Wahehe

Kabila la Tanzania

Wahehe ni watu wa kabila la Tanzania ambao kiasili wanaishi katika wilaya za Mkoa wa Iringa, yaani Iringa mjini, Iringa vijijini, Kilolo na Mafinga, lakini pia sehemu nyingine, hasa wilaya ya Mpwapwa katika mkoa wa Dodoma.[1]

Wahehe mnamo 1906.

Historia ya Wahehe hariri

Shina la Wahehe linaanzia kwa mtu aliyeitwa Mufwimi (yaani Mwindaji), ambaye mababu walisimulia kwamba alitokea nchini Ethiopia. “Mufwimi alipita akiwinda kutoka Ethiopia, Kenya kabla ya kuingia Tanganyika na kujikuta yupo Usagara na hatimaye eneo la Nguluhe-Dabaga akipitia Ikombagulu, himaya ya Chifu Mwamududa ambaye alikuwa akitawala kabila la Wakombagulu, lililokuwa na watu wachache. Wengi walimfananisha Mufwimi na mtu wa kabila la Wakamba kutoka Kenya kutokana na umbile lake kubwa.”

Wakati huo eneo ambalo sasa linaitwa Iringa lilikuwa na makabila mbalimbali. Walikuwepo:

  • ‘Wahafiwa’ katika Bonde la Milima Welu, Luvango, Wutinde, Lugulu, Makongati, Kalenga, Kipagala, Kihesa, Tambalang’ombe, Ibanagosi, Tipingi, Ikolofya, Nyambila, Kibebe na Isanzala.
  • ‘Vanyategeta’ waliishi Udzungwa, Kitelewasi na Lundamatwe, walikuwa wahunzi hodari.
  • ‘Vanyakilwa’ walilowea Mufindi wakitokea Kilwa.
  • ‘Vasavila’ waliishi milima ya Welu huko Makungu (Kihanga ya sasa), Magubike na Malangali.
  • ‘Vadongwe’ waliishi kando ya milima ya Uhambingeto, Ipogolo, Nyabula na Luhota.

Mufwimi alikuwa mwindaji mkubwa wa nyati ambaye aliichoma nyama yake kwa kuipaka chumvi ambayo ilikuwa haifahamiki kwa wakazi wa himaya hiyo; alimpelekea zawadi ya nyamachoma Chifu Mwamududa aliyeipenda mno kwa ladha yake.

Alipendwa na kukaribishwa na Mwamududa kuishi kwake, lakini akaanzisha mapenzi ya siri na Semduda, binti wa Chifu huyo, ambaye alikuwa amewakataa wachumba wengi. Binti huyo akapata ujauzito. Mufwimi akaogopa kwa kuona amefanya kosa kubwa.

Jioni moja akamwita Semduda na kumweleza kwamba yeye anaondoka, lakini akampa maagizo, ikiwa atajifungua mtoto wa kike amwite Mng’anzagala na akiwa wa kiume amwite Muyinga Mufwimi (maana yake ni Mhangaikaji Mwindaji).

Mufwimi alitoroka kwa hofu ya kuuawa na Mwamududa. Akaendelea kuwinda huko na huko hadi Itamba alikouawa na nyati. Hakuna ajuaye lilipo kaburi lake.

Kumbe mtawala huyo alifurahi kusikia bintiye ana mimba ya Mufwimi, maana alijua sasa angekubali kuolewa. Kwa bahati nzuri, binti huyo alijifungua mtoto wa kiume, hivyo akamwita jina la Muyinga Mufwimi kama alivyokuwa ameelekezwa na Mufwimi mwenyewe.

“Kijana huyo alipokua, kwa vile Chifu Mwamududa hakuwa na mtoto wa kiume, akaamua kuukabidhi utawala wake kwa mjukuu ambaye ni Muyinga Mufwimi aliyekuwa hodari wa vita.

Muyinga Mfwimi akaanza kutawala, akazaa watoto watatu wa kiume ambao ndio wajulikanao hadi leo kama koo kutoka kabila la Wahehe, nao walikuwa Maliga, Nyenza na Mpondwa.

Mtwa Maliga naye akazaa watoto watano wa kiume ambao ni Kitova, Mudegela, Mgayavanyi, Mkini na Kigwamumembe.

Inaelezwa kwamba, katika watoto wake hao, alisema Kitova yeye atakuwa tabibu (mganga wa tiba asilia) na Mudegela atakuwa mtawala. Kwa maana hiyo Kitova alikuwa akitibu maradhi mbalimbali, lakini hasa majeruhi wa vita na kizazi chake ndicho kinachoendelea kutibu mifupa katika kijiji cha Image mpaka sasa.

Mudegela Maliga yeye aliwazaa Lalika, Kalongole, Mbelevele, Wisiko, Kipaule, Mkanumkole, Lusoko na Mwakisonga. Hata hivyo, uchifu wake ulikwenda kwa mwanawe wa tano, ambaye ni Mtwa Kilonge.

Kilonge Mudegela alimuoa Maumba Sekindole aliyemzalia Ngawonalupembe na Munyigumba, lakini pia akamuoa Sekindole mwingine aliyewazaa Gunyigutalamu, mkewe wa tatu aliyeitwa pia Sekindole aliwazaa Magidanga, Mhalwike, Mupoma, Magoyo na Magohaganzali.

“Kilonge alipofariki akazikwa katika eneo ambalo sasa ni kijiji cha Lupembe lwa Senga (maana yake Pembe ya Ng’ombe), ambapo kaburi lake lilikuwa na pembe mbili za tembo, ingawa nasikia pembe zile ziliibwa na tunaambiwa walioiba wote walikufa ukoo mzima. Nasikia serikali ilipeleka pembe nyingine na kuzichimbia ili iwe kumbukumbu,” anasimulia Malugala.

Utawala una mambo yake, wakati mwingine unatumia njia halali na haramu ili kuudumisha. Malugala anasema, Munyigumba, ambaye ni mtoto wa pili wa Mtwa Kilonge, alihisi kwamba angeweza kuukosa uchifu kwa kumhofia kaka yake Ngawonalupembe.

