Mkwawa
Mkwawa au kwa jina refu Mkwavinyika Munyigumba Mwamuyinga (1855 – 19 Julai 1898) alikuwa mtemi na kiongozi mkuu wa kabila la Wahehe katika Tanzania ya leo wakati wa upanuzi wa ukoloni wa Ujerumani mwishoni mwa karne ya 19.
Mkwawa ni maarufu hasa kwa kuongoza vita vya Wahehe dhidi ya Wajerumani.
Upanuzi wa Wahehe
Jina la Mkwawa ni kifupisho cha Mukwava ambalo tena ni kifupisho cha Mukwavinyika, lililokuwa jina lake la heshima likimaanisha "kiongozi aliyetwaa nchi nyingi".
Mkwawa alizaliwa mnamo mwaka 1855 mahali palipoitwa Luhota karibu na Iringa mjini. Alikuwa mtoto wa chifu Munyigumba aliyeaga dunia mwaka 1879.
Baba yake Munyingumba aliwahi kuunganisha temi ndogo za Wahehe na makabila ya majirani kuwa dola moja. Aliiga mfumo wa kijeshi wa Wasangu waliowahi kuwa kabila lenye nguvu kwa kujifunza mfumo huu kutoka kwa Wangoni na impi za Shaka Zulu.
Hadi miaka ya 1870 eneo la Wahehe lilipanuliwa mbali kuanzia kusini hadi katikati ya Tanzania ya leo.
Baada ya kifo cha chifu mzee watoto wake walishindania urithi wake, na Mkwawa alishinda akawa kiongozi mpya.
Aliendelea kupanua utawala wake. Hadi mwisho wa miaka ya 1880 alitawala sehemu muhimu za njia ya misafara kati ya pwani na Ziwa Tanganyika. Misafara hiyo ambayo ilikuwa ikibeba bidhaa za nje kama vitambaa, visu na silaha kutoka pwani, ikirudi na watumwa na pembe za ndovu, ilipaswa kumlipia hongo ikanunua pia wafungwa wa vita vyake. Hapo athiri na uwezo wake wa kugharamia jeshi kubwa ikaongezeka.
Mkwawa na upanuzi wa Wajerumani
Tangu mwaka 1885 hivi Wajerumani walianza kuunda koloni lao katika Afrika ya Mashariki ya Kijerumani (Tanganyika pamoja na Rwanda na Burundi za leo). Kwa njia za mikataba na Uingereza, Dola la Kongo (wakati ule mfalme wa Ubelgiji) na Ureno walio kuwa wakoloni wa maeneo jirani walihakikisha kwamba hao hawataingilia katika sehemu walizolenga.
Mwaka 1888/1889 utawala wao ulitikiswa na vita ya Abushiri lakini baada ya kushinda upinzani wa Waafrika wa pwani Wajerumani walilenga kuimarisha utawala wao juu ya sehemu za bara.
Mkwawa aliwahi kusikia mapema habari za Wajerumani akajaribu kuwasiliana nao lakini bila kuelewana. Hapo aliamua kujenga boma imara lenye kuta za mawe kwenye makao makuu yake huko Kalenga karibu na Iringa ya leo[1].
Katika mwezi Februari 1891 alituma wajumbe kwa kambi la Wajerumani huko Mpwapwa wakapokewa na gavana Mjerumani. Wakati huohuo Mkwawa aliendelea kutuma askari zake hadi Usagara iliyotazamwa na Wajerumani kama eneo lao. [2]
Katika kipindi hicho gavana mpya Julius von Soden alifika Dar es Salaam. Hakuwa na mamlaka juu ya mkuu mpya wa jeshi Emil von Zelewski aliyepokea amri zake kutoka Berlin moja kwa moja. Baada ya kusikia habari za mashambulio ya Mkwawa katika Usagara aliomba kibali cha "kuwaadhibu Wahehe" akakubaliwa.
