ulikubaliwa kabisa na shirika lote, hivi kwamba mkutano mkuu wa mwaka 1266 ukaweza kuagiza yateketezwe maandishi yote yaliyotangulia kuhusu Fransisko. Lengo lilikuwa wote wamkumbuke tu alivyochorwa na Bonaventura katika kitabu chake rasmi na cha kudumu. Kweli hicho kikanakiliwa sana kwanza kwa mikono, halafu kwa mashine na kufuatwa na wengi katika sanaa, mahubiri na liturujia. Kumbe vitabu vya Celano vikapotea kwa zaidi ya karne tano. Hata ndugu waliopinga mabadiliko ya shirika na msimamo wa kati wa Bonaventura, walimlaumu kwa sababu ya kupunguza habari kadhaa, lakini walipendezwa na jinsi alivyomtukuza Fransisko kuliko watakatifu wote. Kwa kitabu hicho sura yake imeshakamilika.

Vitabu vilivyotungwa baadaye, k.mf. “Kioo cha Ukamilifu” (1318), havikuweza kuichangia sana, ingawa vinatusaidia kumuelewa zaidi katika majaribu yake, nia yake na roho yake kwa kuwa vinasimulia bila mpango habari mbalimbali ambazo hazikutumiwa zote na vitabu rasmi. Hasa habari juu ya upinzani uliompata Fransisko ndani ya shirika hazikuweza kuandikwa katika vitabu vyake rasmi, lisije likapata aibu. Basi, maandishi hayo ya mwishomwisho yaliziba pengo hilo na kutuonyesha ukweli, kama picha iliyofyatuliwa kwa kamera bila wahusika kujua wala kujipanga. Vitabu hivyo vilichochea upinzani ndani ya shirika na hata dhidi ya uongozi wa Kanisa.

Baadaye tena (1328-1343) Hugolino wa Montegiorgio na mwenzake fulani wakatunga “Actus” (= “Matendo” ya Fransisko na wenzake) ambacho kikatafsiriwa kwa Kiitalia mwishoni mwa karne XIV. Tafsiri hiyo, yenye jina la “Fioretti” (= “Maua Madogo”, yaani “Visimulizi Bora”), ikasifiwa sana kwa uzuri wake, ingawa visimulizi vyake si vyote vya kihistoria. Ni kama manukato yanayotuvutia kwenye roho na utakatifu wa Fransisko, aliyekwishakufa toka siku nyingi, hivi kwamba anakumbukwa kwa mbali lakini kwa namna ya kupendeza zaidi. Miaka iliyopita imechuja ujumbe wake, ambao hivyo unang’aa kwa namna ya pekee katika kitabu hicho kilichosisitiza jinsi Fransisko alivyofanana na Yesu, wazo lililokazwa na Wafransisko wote wa karne XIV, hasa na Bartolomayo wa Pisa, mwandishi wa “Conformitates” (= “Uwiano Mwingi”).

Tarehe za maisha yake

hariri

1182 Mtoto Yohane alizaliwa na kubatizwa. Baba yake, Petro wa Bernardone, akirudi toka safarini akamtajia jina la Fransisko, yaani Mfaransa Mdogo. Baada ya hapo mtoto akalelewa katika anasa, ingawa hatujui kama ujanani aliulinda usafi wa moyo au sivyo. Kwa tabia alikuwa na uchangamfu na huruma sana kwa maskini ingawa aliogopa wenye ukoma. Pamoja na adabu njema alipewa pia elimu kidogo kupitia mapadri, halafu akawahi kuanza biashara.

1198 Asizi vilianza vita vya wenyewe kwa wenyewe: inawezekana kwamba Fransisko naye alishiriki kushambulia na kubomoa ngome ya kifalme iliyokuwepo juu ya mji huo.

1202 Asizi ulishindwa vitani na jeshi la Perugia; Fransisko mwenyewe akatekwa na kufungwa huko Perugia. Baada ya mwaka mmoja akarudishwa nyumbani kwa sababu ya ugonjwa na kisha kulipiwa pesa nyingi ili aachiliwe; lakini wakati huo wa mateso alianza kukomaa na kubadilika kimawazo.