“Kwa hiyo akafanya hila na kumuua kaka yake Ngawonalupembe ili yeye atawale, halafu akamchukua Sekinyaga, mke wa marehemu kaka yake kuwa mkewe, lakini wakati anamchukua, kumbe tayari Sekinyaga alikuwa mjamzito.

“Baada ya mtoto kuzaliwa, ambaye alikuwa wa kiume, Mama Sekinyaga akamwita Malangalila Gamoto, pengine kwa maelekezo ya marehemu Ngawonalupembe mumewe. Kwa hiyo Malangalila si mtoto wa Munyigumba, bali wa kaka yake ingawa yeye ndiye aliyemlea,” anaeleza Malugala.

Malugala anasimulia kwamba, ugomvi ulitokea baada ya mama huyo kujifungua ambapo alimwambia Munyigumba kwamba huyu si mtoto wake. Hapo Munyigumba akakasirika na kuamua kumfukuza Sekinyaga na mwanawe.

Inaelezwa kwamba, alipomfukuzwa, Sekinyaga akaelekea katika maeneo ya Sadani, lakini baadaye Munyigumba akajirudi kwa kuhisi angepata aibu, hivyo ikabidi amrudishe.

“Sasa wafuasi wake aliowatuma wakamchukue huyo mama wakaenda kumuua huko Sadani, hata kaburi lake halijulikani liliko. Wao wakarudi na mtoto Malangalila Gamoto. Kwa hiyo, Malangalila na Mkwawa ni mtu na mdogo wake kasoro baba zao,” anaeleza.

Munyigumba alikuwa na wake watano – Sengimba, Sendale, Sekinyaga (aliyekuwa mke wa kaka yake), Sembame na Sengimba mdogo. Sengimba mkubwa aliwazaa Kilemaganga, Mkwawa, Mpangile, Mulimbila na Wiyolitwe; Sendale alimzaa Mgungihaka; Sengimba mdogo alimzaa Msengele Kilekamagala; Sekinyaga alimzaa Malangalila Gamoto (kwa Ngawonalupembe); na Sembame alimzaa Mpugumoto.

Utawala wa Munyigumba Kilonge Mwamuyinga ulidumu kwa muda wa miaka 19 tangu alipomuua kaka yake Ngawonalupembe mwaka 1860.

Mtwa Munyigumba alifariki mwaka 1879 katika kijiji cha Lungemba akiwa amefanikiwa kuziunganisha koo zaidi ya 100 ambazo baadaye ndizo zilizozaa kabila la Wahehe. Wakati Munyigumba anafariki, Mtwa Mkwawa, ambaye ni mtoto wake wa kwanza, alikuwa na umri wa miaka 24.

Kutokana na umri mdogo wa Mkwawa, ikabidi asikabidhiwe kwanza uchifu kwa wakati huo, hivyo ukoo ukamteua mdogo wake Munyigumba, Mtwa Mhalwike, aliyezaliwa na mke wa tatu wa Mtwa Kilonge, Mama Sekindole.

Hata hivyo, muda mfupi baada ya Mtwa Munyigumba kufariki na kutawazwa kwa Mhalwike, utawala huo ukapinduliwa na mmoja wa wafuasi wake na pia mkwewe aliyekuwa amemuoa binti yake. Mtu huyo, Mwamubambe Mwalunyungu, alikuwa anatokea eneo la Wassa na enzi za utawala wa Munyigumba ndiye hasa aliyekuwa akitumwa kazi ndogondogo kiasi cha kupendwa na hatimaye akapewa binti wa Chifu.

“Huyu Mwamubambe kwa nini mdogo wake Munyigumba atawale? Nchi hii nitaichukua mimi mwenyewe,” anasimulia Malugala Mwamuyinga, mjukuu wa Msengele Kilekamagana, ambaye ni mdogo wake Mkwawa.

Mwamuyinga anasema, Mwamubambe alimvamia Mhalwike kichakani, akampiga na kumchinja katika eneo hilo la Lungemba. Alipomaliza kazi yake hiyo haramu akaenda mahali ambako watu walikuwa wanakunywa pombe na kusema: “Nchi hii ni yangu. Kama mnabisha nendeni kule kwenye miti mkamtazame Mhalwike.” Walipokwenda huko wakakuta maiti ya Mhalwike ikiwa imechinjwa kama kuku.

Wakati huo Mtwa Mkwawa alikuwa bado mdogo sana kupewa madaraka na kwa vile tayari Mwamubambe alikuwa ameupindua utawala, wakahisi Mtwa Mkwawa angeweza kuuawa kwa sababu ndiye mtoto mkubwa wa Munyigumba na ndiye hasa aliyetarajiwa kutawala. Hivyo ikabidi wamkimbize kwenda kumficha Dodoma kwa Mtemi Mazengo wa Wagogo. Hii ndiyo sababu Wagogo wanawaita Wahehe wajomba zao na wanaheshimiana mno.

Mkwawa arejea hariri

Wahehe hawakufurahishwa na utawala wa Mwamubambe anayechukuliwa kama adui mkubwa zaidi katika historia ya kabila hilo kuliko hata Wajerumani. Kwa hiyo basi, wakapanga mbinu za siri kumrejesha Mtwa Mkwawa kutoka uhamishoni.

Mtwa Mkwawa, wakati huo akiwa amejifunza mbinu za juu za kivita, akaamua kurejea na kuunda jeshi lake ili kupambana na Mwamubambe.

Hata hivyo, wapiganaji wengi wa Mtwa Mkwawa waliuawa na Mwamubambe, mtu ambaye anadaiwa kuwa alikuwa akitumia zaidi mitishamba kushinda vita vingi kwa sababu hata dawa alizokuwa anatumia ndizo zilizokuwa zikitumiwa na Mtwa Munyigumba, huku Mwamubambe mwenyewe ndiye akielekezwa kuzitafuta porini.

Kutokana na wapiganaji wengi kuuawa na Mwamubambe, wapiganaji wengine walikuwa wakilia na kupiga kelele; “Hee Hee Hee! Mtwa tuisila!” wakimaanisha; “Hee Hee Hee! Mtwa tunakwisha!” Hapa hasa ndipo lilipoanza jina la kabila la Wahehe kutokana na kelele walizokuwa wakizipiga.

