Punda milia

(Elekezwa kutoka Equus grevyi)
Punda milia
Punda milia
Punda milia
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Chordata (Wanyama wenye ugwe wa neva mgongoni)
Ngeli: Mammalia (Wanyama wenye viwele wanaonyonyesha wadogo wao)
Oda: Perissodactyla (Wanyama wenye kidole kimoja au vitatu mguuni)
Familia: Equidae (Wanyama walio na mnasaba na farasi)
Jenasi: Equus
Linnaeus, 1758
Nusujenasi: Hippotigris
Ngazi za chini

Spishi 3:

Punda milia au pundamilia ni wanyama wa familia Equidae wa Afrika wanaofahamika sana kwa rangi yao ya pekee ya michirizi myeupe na myeusi. Michirizi yao huwa na mpangilio tofauti kwa kila punda milia mmoja.

Ni wanyama wenye kuchangamana sana na huonekana mara nyingi kwenye makundi madogo na hata makubwa. Mbali na michirizi yao, punda milia wana nywele shingoni.

Tofauti na ndugu zao wa jirani, farasi na punda, pundamilia hajawahi kufugwa kwa mafanikio.

Kuna spishi tatu za punda milia: punda milia nyika, punda milia wa Grévy na punda milia milima, ambazo huainishwa zote kwenye nusujenasi Hippotigris. Zamani punda milia wa Grévy aliwekwa kwenye Delichohippus, lakini utafiti wa ADN umeonyesha kwamba ana uhusiano karibu na punda milia nyika. Kwa kweli, nusujenasi ya punda milia ina asili ya monofiletiki. Wanashiriki jenasi Equus na farasi na punda.

Upekee wa milia na tabia za pundamilia unawafanya kuwa miongoni mwa wanyama wanaofahamika sana kwa binadamu.

Pundamilia hupatikana katika maeneo mbalimbali, kama vile ukanda wa mbuga, savana, ukanda wa misitu, kwenye vichaka vya miiba, milimani na kwenye vilima vya pwani.

Hata hivyo sababu mbalimbali za muingiliano wa jamii na tamaduni huleta athari kubwa katika idadi ya pundamilia, hasa kutafuta ngozi na uharibifu wa makazi. Grévy’s zebra na mountain zebra wapo hatarini kutoweka. Huku plains zebra wakizidi kuwa wengi, nususpishi moja, quagga, ilitoweka kabisa mwishoni mwa karne ya 19.

Jina la ‘zebra’ limetokana na neno la Kireno cha zamani, lisemalo ‘zeura’ likimaanisha punda wa porini.


Uainishaji na mabadiliko

hariri

Punda milia walikuwa ni wa ukoo wa pili kutoka kwa ‘farasi wa mwanzo’, baada ya punda, kama takribani miaka milioni 4 iliyopita. Grévy’s zebra huaminika kuwa ndio aina ya punda milia ya kale zaidi na ya kwanza kutokea. Wanyama wa kwanza wa jenasi ya Equus inaaminika kuwa walikuwa na michirizi na hivyo zebra wamedumu na mistari hiyo mpaka sasa kutokana na kuchangamana kwao hasa katika sehemu za tropiki. Michirizi itakuwa haina kazi/faida yeyote kwa wanyama wa familia ya 'equids' wanaoishi kwa uchache sehemu za jangwani (kama vile punda na baadhi ya farasi) na kwa wale wanaoishi kwenye maeneo yenye baridi na kupukutisha kila mwaka (kama baadhi ya farasi).[1] Mabaki ya ‘equids’ wa kale zaidi yaligunduliwa huko Hagerman Fossil Beds National Monument; Hagerman, Idaho. Kisha yaliitwa 'Hagerman horse’ na jina la kisayansi Equus simplicidens. Inaaminika kuwa walikuwa sawa na Grévy’s zebra; wanyama hawa walikuwa na maumbo mafupi na ya kujaa kama punda milia na fuvu la kichwa jembamba kama la punda. Grévy’s zebra pia walikuwa na fuvu la kichwa mithili ya lile la punda. 'Hagerman horse' pia huitwa punda milia wa Amerika au punda milia wa Hagerman.


Mwainisho

hariri
 
Punda milia huko Botswana.

Kuna spishi tatu ambao wanaeleweka vizuri; kwa pamoja spishi mbili hapa wanajumla ya nususpishi nane. Punda milia ndio waliotawanyika zaidi, na mahusiano kati yao na baadhi ya nususpishi nyingine hazijaeleweka vizuri.

Spishi

hariri
 
Punda milia zeruzeru akifugwa.

Punda milia wa kwenye nyanda ‘Plains Zebra’ (Equus quagga) wana takribani nususpishi sita waliosambaa sehemu kubwa za kusini na mashariki mwa afrika. Ingawa punda milia wana jamii nyingi zenye kufanana, lakini hawachanganyi katika kuzaliana. Kila spishi huweza kuzaa tu kwa uwezo wao mpaka tu kwa msaada wa sayansi.