1204 Fransisko aliendelea kuugua mwaka mzima.

1205 Fransisko aliondoka tena aende vitani kuikomboa nchi takatifu ya Yesu na kujipatia sifa na cheo, lakini kabla hajatoka mkoa wake akarudi Asizi kutokana na njozi na sauti aliyoisikia. Akaenda kuhiji Roma kwenye makaburi ya Mitume, ambapo anabadilishana nguo na fukara na kuanza kuombaomba. Katikati ya mwaka uongofu wake ulikuwa umekomaa: katika karamu ya mwisho aliyowaandalia wenzake alikuwa akifikiria kuoa bibi ufukara. Alipokutana ghafla na mtu mwenye ukoma akashuka kwenye farasi na baada ya kumsaidia pesa akambusu: ndio ushindi mkuu uliofanya kuanzia hapo kusiwe na kitu cha kumzuia. Karibu na mwisho wa mwaka akamsikia Yesu msalabani akimuambia, “Fransisko, nenda ukarekebishe Kanisa langu, kwa kuwa linataka kubomoka”: ndiyo kazi ya utawa atakaoanzisha, ingawa mwanzoni alielewa tofauti, kwamba arekebishe magofu ya kanisa aliposikia sauti hiyo.

1206 Mwanzoni mwa mwaka, baada ya miezi ya mashindano na wazazi wake, waliokuwa wakimshutumu na kumbembeleza na kumtesa, Fransisko aliitwa hukumuni kwa meya: lakini kama mtu wa Mungu akakataa mahakama ya serikali, hivyo kesi akafanyika mbele ya askofu Guido ambapo alimkataa mzazi wake pamoja na mali za urithi hata akamrudishia nguo zake zote. Baada ya kuishi kidogo kama boi kwa Wabenedikto, akahamia Gubbio ambapo akavaa kanzu ya mkaapweke,akisali na kutumikia wakoma. Mnamo Julai akarudi Asizi arekebishe kanisa la mtakatifu Damiano ambapo alitabiri watakuja kukaa masista watakatifu.

1207 Alirekebisha kanisa la mtakatifu Petro na mwisho lile la mtakatifu Maria wa Malaika: kazi za ukarabati zilichukua karibu miaka miwili, kwa kuwa mwenyewe alikuwa akienda kuombaomba mawe ya kujengea, ingawa hakuwa na uzoefu na kazi nzito namna hiyo.

1208 Siku moja wakati wa Misa alisikiliza sehemu ya Injili ambayo Yesu aliwatuma kwa mara ya kwanza mitume wake (Mt. 10:7-10); hapo akaenda kwa padri kupata tafsiri zaidi na maelezo yake, halafu kwa shangwe akaanza kutekeleza, kwa kutupilia mbali mkanda na viatu, kuvaa kamba na kanzu ngumu na kuhubiri toba. Kama siku hiyo, ambapo hatimaye alielewa wito wake, akaendelea daima kuwa mtu wa Injili na mwana wa Kanisa. Tarehe 16 Aprili, baada ya kuhubiri alifuatwa na ndugu Bernardo wa Quintavalle na labda na ndugu Petro Cattani walioamua kujiunga naye; basi akawaongoza kanisani, wakasoma Injili kwa kufungua kitabu mara tatu, wakauza mali zao zote ili kuwagawia maskini kufuatana na waliyoyasoma: ndio mwanzo wa jamaa. Tarehe 23 Aprili ndugu Egidi pia akajiunga nao, na mara wakatawanyika wawiliwawili wahubirie mikoa ya jirani. Ndipo wafuasi walipoongezeka na mwishoni mwa mwaka walifikia kuwa wanane.

1209 Kisha kurudi Asizi wanne wengine wakajiunga nao: hapo wakaamua waende wote Roma ili kupata kibali cha Papa Inosenti III kusudi wawe na hakika ya kuwa maisha yao yanampendeza Mungu, na waeleweke kwa wote kuwa ni Wakatoliki hasa, si wazushi. Baada ya kuvumilia muda fulani wakafaulu kuongea na Papa kwa msaada wa askofu wa Asizi na wa kardinali Yohane wa Mtakatifu Paulo: mara ya kwanza makardinali wengine walibishana na kutaka kupinga ombi hilo; lakini mara ya pili Papa alitoa kwa sauti kibali chake kwa maisha yao ya kitawa na kwa utume wao wa kuhubiri toba. Labda mwaka huohuo Fransisko alianzisha utawa maalumu kwa waamini wanaoishi katika mazingira ya kawaida ya ulimwenguni, waweze kufuata maisha ya Kiinjili kwa ukamilifu mkubwa zaidi.

1210 Jamaa, baada ya kuhama kibanda cha Rivotorto ili kukwepa ugomvi na mkulima mkorofi, walihamia moja kwa moja kwenye kanisa la mtakatifu Maria wa Malaika, ambapo pabaki kielelezo cha kudumu.

1211 Fransisko akaondoka kwa meli aende Sirya akawahubirie Waislamu, lakini safari ikaishia Croatia kutokana na dhoruba; hapo akarudi Italia.