“Wafuasi wake walikuwa wanakufa sana. Siku moja Mkwawa akajiwa kwenye ndoto na baba yake Munyigumba ambaye alimwambia kwamba hilo jitu hawataliweza. Lilikuwa likichomwa mikuki linachomoa na kuwarushia wao na kuwaua,” anasema Malugala Mwamuyinga.

Inaelezwa kwamba, Munyigumba alipomtokea Mkwawa kwenye ndoto akamwambia, roho ya Mwamubambe iko kwenye kidole au kwenye kisigino. Hata wakifanya namna gani hawawezi kumuua. Hivyo akamtaka amtafute Mkimayena Mwakinyaga amwambie akamchome Mwamubambe kwenye kisigino au kidole.

Mwamubambe alikuwa na jeshi kubwa na wafuasi wengi wenye uwezo wa vita, Mtwa Mkwawa akalazimika kujipanga upya ili kuwapiga na kuyarejesha maeneo yote yaliyokuwa yametwaliwa na Mwamubambe.

Mapambano makali kabisa ya Mkwawa na wafuasi ya Mwamubambe yaliianzia eneo ambalo leo hii linafahamika kama Lundamatwe (Lundika Vichwa), lakini yapata kilometa mbili kutoka Barabara Kuu ya Tanzania - Zambia upande wa kusini.

Hapa palikuwa nyumbani kwa mganga Ngondo Kimamula Mbugi, pembezoni mwa Mto Ruaha. Inaelezwa kwamba, mganga huyo aliamua kuchukua jukumu la kuwaandaa wapiganaji wa Mkwawa kukabiliana na maadui zake.

Wapiganaji wa Mkwawa baada ya kuganguliwa wakaondoka kupambana na Mwamubambe na wafuasi wake ambapo waliwapiga na kuwaua zaidi ya wapiganaji 1,000.

Mwamubambe alipona mambo yamemzidia akatimua mbio, lakini wapiganaji wa Mkwawa wakaanza kumfukuza.

Kwa vile Mkwawa alikuwa ameelekezwa na baba yake ndotoni kuhusiana na Mwamubambe, akaamua kumtuma Mukimayena Mwakinyaga, ambaye alikuwa mganga wa kienyeji, ili akamuue.

Mwakinyaga akaenda na kumkuta Mwamubambe anakunywa pombe. Mbele ya umati wa watu, akamchoma mkuki kwenye kidole. Mwamubambe akadondoka chini na kuanza kutapatapa bila kukata roho.

“Mwamubambe akamuuliza Mwakinyaga, ‘Umenifanya nini?’ Mwakinyaga akasema, ‘Aah ni mikuki tu’. Basi alipoona mambo yamekuwa magumu, akamwambia, ‘Kaniitie Mkwawa aje’. Mkwawa alipofika Mwamubambe akamwambia; ‘Wakorofi kama mimi wapo wengi ndani ya utawala wako, kwa hiyo sasa ukazane’.

“Kwenye ndoto, baba yake alikuwa amemwambia Mkwawa kwamba akishafika aukite mkuki wake chini. Basi Mkwawa akaukita mkuki chini. Ndipo Mwamubambe akakata roho,” anaeleza Mwamuyinga.

Mwamuyinga anasema kwamba, kwa vile Mwamubambe alikuwa amewatesa na kuwaua Wahehe wengi, baada ya kufa ikabidi, kwa hasira, wananchi wale wamkatekate vipande vipande na kuila nyama yake ili lisiwepo kabisa kumbukumbu lake.

Baada ya hapo Mtwa Mkwawa akaendesha mapambano ya kuyakomboa maeneo yote yaliyokuwa chini ya utawala wa Munyigumba, kampeni ambayo iliendelea moja baada ya nyingine kwa mafanikio makubwa kuliko hata awali. 

Baada ya kufanikiwa kuurejesha utawala kwenye himaya yake mwaka 1890 kufuatia kumtwanga Mwamubambe Mwalunyungu aliyekuwa na walugaluga kutoka Tabora, Chifu Mkwawa aliendelea kuuimarisha utawala huo kwa ujasiri mkubwa akiwazuia Wamasai wasiende kusini pamoja na kupambana pia na biashara ya utumwa iliyokuwa ikiendeshwa na Waarabu.

Wakati huo alikuwa ameimarisha urafiki wake wa kibiashara na Waarabu katika Pwani ya Tanganyika, ambao walimpatia bunduki pekee aliyokuwa akiitumia mwenyewe.

Hata hivyo, mapambano mengine makubwa zaidi yalikuwa yanajongea ambayo yangehitaji ujasiri mkubwa kuyakabili.

Kufikia mwaka 1890 majeshi ya Ujerumani, maarufu kama Wissmanntruppe (Kikosi cha Wissmann), yalikuwa yamefanikiwa kuyashinda majeshi ya upinzani ya Abushiri na kuitwaa Pwani yote ya Tanganyika (wakati huo ikijulikana kama German East Africa). Mnamo mwezi Mei 1891 Kikosi cha Wissmann kilibadili jina na kuitwa Kaiserliche Schutztruppe na von Wissmann akastaafu kwenye jeshi hilo la Afrika akimwachia Luteni Emil von Zelewski kuliongoza.

Njia zote za misafara ya kibiashara ya pwani hazikuwa salama kutokana na kushambuliwa mara kwa mara na wapiganaji wa makabila ya maeneo hayo, hususan upande wa kusini wa koloni lao kutoka kwa makabila mashuhuri kwa vita kama Wangoni, Wagogo na Wahehe ambao walipora misafara hiyo.

Wakati huo Wahehe walikuwa wameimarisha himaya yao kutoka Iringa ilikokuwa ngome ya Chifu Mkwawa kuelekea pwani ambako Wajerumani walikuwa wameishikilia. Kutoka kwenye kabila lililotawanyika kwenye miaka ya 1850 chini ya Chifu Munyigumba, sasa Wahehe walikuwa himaya kubwa chini ya Mkwawa.

