Yohane Parenti
Yohane Parenti (Carmignano? - 1250) alikuwa mfuasi wa Fransisko wa Asizi ambaye baada yake aliongoza shirika la Ndugu Wadogo (1227-1232).
Maisha
haririLabda alizaliwa Carmignano (Italia), lakini alisoma sheria na kupata nafasi ya hakimu huko Civita Castellana.
Alijiunga na utawa pamoja na mwanae baada ya ziara ya Fransisko mjini Firenze mwaka 1211[1].
Mwaka 1219 Fransisko alimtuma Hispania alipoanzisha konventi ya kwanza ya shirika, mjini Zaragoza.
Akiwa bado mkuu wa kanda ya Hispania, mkutano mkuu wa Assisi (1227) ulimchagua kuwa mkuu wa shirika lote.
Miaka ya mwisho ya maisha yake, Fransisko, pamoja na kuzidi kuheshimiwa, alizidi pia kuonekana anazuia shirika lisifuate mkondo wa historia ndani ya Kanisa. Pamoja na kukiri utakatifu wake na wa karama yake asili, wengi waliona haja ya kuondoa kizuio hicho: ndiyo kazi aliyoikabili ndugu wa kwanza kuchaguliwa mwandamizi wa mwanzilishi baada ya kifo chake: Yohane Parenti (1227-1232).
Uchaguzi wake unaonekana kuwa tokeo la tathmini makini juu ya mahitaji ya shirika: alikuwa mtu mkomavu ambaye alishiriki kwa jirani maisha asili ya Fransisko, lakini pia alipata mang’amuzi mengine kama Mtumishi wa Hispania. Hivyo aliweza kulinganisha mitazamo tofauti na kuchukua maamuzi ya kufaa akitegemea pia ujuzi wake wa sheria.
Tarehe 16 Julai 1228 alifurahia ibada ya fahari ya kumtangaza Fransisko kuwa mtakatifu, akimuachia Elia Bombarone kazi ngumu ya kumjengea kanisa ambalo lionyeshe alivyoheshimiwa na waamini wote.
Lakini ilimbidi pia kukabili masuala yote yaliyojitokeza shirikani kutoka nchi mbalimbali sana. Hasa lile la msingi lililozidi kusumbua ndugu wengi, kadiri walivyozidi kung’amua ugumu wa kutekeleza kanuni jinsi ilivyo bila ya kuifafanua kama ulivyodai wasia wa mwanzilishi.
Basi, yalizuka mabishano makali kati ya walioshikilia wasia huo na wale waliotaka shirika liweze kushindana na mashirika mengine. Yeye na Watumishi wengine kutoka kanda mbalimbali (mmojawao Antoni wa Padua) wakadhani utatuzi unaweza kutokea kwa Papa tu.
Akipokea ombi lao, Papa Gregori IX (1227-1241) alitoa tamko rasmi la kwanza juu ya kanuni (1230), akitumia mamlaka yake ya Kipapa na hasa ujuzi wake wa nia ya Fransisko (ndiye aliyemsaidia kutunga kanuni alipokuwa bado Kardinali, jina lake Ugolino).
Kuhusu wasia alitamka kuwa si sheria inayowabana Wafransisko wasiweze kufafanua kanuni yao wala kufafanuliwa na Kanisa, wala kuomba wala kupewa hati na fadhili za Papa. Sababu ya msingi ni kuwa Kanisa liko juu kuliko kanuni.
Kwa kukabili suala hilo kwa mtazamo wa sheria, alikata hamu ya mwanzilishi ya kuiona kanuni kama kituo cha kuanzia safari tu, si kituo cha mwisho. Kwa namna hiyo aliwaingiza zaidi Ndugu Wadogo ndani ya kawaida ya Kanisa.
Upande wa ufukara kwa jumla alitetea msimamo wa mwanzilishi (kwa jinsi alivyomheshimu hata akamtangaza mtakatifu karibu bila ya kesi), ila aliulegeza kiasi, kwa lengo la kufanikisha zaidi utume wa Ndugu Wadogo na hivyo kurekebisha Kanisa lililokuwa na hali mbaya kiroho.
Kwa ajili hiyo aliwapa pia hati na ruhusa nyingi za pekee dhidi ya mamlaka ya Maaskofu na maparoko. Hivyo njia ikawa wazi kuligeuza shirika la wadogo wanaohubiri toba kwa unyenyekevu chini ya padri yeyote, liwe shirika imara lililo chini ya Maaskofu kwa machache tu.
Mageuzi hayo, yaliyosababisha kwa muda mrefu upinzani mwingi wa Maaskofu na mapadri wanajimbo, yalichangiwa pia na ustawishaji wa elimu ndani ya shirika uliozidi kuwalinganisha Ndugu Wadogo na watawa wengine na kuongeza idadi ya mapadri kati yao.
Baada ya kujiuzulu kwa kusukumwa.[2], alikwenda kuhubiri katika visiwa vya Corsica na Sardinia, alipofariki.
Tanbihi
hariri- ↑ Lucas Wadding, Annales minorum, 1934 : "anno 1211 Beatus Franciscus pervenit Frorentiam, ubi extra civitatem accepit a devotis civibus hospitiolum jiuxta aedem Sancti Galli, ubi multos ad suum sodalitium admisit, quorun praecipuus fuit Johannes Parens ex oppido Carmignani"
- ↑ Colin Morris, The Papal Monarchy: The Western Church from 1050 to 1250, p. 462.
Marejeo
hariri- Rosalind B. Brooke, Early Franciscan Government: Ellias to Bonaventure, Ch. 3