1212 Usiku baada ya Jumapili ya Matawi mtakatifu Klara alitoroka nyumbani, akapokewa na Ndugu Wadogo kwa mienge, akanyolewa kitawa na Fransisko akavikwa kanzu. Baada ya muda akahamia kwenye kanisa la mtakatifu Damiano pamoja na mdogo wake mtakatifu Anyesi aliyemfuata utawani: ndio mwanzo wa utawa wa Mabibi Fukara, ambao wanaishi Kifransisko ndani ya monasteri katika sala na kazi za mikono, bila ya kutoka nje wala kufanya utume wowote.

1213 Alifunga Kwaresima nzima katika kisiwa cha ziwa Trasimeno, halafu akazawadiwa mlima La Verna.

1214 Fransisko aliondoka tena kupitia bara akawahubirie Waislamu wa Moroko, lakini njiani huko Hispania akapatwa na ugonjwa mkali akarudi Asizi, alipowapokea utawani wasomi kadhaa: baadhi yao wakashika kweli njia ya udogo, lakini wengine wakaja kuvuruga utawa kwa kutegemea mno akili yao.

1215 Novemba ulifanyika Mtaguso Mkuu wa IV wa Laterano, ambao Fransisko alihudhuria pamoja na maaskofu na wakuu wengine wa mashirika; labda ndipo alipofunga urafiki na mtakatifu Dominiko, mwanzilishi wa Utawa wa Wahubiri. Baadaye akajitahidi sana kutekeleza maagizo ya mtaguso huo.

1216 Siku mbili baada ya kifo cha Inosenti III makardinali walimchagua Honori III. Fransisko aliendelea kuzungukazunguka Italia kwa ajili ya utume.

1217 Mkutano mkuu wa Ndugu Wadogo ulipoamua wengine waende kuhubiri nje ya Italia kwa Wakristo na wasio Wakristo, Fransisko akaelekea Ufaransa lakini njiani akazuiwa na kardinali Hugolino akarudi Asizi. Kutokana na kutumwa bila ya maandalizi yoyote, ndugu wengi wakapatwa na matatizo mengi.

1218 Honori III alieneza hati yake maalumu ili kuwahakikisha maaskofu wote kuwa Ndugu Wadogo ni Wakatoliki hasa.

1219 Mkutano mkuu ulituma tena ndugu wakahubiri Injili kwa Wakristo na Waislamu. Hapo Fransisko mwenyewe akaenda kati ya Waislamu wa Misri: hakupenda mwenendo wa jeshi la Kikristo lililopigana nao, akatabiri kuwa watashindwa. Upande wake akaenda kumhubiria sultani, lakini kisha kuona hawezi kumuongoa wala kuuawa naye kishahidi akamuomba ruhusa ya kutembelea mahali patakatifu pa Palestina na Sirya.

1220 Tarehe 16 Januari huko Moroko Waislamu waliwaua ndugu Berardo na wenzake wanne waliokwenda kuwahubiria mpaka misikitini: ndio wafiadini wa kwanza wa Kifransisko. Mnamo Aprili au Mei Fransisko, alipopashwa habari za mageuzi ndani ya shirika huko Italia, akarudi kwa ufunuo wa Mungu ashike tena uongozi, lakini alipoona ugumu wa hali ya utawa, na ya kwamba wengi hawataki kumsikiliza tena, akamuomba Papa alipatie shirika kardinali Hugolino kama msimamizi na mkosoaji. Halafu katika mkutano mkuu akajiuzulu akamteua ndugu Petro Cattani aongoze jamaa kwa niaba yake.

1221 Kwa kuwa Petro Cattani kafa mapema tarehe 30 Mei ikambidi Fransisko amchague makamu mwingine, yaani ndugu Elia Bombarone, wakati wa mkutano mkuu uliohudhuriwa na wanashirika elfu tano na uliopata kuwa mkubwa kuliko yote hadi leo. Kwa kuwa walijitengenezea vibanda vya mikeka kutokana na wingi huo, mkutano unajulikana kama mkutano wa mikeka. Mungu alifanya wasikose chakula hata wengi wakashangaa kwa sababu hayakufanyika maandalizi yoyote. Pamoja na kuamua kupeleka ndugu katika nchi mbalimbali, mkutano huo ulipitisha kanuni ndefu iliyohitajika sana kwa sababu ya hali ya shirika, na hasa ongezeko hilo la ajabu. Lakini kanuni hiyo haikuthibitishwa na Papa kwa sababu fulani.