Wakati wa kiangazi cha mwaka 1891 von Zelewski aliamua kupambana na hali hiyo kwa kutumia nguvu ya jeshi kuanzia Kilwa kuelekea Bara.

Awali Emil von Zelewski alikuwa mwanajeshi wa Kikosi cha 99 cha Jeshi la Nchi Kavu cha Rhineland kabla ya kuhamishiwa kwenye Kampuni ya German East Africa mwaka 1886 na hatimaye kwenye kikosi cha Wissmanntruppe mwaka 1889. Alikuwa amefanikiwa kuongoza kikosi cha Wissmanntruppe yeye binafsi na kwa kushirikiana na vikosi vya Wissmann katika matukio mengi wakati wakipambana na Abushiri kule Pangani. Alikuwa na uzoefu wa kutosha katika vita na kiongozi makini.

Muundo wa jeshi lake hariri

Jeshi la von Zelewski lilikuwa na gadi nne ambazo kila moja ilikuwa na askari 90 walioongozwa na maofisa wa Kijerumani na NCO mmoja. Gadi moja iligeuka na kurudi na kuacha gadi tatu kukabiliana na Wahehe. Gadi namba 5 iliongozwa na Luteni von Zitzewitz akisaidiwa na von Tiedewitz, ambapo ilikuwa na askari kutoka Sudan, Gadi namba 6 iliongozwa na Luteni Tettenborn aliyesaidiwa na Feldwebel Kay na ilikuwa na Wasudani pia, wakati Gadi namba 7 iliongozwa na Luteni von Pirch akisaidiwa na Schmidt ambayo iliundwa na askari wa Kizulu.

Pia kulikuwa na kikosi cha bunduki ambacho kiliongozwa na von Heydebreck akisaidiwa na Thiedemann, Herrich na Wutzer wakati ambapo kitengo cha tiba kiliongozwa na Dk. Buschow na Hemprich.

Jeshi la von Zelewiski lililokuwa na maofisa 17 wa Kijerumani, lilikuwa na vyakula vingi pamoja na ng’ombe wao. Kulikuwa na Wapagazi 170 wa Kiafrika ambao kazi yao ilikuwa ni kubeba mizigo, punda 27, ng’ombe 20 na kondoo na mbuzi 60.

Nguo walizotakiwa kuvaa maofisa wa Kijerumani zilikuwa za khaki na kofia nyeupe ngumu (helmeti) ambazo zilikuwa zimeidhinishwa na Ofisi ya Ukoloni jijini Berlin kwa ajili ya Jeshi la Afrika Mashariki mwezi Juni 1891. Lakini nguo hizo zilifika Kilwa mwezi Julai 1891 wakati jeshi la von Zelewiski likiwa limeondoka. Kwa hiyo, von Zelewiski na maofisa wake wa Kijerumani walivaa sare za enzi za Jeshi la Wissmann zilizokuwa na michirizi ya njano mikononi. Wale askari wa Kiafrika walivaa kofia nyekundu za tarbush na sare za khaki.

Wapagazi na watu wengine kwenye msafara huo walivaa nguo kama zilizokuwa zikivaliwa na watu wa makabila mengine wakiwemo Wahehe wenyewe na hawakuwa na kofia wala viatu.

Askari walikuwa na bunduki aina ya Mauser Jägerbüchse 71 pamoja na S71 ambazo pia zilitumiwa na maofisa wadogo wa Kijerumani. Makambanda wao walikuwa na bastola kubwa aina ya 1879 Revolver. Wapiganaji wa Kiafrika wao walikuwa na silaha za jadi ikiwemo mikuki.

Vikosi hivyo, chini ya von Zelewiski, viliondoka Kilwa tarehe 22 Julai 1891 vikipitia himaya ya Ngoni Mafiti kuelekea Kisaki hadi Myombo karibu na Kilosa, ambapo viliwasili Lugalo tarehe 16 Agosti 1891. Huko njiani vikosi hivyo vilikuwa vimeteketeza vijiji kadhaa na havikukutana na upinzani mkali. Walikuwa wamewaona Wahehe wenye silaha njiani, lakini walikimbia baada ya kuwafyatulia risasi. Hali hiyo inaonekana ndiyo iliyompa ujasiri von Zelewiski wa kusonga mbele akiamini kwamba Wahehe wangelazimishwa kusalimu amri.

Jeshi la Mkwawa hariri

Mtwa Mpangile, mdogo wake Chifu Mkwawa, ndiye aliyekuwa kamanda wa jeshi la Wahehe. Ndiye aliyeongoza jeshi hilo katika vita vya Lugalo. Kama ilivyokuwa wa wapiganaji wote wa Kihehe, Mpangile alikuwa na uzoefu mkubwa wa vita ingawa ni vita dhidi ya makabila mengine, lakini si kwa jeshi imara lenye mbinu kama la Wazungu.

Tofauti na makabila mengine ya Kiafrika ambayo machifu wao ndio waliokuwa mstari wa mbele, Wahehe walikuwa na mbinu kama za Wazungu za kumwacha chifu wao nyuma akiamuru namna ya kushambulia.

Jeshi la Wahehe kwenye vita vya Lugalo lilikuwa na wapiganaji 3,000. Ndilo lililokuwa imara zaidi kulinganisha na makabila mengine yote yaliyolizunguka.

Ushindi dhidi ya makabila mengine ya jirani ulikuwa umewapa ujasiri mkubwa na uzoefu wa vita na kwa hakika walikuwa wamejitolea kuhakikisha wanapambana kufa au kupona kuhakikisha wanailinda nchi yao dhidi ya wavamizi wa kigeni.

Wengi kati ya wapiganaji wa Kihehe walikuwa na mikuki na ngao zilizotengenezwa kwa ngozi kama zile zilizokuwa zikitumiwa na Wazulu. Wengine walikuwa na mashoka.

Chifu Mkwawa alikuwa anafahamu kwamba majeshi ya Wajerumani yalikuwa yanakuja kwenye himaya yake. Taarifa zilikuwa zimemfikia mapema mno na kuifahamu mikakati yao yote. Vijana wake mashujaa waliviona vikosi vya Wajerumani wakati vikikaribia Uhehe na kupeleka taarifa za uwezo wa jeshi hilo la Wazungu, hivyo alikuwa amejiandaa kuwakabili.

