Magonjwa ya kuku

(Elekezwa kutoka Magonjwa ya Kuku)

Magonjwa ya kuku ni maradhi yanayoathiri afya ya kuku na kusumbua wafugaji wengi wa kuku, hasa wafugaji wadogowadogo.

Ndui ya Kuku

Kuku, kama walivyo viumbehai wengine, hupatwa na magonjwa mbalimbali. Kwa kuwa kuku ni mifugo ya binadamu, hivyo ni jukumu la mfugaji kutatua tatizo linapotokea ambalo hujumuisha afya ya mfugo wake - kuku.

Makala hii inaelezea baadhi ya magonjwa ya kuku yanayowakabili wafugaji wengi na baadhi ya njia za kupunguza au kujilinda na magonjwa haya.

Mfugaji wa kuku hana budi ajitahidi kuyazuia magonjwa kuliko kuyaponya kwa kuwalisha kuku chakula bora na cha kutosha. Kama itawezekana chakula chao kichanganywe na dawa zinazotumika kwenye chakula.

Pia usafi wa nyumba ya kuku ni muhimu sana. Sehemu zinazozunguka nyumba pia zisafishwe. Vyombo vya maji, chakula na vitu vinginevyo lazima viwe safi.

Nyumba za kuku zisiruhusiwe wageni kuingia mara kwa mara kwa sababu wanaweza kuingiza magonjwa kutoka sehemu walizotoka. Panya na wadudu wengine wazuiwe kabisa kuingia ndani ya nyumba za kuku. Kwenye milango ya nyumba za kuku ziwekwe dawa za kuua wadudu wanaoeneza magonjwa.

Pamoja na kulinda usafi katika nyumba za kuku, kuna baadhi ya magonjwa ambayo ni ya hatari sana kwa sababu yanapoingia huua kuku wengi kwa mara moja. Baadhi ya magonjwa ni kama ifuatavyo.

Mharo Mweupe (Pullorum au Bacillary White Diarrhoea)

hariri

Dalili za ugonjwa huu ni kama ifuatavyo:

  • Toka siku tatu hadi majuma mbili baada ya kupata vijidudu vya ugonjwa, vifaranga huharisha kinyesi cheupe na vingi hufa.
  • Kuku wakubwa wanaotaga, hupunguza kutaga mayai ghafla na baadhi yao hufa ghafla.

Mpaka sasa hakuna matibabu ambayo yanafahamika yanayoweza kutibu ugonjwa huu. Kitu ambacho mfugaji anawezaa kufanya ni kuchoma moto kuku wote wanaougua, na kusafisha nyumba nzima kwa dawa. Mfugaji amjulishe haraka bwana mganga wa wanyama aliye karibu naye.

Njia nzuri ya kuzuia magonjwa, kwa mfugaji kununua vifaranga kutoka vituo vyenye sifa nzuri ya kutokuwa na ugonjwa huu, hasa vituo ambavyo hupitisha uchunguzi wa mara kwa mara kutafuta kama ugonjwa huu upo kwenye kutuo chao. Kituo hicho cha kuangua vifaranga lazima kiwe kinatumia dawa za kusafisha mashine za kuangua vifaranga.

Mharo Mwekundu (Coccidiosis au Red Diarrhoea)

hariri

Kuku walioathiwa na ugonjwa huu huonyesha dalili zifuatazo. Kati ya majuma manne hadi kumi hivi, baada ya kuambukizwa kuku huharisha damu, Kuku ambao wameshikwa sana na ugonjwa huu, huonekana wemedhoofika sana na huwa kama wemavaa koti, na shingo yao huinama chini.

Kuku hao hawashughuliki kutafuta chakula wala maji, na husinzia mara kwa mara kwenye pembe za nyumba. Vifo hutokea vingi kila siku. Kuku wakubwa ambao hawakufa hukuwa taratibu sana. Utagaji wa mayai hucheleweshwa au hupunguzwa. Wakati mwingine kinyesi cha kuku hao huwa na rangi ya kahawia baadaye kuwa na damu.

Ugonjwa huu hupona haraka kama matibabu yaanza mapema. Mfugaji amwone haraka bwana mganga wa wanyama aliye karibu naye, ili amshauri dawa ambazo zinatumika, kwa sehemu mbalimbali. Uzingatiaji wa masharti ya dawa ni jambo muhimu sana. Kuushinda ugonjwa huu kunategemea usafi wa mfugaji. Mfugaji inampasa ahakikishe kuwa haruhusu unyevunyevu kwenye takataka zinazowekwa ndani ya chumba kwa kulalia kuku, hasa kwenye nyumba ya kulelea vifaranga sehemu ambazo humwagwa sana maji ovyo kuzunguka vyombo vya maji. Sehemu hizi ni lazima zitupiwe macho mara kwa mara. Ikiwezekana vyombo vya maji na chakula viwekwe kwenye chakula au maji.