1222 Fransisko alizunguka sana Italia kwa ajili ya utume.

1223 Miezi ya kwanza alikwenda pamoja na ndugu Leo na ndugu Bonisyo kwenye mlima wa Fonte Colombo ili kuandika kanuni fupi na yenye mtindo wa kisheria zaidi kama alivyodaiwa. Upinzani wa ndugu Elia na wengineo ukashindwa katika mkutano mkuu wa Juni, hivyo kanuni ikapelekwa kwa Honori III ambaye akaithibitisha kwa maandishi tarehe 29 Novemba. Katika Misa ya usiku wa Noeli, iliyoadhimishwa huko Greccio katika pango lililoandaliwa na Fransisko, alitokea mtoto Yesu.

1224 Mnamo Julai ndugu Elia alijulishwa katika njozi kwamba Fransisko ataishi bado miaka miwili tu. Mnamo Agosti Fransisko akapanda mlima La Verna afanye mfungo mpaka sikukuu ya Malaika mkuu Mikaeli; huko upwekeni, akiwa katika malipizi na majaribu makali ya usiku wa roho, akatokewa na Yesu mwenye sura ya serafi msulubiwa akajaliwa mwilini madonda yake matano ya msalabani.

1225 Baada ya kurudi kutoka safarini mwezi wa tatu Fransisko alienda kwa mtakatifu Klara, ambapo akabaki mpaka mwezi wa tano kwa sababu ya ugonjwa na ya matibabu yasiyomsaidia kitu. Katika mateso hayo na majaribu ya Shetani, usiku mmoja akaahidiwa uzima wa milele. Kesho yake asubuhi akamshukuru Mungu kwa kumtungia Wimbo wa Ndugu Jua. Mwezi Juni akawapatanisha askofu na meya wa Asizi kwa kuwaimbishia wimbo huo baada ya kuuongezea ubeti kuhusu msamaha. Halafu akaenda kukaa Rieti kwa ajili ya matibabu mbalimbali aliyoyavumilia yote kwa moyo mkuu.

1226 Kuanzia tarehe 6 Februari alisafiri tena kwa matibabu. Mnamo Aprili huko Siena akazidiwa hata usiku fulani alikubali ombi la kuwaandikia ndugu zake wote wasia mfupi kwa maneno matatu, yaani kwamba wapendane, wafuate ufukara na kulitii Kanisa. Baada ya kupata nafuu akaandika sehemusehemu wasia mrefu zaidi ili kuchochea karama ya shirika. Waasizi wakiogopa kwamba mtakatifu wao atakuja kufa mbali wakafanya mpango wa kumrudisha kwao wakamlaza kwenye nyumba ya askofu, lakini Fransisko alipokaribia kufa akaamua kurudi kwenye kanisa la mtakatifu Maria wa Malaika. Katika hiyo safari yake ya mwisho, katikati ya njia, akabariki mji wake. Halafu kabla hajafa akawabariki wafuasi wake wote, hata wale watakaoingia utawani mpaka mwisho wa dunia. Halafu tena akaomba wamlaze ardhini kabisa bila ya nguo afe uchi kama Yesu msalabani tarehe 3 Oktoba; hapo sifa ya madonda yake ikaanza kuenea, na wengi wakaja kuyashuhudia katika maiti yake. Kesho yake, kwa maandamano ya shangwe pamoja na huzuni, akaenda kuzikwa katika kanisa kuu, lakini njiani waliwapitia mtakatifu Klara na wenzake.

1227 Tarehe 19 Machi, baada ya kufa Honori III, kardinali Hugolino alichaguliwa kuwa Papa kama alivyotabiriwa na Fransisko akajichagulia jina la Gregori IX.

1228 Mwenyewe alikwenda Asizi kusudi amtangaze rafiki yake Fransisko kuwa ni mtakatifu mbinguni (16 Julai).

1230 Masalia ya Fransisko yalihamishiwa katika kanisa kubwa lililojengwa kwa heshima yake: ndio kanisa kuu la shirika lote.

Sala yake

hariri

Ndiwe Bwana Mungu mtakatifu unayetenda maajabu.

Wewe una nguvu. Wewe ni mkuu. Wewe ndiwe mkuu kabisa.

Wewe ndiwe mfalme mwenyezi.

Wewe, Baba mtakatifu, mfalme wa mbingu na nchi.

Wewe ni utatu na umoja, Bwana Mungu wa miungu; ndiwe wema, wema wote, wema mkuu, Bwana Mungu hai na wa kweli.

