Tom von Prince (Port Louis, Morisi, 9 Januari 1866 - Tanga, leo nchini Tanzania, 4 Novemba 1914) alikuwa afisa wa kijeshi wa Kampuni ya Kijerumani kwa Afrika ya Mashariki (kwa Kijerumani: Deutsch-Ostafrikanische Gesellschaft(DOAG)), mwenye shamba Afrika Mashariki ya Kijerumani, na mtu maarufu huko, kama kapteni katika Schutztruppe, aliwaongoza vikosi vya Wajerumani katika Afrika Mashariki wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia kwa kunyakua Taveta tarehe 15 Agosti 1914. Baadaye, akauawa katika Vita vya Tanga mnamo Novemba mwaka ule ule.

Tom na Magdalene von Prince, kabla ya 1908

Utoto

Alizaliwa mnamo 9 Januari 1866, mtoto wa Mskoti Thomas Henry Prince, wakati baba yake alikuwa mkuu wa polisi wa Morisi, kisiwa kilichotawaliwa na Uingereza. Mama yake alikuwa Mjerumani. Baada ya kifo cha mapema cha baba yake, mama alirudi Ujerumani. Akiwa kijana, aliishi kwa muda mrefu huko Liegnitz, Silesia aliposoma kwenye shule ya mabweni iliyolenga hasa vijana vya familia za makabaila wa Prussia. Shuleni, alikuwa mwanafunzi pamoja na mkuu wake wa baadaye Paul von Lettow-Vorbeck, na alikutana na mkewe wake Magdalene von Massow hapa hapa.

Kazi ya kijeshi

Mwaka wa 1887 alijiunga na Jeshi la Dola la Ujerumani na alihudumu katika kikosi cha wanajeshi wa Prussia, ambacho kilikuwa karibu na Strasbourg. Mwaka 1889, aliacha jeshi akiwa luteni; mnamo 1890 alijiunga na Kikosi cha Wissmann, kilichoendelea baadaye kama Jeshi la Schutztruppe (jeshi la ulinzi wa koloni). Baada ya kufika Afrika Mashariki, Tom Prince, mwenye cheo cha luteni, slishiriki katika ukandamizaji wa upinzani wa wenyeji wa pwani dhidi ya ukoloni ya Kijerumani katika Vita ya Abushiri. Baadaye alipewa kazi ya usalama kwenye njia za misafara kati ya pwani na maziwa makubwa ya Afrika.

Katika miaka iliyofuata alipewa kazi ya kupambana na Wahehe waliowahi kuangamiza kikosi kikubwa cha Schutztruppe kwenye mapigano ya Lugalo chini ya chifu Mkwawa. Prince alianzisha kituo kipya cha kijeshi kwa kujenga boma la Iringa, si mbali na mji mkuu wa Mkwawa huko Kalenga. Kutoka hapa gavana mpya von Schele alishambulia Kalenga kwenye mwaka 1894 na kuteka mji huo ilhali Mkwawa aliweza kukimbia. Ilhali Mkwawa aliendelea na vita ya msituni dhidi ya Wajerumani, Prince alipewa kazi ya kumdhibiti na kumshinda. Prince alifaulu kuvuta sehemu ya Wahehe upande wake na hivyo kupunguza athira ya Mkwawa. Mnamo mwaka 1898 Mkwawa alibaki na wasaidizi wachache, alizingirwa na kikosi cha Kijerumanimilhali alikuwa mgonjwa akajiua kwa kujipigia risasi.

 
Jumba la Prince katika shamba la Sakkarani (Usambara, Afrika Mashariki ya Ujerumani)

Wakati alikuwa barani Afrika, Prince alirudi mara kadhaa kwenda Ujerumani. Huko alimwoa Magdalene von Massow, akarudi naye Afrika. Mwaka wa 1896 alipandishwa cheo cha kapteni. Baada ya kifo cha Mkwawa, aliondoka Iringa na kazi ya jeshi akaendelea kama afisa ya serikali huko Ziwa Nyasa na Iringa.  Mnamo mwaka 1900, Prince aliacha pia kazi ya serikali kutulia na mkewe akanunua shamba katika Milima ya Usambara na kuanza shughuli za kilimo. Mnamo 1906, Kapteni von Prince alipewa cheo cha kikabaila cha heshima akajiita sasa "von Prince".

Vita ya Kwanza ya Dunia na Tanga

Wakati wa kuzuka kwa Vita ya Kwanza ya Dunia, Prince alirudi katika jeshi na akapewa amri juu ya kikosi cha 13 cha Schutztruppe kilichofanywa na askari Waafrika, pamoja na vikosi viwili vya walowezi Wajerumani waliojiunga na jeshi la Schutztruppe. Askari wake kwa sababu ya ushujaa wa Prince walimwita kwa jina la Bwana Sakarani - yaani, 'mwinyaji mwavita '.

Siku ya 15 Agosti 1914, katika mwanzo wa mapigano ya vita huko Afrika Mashariki, vikosi vya von Prince vilivamia na kuteka mji wa Taveta upande wa Kenya kwa kufuata amri ya kamanda wa majeshi ya Kijerumani, Paul von Lettow-Vorbeck. Lengo lilikuwa kuimarisha ulinzi wa kaskazini mwa koloni la Kijerumani na kulinda Reli ya Usambara. [1]

Tom von Prince alisahiriki katika Mapigano ya Tanga tarehe ya 4 Novemba 1914.  Aliamriwa kuongoza wanajeshi wake katikati ya mji na hapo aliuawa na risasi wakati wa kupigana kikosi cha Kiingereza kilichokuwa kilivamia Tanga pamoja na wanajeshi kutoka Uhindi ya Kiingereza. Alizikwa pamoja na maafisa wengine kumi na wawili wa Ujerumani waliouawa huko mjini Tanga.

Marejeo

  1. Paice, Edward (2007). Tip and Run: The Untold Tragedy of the Great War in Africa. London: Weidenfeld & Nicolson. uk. 19,57,244. ISBN 9-780297-847090.

Machapisho

  • Tom von Prince: Gegen Araber und Wahehe - Erinnerungen ainer meiner ostafrikanischen Leutnantszeit 1890-1895 . Mittler, Berlin 1914

Fasihi

  • Herbert Viktor Patera : Der Weiße Herr Ohnefurcht - Das Leben des Schutztruppenhauptmanns Tom von Prince . Deutscher Verlag, Berlin 1939.
  • Hans Schmiedel: "Bwana Sakkarani - Der Schutztruppenhauptmann Tom von Prince und seine Zeit" . Handschriftliches Manuskript