Maumbile ya punda milia na matumizi yake

hariri

Michirizi

hariri

Iliaminika hapo awali kuwa punda milia walikuwa kwanza na rangi nyeupe ndipo mistari ikatokea, sababu tu wana sehemu nyeupe ya chini ya tumbo. Hata hivyo utafiti katika ukuaji hasa hatua nyakati za kijusi, imeonekana kuwa mnyama huyu ana rangi nyeusi na michirizi myeupe na tumbo nyeupe kuja baadaye kama nyongeza.

 
Punda milia mama akimlea akiwa na mwanae kichakani.

Michirizi ya wima huwa kichwani, shingoni na sehemu kubwa ya mwili wake, huku michirizi ya ulalo ikiwa hasa maeneo ya nyuma na miguuni. Alama za punda milia za barabarani ziliitwa hivyo kutokana na michirizi hii ya punda milia. Hufikiriwa kuwa michirizi hii hutumiwa kwa utambulisho baina yao.[1] Kwa kuwa na mtindo tofauti wa michirizi kwa kila punda milia basi wao huweza kutambuana kwa michirizi hiyo.

Wengine huamini kuwa michirizi hii ni kwa ajili ya kumsaidia kujificha na kujihami na mazingira yao. Hii huwa kwa namna mbalimbali. Michirizi ya wima huwasaidia punda milia kujificha kwenye nyasi, na huwa na manufaa makubwa hasa kujificha ili simba wasiwaone, sababu simba hawatambui rangi.[2] Kwa kawaida punda milia aliyesimama kwenye nyasi ndefu hawezi kuonwa kabisa na simba. Pia kwa wanyama wafananao kama punda milia hukaa pamoja na hutembea pamoja. Michirizi husaidia kuwachanganya wanyama wanaowawinda na kufanya vigumu kwa wao kuwakamata. Pindi waanzapo kukimbia huelekea pande tofauti ili kuendelea kuwachanganya zaidi; washambuliaji wana shida kumchagua punda milia mmoja na kufanikiwa kumkamata; japokuwa wanabaiolojia hawajaona bado simba anapochanganywa na punda milia.

 
Punda milia akitembea.

Mwendo

hariri

Kama farasi punda mila hutembea, huenda kwa mwendo wa shoti na kukimbia kwa kawaida huwa na mwendo wa taratibu na stamina yao sana ndio huwasaidia kuwashinda adui zao. Wanapofukuzwa punda milia huenda kwa mwendo wa zig-zag kila upande kumpumbaza mwindaji. Adui anapokaribia, punda milia humshambulia adui kwa nyuma, na kupiga teke au kumng'ata adui.

 
Punda milia kwa karibu.

Milango ya fahamu

hariri

Punda milia wana uoni mzuri, inafahamika kuwa wanaona kwa rangi. Pia macho yao yapo kwa pembeni huwapa uwanja mkubwa wa kuona. Punda milia pia huona nyakati za usiku japo si kama adui zao wanaowawinda lakini uwezo wao mwema wa kusikia ni fidia.

Punda milia husikia vizuri sana na masikio yao ni ya duara zaidi kuliko ya farasi. Kama ilivyo kwa farasi, punda milia wanaweza kuzungusha masikio yao upande wowote. Zaidi ya hayo, punda milia wana uwezo mzuri wa kunusa na kuonja.

Ikolojia na tabia

hariri

Makundi ya punda milia

hariri
 
Punda milia katika Tanzania.

Kama ilivyo kwa familia ya farasi, punda milia pia huchangamana na jamii zao pia kutegemea na spishi husika. Punda milia wa mlimani na nyikani huishi kwenye makundi wenye dume mmoja na walau majike sita na watoto wao. Madume ambao hawana familia huishi kila mmoja peke yake kwenye makundi makubwa ya madume wasio na familia mpaka pale watakapoweza kutafuta jike kwa ajili ya kuanzisha familia. Wanapovamiwa na fisi au mbwa mwitu punda milia hujikusanya pamoja na watoto katikati huku wakijitahidi kuwafukuza adui.

Kama farasi wengine, punda milia hulala (husinzia) huku wamesimama na hulala tu wakati majirani wakiwalinda na maadui.

Mawasiliano

hariri
 
Punda milia akila nyasi.

Punda milia huwasiliana kwa kubweka kwa sauti kubwa na kulialia. Masikio ya punda milia huonyesha namna anavyojisikia. Akiwa kwenye hali ya utulivu na kirafiki masikio yake husimama. Anapoogopeshwa, masikio yake husukumwa mbele. Anapokuwa na hasira, masikio yanavutwa nyuma. Anapokuwa akiangalia adui, husimama kwenye msimamo wa utayari, masikio yamesimama, kichwa kipo juu, huku akiangalia. Hisia zinapozidi hususani, watakoroma pia. Anapomwona au kuhisi adui, punda milia hubweka kwa sauti.