Wewe ni pendo, upendo; wewe ni hekima, wewe ni unyenyekevu, wewe ni uvumilivu, wewe ni uzuri, wewe ni upole, wewe ni usalama, wewe ni utulivu, wewe ni furaha na heri, wewe ni tumaini letu, wewe ni haki, wewe ni kiasi, wewe ni mali yetu yote ya kututosha.

Wewe ni uzuri, wewe ni upole, wewe ndiwe msimamizi, wewe ni mlinzi na mtetezi wetu, wewe ni nguvu, wewe ni burudisho.

Wewe ni tumaini letu, wewe ni imani yetu, wewe ni upendo wetu, wewe ni utamu wetu wote, wewe ni uzima wetu wa milele: Bwana mkuu na wa ajabu, Mwenyezi Mungu, Mwokozi mwenye huruma.

Sala iliyosambazwa kwa jina lake

hariri

Ee Bwana unifanye niwe chombo cha amani yako.

Palipo chuki nilete mapendo,

Palipo makosa nilete msamaha,

Palipo nshaka nilete imani,

Pasipo matumaini nilete tumaini,

Palipo giza nilete mwanga,

Palipo huzuni nilete furaha.

Ee Bwana unisaidie nitamani zaidi:

Kufariji kuliko kufarijiwa,

Kuelewa kuliko kueleweka,

Kupenda kuliko kupendwa.

Kwa kuwa:

Ni katika kutoa ndipo tunapopokea,

Ni katika kusamehe ndipo tunaposamehewa,

Ni katika kufa ndipo tunapozaliwa katika uzima wa milele. Amina.

Tazama pia

hariri

Tanbihi

hariri

Marejeo

hariri
 
Basilika la Mt. Fransisko mjini Asizi.
 • Ngano za Wenzi Watatu – Kumbukumbu ya maisha ya Mtakatifu Fransisko wa Asizi ilivyoandikwa na Ndugu Leo, Rufino na Angelo – tafsiri ya Ndugu Wafransisko Wakapuchini – ed. T.M.P. Book Department – Tabora 1987
 • Fioretti – Visimulizi Kuhusu Mtakatifu Fransisko wa Asizi – tafsiri ya Rikardo Maria, U.N.W.A. n.k. – ed. Benedictine Publications Ndanda Peramiho – Ndanda 1996 – ISBN 9976-63-468-4
 • V. TURETTA, Mt. Fransisko wa Asizi – tafsiri ya Ndugu Wafransisko Wakapuchini – ed. Santuario Porziuncola – Assisi 1990
 • G. NIKOLAI, Ndugu Fransisko wa Asizi – Katuni zilizotolewa na Ndugu Wafransisko wa TanzaniaDar es Salaam 1982

Vitabu vya lugha nyingine

hariri
 • Bonaventure; Cardinal Manning (1867). The Life of St. Francis of Assisi (from the Legenda Sancti Francisci) (1988 ed.). Rockford, Illinois: TAN Books & Publishers. ISBN 978-0-89555-343-0
 • Chesterton, Gilbert Keith (1924). St. Francis of Assisi (14 ed.). Garden City, New York: Image Books.
 • Englebert, Omer (1951). The Lives of the Saints. New York: Barnes & Noble.
 • Karrer, Otto, ed., St. Francis, The Little Flowers, Legends, and Lauds, trans. N. Wydenbruck, (London: Sheed and Ward, 1979)
 • Robinson, Paschal (1913). "St. Francis of Assisi". Catholic Encyclopedia. New York: Robert Appleton Company.   "St._Francis_of_Assisi". Catholic Encyclopedia. New York: Robert Appleton Company. 1913.
 • Friar Elias, Epistola Encyclica de Transitu Sancti Francisci, 1226.
 • Pope Gregory IX, Bulla "Mira circa nos" for the canonization of St. Francis, 19 Julai 1228.
 • Friar Tommaso da Celano: Vita Prima Sancti Francisci, 1228; Vita Secunda Sancti Francisci, 1246–1247; Tractatus de Miraculis Sancti Francisci, 1252–1253.
 • Friar Julian of Speyer, Vita Sancti Francisci, 1232–1239.
 • St. Bonaventure of Bagnoregio, Legenda Maior Sancti Francisci, 1260–1263.
 • Ugolino da Montegiorgio, Actus Beati Francisci et sociorum eius, 1327–1342.
 • Fioretti di San Francesco, the "Little Flowers of St. Francis", end of the 14th century: an anonymous Italian version of the Actus; the most popular of the sources, but very late and therefore not the best authority by any means.
 • The Little Flowers of Saint Francis (Translated by Raphael Brown), Doubleday, 1998. ISBN 978-0-385-07544-2

Viungo vya nje

hariri