Mmumunyo au myeyusho[1] (kwa Kiingereza solution) ni tokeo la kuchanganya kabisa dutu mbili hadi kupata mchanganyiko wa aina moja usioonyesha sehemu zake. Mfano ni kukoroga sukari katika maji. Hapo sukari haionekani tena imechanganika kabisa na maji.

kukoroga sukari katika maji

Kwa lugha ya kemia sukari ni kimumunyika, maji ni kimumunyi (kiyeyushi[2]) na tokeo ni mchanganyiko wa aina moja au mmumunyo,

Mara nyingi kimumunyi ni kiowevu lakini kuna pia mifano mingine.

Gesi zinaweza kumumunyika katika kiowevu, kwa mfano oksijeni katika maji ambayo ni msingi wa uhai baharini au mtoni. Gesi inamumunyika pia katika gesi nyingine. Hewa kwa mfano ni mchanganyiko wa aina moja; oksijeni na gesi nyingine zimemumunyika katika nitrojeni.

Kiowevu kinaweza kumumunyika katika kiowevu kingine, lakini kuchanganya maji na mafuta hakuleti mchanganyiko wa aina moja, tokeo lake ni kiolei au emalshani (ing. emulsion).

Kuna pia mifano ya mmumunyo kama kimumunyi ni mango. Aloi zote ni mimumunyo ya metali mbili, kwa mfano bronzi ni mmumunyo wa stani iliyomumunika katika shaba. Mmumunyo wa aloi unatokea katika hali kiowevu wakati metali zote mbili zilipashwa moto na kuyeyuka.

Marejeo

hariri
  1. "Mmumunyo" ni chaguo la kitabu cha "Furahia Kemia - Enjoy Chemistry", Dar es Salaam 2011, pia cha KAST; "Myeyusho" ni chaguo la kwanza la KKK/ESD
  2. Kiyeyushi ni pendekezo la KAST