Chuo
Chuo ni taasisi ya elimu ya pekee. Inatoa mafunzo ya kazi fulani. Mifano ni chuo cha ufundi, chuo cha kilimo au chuo cha ualimu. Kwa kila namna chuo kinaanza kufundisha watu baada ya kumaliza ngazi fulani ya shule.
Asili na maana ya neno "chuo"
haririKiasili maana ya neno "chuo" ilikuwa sawa na "kitabu". Kwa maana hiyo linatumiwa kwa mfano katika tafsiri za Biblia kama vile Injili ya Luka 4:17 "Yesu akapewa chuo cha nabii Isaya, akakifungua chuo".[1]
Kutokana na maana hii asilia "chuo" kimekuwa pia neno la kutaja mahali pa kujifunza kusoma, kwa hiyo katika Kiswahili cha miaka iliyopita kiliweza kutaja pia shule.[2].
Leo hii matumizi ya neno yamebadilika, kwa maana ya "kitabu" hupatikana tu katika matini zenye Kiswahili cha zamani na kama mahali au taasisi ya elimu kwa jumla, neno "shule, skuli"[3] limechukua nafasi pana zaidi.
Viwango vya vyuo
haririJina la "Chuo" linaweza kutaja taasisi zinazotoa elimu kwa ngazi tofauti sana. Hii itategemea na muundo wa elimu katika nchi mbalimbali.
- Chuo cha ufundi stadi, kwa mfano useremala, mara nyingi kitafundisha wanafunzi waliotoka shule ya msingi na kuwafundisha ufundi fulani kama useremala, yaani matumizi ya vifaa vya fani hii na kuwawezesha kutengeneza fenicha au kushughulikia kazi zinazohusu matumizi ya ubao katika ujenzi.[4]
- Chuo cha uganga kinapokea watu waliomaliza shule ya sekondari na kuwapa elimu wa kuwa msaidizi wa mwuguzi au daktari aliyesoma tiba kwenye chuo kikuu ("medical assistant").
- Vyuo vingine vinaweza kuwapeleka wanafunzi wao hadi ngazi ya diploma au hata bachelor.
- Katika nchi kadhaa chuo kinatoa elimu ya juu lakini katika fani moja tu, tofauti na chuo kikuu kinachofundisha fani mbalimbali na pia kuweka uzito kwenye uchunguzi wa kitaalamu, si mafundisho pekee.
Wanafunzi na walimu
haririWatu wanaoingia katika chuo kwa shabaha ya kujifunza huitwa wanafunzi, pia wanachuo au wanazuo(ni). Wale wanaotoa elimu huitwa walimu, kwenye ngazi za juu zaidi wanaweza kuitwa pia profesa au wakufunzi.
Vyuo nchini Tanzania
haririNchini Tanzania vyuo huratibiwa na tume ya vyuo vikuu nchini humo inayoitwa TCU (Tanzania commission for university).[5] Tume ya vyuo vikuu Tanzania imeonyesha orodha ya vyuo nchini Tanzania kwamba mpaka mnamo waka 2019 Tanzania ilikua tayari na vyuo zaidi ya hamsini (50), Orodha ya vyuo vilivo idhinishwa ta tume ya vyuo vikuu nchini Tanzania (bofya hapa) Ilihifadhiwa 5 Desemba 2020 kwenye Wayback Machine..
Marejeo
hariri- ↑ Hii ni toleo la "Union version" (1952) linalofuata hapa tafsiri ya Edward Steere ya 1883; tafsiri za kisasa hutumia hapa "kitabu" badala ya "chuo". Tafsiri ya "Qurani Tukufu Ilihifadhiwa 13 Novemba 2017 kwenye Wayback Machine." ya Sheikh Ali Muhsin Al Barwani inatumia kote neno "kitabu", si "chuo".
- ↑ A. C. Madan Swahili-English Dictionary Oxford 1903: "Chuo, n. {vy-), (i) book; (2) school" (online hapa)
- ↑ "Shule" kutoka Kijerumani Schule, "skuli" kutoka Kiingereza school
- ↑ Kwa jumla linganisha tovuti ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) http://www.veta.go.tz/index.php/sw Ilihifadhiwa 13 Machi 2017 kwenye Wayback Machine.
- ↑ https://www.tcu.go.tz