Historia ya Gambia

Historia ya Gambia inahusu eneo la Afrika Magharibi ambalo wakazi wake leo wanaunda Jamhuri ya Gambia.

Eneo la Gambia lilikuwa sehemu ya Dola la Mali na Dola la Songhai.

Nchi kama ilivyo leo imepatikana kutokana na mvutano kati ya Uingereza na Ufaransa wakati wa ukoloni.

Mwanzoni Uingereza ulitafuta tu njia ya maji kwa ajili ya biashara, bila kujali utawala wa nchi.

Mapatano kati ya Ufaransa na Uingereza baada ya vita vya Napoleon Bonaparte yaliimarisha hali hiyo. Wafaransa walichukua eneo lote kubwa la Senegal, na Waingereza ile kanda ndogo ndani ya Senegal.

Tangu uhuru wa nchi zote mbili palikuwa na mpango wa kuziunganisha kwa njia ya shirikisho lililoanzishwa mwaka 1982 lakini Gambia ilitoka katika mapatano hayo mwaka 1989.

Hadi 1994 Gambia ilifuata mfumo wa demokrasia ya vyama vingi lakini mwaka ule uasi wa wanajeshi ulipindua serikali na kuwa chanzo cha utawala wa Yahya Jammeh aliyekuwa kiongozi, kwanza kama mwenyekiti wa kamati ya kijeshi, baadaye kama rais aliyechaguliwa mwaka 1996 na tena miaka 2001, 2006 na 2011. Isipokuwa mwaka 2001 wapinzani na watazamaji wa nje walilalamika ya kwamba kura hizi hazikuwa huru.

Mwaka 2013 Jammeh alitoa Gambia katika Jumuiya ya Madola kama chombo cha ukoloni mamboleo.

Mwaka 2015 Jammeh alitangaza Gambia kuwa nchi ya Kiislamu na mwaka uliofuata alitangaza Kiarabu kuwa lugha rasmi badala ya Kiingereza.

Katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2016 vyama vya upinzani viliungana, na mgombea wao Adama Barrow alishinda. Awali Jammeh alikubali kushindwa, lakini baada ya siku nane alitangaza ya kwamba alitaka kubatilisha matokeo na kuwa na uchaguzi mpya.[1]

Wananchi walianza kukimbilia nchini Senegal.

Tarehe 19 Januari 2017, rais mteule aliapishwa katika ubalozi wa Gambia huko Dakar, halafu wanajeshi wa Senegal, Nigeria na Ghana walivamia nchi ili kumuondoa madarakani kwa idhini ya Umoja wa Mataifa.

Tarehe 21 Januari Jammeh alikubali kuachia.

Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Historia ya Gambia kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
  1. Gambia: troops deployed to streets as president rejects election defeat theguardian.com 10-12-2016, imeangaliwa 10-12-2016