Wengi wanaikumbuka Vita ya Maji Maji iliyodumu kwa miaka miwili baina ya Watanganyika na Wajerumani kati ya mwaka 1905 hadi 1907. Kinachofanya waendelee kuikumbuka ni mbinu zilizotumiwa na Mtawala wa Wangindo kule Kilwa, Kinjekitile Ngwale huko kwenye Bonde la Ngalambe alipowapaka na kuwanywesha dawa wapiganaji wake na kuwasadikisha kwamba risasi za Wajerumani zingegeuka kuwa maji.

Utaalamu huo ulisambaa karibu sehemu kubwa ya Kusini mwa Tanzania pamoja na Nyanda za Juu ambapo uliwaongezea ujasiri mkubwa wapiganaji hao waliokuwa wakiitetea ardhi yao isitawaliwe na Wazungu.

Hata hivyo, ukweli ni kwamba, Chifu Mkwawa na watemi wengine wengi wa wakati huo, pamoja na kuwa na mbinu za kupigana vita, walitumia jadi, kwa maana ya dawa za kienyeji, katika kupanga na kupambana na maadui zao.

Kama ambavyo tunaelezwa katika Biblia kwamba, Wafalme wa Israeli – tangu enzi za Nabii Musa – walikuwa wanawauliza makuhani kabla ya kupanga vita, ndivyo watawala wa Kiafrika walivyofanya nao kwa kuomba miungu yao iwasaidie, hasa wakati huo kwa vile dini ya Kikristo ilikuwa haijaenea.

Kwa kutambua mafanikio ambayo alikuwa ameyapata katika vita dhidi ya Mwamubambe Mwalunyungu na wafuasi wake, Chifu Mkwawa alimtumia pia mganga wa jadi Ngondo Kimamula Mbugi katika timu yake ya kumtabiria nini ambacho kitatokea, kama anavyoeleza kitukuu wa mganga huyo, Robert Gabriel Meza Mwaigoga.

Mwaigoga anaeleza kwamba, wapiganaji wa Chifu Mkwawa walikunywa dawa Lundamatwe, mahali palepale waliponywea kabla ya kupambana na Mwamubambe, katika eneo linaloelekea Mto Ruaha, takriban kilometa tisa hivi kutoka Lugalo ambako ndiko walikotakiwa kupambana na Wajerumani.

Chifu Mkwawa alikuwa na bunduki moja aliyopewa na Waarabu wakati ule wa biashara ya watumwa, lakini wapiganaji wake wote walikuwa na silaha za jadi kama mikuki, kombeo, pinde na mishale na mapanga.

Inaelezwa kwamba, akiwa tayari amepewa siri zote za lilivyokuwa jeshi la Wajerumani chini ya Emil von Zelewiski na silaha walizokuwa nazo, Chifu Mkwawa aliwaeleza wapiganaji wake kwamba, watajipanga vyema katika kingo za bonde ambalo Wajerumani wangepita, lakini hakuna ambaye alitakiwa kushambulia mpaka yeye atakapofyatua risasi ya kuashiria mapambano. Ngondo Kimamula Mbugi alikuwa amewapaka dawa ambazo aliwasadikisha kwamba, hakuna Mjerumani ambaye angeweza kuwaona kabla ya mapambano, na wakati huo Wahehe wangekuwa tayari wamewavamia na kuwashambulia, hivyo hata kama wangefyatua risasi zao zingetoka maji.

Sehemu waliyopita Wajerumani pale Lugalo ilikuwa nyembamba kama mkia, kukiwa na kingo kila upande, hivyo kuwawia vigumu kuweza kufanya mashambulizi ya aina yoyote. Zaidi ya hayo, msitu uliokuwepo ulitoa hifadhi nzuri kwa wapiganaji wa Chifu Mkwawa.

Kosa alilokuwa amelifanya Von Zelewiski, pamoja na uzoefu mkubwa wa vita aliokuwa nao, ni kujiamini kupita kiasi na kutotuma wapelelezi wakachunguze njia na uimara wa jeshi la Mkwawa. Aliamini kwamba, jeshi hilo lilikuwa kama yale mengine aliyoyapiga sehemu nyingine na kwamba huenda Chifu Mkwawa hakuwa na nguvu kama za Abushiri wa kule Pangani aliyepigwa mwaka mmoja nyuma.

Inasimuliwa kwamba, malengo ya Von Zelewiski yalikuwa kwenda kuivamia ngome ya Chifu Mkwawa kule Kalenga, lakini hakujua kama tayari Wahehe walikuwa wamejipanga njiani kukifanya kile ambacho hakuna aliyekitarajia.

Ili kuwazuia Wajerumani wasithubutu kufanya shambulio lolote, Wahehe ambao tayari walikuwa wanafahamu uwezo wa jeshi hilo la maadui pamoja na kulifahamu eneo lote na kupanga ni mahali gani waanze kushambulia, walipanga kuwazuia wasitumie mtindo wao wa nusu duara kushambulia. Kwa kuwa walikuwa wamepata taarifa za Wajerumani walivyopigana huko Pwani, Wahehe walikuwa wamejiandaa kuhakikisha wanakabiliana vilivyo na askari hao.

Awali Wahehe walitaka kufanya mashambulizi katika eneo la Ruaha Mbuyuni ambako Mto Ruaha unakatisha (kwa sasa ndipo ulipo mpaka wa Mkoa wa Morogoro na Iringa), lakini inaelezwa kwamba binamu wa Chifu Mkwawa aliyeitwa Kilonge, ambaye alikuwa anashughulikia masuala ya habari na ujasusi, alikuwa ameota kwamba wangeweza kushindwa.

Yeye ndiye aliyetoa ushauri kwamba mapambano hayo yakafanyike karibu na kijiji cha Lula-Lugalo, mbele ya Mto Mgella.

