Nyumba ya hekima (kwa Kiarabu بيت الحكمة bait-al-hikma) ilikuwa taasisi ya elimu ya juu mjini Baghdad (leo nchi ya Irak) wakati wa utawala wa makhalifa Waabbasi.

Wataalamu na wanafunzi wakikaa kwenye maktaba ya Baghdad

Baghdad iliundwa mwaka 762 kuwa mji mkuu wa khalifa yaani mtawala juu ya milki ya Waislamu baada ya Waabbasi kushinda vita vya wenyewe kwa wenyewe. Ikiwa kitovu cha milki kubwa iliyoenea kutoka Moroko hadi mipaka ya Uhindi na China, watu, habari na utaalamu wa maeneo mengi yalikutana kwenye ikulu ya khalifa.

Makhalifa kama Harun ar-Rashid na Al-Ma'mun walielewa umuhimu wa kutumia elimu ya mataifa yaliyovamiwa na kutawaliwa na Waislamu. Hapo maktaba ya Harun ar Rashid iliendelea kuwa taasisi ya utafiti na mafundisho iliyotimiza hasa kazi ya kutafsiri vitabu vya Kiajemi kwenda Kiarabu.

Harakati ya ufasiri iliendelea kuangalia pia elimu pana iliyopatikana kwa Kigiriki na Kisiria. Zamani iliaminiwa kwamba shughuli hizo zote ziliendeshwa katika nyumba ya hekima lakini uchunguzi wa kisasa umeonyesha hakuna ushuhuda wa kuthibitisha wazo hili[1]. Kuna taarifa kuwa mwanaastronomia Muhammad ibn Musa al-Khwarizmi aliajiriwa kwenye nyumba ya hekima lakini hakuhusika na kazi ya kutafsiri, kwa hiyo haikuwa maktaba tu lakini mahali pa utafiti na mafundisho[2].

Baghdad ilikuwa mahali muhimu pa utafsiri; Mkristo Hunayn ibn Ishaq alikuwa mfasiri mashuhuri wa vitabu vya Kigiriki na Kisiria kwenda Kiarabu lakini hakuna dalili kuwa alifanya kazi yake kwenye nyumba ya hekima[3].

Hata hivyo kazi ya kutafsiri rasmi vitabu visivyotungwa na Waislamu kutoka Kiajemi kwenda Kiarabu katika nyumba ya hekima inaaminiwa imefungua milango kwa kazi ya kutafsiri pia kutoka lugha nyingine. Ufasiri huu uliweka msingi wa maendeleo ya elimu na sayansi katika himaya ya Waislamu yaliyopita tamaduni nyingine za wakati wake.

Tanbihi hariri

  1. Bayt al-Hikmah, The Oxford Dictionary of Islam. Ed. John L. Esposito. Oxford Islamic Studies Online, iliangaliwa Mei 2019
  2. Gutas (1998), uk. 58
  3. Gutas (1998), uk. 59

Marejeo hariri

  • Dimitri Gutas: Greek Thought, Arabic Culture: The Graeco-Arabic Translation Movement in Baghdad and Early ʻAbbāsid Society (2nd-4th/8th-10th Centuries), Psychology Press 1998, ISBN 9780415061339, online hapa
  Makala hii kuhusu mambo ya elimu bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Nyumba ya hekima kama historia yake, uenezi au maendeleo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.