Moroko
Moroko (pia Maroko, kwa Kiarabu المغرب), au kirefu Ufalme wa Moroko (المملكة المغربية al-mamlaka al-maghribiya yaani "ufalme wa magharibi") ni nchi ya Afrika ya Kaskazini-Magharibi.
| |||||
Kaulimbiu ya taifa: الله، الوطن،الملك (Allāh, al Waţan, al Malik = Mungu, Taifa, Mfalme) | |||||
Wimbo wa taifa: Wimbo la Sharifa | |||||
Mji mkuu | Rabat | ||||
Mji mkubwa nchini | Casablanca | ||||
Lugha rasmi | Kiarabu | ||||
Serikali | Ufalme wa kikatiba Muhammad VI (محمد السادس, ⵎⵓⵃⵎⵎⴷ ⵡⵉⵙⵙ ⵚⴹⵉⵚ) Aziz Akhannouch (عزيز أخنوش, ⵄⴰⵣⵉⵣ ⴰⵅⵏⵓⵛ) | ||||
Uhuru - Kutoka Ufaransa - Kutoka Hispania |
2 Machi 1956 | ||||
Eneo - Jumla - Maji (%) |
446,550 km² (ya 58) 0.056 | ||||
Idadi ya watu - Julai 2014 kadirio - Msongamano wa watu |
33,848,242 (ya 39) 73.1/km² (122) | ||||
Fedha | Dirham (MAD )
| ||||
Saa za eneo - Kiangazi (DST) |
UTC (UTC+0) UTC (UTC+0) | ||||
Intaneti TLD | .ma | ||||
Kodi ya simu | +212
- | ||||
Namba zote bila Sahara ya Magharibi |
Imepakana na bahari za Atlantiki na Mediteranea; upande wa bara imepakana na Algeria na Mauretania.
Maeneo ya Kihispania ya Ceuta na Melilla yamezungukwa na Moroko kwenye pwani ya Mediteranea.
Mpaka wa kusini haueleweki vizuri kwa sababu Moroko inadai ya kwamba Sahara ya Magharibi ni sehemu ya eneo lake, hali isiyokubaliwa na jumuiya ya kimataifa tangu Moroko ilipovamia Sahara ya Kusini mwaka 1975.
Jina
Jiografia
Eneo la Moroko ni km² 446,550. Sehemu kubwa ni jangwa la Sahara. Watu walio wengi huishi kwenye sehemu za rutuba karibu na pwani.
Kuna milima inayofunika maeneo makubwa. Milima ya Rif inaongozana na pwani ya Mediteranea yenye mwelekeo kutoka kaskazini-magharibi kwenda kaskazini-mashariki. Milima ya Atlas iko katikati ya nchi kutoka kusini-magharibi kwenda kaskazini-mashariki.
Miji mikubwa
Mji mkuu ni Rabat wenye wakazi milioni 1.2. Mji mkubwa ni Casablanca (kwa Kiarabu: الدار البيضاء dar al-baiDa = nyumba nyeupe). Miji yote miwili mikubwa ni miji ya bandari.
Miji mitano mikubwa ni kama ifuatavyo (namba za sensa ya mwaka 2004):
- 1. Casablanca: wakazi 2.933.684
- 2. Rabat: wakazi 1.622.860
- 3. Fes: wakazi 946.815
- 4. Marakesh: wakazi 823.154
- 5. Agadir: wakazi 678.596
Historia
- Makala: Historia ya Moroko
Moroko ya Kale
Habari za kimaandishi za kwanza ni kutoka karne za kwanza KK. Wafinisia walijenga miji yao pwani lakini eneo la ndani lilibaki nchi ya Waberber waliounda ufalme wa Mauretania ya Kale (usiuchanganye na nchi ya kisasa Mauretania) uliounganisha sehemu kubwa ya Moroko ya kaskazini.
Wamauretania wa kale walishirikiana na Dola la Roma hadi kuwa jimbo la dola hili kwa jina la "Mauretania Tingitana".
Wakati wa kudhoofika kwa Dola la Roma kuanzia mwaka 400 BK kukawa na uvamizi wa Wavandali.
Uvamizi wa Kiarabu
Karne ya 7 BK ilileta uvamizi wa Waarabu walioteka nchi na kusababisha polepole Waberber (waliokuwa Wayahudi, Wakristo au wafuasi wa dini za jadi) kuwa Waislamu.
