Afeli (kutoka Kiing. aphelion) ni mahali katika obiti ya sayari au magimba mengine ya angani ambako yako mbali zaidi na Jua. Jina linatokana na Kigiriki από "apo" (mbali) na Ήλιο "helio" (jua).

1. Sayari kwenye afeli yake 2. Sayari kwenye periheli yake 3. Jua

Kinyume chake ni periheli inayomaanisha sehemu ya njiamzingo iliyo karibu kabisa na jua.

Majina hayo hutumiwa kwa sababu obiti au njiamzingo ya Dunia si duara kamili, bali lina umbo la duaradufu. Yasingekuwa na maana kama njiamzingo ingekuwa duara kamili lakini hii haitokei hali halisi.

Afeli ya Dunia

Afeli ya Dunia ina umbali wa kilomita milioni 152.1 kutoka Jua, ilhali periheli ina umbali wa kilomita 147.1. Umbali wa wastani ni kilomita milioni 149.6, kwa hiyo umbali kati ya Jua na Dunia inacheza kidogo katika muda wa mwaka. Wakati wa kukaa mbali zaidi mnururisho tunaoupokea kutoka Jua unapungua kidogo, kama asilimia 2.

Lakini tofauti hiyo hatuwezi kuisikia kwa sababu majira ya baridi na ya joto yanatawaliwa na athira nyingine, hasa na mwinamo wa mhimili wa Dunia. Mwinamo huo unasababisha sehemu za kaskazini na za kusini za Dunia kupokea viwango tofauti vya mwanga kutoka Jua katika mwendo wa mwaka. Afeli ya Dunia hutokea takriban tarehe 5 Julai. Majira ya joto kwenye kaskazini ya Dunia yanatokea takriban wakati wa afeli na majira ya joto kwenye kusini ya Dunia hutokea takriban wakati wa periheli.

Umbali wa sayari na sayari kibete kadhaa kutoka Jua kwa vizio astronomia na kilomita (umbali wakati wa afeli na periheli)
Sayari
(kibete)
Periheli Afeli Tofauti na
duara
Vizio astronomia kilomita
milioni
Vizio astronomia kilomita
milioni
.
Utaridi (Mercury) 0.307 46.0 0.467 69.8 0.20564
Zuhura (Venus) 0.718 107.5 0.728 108.9 0.00678
Dunia (Earth) 0.983 147.1 1.017 152.1 0.01671
Mirihi (Mars) 1.381 206.7 1.666 249.2 0.09339
Mshtarii (Jupiter) 4.951 740.7 5.455 816.0 0.04839
Zohali (Saturn) 9.023 1,349.8 10.050 1,503.5 0.05386
Uranus 18.282 2,735.0 20.096 3,006.3 0.04726
Neptun 29.812 4,459.8 30.328 4,537.0 0.00859
Pluto 29.658 4,436.8 49.306 7,376.1 0.24883
Haumea 34.477 5,157.6 51.514 7,706.4 0.19813
Makemake 37.915 5,671.9 52.773 7,894.8 0.16384
Eris 38.542 5,765.7 97.558 14,594.5 0.43363
Sayari kibete huonyeshwa kwa rangi  kijivu 

Tazama pia

  • Periheli (sehemu ya karibu kwenye obiti ya kuzunguka dunia)