Hija kwa maana ya kawaida ni safari au matembezi ya kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine kwa lengo maalum. Yaweza kuwa safari ya mtu binafsi au ya kikundi cha watu. Inaweza kuwa safari ya siku moja au siku kadhaa. Hii inategemea umbali wa safari au matembezi hayo maalum au nia halisi ya kufanya safari hiyo au maamuzi ya mtu au kikundi husika kinachofanya hija hiyo.

Hija ya kiroho ni safari maaalum ya kiroho ndani ya Mkristo yenye lengo la kufanya mabadiliko ya kiroho kwa ajili ya wokovu wa roho yake.

Kwa namna ya pekee Wakristo wengi hufanya hija hii maalum katika kipindi cha Kwaresima. Kwaresima siyo tu kipindi cha kufunga chakula bali pia ni kipindi maalum cha kusali na kutafakari kwa kina safari ya maisha ya kiroho. Ni kipindi cha kujichunguza bila kujihurumia na kujitathimini bila unafiki na kufanya maamuzi ya kweli ya kubadilika na kuanza upya safari ya kiroho katika kipindi cha Kwaresima.

Lengo la mwanadamu kuumbwa kwa sura na mfano wa Mungu ni kwamba amjue Mungu, ampende, amtumikie na hatimaye aweze kuumfikia Mungu na kukaa naye katika heri ya milele mbinguni mara safari yake ya kuishi duniani inapofikia tamati. Kweli ni raha sana siku moja kufika mbinguni katika heri ya milele lakini ni safari yenye kila aina ya changamoto kabla ya kufikia tamati.

Pamoja na binadamu kuumbwa kwa sura na mfano wa Mungu bado amekuwa kiumbe dhaifu sana, hivyo ni lazima kweli kupambana katika safari ya kumwelekea Baba. Mama Kanisa kwa kuzingatia udhaifu huo wa mwanadamu amekuwa mwalimu wa huruma ya Mungu na kuamua kutenga kipindi maalum kwa ajili ya kumsaidia Mkristo kujitafiti ili kufanya mabadiliko chanya kwa pale anapokuwa amepoteza uaminifu na kipindi hicho ni cha hija ya kiroho.

Kumbe kipindi cha Kwaresima ni kipindi cha kumsaidia mwanadamu kutembea siku zote katika njia ya unyofu kwa sababu hakuna ajuaye siku wala saa ya kufa kwake, kwani baada ya kifo atahukumiwa kwa kadiri ya alivyotumia akili yake kuwaza, utashi wake kuamua na uhuru wake kutenda.

Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Hija ya kiroho kama historia yake, matokeo au athari zake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.