Kuhusu matumizi ya jina Zohali kwa sayari hii tazama kipengele cha "Jina"

Uranus, bangili na miezi yake

Uranus (alama: ⛢) ni sayari ya saba kutoka jua letu.

Tabia

Ni sayari kubwa ya tatu ya mfumo wa jua hata kama mada yake ni hasa gesi iliyoganda. Jumla ya masi yake ni mara 14 ya dunia hivyo ni sayari nyepesi kulingana na ukubwa wake. Kipenyo chake ni takriban kilomita 50,000[1].

Inazunguka Jua kwenye obiti inayochukua miaka 84. Umbali wake na Jua ni takriban mara 19 umbali wa Jua na Dunia au kilomita bilioni 2.9; afeli yake ni vizio astronomia 20.11 na periheli yake ni vizio astronomia 18.33.

Hadi mwaka 2020 miezi 27 iligunduliwa. Miezi mikubwa huitwa Miranda, Ariel, Umbriel, Titania na Oberon. Ina pia pete kadhaa yaani mawingu ya vumbi, barafu na mawe madogo ambayo ni nyembamba na kuzunguka sayari kwa umbo la pete. Pete za Uranus ni hafifu kuliko zile za Zohali.

Uranus inaonekana kama nyota hafifu sana yenye mwangaza wa mag 5.6-6. Kutokana na kuwa hafifu vile na mwendo wake wa pole hakuna utamaduni wowote wa kale ulioitambua kuwa sayari. Ilitambuliwa mara ya kwanza kuwa sayari na tarehe 13 Machi 1781 na William Herschel.

Jina

Waswahili wa kale hawakujua sayari hii. Uranus ni jina la kimataifa lililoteuliwa katika karne ya 19 baada ya majadiliano marefu kati ya wanaastronomia wa Ulaya. Ni jina la mungu wa Ugiriki ya Kale Urano (Οὐρανός) aliyeaminiwa kuwa mungu wa anga. Lugha nyingi duniani zimepokea jina hili kwa sababu astronomia ya zamani haikujua sayari hii.

Vitabu kadhaa vinatumia jina la Kiswahili Zohali[2][3][4] kwa kufuata kamusi ya KAST; lakini hili ni jina la Kiswahili kwa sayari ya sita (ing. "Saturn").[5]

Tazama pia

Marejeo

  1. Uranus - by the numbers, tovuti ya NASA, iliangaliwa Januari 2021
  2. Wallah, W.B. & Mwamburi, J. Kiswahili mufti darasa la 8: Mwongozo wa mwalimu. Longhorn, 2009. ISBN 99966491066
  3. TESSA - Teacher Education in Sub Saharan Africa. Nishati na Mwendo: Kutoka Ardhini kenda kwenye nyota – kutumia Zana Kifani Archived 9 Aprili 2016 at the Wayback Machine.. Available at: www.tessafrica.net
  4. Waweru, M.; Makombo, H; Vonuoli, A.; Kashihiri, C.; Mwayani, J.Hutua za Kiswahili: Masomo ya Msingi 8. East African Educational Publishers ltd., 1ed, 290p., 2005. ISBN 9966-25-403-X
  5. KAST ni kamusi ya pekee inayotumia "Zohali" kwa sayari hii. Kamusi za KKK/ESD ya TUKI na M-J SES zinaonyesha "Zohali" kwa sayari ya sita na "Uranus" kwa sayari hii. Linganisha ukurasa wa Majadiliano:Sayari
  Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Uranus kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.