Fresh
Fresh ni wimbo uliotoka tarehe 13 Agosti 2017 kutoka kwa msanii wa muziki wa hip hop wa Tanzania, Fid Q. Utunzi wa wimbo ulikuwa kama mzaha vile. Siku moja Fid Q anaamka anakuta ujumbe kutoka kwa Tiddy Hotter, ndani yake kulikuwa na biti. Kuanzia hapo akajaribu kutungia mashairi, lakini haikuwa sawa kwake. Awali Tiddy alimtumia biti nyengine kabla ya hizi, ndipo aloporudi nyuma zaidi na kuikuta biti hii ya Fresh na kuanza kuandika mistari minne tu, mwanzoni, nayo ni:
"Fresh" | ||
---|---|---|
Kava la Fresh | ||
Wimbo wa Fid Q | ||
Umetolewa | 13 Agosti, 2017 | |
Umerekodiwa | 2017 | |
Aina ya wimbo | Hip hop | |
Lugha | Kiswahili | |
Urefu | 3:15 | |
Studio | One Love Records | |
Mtunzi | Fid Q | |
Mtayarishaji | Tiddy Hotter |
"Nikipata cash.. nakuwa FRESH kama cucumber",
"Nikiwa na dash nakuwa mjeshi bila full ngwamba",
"Kwenda resi sioni kesi Mr Ku-banda",
"Yakijiset.. sikwepeshi naweka juu chanda",
Kwa msingi huo, ndio ukawa mwanzo mzuri wa mashairi ya wimbo mzima. Kutokana na hali ya kuwa Fresh, akatunga Fresh. Baada ya kumaliza hatua za awali, akaenda studio na kurekodi ubeti wa kwanza. Ajabu iliyoje, kiitikio kilikuwa hakuna. Akaishia kuimba tu, Fresh, fresh, fresh bila kuongeza neno lolote lile.
Utayarishaji, utunzi na mikasa
haririMtayarishaji wake akaona heri ibaki kama ilivyo bila kuongeza manjonjo mengine. Tiddy Hotter ndiye mtayarishaji wa wimbo huu. Video imeongozwa na Destro wa Wanene Entertainment. Walipiga huko Kigamboni, Dar es Salaam - katika Fukwe za Malaika Beach. Lengo hasa kwa kutafuta mazingira kama ya Zanzibar, katika sehemu ya mashairi ya ubeti wa pili alitaja Zanzibar hivyo basi ili kupata walau uhalisi ikalazimu kwenda katika fukwe hizo huko Kigamboni. Siku ya kufanya video yake, Fid alikamatwa na trafiki kwa kosa la kuchomekea ili awahi safari yake. Aligandishwa sio chini ya masaa manne na trafiki, licha ya kuomba kuandikiwa makosa yake aliyofanya. Askari mwenye nongwa aliendelea kumgandisha hasa kwa kuona anaomba gharama za kosa kwa pupa.
Baada ya mabishano ya muda mrefu, hatimaye walimwachia.
Baada ya wimbo kutoka, ulipokewa vizuri. Kiasi hata kumfanya Diamond Platnumz aombe kuurudia akiwa na Rayvanny. Wimbo umerudiwa na Fid kaanza ubeti wa kwanza tofauti na toleo halisi. Wimbo umepakiwa katika akaunti ya Youtube mnamo tarehe 21 Agosti, 2017, wiki moja baada ya kutoka toleo halisi. Matokeo ya wimbo huu yalita gumzo kubwa katika mitandao ya kijamii nchini Tanzania, hasa kwa kufuatia mstari wa Diamond alitia maneno ya:
"Ukinichukia sikose hela hivyo kwangu sio kesi/ Kunicompare na Cinderella haiwezi kuwa fresh"[1]
Zogo likawa kubwa mno, matusi na kejeli nyingi zilielekea kwa Fid Q kutoka kwa mashabiki wa Ali Kiba ambao wanadhani wamekejeliwa. Japo alidai kama hakujua kama kazungukwa katika wimbo huo. Fid Q alisema yeye ni fundi wa kuficha maneno katika mistari, lakini hapo alizidiwa kete. Hasa ukizingatia yeye sio mpenzi wa kufuatilia maugomvi ya wasanii wa Bongo Flava. Wala hajui masuala ya makundi (Team-Kiba na Team-Diamond). Baada ya matusi mengi, hata ile ari ilipungua kuhusu Fresh. Ukimuuliza fresh, anasema sio fresh.[2]
Pamoja na matusi na kejeli zote kutoka kwa mashabiki wa Ali Kiba, Fid bado alisema mashabiki wa Kiba wasimpangie nani wa kuimba au kurudia wimbo wake.[3] Mashindano haya, sio tu kutoka kwa mashabiki, hata Kiba nae alionekana kutupia vijembe mistari ya Diamond kwa kuandika katika akaunti yake ya Twitter "The KING ll always Be a KING. je Umeshakitandika nilale MALKIA wangu wa nguvu ??".
Maneno hayo Kiba anarejea mstari wa Diamond aliosema:
"Toka mbuga ya Tandale,
Naona swala wana-force tuwe sare,sare,
Viuno vidogo wanataka pensi ya pepe kale,
Si walitaka kiti nimewapa hadi kitanda wakalale".[4]
Malumbano yote hayo, haikusaidia kitu, kwani hadi mwisho wa siku wimbo ulibaki kama ulivyo na video yake ya remix ilitolewa mnamo tarehe 31 Disemba, 2017.[5] Na ndiyo video ya kwanza ya Fid Q kuwa watazamaji wengi sana ndani ya muda mfupi tangu kutolewa. Imekuwa ikishika nafasi ya kwanza katika Youtube kwa ukanda wa Afrika Mashariki karibia katika juma zima tangu ilipotolewa.[6][7] Video imeongozwa na Nicroux, rangi zimepangwa na Destro FX wa Wanene Entertainment.
Marejeo
hariri- ↑ Ali Kiba Ajibu Mashairi ya Diamond Kwa kejeli nzito ???? Ilihifadhiwa 18 Februari 2018 kwenye Wayback Machine. kutoka katika blogu ya "8020fashionsblog" ingizo la 22 Agosti, 2017.
- ↑ FID Q; NIMEOGA MATUSI, NENO ZITO KWA DIAMOND NA KIBA ingizo la Agosti 24, 2017 - kwenye idhaa ya Mo Faze, YouTube.
- ↑ FID Q KAWAFUNGUKIA TEAM KIBA: "huwezi kunipangia" Fid katika idhaa ya Millard Ayo - YouTube mnamo Agosti 25, 2017.
- ↑ Alikiba ajibu diss ya Diamond ‘Malkia wangu wa nguvu umeshanitandikia kitanda? blogu ya TeamTZ ingizo la 22 Agosti, 2017.
- ↑ Fid Q Feat. Diamond Platnumz & Rayvanny - Fresh Remix (Official Video) idhaa ya Fid Q katika YouTube
- ↑ New Video: Fid Q Ft. Diamond Platnumz & Rayvanny – Fresh Remix wavuti ya Bongo5 ingizo la 31 Disemba, 2017.
- ↑ VideoMPYA: Fid Q ametuletea video ya wimbo wa Fresh Remix aliomshirikisha Diamond, Rayvanny wavuti ya Millard Ayo ingizo la 31 Disemba, 2017.
Viungo vya Nje
hariri- Video ya Fresh Remix katika YouTube
- Video ya Fresh (orijino) katika YouTube