Mapigano ya Lugalo
Katika mwezi Julai 1891 von Zelewski aliongoza kikosi cha maafisa Wajerumani 13 na askari Waafrika hasa kutoka Sudan 320, pamoja na wapagazi 113. Walikuwa na bunduki za kisasa, bunduki za mtombo na mizinga midogo. Zelewski aliwadharau Wahehe kama washenzi ambao walikuwa na mikuki na pinde tu. Kwa hiyo hakuona haja ya kutuma wapelelezi wa awali.
Njiani aliangamiza vijiji alivyokuta na katika mwezi Agosti alipoona Wahehe 3 waliomkaribia aliagiza kuwaua bila kuongea nao. Kumbe walikuwa mabalozi wa Mkwawa aliyetaka kujadiliana na Wajerumani.
Tarehe 17 Agosti 1891 Zelewski na jeshi lake walipita kwenye manyasi marefu karibu na Lugalo. Mkwawa alikuwa alimsubiri na Wahehe 3,000 walionyamaza hadi Wajerumani waliotembea kwa umbo la safu ndefu walipokuwa karibu kabisa wakawashambulia.
Wajerumani walikosa muda wa kuandaa silaha zao wakashtushwa kabisa. Sehemu kubwa ya askari waliuawa katika muda wa dakika chache pamoja na jemadari von Zelewski. Sehemu ya kombania ya nyuma ilirudi nyuma na kusimama kwenye kilima kidogo walipoweza kutumia bunduki la mtombo wakajitetea na kuua Wahehe wengi. Sehemu hii ilijumlisha maafisa 2 na maafande 2 Wajerumani waliweza kukimbia na kujiokoa pamoja na askari 62 na wapagazi 74.
Kutokana ushindi huu Wahehe walipata bunduki 300 za kisasa walizokusanya kati ya maiti za askari wa Schutztruppe, pia mizinga 2 na bombomu 1. Lakini Mkwawa alitupa ramia zote za mizinga mtoni baada ya Mhehe mmoja alikufa alipojaribu kufungua ramia kubwa na kusababisha mlipuko. Silaha zote pamoja na ramia ndogo zilizotekwa zilipelekwa kwenye Iringa-Kalenga na kuhifadhiwa ghalani.
Kipindi cha vita vidogo
Baada ya mapigano Mkwawa alihesabu wafu wake waliokuwa wengi. Alikataza mila za kilio kwa sababu alitaka kuficha idadi ya askari waliokufa. Akielewa sasa kwamba silaha za Wazungu zilikuwa hatari alituma tena mabalozi kwa gavana von Soden walioeleza ya kwamba Wahehe walikuwa walijihami tu dhidi ya shambulio na walitaka amani.
Lakini madai ya Wajerumani yalikuwa magumu, eti kuwaruhusu wafanyabiashara kupita bila matata na kutoshambulia majirani tena.
Mkwawa hakuwa tayari kuahidi yote akachelewesha mikutano. Wakati huo kamanda mpya Mjerumani Tom von Prince alijenga boma jipya la Wajerumani katika Uhehe na Mkwawa alijibu kwa kusambulia vikosi vidogo vya jeshi la kikoloni. Gavana Soden alidai kutoendelea na mapigano. [3], lakini mwaka 1893 aliondoka Afrika, na gavana mpya von Schele alitaka kulipiza kisasi akaamuru mashambulio dhidi ya Mkwawa.
Anguko la Kalenga
Mwezi Oktoba 1894 von Schele aliongoza kikosi cha maafisa Wajerumani 33 na askari Waafrika pamoja na wapagaji zaidi ya 1000 kuelekea Kalenga. Walikuwa na mizinga 4 na bunduki bombomu.
Walipofika mbele ya Kalenga Wahehe walijisikia salama kutokana na kuta imara lakini Wajerumani walijipanga kilomita kadhaa nje ya mji wakaanza kufyatulia mizinga yao na kuua watu kadhaa ndani ya mji. Lakini kwa jumla ukuta ulikuwa imara na mizinga midogo mno ili iweze kuvunja kuta.