Mwanzoni Moroko ilikuwa sehemu ya milki ya khalifa ya Waomawiyya waliotawala Dameski (Siria). Baada ya kupinduliwa kwa Waomawiyya na Waabasiya wa Baghdad (Iraq) mkimbizi Mwarabu Idris ibn Abdallah (788-791) alikusanya makabila ya Waberber na kuunda milki ya kujitegemea. Hii ilikuwa mwanzo wa Moroko kuwa milki ya Kiislamu inayojitawala.
Watawala wa kienyeji
Vipindi vya historia husebabiwa kufuatana na familia zilizofuatana za wafalme Waarabu au Waberber.
Moroko ilitawaliwa na familia za (miaka BK)
- Waidrisi (788-974)
- Wamaghrawa (987-1070)
- Wamurabitun (Almoravi)(1073-1147)
- Wamuwahidun (Almohad) (1125-1269)
- Wamarini (1258-1420)
- Wawattasi (1420-1547)
- Wasaadi (1509-1659)
- Waalawi (1631 hadi leo)
Murabitun na Muwahidun
Wafalme wa Wamurabitun (Almoravi) (1073-1147) na wa Wamuwahidun (Almohad) (1147-1269) walieneza utawala wao hadi Afrika ya Magharibi (Mauretania, Senegal na Mali ya leo) na sehemu kubwa ya Andalusia (Hispania ya Kiislamu), tena hadi mipaka ya Misri.
Wamuwahidun waliendelea kupanuka kuelekea Misri lakini baadaye walidhoofika wakapaswa kuwaachia Wahispania Wakristo sehemu za Andalusia. Athira ya milki ya Moroko ilipungua baadaye hadi Hispania yote ikarudishwa kwa watawala Wakristo mwaka 1492; pia utawala kusini kwa Sahara haukuendelea.
Wareno wa Wahispania waliendelea kuteka miji kwenye pwani za Moroko. Utawala wa Hispania juu ya Ceuta na Melilla leo ni mabaki ya nyakati zile.
Sehemu za nchi zilianza kujitawala bila kukubali tena mamlaka wa juu, kwa mfano makabila ya Waberber milimani au miji ya Rabat na Sale iliyounda dola dogo la Jamhuri ya Bou Regreg katika karne ya 17 na kujishughulisha na uharamia.
Waalawi (1666 hadi leo)
Katika karne ya 17 familia ya Waalawi walishika mamlaka wakaendelea nayo hadi leo. Waliweza kutunza uhuru wa nchi hadi mwanzo wa karne ya 20. Lakini mwanzo wa karne ya 20 Ufaransa na Hispania walimlazimisha mfalme Mulay Abdelaziz kukubali mkataba uliofanya Moroko kuwa kama koloni chini ya nchi hizo mbili.
Vita Kuu ya Pili ya Dunia ilidhoofisha Ufaransa pamoja na kuingia kwa wanajeshi Waamerika na Waingereza na ahadi zao za kuleta uhuru tokeo lililohamasisha wazalendo wa Maroko kupigania upya uhuru wa nchi.
Baada ya vita Wafaransa walijaribu kukandamiza mwendo huo wakamwondoa Sultani Mohammed V nchini 1953. Ghasia zikaongezeka, Sultani akarudi na nchi ikapewa uhuru mwaka 1956.
Utawala wa mwanae Hassan II kuanzia mwaka 1961 uliitwa "miaka ya risasi" kwa sababu mfalme alikataa kukubali utaratibu wa kidemokrasia. Chaguzi zilikuwa za uwongo, wapinzani wakatupwa jela au kuuawa. Hassan II alishinda majaribio mbalimbali ya kumpindua. Siasa ya kushikamana na Marekani ilimsaidia mfalme kimataifa lakini baada ya mwisho wa "vita baridi" alilazimishwa na Wamarekani kulegeza utawala wake.
Mtoto wake Muhamad VI akawa mfalme kijana mwaka 1999 akaanza mageuzi ya kisiasa ya wazi zaidi.
Watu
Mnamo 60 % (Januari 2005) za wakazi milioni 32.7 huishi mijini.
Kiasili wakazi wengi ni Waberber na Waarabu, pamoja na watu wa asili ya Andalusia (Hispania) na wa Afrika kusini kwa Sahara. Waberber ndio wenyeji asilia.
Kaskazini mwa nchi ambako kitovu chake ni Fes kuna zaidi tabia ya Kiarabu, wakatu kusini ambako kitovu chake ni Marakesh kuna tabia ya Kiberber zaidi.
Lugha
Lugha rasmi ya nchi ni Kiarabu na Kiberberi. Waberber wengi, hasa kaskazini, wameacha lugha yao na kutumia Kiarabu lakini walileta maneno yao katika lahaja ya Kiarabu cha Kimaroko. Hata Kifaransa kinatumika sana.
