Waishaak

(Elekezwa kutoka Isaaq)

Waishaak (pia Isaaq, Isaac) (kwa Kisomali: Reer Sheekh Isaxaaq, kwa Kiarabu: بني إسحاق bani isḥaq) ni moja ya makabila makubwa kati ya Wasomali.[1]

Waishaak (Ishaaq)
ال إسحاق
Maeneo penye idadi kubwa kiasi
Bendera ya Somaliland Somaliland

Bendera ya Yemen Yemen

Bendera ya Jibuti Djibouti

Bendera ya Kenya Kenya

Lugha

Kisomali,Kiarabu

Dini

Uislamu (Wasunni)

Makundi yaliyo karibu kiukoo au kiutamaduni

Dir, Darod, Hawiye, Rahanweyn,Wasomali wengine

Wanakalia hasa maeneo ya Somaliland kaskazini mwa Somalia na ya Jimbo la Somali nchini Ethiopia.

Picha ya Abdillahi Deria, Sultani Mkuu wa 4 wa Usultani wa Waishaak.
Wapiganaji Waishaak wakiwa wamepanda farasi

Kulingana na mapokeo ya jadi ya Wasomali, ukoo wa Waishaak ulianzishwa katika karne ya 13 au 14 wakati alipowasili Ishaaq Bin Ahmed Bin Mohammed Al Hashimi (Sheikh Ishaaq) kutoka Uarabuni aliyezaliwa katika uzao wa Ali ibn Abu Talib.[2] [3] Alikaa katika mji wa pwani wa Maydh kaskazini mashariki mwa Somaliland, ambapo alioa mke kutoka ukoo wa Magaadle. [4]

Kaburi la Sheikh Ishaaq liko Maydh, na ndilo eneo wanapofika mahujaji mara kwa mara. [5] Maulid (siku ya kuzaliwa) ya Sheikh Ishaaq pia huadhimishwa kila Alhamisi kwa kusoma manaaqib yake (mkusanyiko wa matendo matukufu). [4]

Waishaak ndio kabila au ukoo mkubwa wa Wasomali huko Somaliland. Miji mikubwa mitano ya Somaliland - Hargeisa, Burao, Berbera, Erigavo na Gabiley - yote hukaliwa na Waishaak hasa.[6] Vivyo hivyo mikoa mbalimbali ya Somaliland huwa na Waishaak wengi kati ya wakazi yake.[7]

Uchoraji wa mwanamke Mishaak uliochapishwa katika Bilder-Atlas mnamo 1870

Historia

hariri

Waishaak walishiriki katika vita vya Usultani wa Adal. Baadaye wakati wa karne ya 18 Sultani Guled Abdi alianzisha Usultani wa Waishaak uliodumu kuanzia mwaka 1750 hadi 1884.

Baadaye Waishaak walio wengi waliishi chini ya usimamizi wa Uingereza katika Somalia ya Kiingereza na chini ya utawala wa Ethiopia katika maeneo ya Ogaden.

Wakati wa uhuru mwaka 1960 Somalia ya Kiingereza iliamua kuungana na Somalia ya Kiitalia. Waishaak walishiriki katika harakati ya kuunda Somalia Kubwa iliyolenga kuunganisha pia Wasomali katika Kenya na Ethiopia na nchi ya Somalia.

Wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe ya Somalia Waishaak wengi waliuawa na jeshi la dikteta Siad Barre.

Baada ya kuporomoka kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Somalia mnamo 1991, maeneo ya Somaliland yaliyokaliwa na Waishaak hasa yalitangaza uhuru wao kama taifa la pekee. [8]

Marejeo

hariri
  1. Lewis, I. M. (1994). Blood and Bone: The Call of Kinship in Somali Society. The Red Sea Press. uk. 102. ISBN 9780932415936. isaaq noble.
  2. Rima Berns McGown, Muslims in the diaspora, (University of Toronto Press: 1999), pp. 27–28
  3. I.M. Lewis, A Modern History of the Somali, fourth edition (Oxford: James Currey, 2002), p. 22
  4. 4.0 4.1 I.M. Lewis, A Modern History of the Somali, fourth edition (Oxford: James Currey, 2002), pp. 31 & 42
  5. Roland Anthony Oliver, J. D. Fage, Journal of African history, Volume 3 (Cambridge University Press.: 1962), p.45
  6. Somaliland: With Addis Ababa & Eastern Ethiopia By Philip Briggs. Google Books.
  7. "EASO Country of Origin Information Report" (PDF). Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo 15 Juni 2016. Iliwekwa mnamo 2020-01-27.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  8. "History". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 20 Agosti 2017. Iliwekwa mnamo 2017-10-26.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)