Mkwawa alikuwa na makamanda wenye nguvu kwenye jeshi lake kama Ngosi Ngosi Mwamugumba, Mtemimuma na kaka yake Mtwa Mpangile, ambaye baada ya kuanguka kwa Kalenga, Wajerumani walimtawaza kuwa ndiye Chifu wa Uhehe tarehe 24 Desemba 1896, lakini akanyongwa mnamo Februari 1897 kwa tuhuma kwamba alikuwa akivujisha siri na kumpa Mkwawa.

Mbali ya Wahehe, jeshi la Chifu Mkwawa lilikuwa na wapiganaji kutoka kabila la Wabena, ambao waliwekwa akiba na walikuwa wakilinda kijiji cha Lula-Lugalo ili kama Von Zelewiski angefanikiwa kupenya kwenye mtego uliowekwa na Chifu Mkwawa, basi wao waweze kupambana na jeshi lake.

Wakati Von Zelwiski na vikosi vyake walianza safari ya kuelekea Kalenga saa 12:00 alfajiri, tayari Wahehe walikuwa wamekwishajipanga katika njia ambayo waliamini ndiyo watapitia. Vikosi vya Wajerumani, kama ilivyoelezwa awali, vilipita katika mstari mmoja kutokana na mazingira ya eneo lenyewe.

Wahehe walikuwa wakisubiri tu amri ya kamanda wao, Chifu Mkwawa, ili waanze kushambulia. Majira ya saa 1:00 asubuhi, wakati Wajerumani wakipita kwenye bonde hilo, ofisa mmoja Luteni Zitewitz akaliona kundi la ndege na kufyatua risasi kwa lengo la kupata kitoweo. Mlio huo wa risasi ukaonekana kama ishara ya kuanza mashambulizi. Baadaye milio mitano au kumi ya bunduki aina ya Shenzi ikasikika. Wahehe nao wakadhani kwamba ndiyo ishara ya wao kuanza mashambulizi wakati vikosi vya Wajerumani havijafika kwenye eneo walilopanga kushambulia. Mamia ya askari wa Kihehe wakavamia kwenye kilima hicho na kuanza kuwashambulia Wajerumani waliokuwa wakipita bondeni, wakipiga kelele zao za vita “Hee hee Twahumite! Hee Heeee!” (yaani “Hee Heee Tumetoka! Hee Heeee!”).

Askari wengi wa Wajerumani walikuwa wanatembea bila kuzikoki bunduki zao na hawakuwa na muda wa kuzikoki, achilia mbali kutengeneza mfumo wa kujitetea kabla ya kushuhudia Wahehe wamewavamia. Muundo wa bunduki aina ya Mauser M71 iliyotengenezwa mwaka 1887 haukuwa unaeleweka vyema kwa askari wengi na walitumia dakika kadhaa kabla ya kuanza kufyatua risasi. Kelele ziliposikika wapagazi wote wakakimbia. Punda waliokuwa wamebeba silaha wakaingia katika Kikosi Namba 5 ambapo askari wengi Wasudani wakaanza kukimbia kuokoa maisha yao.

Hadi wakati huo, tayari von Heydebreck – mmoja wa manusura katika vita hivyo – alikuwa amekwishajeruhiwa na kuanguka akiwa amepoteza fahamu, lakini baadaye aliandika kwenye ripoti yake: “…Mfululizo wa matukio hadi wakati huu ulikuwa umetumia dakika mbili au tatu tu. Nilitambua hilo kabla ya kujeruhiwa, Wasudani tayari walikuwa wamekimbia kurudi nyuma vichakani baada ya kufyatua risasi mara mbili hivi. Mimi na askari wa Kikosi cha Tano tulilazimika kujilinda na kujitetea baada ya kuona Wahehe wakija katika umbali wa hatua 30. Kama sikosei, nilimsikia Sajini Tiedemann akisema alikuwa ameumia kabla hajafyatua risasi. Haikuwa rahisi kuona zaidi ya umbali wa hatua tano msituni kutoka pale njiani. Pia hakuna ambaye aliweza kunusurika kwa sababu Wahehe walikuja kwa kasi… Ni wazi walipanga kutushambulia baada ya kufika katikati msitu. Kuvurugika kwa mipango yao kulichangiwa hasa na kitendo cha Luteni von Zitewitz kufyatua risasi…”

Mwanzilishi wa Himaya ya Ujerumani Afrika Mashariki, Carl Peters, baadaye tarehe 23 Novemba 1891 alimwandikia Gavana von Soden akisema kwamba, katika mapambano mengine na makabila mbalimbali ya Tanganyika, ilikuwa ni bahati tu kwao kutoweza kupata madhara kama waliyopata Wajerumani pale Lugalo, kwani mafunzo yao ya vita yalikuwa yanalenga zaidi kupigana wakiwa wamejipanga pamoja kwa mbinu maalumu. Hawakuwa wamejifunza kupigana kila mtu kwa uwezo wake, bali walitegemea zaidi kushambulia kwa pamoja.

Iliwachukua Wahehe dakika 15 tu (kuanzia saa 1:15 hadi 1:30 asubuhi) kuwafyeka Wajerumani na majeshi yao. Von Zelewiski aliuawa kwa kupigwa nyundo kichwani akiwa amepanda punda wake wakati akijiandaa kuwafyatulia risasi wapiganaji wa Mkwawa. Kabla hajadondoka akachomwa mkuki ubavuni.

Hii ndiyo asili hasa ya jina la ‘Nyundo’ kutokana na kamanda huyo wa Wajerumani kuuawa kwa nyundo!

Kuhusiana na kifo cha Kamanda von Zelewiski, kama Mjerumani Tom von Prince alivyoandika baadaye, “Kama nilivyosimuliwa baadaye… na Wahehe walioshuhudia, alijitetea mwenyewe kwa kutumia bastola yake kubwa na kuwapiga risasi watu watatu, wakati kijana mmoja wa Kkihehe alipomchoma na mkuki ubavuni. Kijana huyo alikuwa na umri wa miaka 16 tu na alizawadiwa ng’ombe watatu na Mkwawa kwa kitendo hicho.”

