Mjusi (kundinyota)

(Elekezwa kutoka Lacerta)

Mjusi (kwa Kilatini na Kiingereza Lacerta) [1] ni jina la kundinyota ndogo kwenye nusutufe ya kaskazini ya Dunia.

Nyota za kundinyota Mjusi (Lacerta ) katika sehemu yao ya angani
Mjusi (Lacerta sive Stellio) kwenye atlasi ya nyota ya Hevelius ya mwaka 1690

Mahali pake

hariri

Mjusi linapakana na makundinyota ya [[Kifausi (kundinyota)|Kifausi] (Cepheus), Mke wa Kurusi (Cassiopeia), Mara (Andromeda), Farasi (Pegasus) na Dajaja (Cygnus).

Nyota angavu ya Dhanabu ya Dajaja (ing. Deneb) iko jirani.

Kundinyota hili halikujulikana kwa mabaharia Waswahili wa Kale wala kwa Waarabu au Wagiriki kwa sababu nyota zake ni hafifu sana. Katika enzi ya kale nyota hizi hazikupangwa kuwa sehemu ya kundinyota maalumu. Mjusi ni kati ya makundinyota yaliyoanzishwa na mwanaastronomia Johannes Hevelius wa Danzig (Gdansk) mnamo mwaka 1690 BK. Akiwa mpika pombe na mfanyabiashara tajiri aliyeshika kwa muda pia umeya wa mji wake alikuwa hasa maarufu kwa kuangalia, kupima na kuorodhesha nyota pamoja na mke wake Elisabeth Hevelius.

Hevelius aliyelenga kujaza mapengo kati ya kundinyota akiandika kwa Kilatini alichagua jina “Lacerta sive Stellio ” (Mjusi au Salamanda) lakini jina la pili halikutumiwa baadaye.

Lacerta - Mjusi lipo kati ya makundinyota 88 yanayoorodheshwa na Umoja wa kimataifa wa astronomia kwa jina la Lacerta. Kifupi chake rasmi kufuatana na Ukia ni 'Lac'.[2]

Mjusi –Lacerta ina nyota hafifu tu. Nyota angavu zaidi ni Alfa Lacertae ambayo ni nyota yenye mag 3.8 ikiwa na umbali wa miakanuru 102 kutoka Dunia.[3].

Beta Lacertae ina mag 4.4 ikiwa na umbali wa miakanuru 170 kutoka kwetu.

Tanbihi

hariri
  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya neno "Lacerta " katika lugha ya Kilatini ni "Lacertae" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Lacertae, nk.
  2. The constellations, tovuti ya Ukia, iliangaliwa Oktoba 2017
  3. Alpha Lacerta, tovuti ya Prof Jim Kaler wa Chuo Kikuu cha Illinois, iliangaliwa Oktoba 2017

Viungo vya Nje

hariri