Vifaranga wasisongamane sana kwenye chumba kidogo. Chakula cha vifaranga kitiwe dawa ya kuzuia ugojwa huu, na hii ndio njia iliyo bora zaidi na yenye uhakika katika kuzuia ugonjwa huu. Dawa huleta matokeo mazuri sana iwapo itaambatana na usafi.

Magonjwa ya Kupumua (Respiratory Diseases)

hariri

Haya ni magonjwa ya kooni, nayo hutokana sana katika kuku waliosongamana, na kwenye nyumba zilizojengwa vibaya. Sehemu za joto kama Tanzania magonjwa haya ya kooni yanaweza kuzuiliwa kwa urahisi kwa kujenga nyumba zenye kupitisha hewa ya kutosha, kwa sababu hakuna hofu ya baridi kali. Kuku wadogo wanaweza kuugua ugonjwa huu kama kuna upepo mkali. Kwa hiyo nyumba za kulelea vifaranga ziwekewe pazia la gunia, au vitamba au makaratasi. Vumbi lipanguswe mara kwa mara kwenye kuta za nyumba za kuku.

Ndui ya Kuku (Fowl Pox)

hariri

Hii ni ndui ya kuku. Kuku huonekana na vipele vya rangi ya kijivujivu, kwenye ngozi yake, hasa kwenye upanga wa kichwa. Baada ya muda mfupi vipele hivi huwa vikubwa na kukutana na kufanya majeraha mabichi na yenye kutoa damu. Baada ya siku kumi hadi kumi na nne hivi, majeraha haya hukauka na kufanya makovu meusi. Kuku wanaougua wanaweza kutibiwa lakini mfugaji inampasa atoe taarifa haraka kwa bwana maganga wa wanyama aliye karibu naye ili ampatie dawa zinazofaa. Kuku wanaougua watengwe haraka wanapoonekana ili wasiambukize wazima. Usafi ni muhimu katika kuzuia ugonjwa huu usitokee. Kuku wapewe nafasi ya kutosha na wasisongamane. Ugonjwa huu unaweza kuzuiwa kabisa kwa kuchanja dawa kuku wote mapema.

Sotoka au Ndigana (Newcastle Disease)

hariri

Kuku walioshikwa na ugonjwa huu huwa wazembe na hutokwa na hamu ya chakula. Shingo ya kuku hulegea na manyoya hukunjamana. Upanga na ndevu hugeuka na kuwa na rangi ya bluu. Koo la chakula huwa kubwa na hutoa mate yanayotoa harufu mbaya. Kuku huyu hulemewa kuvuta pumzi, na huharisha kinyesi chenye rangi ya kijani. Kichwa cha kuku huinamia nyuma au mbele au pembeni. Kuku wengi, hasa wachanga hufa. Ugonjwa huu haujapata dawa maalum ya kutibu. Mfugaji awatenge kuku haraka na amwarifu mganga wa wanyama aliye karibu naye. Usafi wa nyumba na uwanja wa kuku ni jambo muhimu sana katika uzuiaji wa ugonjwa huu. Kuku wachanjwe dawa mapema. Kuku ambao wamepata ugonjwa huu wachomwe moto au wazikwe kwenye shimo lenye kina kirefu kwenda chini.

Kipindupindu cha Kuku (Fowl Cholera)

hariri

Ugonjwa huu unapomjia kuku kwa nguvu, hufa ghafla. Unapomjia taratibu kuku husinzia na manyoya yake huvurugika. Shingo huinamia nyuma. Upanga na ndevu hupanuka. Kuku huishiwa hamu ya kula chakula, na kuharisha kinyesi cheupe. Baadhi ya kuku huvuta pumzi kwa shida na kutoa sauti ya mkwaruzo. Mfugaji amwarifu bwana mganga wa wanyama aliye karibu naye, na atamshauri dawa za kutumia. Usafi wa nyumba na uwanya wa kuku ndiyo msingi wa kuzuia ugonjwa huu. Kuku walioshikwa na ugonjwa huu watengwe haraka na baadaye wachomwe moto. Kuku wachanjwe dawa mapema kwenye sehemu ambazo ugonjwa huu hutokea mara kwa mara.

