Lugalo
Lugalo (pia: Rugaro) ni kata ya Wilaya ya Kilolo, Mkoa wa Iringa nchini Tanzania yenye Postikodi namba 51313.
Katika sensa iliyofanyika mwaka 2022 wakazi walihesabika kuwa 13,970 [1]. Kwa mujibu wa sensa iliyofanyika mwaka wa 2012, kata ilikuwa na wakazi wapatao 12,359 waishio humo.[2]
Lugalo iko karibu na barabara kuu ya TANZAM, takriban kilomita 45 kutoka Iringa kwenda Dar es Salaam.
Lugalo ni mahali pa kihistoria kutokana na kwamba ilikuwa sehemu ya mapigano mnamo mwaka wa 1891 kati ya jeshi la kikoloni la Kijerumani na mtemi Mkwawa kiongozi wa Wahehe. Kuna jiwe kubwa la kumbukumbu mahali ambako Wahehe walishinda kikosi cha Kijerumani kilichoongozwa na Emil von Zelewski.
Mapigano ya 17 Agosti 1891
haririMwezi Julai mwaka 1891 von Zelewski alielekea Uhehe kwa lengo la kuvamia eneo la Mkwawa kwa sababu Wahehe walikuwa tishio kwa uenezaji wa koloni la Afrika ya Mashariki ya Kijerumani. Kikundi chake kilikuwa na kombania 3 zenye maafisa Wajerumani 13, maaskari Waafrika 320 na wapagazi 170 waliobeba mizinga mepesi na bunduki bombomu.
Baada ya kuangamiza vijiji kadhaa Zelewski alianza kuwapuuza Wahehe, akiendelea bila upelelezi wa awali, akashambuliwa tarehe 17 Agosti 1891 alipopita kwenye manyasi marefu huko Lugalo. Mkwawa alikuwa akimsububiri na Wahehe 3,000 walionyamaza hadi Wajerumani waliotembea kwa umbo la safu ndefu walikuwa karibu kabisa wakawashambulia.
Wajerumani walikosa muda kuandaa silaha zao wakashtushwa kabisa. Sehemu kubwa ya askari waliuawa kwa dakika chache pamoja na jemadari von Zelewski. Sehemu ya kombania ya nyuma ilirudi nyuma na kusimama kwenye kilima kidogo walipoweza kutumia bunduki la mtombo wakajitetea na kuua Wahehe wengi. Sehemu hii ilijumlisha maafisa 2 na maafande 2 Wajerumani waliweza kukimbia na kujiokoa pamoja na askari 62 na wapagazi 74.
Mapigano hayo yalikuwa mwanzo wa vita ya Uhehe ambako Wajerumani walitumia wanajeshi wengi pamoja na silaha za kisasa wakafaulu kuwashinda Wahehe baada ya miaka 7, hadi kifo cha Mkwawa mwaka 1898.
Marejeo
haririViungo vya nje
hariri- Makala „Lieutenant von Zelewski“ kwa ntz.info - Kiing.
- Jan-Bart Gewald, Colonial Warfare: Hehe and World War One, the wars besides Maji Maji in south-western Tanzania, ASC Working Paper 63/2005 Archived 7 Novemba 2007 at the Wayback Machine. (PDF-Kiingereza; 78 kB)
- Mapigano ya Lugalo kwenye mkwawa.com (Kiswahili) Archived 30 Mei 2007 at the Wayback Machine.
- Paul Beck, German Colonial Wars; ndani yake maelezo juu ya shambulio la Zelewski dhidi ya Mkwawa
Kata za Wilaya ya Kilolo - Tanzania | ||
---|---|---|
Boma la Ng'ombe | Dabaga | Ibumu | Idete | Ihimbo | Ilula | Image | Irole | Kimala | Kising'a | Lugalo | Mahenge | Masisiwe | Mlafu | Mtitu | Ng'ang'ange | Ng'uruhe | Nyalumbu | Nyanzwa | Ruaha Mbuyuni | Udekwa | Uhambingeto | Ukumbi | Ukwega |
Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Iringa bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Lugalo kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |