Mnyoo-kichocho

Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia
Nusuhimaya: Eumetazoa
(bila tabaka): Bilateria
(bila tabaka): Prostomia
Faila ya juu: Platyzoa
Faila: Platyhelminthes (Minyoo-bapa)
Ngeli: Rhabditophora
Nusungeli: Trepaxonemata
(bila tabaka): Neodermata
Oda: Trematoda
Nusuoda: Diplostomata
Familia ya juu: Schistosomatoidea
Familia: Schistosomatidae
Jenasi: Schistosoma
Weinland, 1858
Ngazi za chini

Spishi 6 za minyoo-kichocho:

Minyoo-kichocho ni spishi za minyoo vidusia za jenasi Schistosoma zinazosababisha ugonjwa wa kichocho kwa watu. Spishi zinaweza kugawanywa katika vikundi viwili kwa njia mbili tofauti. Njia ya kwanza ni mgawanyiko kulingana na ogani ambamo wapevu wanaishi, matumbo au kibofu. Njia ya pili ni kulingana na mahali pa mwiba kwenye mayai, kwa upande au kwenye ncha.

Spishi nyingine za Schistosoma huambukiza vertebrata wengine.

Minyoo wa familia Schistosomatidae hutofautiana na minyoo-bapa wengine kwa kuwa wana jinsia mbili tofauti ambazo zina ukubwa tofauti. Wana vidusiwa wawili, kidusiwa cha kati (konokono) na kidusiwa cha mwisho (vertebrata). Wanafika hatua ya upevu katika damu ya kidusiwa cha mwisho.

Spishi (ogani inayoambukizwa, mahali pa mwiba wa yai) hariri

  • Schistosoma guineensis (matumba, ncha)
  • Schistosoma haematobium, Mnyoo-kichocho wa kibofu (kibofu, ncha)
  • Schistosoma intercalatum (matumbo, ncha)
  • Schistosoma japonicum (matumbo, upande)
  • Schistosoma mansoni, Mnyoo-kichocho wa matumbo (matumbo, upande)
  • Schistosoma mekongi (matumbo, upande)

Mofolojia hariri

Minyoo-kichocho wapevu wana ulinganifu wa kimsingi wa pande mbili, vidonge vya kufyonza upande wa kinywa na wa tumbo, mwili uliofunikwa kwa ngozi ya seli zilizounganishwa, mfumo wa mmeng'enyo bila mkundu ulio na kinywa, umio na pochi yenye panda. Nafasi kati ya ngozi na mfereji wa chakula hujazwa na mtandao huru wa seli za mesodermi. Mfumo wa kinyesi na udhibiti wa osmosisi unategemea seli za viali. Minyoo wapevu huwa na urefu wa mm 10-20 na hutumia globini kutoka kwa hemoglobini ya vidusiwa vyao kwa mfumo wao wa mzunguko.

Uzazi hariri

Kinyume na Trematoda wengine minyoo-kichocho wana jinsia tofauti. Jinsia hizo mbili zinaonyesha kiwango kikubwa cha maumbo mawili tofauti ya kijinsia na dume ni mkubwa sana kuliko jike. Dume huzunguka jike na kumfunga ndani ya mfereji wake wa kubebea jike kwa maisha yote ya minyoo wapevu. Dume akijilisha kwa damu ya kidusiwa, anampitishia jike kidogo. Dume pia hupitisha kemikali ambazo hukamilisha ukuaji wa jike, na kisha watazaana kijinsia. Ingawa nadra pengine minyoo-kichocho walioungana "wataachana", maana jike atamwacha dume ili kuunga mwingine. Sababu halisi haieleweki, ingawa inafikiriwa kuwa majike watawaacha wenzao ili kuunga madume walio mbali zaidi kijenetiki. Utaratibu kama huo wa kibiolojia utasaidia kupungua uzaanamumo na unaweza kuchangia anuwai kubwa sana ya kijenetiki ya minyoo-kichocho.

Mzunguko wa maisha hariri

Minyoo wapevu huishi kwenye vena za matumbo au kibofu. Wanazalisha idadi kubwa ya mayai, ambayo huamili kupitia ukuta wa matumbo au kibofu kuingia uwazi. Kisha hutolewa pamoja na kinyesi au mkojo. Walakini mayai mengine yanaweza kubebwa na damu kwenda sehemu nyingine za mwili, ambapo wanaweza kuingia kwenye tishu nyingine na kuzingirwa. Hii inaweza kusababisha kila aina ya shida.

Mayai yakitomba ndani ya maji lava hutoa wanaoitwa mirasidio na waliofunikwa na silio na ambao hutafuta konokono wa maji ili kuwaambukiza. Konokono hao hutumika kama vidusiwa vya kati na spishi tofauti huwa na lava wa minyoo tofauti. K.m. konokono vidusiwa wa S. mansoni ni spishi za Biomphalaria na wale wa S. haematobium ni spishi za Bulinus. Lava huzaana bila ngono katika konokono kidusiwa wao hadi watoke kama aina tofauti ya lava inayoitwa serkari ambaye ana mkia wa kuogelea. Serkari hutafuta kidusiwa cha mwisho na wakipata mmoja hupenya ngozi yake wakipoteza mkia wao wakati wa mchakato huo.

Mara tu ndani ya mwili lava sasa huitwa skistosomula. Wanaingia kwenye mishipa ya damu na kusafiri kupitia moyo na ini hadi kwenye vena ya matumbo au kibofu, ambapo hukomaa. Skistosomula nyingi huuawa njiani na seli za kinga. Wapevu huepuka ]]mfumo wa kingamaradhi]] kwa kujifunika na antijeni za kidusiwa.

Picha hariri