Mauti (kutoka Kiarabu موت, maut) au kifo (kutoka kitenzi cha Kibantu kufa) ni mwisho wa uhai wa kiumbe; kwa lugha ya biolojia mwisho wa michakato yote ndani ya kiumbehai ambayo ni dalili za uhai, hivyo mwili hupoteza uwezo wa kufanya kazi za kiasili kama vile kupumua, kudunda kwa mapigo ya moyo, na mzunguko wa damu. Mauti inaweza kutokea kwa sababu mbalimbali, ikiwemo magonjwa, ajali, au hali ya kimaumbile kama umri mkubwa.

Fuvu la kichwa, ishara maarufu ya kifo.
Mauti ikishughulikia maua yake, katika Kuoleman puutarha, kazi ya Hugo Simberg (1906).
Idadi ya vifo kati ya watu milioni moja mwaka 2012
     1054-4,598     4,599-5,516     5,517-6,289     6,290-6,835     6,836-7,916     7,917-8,728     8,729-9,404     9,405-10,433     10,434-12,233     12,234-17,141

Chanzo

Mauti hutokea kutokana na sababu mbalimbali kama vile

  • umri mkubwa unaosababisha michakato ya kimsingi mwilini kusimama polepole
  • muda mrefu wa maisha unaoruhusu makosa na kasoro kujumuika na kusababisha madhara (mfano: kansa)
  • magonjwa yanayovuruga michakato ya uhai hadi kuisimamisha
  • ajali zinazoharibu viungo muhimu mwilini
  • ukosefu wa chakula, maji, hewa au kinga dhidi ya mazingira magumu
  • athari haribifu kutoka viumbe wengine (k.m. kushambuliwa) au kutoka mazingira

Hakikisho

Kwa binadamu kutokea kwa kifo mara nyingi hakutokei mara moja; katika mazingira ya kawaida kifo kinaonekana kama moyo hausikiki tena na mapafu hayakupumua kwa dakika kadhaa.

Hata hivyo kuna uwezekano wa kwamba kazi ya moyo na mapafu ni hafifu kiasi kwamba haitambuliki. Penye hospitali nzuri na mitambo ya kiganga mara nyingi mtu anarudi kuishi ingawa mahali pengine ametazamwa ameshaaga dunia. Kama mashine zinaendelea kuchukua kazi ya moyo na mapafu si rahisi kujua kifo kinatokea lini.

Wataalamu wengi siku hizi wanapoona michakato ya kawaida ya ubongo imekwisha kwa muda fulani, wanasema kifo kimetokea. Hata hivyo kuna kesi za watu wanaozinduka baada ya muda huo.

Mauti na utamaduni

Katika utamaduni na imani za watu mauti ni jambo muhimu. Lugha ina njia nyingi za kuitaja kwa mfano kuaga dunia, kufariki dunia n.k.

Katika dini na falsafa kuna misimamo mbalimbali kuhusu mauti kama vile

  1. Mauti ni mwisho wa binadamu kimwili na kiroho; hakuna kinachobaki baada ya kifo
  2. Mauti ni hatua tu katika mzunguko wa maisha; nafsi au roho inarudi katika maumbile mengine
  3. Kifo ni kupita penginepo: uzima wa milele, mbinguni, upeo wa wafu n.k.

Katika Ukristo

Hasa kadiri ya Ukristo, ni muhimu tujiandae kufa wakati wowote na namna yoyote kwa kuishi kitakatifu sasa na kwa kujiombea neema tutakazohitaji saa ya kufa kwetu, tukijua tumewekewa “kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu” (Eb 9:27). “Katika mambo yako yote uukumbuke mwisho wako, hivyo hutakosa kamwe hata hatima” (YbS 7:36). “Hamjui yatakayokuwako kesho! Uzima wenu ni nini? Maana ninyi ni mvuke uonekanao kwa kitambo, kisha hutoweka” (Yak 4:14). “Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni” (Math 26:41).

“Ina thamani machoni pa Bwana mauti ya wacha Mungu wake” (Zab 116:15). Hasa utiifu wa Yesu msalabani umegeuza laana ya kifo iwe baraka kwa waamini wake. “Heri wafu wafao katika Bwana tangu sasa. Naam, asema Roho, wapate kupumzika baada ya taabu zao; kwa kuwa matendo yao yafuatana nao” (Ufu 14:13).

Tutakapofariki dunia roho yetu isiyokufa, mbali na mwili unaooza, itapewa tuzo au adhabu tuliyostahili kwa maisha yetu. “Ikawa yule maskini alikufa, akachukuliwa na malaika mpaka kifuani kwa Ibrahimu. Yule tajiri naye akafa, akazikwa. Basi, kule kuzimu aliyainua macho yake, alipokuwa katika mateso, akamwona Ibrahimu kwa mbali, na Lazaro kifuani mwake” (Lk 16:22-23). “Kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida… ninatamani kwenda zangu nikae na Kristo, maana ni vizuri zaidi sana” (Fil 1:21,23). “Nasi tunaona ni afadhali kutokuwamo katika mwili na kukaa pamoja na Bwana” (2Kor 5:8). Kwa kuwa kifo ni “mavumbi kuirudia nchi kama yalivyokuwa, nayo roho kumrudia Mungu aliyeitoa” (Mhu 12:7). Siku ya ufufuo roho na mwili vitaungana tena kwa ajili ya uzima au moto wa milele. “Pumzi iliwaingia, wakaishi, wakasimama kwa miguu yao, jeshi kubwa mno” (Ez 37:10).