Volkeno (pia: volkano au volikano) ni mahali ambako zaha inatoka nje ya uso wa ardhi. Mara nyingi - lakini si kila mahali - volkeno imekuwa mlima. Volkeno huwa na kasoko yaani shimo ambako zaha na gesi zinatoka nje.

Volkeno hai.

Asili ya jina

hariri

Asili ya jina ni mungu wa dini ya Roma ya Kale aliyeitwa "Vulcanus". Kati ya miungu ya Kiroma alihusika na moto, radi na uhunzi; kwa hiyo aliheshimiwa hasa na wote waliotumia moto kwa kuyeyusha metali kama chuma au shaba.

Volkeno na ganda la dunia

hariri

Volkeno ni dalili ya kwamba mahali pake ganda la dunia si nene sana, hivyo joto la ndani linapata njia ya kutoka nje. Volkeno huanza katika tambarare. Zaha hutoka katika hali ya kiowevu; ikipoa haraka inaganda kuwa mwamba na hujenga mlima wa kuzunguka shimo la kasoko yake. Milima ya aina hiyo inaweza kukua sana. Mfano wa volkeno kubwa ni Kilimanjaro. Miamba yake yote ilijengwa na zaha iliyotoka ndani ya dunia.

Volkeno nyingi hutokea pale ambako mabamba ya ganda la dunia yanaachana au kusukumana. Hivyo volkeno hutokea hasa kwenye mistari ya kukutana kwa mabamba hayo.

Sababu nyingine ya kutokea kwa volkeno ni kuwepo kwa chumba cha magma ndani ya ganda la dunia.

Volkeno hai na volkeno bwete

hariri

Volkeno inaweza kupatikana kama volkeno hai inayoendelea kutema moto, gesi na majivu. Inaweza pia kuonekana kama volkeno bwete inayokaa kama milima mingine bila kuonyesha dalili za moto. Lakini kutokana na umbo na tabia za miamba yake inaonekana mlima huu ulijengwa kwa njia ya kivolkeno.

Volkeno bwete inaweza kuamka tena. Mara nyingi kuwepo kwa chemchemi za maji ya moto au kutokea kwa gesi kwenye sehemu fulani ni dalili ya kwamba bado kuna njia kati ya mlima na magma ya chini. Kipindi kati ya milipuko kinaweza kuwa cha miaka mingi.

Mlipuko wa volkeno

hariri

*Angalia makala kuu: Mlipuko wa volkeno

 
Wingu la mlipuko wa volkeno Raikoke kwenye visiwa vya Kurili jinsi lilivyoonekana kutoka satelaiti ya NASA tarehe 22 Juni 2019.

Mlipuko wa volkeno ni hatari kwa ajili ya wanadamu na mazingira. Mlipuko unaweza kurusha idadi kubwa ya gesi sumu na mawe ya moto hewani na kumwaga lava nje inayosambaa kama mto wa moto kwa umbali wa kilomita kadhaa.

Hiyo hatari ni kubwa zaidi pale ambako volkeno ililala kama volkeno bwete kwa miaka mingi, labda elfu kadhaa. Hapo mara nyingi watu wamevutwa na udongo wenye rutuba kutokana na majivu ya volkeno wajenge makazi na kulima. Kama hapo volkeni inageuka kuwa hai tena hatari ni kubwa. Kuna mifano ya vifo vingi vilivyosababishwa na volkeno. Hasara inategema kama miji iko karibu na volkeno au la, na kama serikali zina huduma za kutazama volkeno na kuonya watu watoke mapema wakati dalili za kwanza zinatokea.

Kati ya mifano ya milipuko mikali inayojulikana zaidi ni:

Katika karne ya 21 volkeno ya Nyiragongo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ililipuka mara mara mbili mwaka 2002 na mwaka 2021 na kusababisha vifo katia miji jirani ya Gisenyi na Goma.

Ol Doinyo Lengai ni volkeno ndogo iliyolipuka Tanzania kaskazini mwaka 2006.

Tazama pia

hariri
  Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Volkeno kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.