Luteni von Pirch na Dk. Buschow pia waliuawa wakiwa juu wa punda wao ambapo majeraha yao yalikuwa makubwa mno. Karibu askari wote wa Kikosi cha 7, Kikosi cha Silaha, Kikosi cha 5 na baadhi ya askari wa Kikosi cha 6 waliuawa kabla hata hawajajua wafanye nini.

Luteni von Heydebreck, Luteni Usu Wutzer na Murgan Effendi pamoja na askari 20 hivi ndio waliofanikiwa kukimbia kutoka eneo hilo la mapigano na kukimbilia upande mwingine wa mlima na kuweka ngome wakijilinda dhidi ya mashambulizi ya Wahehe. Wapiganaji hao wa wajerumani walijificha kwenye pagala moja la tembe lililokuwa limetelekezwa mlimani. Askari mmoja Msudani ndiye aliyekiona kibanda hicho.

Lakini von Heydebreck aliishuhudia vita hiyo katika kipindi cha dakika mbili au tatu tu kabla ya kupoteza fahamu. “Kulingana na ushuhuda wa Wahehe walioshiriki mapigano yale, vita hivyo havikumalizika mapema kama ambavyo Wazungu wa mstari wa nyuma walivyotegemea, badala yake askari walionusurika waliendelea kupambana hadi saa 4:30 asubuhi na kuwaua maadui wengi (Wahehe).”

Askari wa mwisho wa kikosi cha Luteni von Tettenborn ndio hawakupata madhara makubwa ya mashambulizi ya Wahehe, washukuru kutokana na makosa ya ishara, vinginevyo wote wangeangamia katika kipindi hicho cha dakika 15 tu. Von Tettenborn, Feldwebel Kay na askari kama 20 hivi Wasudani wakahamia upande wa kushoto wa eneo la mapigano na kutengeneza nusu duara kwa ajili ya mashambulizi huku wakiwa wameumia. Wakiwa hapo walipandisha bendera ya Ujerumani juu ya mti na kupiga mbinja ili kuwaita manusura wengine.

Wakati huo Wahehe waliendelea kuwakimbiza manusura na kushambulia kila waliyemuona mbele yao. Mkanganyiko ukaongezeka baada ya kuwasha nyasi.

Mnamo saa 2:30 asubuhi hiyo, Luteni von Heydebreck, Luteni Usu Wutzer na Murgan Effendi wakiwa na askari wao 12 walipenya na kuungana na kikosi cha von Tettenborn. Von Heydebreck alikuwa anavuja sana damu kutokana na majeraha mawili makubwa ya mikuki. Kwa kuwatazama tu watu hao, von Tettenborn akatambua kwamba vikosi vyao vyote vilikuwa vimesambaratishwa na kikosi cha silaha kutekwa, ambapo Mkwawa aliteka bunduki 300. Askari wa jeshi la Wajerumani waliouawa siku hiyo walikuwa zaidi ya 500.

Ilipofika saa 3:00 Luteni Usu Thiedemann, akiwa na majeraha makubwa ya moto aliingizwa kwenye kikosi cha Luteni von Tettenborn akiwa amebebwa na askari waliokuwa wanafanya doria. Nyasi zilizokuwa zinaungua sasa zilimtisha von Tettenborn na manusura wengine.

Hadi kufikia saa 10:00 jioni Luteni von Tettenborn alikuwa amewakusanya majeruhi wengi na kuokota baadhi ya mizigo yao. Wahehe waliokuwa wamepagawa kwa hasira pamoja na moto mkubwa uliokuwa ukiendelea kuteketeza msitu viliifanya kazi ya kuwatafuta majeruhi wengine kuwa ngumu, hivyo wengi waliteketea kwa moto. Von Tettenborn akaamua kuanza kurudi nyuma kabla hajazuiwa na Wahehe.

Wakati wa usiku wa manane kikosi kilichokuwa na Luteni von Tettenborn kikapiga kambi ng’ambo ya pili ya mto tofauti na mahali walipolala kabla ya kuanza mapambano. Kikosi chake sasa kilikuwa na yeye mwenyewe na Luteni von Heydebreck, ma-NCO watatu wa Kijerumani (ingawa Luteni Usu Thiedemann alikufa baadaye njiani), maofisa wawili wa Kiafrika, ma-NCO 62 wa Kiafrika, wapagazi 74 na punda 7. Kutoka hapo wakaanza kutembea hasa nyakati za usiku kurudi nyuma ambapo walifika Myombo tarehe 29 Agosti.

Baada ya ushindi wa Lugalo, Chifu Mkwawa hakutulia, bali aliendelea kuimarisha himaya yake pamoja na jeshi lake. Lakini pia kipindi hicho Wajerumani nao walikuwa wakipanga mikakati ya namna ya kuisambaratisha himaya hiyo.

Kitendo cha kupigwa kwa jeshi lao imara lenye silaha kali, tena na wapiganaji wenye mikuki na mishale tu, kiliichanganya Berlin kwa sababu hakikuwahi kutokea hapo kabla. Hivyo Gavana Julius Freiherr von Soden aliyekuwa anaongoza koloni hilo la Afrika Mashariki alikuwa katika presha kubwa kutoka kwa wakubwa wake kuhusiana na namna atakavyomshinda Mkwawa.

Gavana huyo alijitahidi kukabiliana na presha ya Wahehe waliokuwa wakivamia misafara yake hadi miaka miwili baadaye alipoondoka nchini. Wajerumani walikuwa na mbinu ya kuidhoofisha himaya ya Wahehe kwa mazungumzo, si kwa vita, kwa sababu walitambua kwamba hiyo ingeweza kuwagharimu tena.

Historia inaeleza kwamba, uamuzi wa Von Soden wa kutotumia jeshi kupambana na Mkwawa ulimfanya aonekane gavana bomu kati ya magavana wote walioongoza koloni hilo, lakini hiyo ilitokana na historia yake. Yeye ndiye alikuwa gavana pekee aliyetokea uraiani, kwani aliyemtangulia von Wissmann na wafuasi wake wa baadaye walikuwa makamanda wa jeshi.