Wakati wa giza kwenye asubuhi wa tarehre 30 Oktoba 1894 askari wa jeshi la Schutztruppe walipanda ukuta katika sehemu uliyodhoofishwa tayari na kuingia mjini. Hadi jioni walikuwa wameteka mji wote.
Gobori na mikuki ya Wahehe hazikuweza kushindana na bombomu za Wajerumani. Kwa sababu zisizojulikana Mkwawa hakugawa bunduki za kisasa zote alizokuwa nazo katika ghala yake kutoka ushindi wake juu ya Zelewski; alitoa 100 tu, 200 zilibaki ghalani. Mkwawa mwenyewe aliamua kukimbia pamoja na askari 2000 - 3000, lakini kabla ya kukimbia alimwua mganga mzee aliyewahi kutabiri ya kwamba atawashinda Wajerumani waliokuja.
Gavana von Schele aliandika taarifa kwa serikali ya Ujerumani "tulizika maadui 250, wengine walichomwa katika nyumba zao, wanawake na watoto 1500 kutekwa nyara" [4].
Mkwawa alijificha msituni pamoja na askari zake akasubiri. Gavana von Schele alishindwa kuendelea na mashambulio kwa sababu gharama za vita zilishinda makisio yake na wabunge wa upinzani katika Reichstag huko Berlin walipinga vita vya kikoloni; walikataa kuongeza makisio na kiongozi wa wasoshalisti Agosti Bebel aliita mtindo wa kuchoma mji na kuteka nyara watoto na wanawake "ushenzi mkuu".
Amani fupi
Baada ya kuondoka kwa Wajerumani, Mkwawa aliweza kurudi na kujenga tena nyumba mahali pa Kalenga.
Mnamo Septemba 1895 Mkwawa alikuwa tayari kujadiliana na Wajerumani na tarehe 12 Oktoba walipatana amani. Wajerumani walimkubali Mkwawa kama chifu wa Wahehe, Wahehe waliahidi kukabidhi gobori zote, kupandisha bendera ya Ujerumani na kuwaruhusu wafanyabiashara na wasafiri kupitia Uhehe. Mkwawa alimwagiza mjombawake kutia sahihi akakataa mwenyewe akisema hii ingemwua.
Hata hivyo miezi kadhaa baadaye alitafuta msaada wa Wajerumani kwa shambulio dhidi ya Wabena.
Afisa mmoja Mjerumani aliyefika Kalenga mpya alizuiliwa kuingia na kumwona chifu akaambiwa alipe hongo ya bunduki 5 ili kuingia katika eneo la Mkwawa. Hapo maafisa wa jeshi la Wajerumani waliolinda mpaka, ambao bado walikuwa wakitafuta nafasi ya kulipiza kisasi cha Lugalo, walidai kuwa chifu amevunja mkataba.
Kapteni Tom von Prince alijenga boma jipya karibu na Kalenga ("Iringa Mpya") alianza kuwasiliana na machifu wadogo wa Wahehe. Mkwawa alijaribu kujenga mapatano na majirani lakini Wabena na makabila mengine walikumbuka vita na mashambulio ya awali kutoka Uhehe walipendelea kushikamana na Wajerumani.
Mkwawa aliwaua machifu wawili Wahehe waliowahi kukaa na von Prince, lakini aliona hawakuwa peke yao kusita kumtii tena. Alipata habari ya kwamba hata mdogo wake Mpangile alishikamana na Wajerumani.
Wakati wa Septemba 1896 Wahehe waligawanyika na sehemu kubwa ya viongozi waliochoka vita ilikuwa tayari kuwakubali Wajerumani.[5]. Wajerumani waligawa eneo lao. Wasangu walirudishwa katika eneo lao la awali wakarudi kutoka Usafwa katika mji mkuu wa Utengule Usangu. Mpangile alisimikwa kama kiongozi mpya wa Uhehe penyewe, lakini baaa ya siku 50 alisimamishwa na kuuwa na Wajerumani waliomshtaki, eti anamsaidia kaka yake kisiri.