Homa ya Matumbo ya Kuku (Fowl Typhoid)

hariri

Kuku anapojiwa na ugonjwa huu kwa nguvu sana upanga na ndevu zake hukunjamana. Kuku hufa ghafla japokuwa huonekana bado ana afya sana. Ikiwa ugonjwa unamjia kwa taratibu hadi ukakomaa, upanga na ndevu hufifia na kunyauka. Kuku huhara kinyesi cha rangi ya manjano. Hamu ya chakula humtoka, isipokuwa hunywa maji mengi, na kuku huyo huonekana ana wasiwasi sana. Kuna dawa nyingi ambazo zinaweza kusaidia kuponya baadhi ya kuku wakati ugonjwa huu unapoingia. Dawa hizi mara nyingi hutengenezwa ili zitumiwe kwenye chakula au maji. Mfugaji amwone bwana mganga wa wanyama aliye karibu naye ili amshauri dawa ya kutumia. Nyumba za kuku ziwekwe kwenye hali ya usafi, na uwanja usafishwe pia. Vyombo vya maji na chakula visafishwe kwa dawa. Kuku wanaougua wote wachomwe moto. Kuku wazima wachanjwe dawa mapema na ikiwezekana wachunguzwe kila mmoja kuona kama wapo wenye ugonjwa huo.

Wadudu wanaokaa kwenye manyoya

hariri

Mfugaji inampasa awachunguze kuku wake mara kwa mara, ili ahakikishe kuwa kuku wake hawana viroboto, chawa, papasi au wadudu wengine ambao ni wadogo sana hata ni vigumu kuwaona kwa urahisi kwa macho. Wadudu hawa huwasumbua kuku na kuwapunguzia uwezo wao wa kutoa mazao mengi ya mayai au nyama. Ni jambo la busara kutumia dawa za wadudu ambazo hutengenezwa katika hali ya unga. Dawa hizi hutumika kwa kuwapaka kuku au kumwagia sakafu, au kwenye masanduku ya kutagia, au kwenye ngazi za kupumzika kuku. Mfugaji amwone maganga wa wanyama aliye karibu naye ili amshauri dawa zinazofaa kwa sehemu yake. Kuna baadhi ya wadudu wa kuku ambao wanakaa kwenye miguu ya kuku na kufanya magamba miguuni. Mfugaji anaweza kutumia mafuta ya taa kwa kupaka miguu mpaka atakapoona kuwa wadudu wote wametoweka.

Wadudu wa tumboni

hariri

Kuku hushambuliwa na aina nyingi za minyoo ambayo huishi tumboni na kuwanyonya damu au chakula na kuwadhoofisha, au kuwauwa kabisa. Njia iliyo bora ya kuzuia minyoo hii ni usafi wa nyumba na uwanja wa kuku. Hali ya kuambukiza ya minyoo ikizidi, mfugaji amwarifu bwana mganga wa wanyama aliye karibu naye, ili amshauri dawa za kutumia.

Kudonoana manyoya, vidole, kulana wenyewe kwa wenyewe na kula mayai

hariri

Tabia hizi mbaya za kuku hutokana na sababu nyingi mbalimbali. Sabubu mojawapo ni upungufu wa nafasi ambayo hufanya kuku wasongamane sana. Kwa hiyo kuku wapewe nafasi ya kutosha ya chakula maji na ya kupumzika. Kuku wanaweza kuanzisha tabia hizi ikiwa chakula chao hakina aina zote za chakula hasa nyama au chumvi au vitamini. Kwa hiyo njia mojawapo ya kuepukana na tabia hizi mbaya ni kuwapa kuku chakula bora. Wakati mwingine kuku hushawishiwa kula mayai kutokana ukosefu wa kuondoa mayai kwenye nyumba ya kutagia, mara kwa mara. Kwa hiyo mayai ni lazima yaondolewe kwenye nyumba za kutagia mara tatu au zaidi kwa siku.

Uchovu wa kukaa mahali pamoja unaweza kuwafanya kuku waanze baadhi ya tabia hizi mbaya. Wafugaji wengi wenye busara huwazuia kuku wasianze tabia hizi kwa kuwapatia majani mabichi ambayo huwafanya wawe na mchezo wa kupoteza na kusahau kudonoana. Majani hayo hutundikwa kwa kamba. Njia nyingine ambazo hutumika kwa kuzuia tabia hizi mbaya za kuku ni kuwakata midomo kwa kutumia kisu kilichopashwa moto, au chuma cha moto wanachotumia mafundi kuungia. Ubora wa chombo kilichopashwa moto ni kwamba mdomo wa kuku hukatwa na kuzuia damu isitoke. Kwa hiyo jeraha hupona haraka. Kuku wakubwa na wadogo wanaweza kutumia vyombo hivi, lakini mfugaji inambidi kukata kuku midomo kati ya majuma matatu hadi tano. Mdomo unaokatwa ni wa juu, na ukatwe kuanzia robo hadi nusu ya mdomo. Majogoo ya kupandisha yasikatwe kwa sababu yatashindwa kupanda.

Tazama pia

hariri

Marejeo

hariri
  1. Kirumbi, D.M. (1980) Ufugaji wa Kuku (Dar es Salaam: Tanzania Publishing House)
  2. Kuendeleza Ufugaji wa Kuku Ilihifadhiwa 15 Desemba 2007 kwenye Wayback Machine.

Viungo vya nje

hariri