 
Mama na ndama katika Dallas Zoo.

Chakula na malisho

hariri

Punda milia ni wanyama wala nyasi wanaozoea mazingira mbalimbali. Hula hasa kwenye nyasi lakini pia hula majani ya miti, mashina mizizi na magamba ya miti. Mfumo wao wa mmeng'enyo wa chakula huwawezesha kula chakula imara hata chenye virutubisho kidogo na kuishi.

Kama ilivyo kwa wanyama wengi, punda milia jike hukua haraka kuliko punda milia dume. Jike huweza kupata mtoto akiwa na miaka mitatu tu wakati kwa dume ni mpaka miaka mitano au sita. Jike huweza kupata kila mtoto baada ya miezi kumi na mbili na hukaa na mtoto kwa takribani mwaka mmoja. Kama ilivyo kwa farasi, ndama wa punda milia huweza kusimama, kutembea na kunyonya muda mfupi tu kisha kuzaliwa. Wanapozaliwa ndama wa punda milia huwa na rangi ya kahawia na nyeupe badala ya nyeusi na nyeupe. Ndama na punda milia wa mlimani na wale wa nyikani hutunzwa na mama zao na baba zao pia.

Mwingiliano na binadamu

hariri
 
Lord Rothschild akiwa na punda milia wakikokota mkokoteni (Equus burchelli), ambao alienda nao London mara kadhaa.

Ufugwaji

hariri

Majaribio kadhaa yalifanywa kujaribu kumtumia punda milia kukokota mkokoteni kwa sababu ya ustahimilivu wake wa magonjwa kuliko farasi, hata hivyo mengi ya majaribio haya yalishindikana kutokana na tabia za asili za punda milia kucharuka pindi anapobughudhiwa.

 
Punda milia aliyefugwa akiendeshwa katika Afrika Mashariki.

Captain Horace Hayes, katika “Points of the Horse” (circa 1893) aliainisha matumizi ya aina mbalimbali za punda milia. Huyu bwana alitumia punda milia wa milimani na kumwendesha kwa siku mbili na punda milia alimudu pamoja na mkewe na kupiga naye picha. Aligundua kuwa punda milia wa aina ‘Burchell’ ni rahisi kuwatumia na ndio chaguo sahihi hasa kwa kufuga sababu walikuwa na kinga ya kung'atwa na mbung’o. Pia alionelea wengine waitwao ‘quagga’ wanafaa vilevile kwa sababu ilikuwa rahisi kuwafundisha kupandwa na kuvuna.

Uhifadhi

hariri

Binadamu leo ana athari kubwa sana kwa punda milia. Punda milia mpaka sasa bado wanawindwa sana kwa ajili ya ngozi zao, Huko Afrika ya Kusini punda milia waliwindwa na kufikia kiasi cha pungufu ya 100 mnamo mwa 1930; hata hivyo sasa wameongezeka na kufikia 700 kutokana na juhudi za utunzaji.

Hadithi za kitamaduni

hariri

Punda milia wamehusishwa na hadithi za kale za Afrika zinazoelezea ni kwa namna gani walipata mistari ya myeusi. Kutokana na hadithi ya Bushmen ya huko Namibia, punda milia hapo awali alikuwa ana rangi nyeupe lakini alipata mistari myeusi baada ya kupigana na nyani kwenye tundu la maji. Baada ya kumpiga nyani mara kadhaa, punda milia alikosa stamina na kuangukia vijiti vilivyokuwa vinawaka moto vilivyomwunguza na kuacha makovu juu ya ngozi yake nyeupe. Kwenye filamu ya Fantasia, kentaro wawili walionyeshwa kama nusu punda milia na nusu mwanadamu badala ya nusu farasi na nusu binadamu kama ilivyozoeleka.

 
Mchoro wa punda milia uliochorwa na Ludolphus.

Punda milia ni kiungo muhimu kwenye sanaa. Kiongozi wa Mughall, jJahangir (v.1605-24) alidhihirisha mchoro wa punda milia uliochorwa na Ustad Mansur. Michirizi ya punda milia pia ni maarufu kwenye fanicha, mazulia, na mitindo.

Kwenye filamu na katuni, punda milia huwa washiriki wa kawaida, lakini huwa na uongozi fulani mfano Madagascar and Racing Stripes. Punda milia pia hutumika kama alama ya bidhaa na mashirika, kama vile Zebra Technologies and Fruit Stripe. Pia punda milia wanaonekana kwenye alama ya taifa ya Botswana.

Marejeo

hariri
  1. 1.0 1.1 Prothero D.R, Schoch R. M (2003). Horns, Tusks, and Flippers: The Evolution of Hoofed Mammals. Johns Hopkins University Press.
  2. "How do a zebra's stripes act as camouflage?". How Stuff Works. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2006-11-08. Iliwekwa mnamo 2006-11-13.