Katika maficho na kifo
Mkwawa alikuwa ameondoka sehemu za Iringa mwezi Agosti 1896 alipoona mgawanyiko. Alifuata mwendo wa mto Ruaha akilindwa na wenyeji waliokuwa tayari kumficha na kumlinda dhidi ya vikosi vya Wajerumani waliomtafuta.
Mnamo Desemba 1896 alihamia milima ya Uzungwa alipojificha. Kutoka huko alitelemka mara kwa mara kwenye mabonde alipopata vyakula na kushambulia vikosi vidogo vya askari vya Kijerumani.
Katika Julai 1897 kikosi kikubwa cha Wasangu pamoja na Wahehe chini ya uongozi wa Wajerumani walikuta kambi la Mkwawa mlimani wakalishambulia lakini Mkwawa aliweza kukimbia. Wajerumani waliahidi zawadi ya pembe za ndovu yenye thamani ya rupia 5000 kwa kila mtu atakayewasaidia kumkamata Mkwawa, akiwa hai au amekufa.[6]
Mwaka 1898 Mkwawa aliendelea kujificha kwenye misitu akiongozana na watu wachache sana. Aliishi hasa kwa njia ya kuvinda.
Wakati wa Julai 1898 aliongozana na wavulana 4 pekee, halafu Wazungwa 2, mume na mke. Tarehe 16 Julai Wajerumani waliowahi kusikia habari zake walimkuta huyu mama Mzungwa alipotafuta chakula wakamkamata hata akawaambia Mkwawa alielekea kusini. Wakamfuata na tarehe 18 Julai Mkwawa alimwua mume Mzungwa kwa hofu ya kusalitiwa.
Aliendelea na wavulana 2 tu walioitwa Musigombo na Lifumika. Watoto waliogopa angeweza kuwaua pia. Hapo Lifumika aliamua kukimbia asubuhi ya tarehe 19 Julai. Lakini siku ileile alipotelemka kutoka mlimani alikutana na kikosi cha Wajerumani kilichoongozwa na sajinitaji Johann Merkl. Akakimbia lakini wakamshika wakamlazimisha kuwaambia habari za Mkwawa. Kijana alimwambia Merkl kuwa chifu alikaa mgonjwa mahali kwa umbali wa masaa 3. Walimlazimisha kuwaongoza. Njiani walisikia kwa mbali sauti ya bunduki, risasi 1. Wakaendelea na baada ya masaa mawili walikuta maiti za Mkwawa na yule kijana mwingine. Inaonekana waliwahi kujiua na sauti ya bunduki ilikuwa Mkwawa aliyejipigia risasi.[7].
Merkl aliagiza kukatwa kwa kichwa cha Mkwawa ili awe na uthibitisho amekufa kweli. [8]
Zawadi ya rupia 5,000 iligawiwa kwa kikosi cha Merkl, ilhali yeye mwenyewe alipata theluthi mbili yaani zaidi ya rupia 3,000.
Fuvu la Mkwawa
Kichwa cha mtemi kilikabidhiwa kwa Kapteni von Prince pale Iringa Mpya na kuonyeshwa mtaani kwa Wahehe waliokuwepo. Kikasafishwa katika hospitali na kutumwa Berlin kilipohifadhiwa katika makumbusho, awali Berlin na baadaye Bremen. [9]
Waingereza waliochukua utawala wa koloni mwaka 1918 baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia walitaka kuonekana kama mabwana wema. Mkuu wa serikali ya kikoloni ya Tanganyika alipendekeza kurudisha fuvu kwa sababu Wahehe walishirikiana na Waingereza wakati wa vita. Hivyo kuna kipengele 246 katika mkataba wa Versailles kinachosema: "Katika muda wa miezi 6 baada ya kuthibitishwa kwa mkataba huu ... Ujerumani utakabidhi fuvu la Sultani Mkwawa iliyohamishwa kutoka Afrika ya Mashariki ya Kijerumani na kupelekwa Ujerumani kwa serikali ya Mfalme wa Uingereza."
