Chamko la volkeno

(Elekezwa kutoka Mlipuko wa volkeno)

Chamko la volkeno hutokea kama lava (zaha) na gesi kutoka vilindi vya ganda la Dunia zinatoka nje ya ardhi. Kutegemeana na tabia ya magma (mwamba wa joto katika hali ya kiowevu) na mazingira chamko hilo linaweza kuwa kama mlipuko au kama kumwaga kwa lava ya moto inayosambaa kwa utaratibu zaidi.

Mlipuko wa Ol Doinyo Lengai, mkoani Arusha, mwaka 1966.
Mlipuko wa Mount St. Helens (Marekani) mwaka 1980.

Volkeno hupatikana hasa pale ambapo vipande vya ganda la dunia vinaachana au kusukumana. Kuna pengo ambako magma joto kutoka ndani ya dunia inapanda juu kufika usoni mwake. Volkeno hutokea pia juu ya sehemu ya joto (hotspot) inayopanda juu kutoka kiini cha Dunia kupitia koti la Dunia.

Pale ambapo lava inatoka ardhini inapoa na kuganda; hivyo inajenga ukuta kuviringisha shimo linapotoka; kwa njia hiyo kutoka kwa lava inaweza kujenga milima inayokua na kuwa mirefu yenye njia ya lava ndani yake.

Volkeno nyingi hutoa zaha yake mara kwa mara. Hii inawezekana kama njia ya kasoko yake ni wazi. Aina hiyo ya volkeno inaweza kuachana na nguvu yake mara kwa mara. Haielekei kuwa na mlipuko mkali sana isipokuwa kama maji yameingia katika chumba cha magma (soma chini).

Kama volkeno imelala kwa muda mrefu njia ya kasoko yake inafungwa kwa sababu zaha ndani yake imeganda kuwa mwamba imara. Ikitokea ya kwamba joto la chini linaongezeka tena magma inaanza kupanda juu lakini haiwezi kutoka nje. Inakwama chini ya volkeno na shindikizo ndani yake linaongezeka. Kama shindikizo linazidi husababisha mlipuko na kutoka ghafla kwa lava (zaha) na gesi nyingi mara moja. Ukali unaongezeka kama maji ya chini ya ardhi yanaingia katika chumba cha magma chini ya volkeno.

Milipuko mikubwa ya aina hiyo iliwahi kurusha mlima wote hewani kwa mfano mlima wa Krakatau mwaka 1883 BK. Mlima wenye urefu wa mita 813 juu ya UB ulipotea kabisa pamoja na kisiwa chake.

Ukitokea baharini mlipuko unaweza kusababisha mawimbi makubwa ya tsunami yanayofyeka mwambao.

Hatari nyingine ya milipuko ni kiasi kikubwa cha gesi na majivu pamoja na tefra, yaani mawe na miamba ya moto. Gesi na majivu yenye halijoto hadi 800 °C zinaweza kusambaa haraka sana zikiteketeza kila kitu njiani. Pia gesi zinazotoka zinaweza kuwa za sumu. Wakati wa mlipuko wa Vesuvio watu wengi wa Pompei waliuawa na gesi pamoja na majivu.

Milipuko inaweza kutokea sambamba na tetemeko la ardhi.