Dini
Uislamu ndio dini rasmi na ndio unaofuatwa na wakazi wengi sana (98.9%), hasa Wasunni. Wengine ni Wakristo (0.9%) na Wayahudi (0.2%). Wakristo karibu wote ni wa asili ya Ulaya. Wayahudi waliwahi kuwa wengi kidogo, lakini idadi yao imepungua katika miaka ya nyuma kutokana na uhamaji hata kama hali yao katika taifa ni nzuri kulingana na nchi nyingine za Kiarabu.
Uchumi
Nguzo za uchumi wa nchi ni kilimo na magodi ya kuchimba madini, pamoja na uvuvi na utalii.
Zaidi ya asilimia 40 za wananchi hulima. Kwa jumla asilimia 18 za eneo la Moroko zinatumiwa kwa kilimo, hasa katika magharibi na kaskazini-magharibi.
Nchi hii ina akiba kubwa ya fosfati inayochimbwa na kuuzwa nje kwa matumzi ya mbolea. Akiba ya fosfati ni kubwa duniani. Moroko ina nafasi ya tatu katika uzalishaji baada ya China na Marekani[1].
Umuhimu wa utalii kwa uchumi umezidi kukua; mwaka 2018 idadi ya watalii ilifikia milioni 12.3[2] Vivutio vya kitalii ni pamoja na mahali pa urithi wa dunia kama vile
- Medina ya Fez
- Medina ya Marrakesh
- Ksar au mji-ngome wa Ait Benhaddou
- Mji wa kihistoria ya Meknes
- Eneo la akiolojia la Volubilis
- Medina ya Tetouan
- Medina ya Essaouira
- Mji wa Kireno wa Mazagan
- Rabat
Tazama pia
Viungo vya nje
- Official website of the government of Morocco Ilihifadhiwa 25 Aprili 2006 kwenye Wayback Machine.
- Official bulletins of the government of Morocco
- Parliament of Morocco
- Census results of 1994 and 2004 Ilihifadhiwa 5 Januari 2019 kwenye Wayback Machine.
- Forum press Morocco Ilihifadhiwa 17 Mei 2018 kwenye Wayback Machine.
- Morocco entry at The World Factbook
- Moroko katika Open Directory Project
- Morocco profile from the BBC News
- Maroc Paradise, Beauty of Morocco Ilihifadhiwa 6 Januari 2015 kwenye Wayback Machine.
- Wikimedia Atlas of Morocco
- Tribes of Morocco
- Key Development Forecasts for Morocco from International Futures
- EU Neighbourhood Info Centre: Morocco Ilihifadhiwa 11 Septemba 2015 kwenye Wayback Machine.
- World Bank Summary Trade Statistics Morocco
Nchi za Afrika | |
---|---|
Afrika ya Kati (Jamhuri ya) | Afrika Kusini | Algeria | Angola | Benin | Botswana | Burkina Faso | Burundi | Cabo Verde | Chad | Cote d'Ivoire | Eritrea | Eswatini | Ethiopia | Gabon | Gambia | Ghana | Guinea | Guinea Bisau | Guinea ya Ikweta | Jibuti | Kamerun | Kenya | Komori | Kongo (Jamhuri ya) | Kongo (Jamhuri ya Kidemokrasia ya) | Lesotho | Liberia | Libya | Madagaska | Malawi | Mali | Misri | Morisi (Visiwa vya) | Mauritania | Moroko | Msumbiji | Namibia | Niger | Nigeria | Rwanda | Sahara ya Magharibi | Sao Tome na Principe | Senegal | Shelisheli | Sierra Leone | Somalia | Sudan | Sudan Kusini | Tanzania | Togo | Tunisia | Uganda | Zambia | Zimbabwe | |
Maeneo ya Afrika ambayo ni sehemu za nchi nje ya Afrika | |
Hispania: Kanari · Ceuta · Melilla | Italia: Pantelleria · Pelagie | Ufaransa: Mayotte · Réunion | Uingereza: · St. Helena · Diego Garcia | Ureno: Madeira |
Makala hii kuhusu maeneo ya Afrika bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Moroko kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |
- ↑ Phosphorus A Looming Crisis, Vaccari, David A. (2009). "Phosphorus: A Looming Crisis" (PDF). Scientific American. 300 (6): 54–9.
- ↑ Over 12 Million Tourists Visited Morocco in 2018 Bazza, Tarek (2019). "Over 12 Million Tourists Visited Morocco in 2018, Up 8% from 2017". Morocco World News. Retrieved 2019-03-21.