Wajerumani walikataa habari za fuvu hili na Waingereza waliamua ya kwamba ilishindikana kulipata.
Lakini baada ya Vita vikuu vya pili ambako Ujerumani penyewe ilivamiwa na wanajeshi wa Uingereza gavana Twining wa Tanganyika alikumbuka habari za fuvu akatembelea Ujerumani na kutazama mafuvu ya makumbusho ya Bremen.
Katika mkusanyiko wa mafuvu 2000, 84 yalikuwa na namba zilizoonyesha yalitokea Afrika ya Mashariki ya Kijerumani. Hapo aliyapanga kufuatana na ukubwa na kutazama yale yaliyokuwa na vipimo vya karibu na ndugu wa Mkwawa aliowahi kuwapima kabla ya safari yake. Hapo aliteua fuvu lenye shimo kwa sababu taarifa ya kale ilisema Mkwawa alijiua kwa kujipiga risasi kichwani.
Fuvu hilo lilipelekwa Tanganyika tarehe 9 Julai 1954 na kuhifadhiwa katika jengo la makumbusho ya Mkwawa kwenye kijiji cha Kalenga.
Athari yake upande wa dini
Mkwawa alifuata dini za jadi, na alikataa ombi la Walutheri la kuanzisha misheni Uhehe, lakini baadaye alikubali wamisionari Wabenedikto wa Kanisa Katoliki wahamie Tosamaganga na kuanza kazi yao kati ya Wahehe.
Hata wakati wa vita vyake dhidi ya Wajerumani, Mkwawa aliwaheshimu wageni wake hawa.
Matokeo yake Wahehe wengi waliingia taratibu Ukristo kupitia madhehebu ya Kikatoliki hadi leo.
Tanbihi
- ↑ Kalenga iliitwa pia "Iringa"; baada ya kuchomwa na Wajerumani 1894, Kapteni von Prince alianzisha kituo kipya kilomita 15 upande wa mashariki akaiita "Iringa Mpya": ndio mji wa leo
- ↑ John Iliffe, A modern history of Tanganyika, 1979, uk 108
- ↑ Iliffe uk. 109-110
- ↑ David Pizzo, "To devour the land of Mkwawa": Colonial violence and the German-Hehe War in East Africa, 2007, uk 173
- ↑ John Iliffe, A modern history of Tanganyika, 1979, uk 113 / 114
- ↑ Prince, Magdalene v.(1908), uk. 166
- ↑ John Iliffe, A modern history of Tanganyika, 1979, uk 115 /116
- ↑ Baadaye alipata theluthi mbili za zawadi iliyoahidiwa na serikali ya kikoloni akanunua shamba Kilimanjaro akafaulu kulima na kutajirika. Kabla ya Vita Kuu ya Kwanza Merkl alirudi Ujerumani, akanunua shamba kubwa pale akaingia katika siasa. Hadi 1933 alishika kiti katika Bunge la Bavaria. Baada ya Vita Kuu ya Pili alishiriki kuunda chama cha Christian Social CSU kabla hajaaga Dunia.
- ↑ Siku zile Ujerumani kulikuwa na mkusanyo wa mafuvu mengi kutoka pande zote za Dunia kwa imani kuwa umbo la mifupa linasaidia kuelewa tabia za watu na mataifa.
Marejeo
- Alison Redmayne: Mkwawa and the Hehe Wars; The Journal of African History Vol. 9, No. 3 (1968), pp. 409-436, Cambridge University Press online hapa
- Magdalene von Prince, Eine deutsche Frau im Innern Deutsch-Ostafrikas, Berlin 1908 (online hapa)
- Pugu Hadi Peramiho - kimehaririwa na P. Gerold Rupper, OSB, BPNP, Peramiho 1988, ISBN 9967 67 031 1
- Martin Baer and Olaf Schroeter: Eine Kopfjagd. Deutsche in Ostafrika. Christoph Links, Berlin 2001, ISBN 3-86153-248-4.