Katika kipindi hicho cha Von Soden, Mkwawa naye alifanya majaribio kadhaa ya mazungumzo na Wajerumani akituma ujumbe wake Dar es Salaam. Mazungumzo hayo yalichukua muda wa miezi kadhaa kupitia kwa wawakilishi wake, lakini hayakuwa na mafanikio kwa sababu watawala wa Kijerumani walikuwa na mashaka na msimamo wa Mtawala huyo wa Wahehe kwamba ataweza kuwabadilikia. Kwa kifupi, hawakumwamini.

Pamoja na Von Soden kuwa na nia njema ya kufanya mapatano, maofisa wengine wa Kijerumani walikuwa na mawazo kwamba hakukuwa na haja yoyote ya kufanya mazungumzo na mtawala wa Kiafrika ambaye alikuwa ameidhalilisha Ujerumani kama alivyofanya Mkwawa.

Luteni Tom von Prince (Kapteni baada ya kuiangusha Kalenga) aliwahi kusema: “Tangu kuangushwa kwa kikosi cha Zelewski, hasa nikiwa askari wa jeshi lile la zamani, haja yangu kubwa ilikuwa kulipa kisasi kwa kudhalilishwa kwa jeshi letu, na tangu hapo nikaweka mkakati, sikuhitaji kuingia kwenye vita yoyote, sikufanya chochote ambacho kingeweza kuingilia kati mpango huu.”

Wajerumani wakati huo walikuwa na mashaka kwamba watawala wa Kiafrika, hususan Mkwawa, walikuwa wameanza kuonyesha upinzani wa wazi, hasa Mtemi Isike wa Tabora na Mbunga wa Ungoni ambao himaya zao zilipakana na Uhehe. Chifu mmoja wa Usagara aliwahi kutamka wazi, “Watu hawa (Wahehe) ndio pekee walioweza kuoga mchanga wa damu ya Mzungu ambao ‘bomba zao za moto’ ziliwafanya wengi washindwe kujitetea. Na kweli, vijiji vingi vilivyokuwa jirani na boma la Wajerumani viliendelea kutoa msaada kwa Mkwawa na Himaya yote ya Uhehe mpaka pale Kalenga ilipoangushwa.

Sababu za Mkwawa kutochukua uamuzi wa kuwafukuzia Wajerumani baada ya vita vya Lugalo zinatajwa kuwa nyingi, ingawa kubwa zaidi, kwa mujibu wa waandishi wa zamani wa historia Erick Mann, Alison Redmayne, na wengineo, ilikuwa ni kupoteza askari wake wengi. Vikosi vya Mkwawa havikuwahi kuvamia eneo lililokuwa likikaliwa na Wajerumani. Katika vita vya Lugalo, Mkwawa alipompoteza makamu kiongozi wa Kalenga, Ngosi Ngosi Mwamugumba.

Pia inaonekana kwamba, Mkwawa alitegemea mazungumzo ya amani dhidi ya Isike wa Wanyamwezi, Chifu Songea wa Wangoni, na Mbunga wa Wandebele na wengineo yangeweza kuweka umoja na kuwapiga Wazungu. Kwa maana nyingine, Mkwawa ndiye mtu pekee aliyeanzisha umoja ambao leo hii tunajivunia na kama machifu wenzake wangetambua azma hiyo, pengine Wajerumani wangeweza kuondolewa kwa nguvu hata kabla ya jaribio la Vita vya Maji Maji vya mwaka 1905 hadi 1907. Kama mpango wa Mkwawa ungefanikiwa, Wajerumani wangepigwa kuanzia Tabora hadi Songea, ambapo ungeligawa koloni hilo katikati.

Mbali ya mkakati huo mkubwa, Wahehe walilazimika kupambana na Wajerumani ambao walikuwa wamejitanua kutoka kaskazini hadi mashariki: kasi ya kuongezeka kwa Avadaliki (kama Wajerumani walivyokuwa wakiitwa na Wahehe) ilimaanisha kwamba Wahehe wangeweza kuzuiwa kwenye msafara wa wafanyabiashara kutoka Bagamoyo hadi Tabora.

Ili kudumisha fursa ya uchumi, na hatimaye heshima ya utawala, Wahehe wakaendelea kuvamia misafara hiyo. Miongo kadhaa nyuma, juhudi zao za kuvamia misafara hiyo zilikuwa zimelenga kuteka watumwa, fedha, silaha, na kudumisha hadhi yao. Kwa ujumla, himaya hiyo kubwa ilikuwa imefanya uvamizi wa misafara kama ndiyo njia yao kuu ya uchumi ambayo watawala wa kigeni walikuwa wakiitegemea.

Taarifa zinasema kwamba, Mkwawa pia alikuwa na hofu ya uasi ndani ya jeshi lake. Wakati ambapo Vita vya Lugalo vilikuwa vimewafanya Wakinga, Wasagara, Wabena na makabila mengine kuwa ‘watwana’ na kwamba Wahehe ndio waliokuwa na sauti zaidi, lakini kwa kuangalia hali ya baadaye, kuendelea kuwepo kwa kambi za Wajerumani katika maeneo ambayo awali yalitambuliwa kwamba ya Wahehe yaliwapa fursa makabila hayo kuasi, japo si moja kwa moja, huku wakimwita Mkwawa ‘chinja chinja’.

Wajerumani sasa walionekana wema kuliko Mkwawa, na Wasagara pamoja na makabila mengine ambayo yalikuwa yakinyanyaswa na Wahehe waliona kwamba Wazungu hao ndio kimbilio lao na wangeweza kuwatetea.

Hivyo mpango wa Wajerumani wa kumtia Nguvuni Mkwawa ulizidi kuwa na Nguvu, ambapo makabila Baadhi ya Waafrika yalishiriki vyema katika kutoa ushirikiano Kwa Wajerumani ili kufanikisha kifo chake.

Viungo vya nje hariri

  Makala hii kuhusu utamaduni wa Tanzania bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Wahehe kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
  1. "URITHI WETU: Hawa ndio Wahehe na chimbuko lao-1". Mwananchi (kwa Kiingereza). 2021-12-29. Iliwekwa mnamo 2024-01-13.