Kizio astronomia
Kizio astronomia (ing. astronomical unit, kifupi "au"[1]) ni kipimo cha umbali katika elimuanga. Kinalingana na umbali wa wastani kati ya dunia na jua.
Urefu wake ni mita 149,597,870,691[2] au kwa kifupi takriban kilomita milioni 150. Umbali huu ni sawa na wastani wa umbali kutoka kitovu cha Dunia hadi kitovu cha Jua.
Vipimo vilivyo kawaida duniani kama kilomita vinaweza kutumiwa katika astronomia lakini vinaleta namba kubwa mno. Hivyo astronomia imebuni vipimo vyake vinavyorahisisha kutaja umbali wa magimba katika anga-nje. Mara nyingi astronomia hutumia kipimo cha mwakanuru kwa kupima umbali katika ulimwengu. Lakini kwa umbali za karibu zaidi jinsi ilivyo ndani ya mfumo wa Jua letu kizio astronomia kimechaguliwa.
63,241.077 vizio astronomia vinafanya mwakanuru 1.
Jina la sayari / gimba | Umbali hadi jua kwa vizio astronomia |
---|---|
Utaridi (Mercury) | 0.39 |
Zuhura (Venus) | 0.72 |
Dunia | 1 |
Mirihi (Mars) | 1.52 |
Mshtarii (Jupiter) | 5.2 |
Zohari (Saturn) | 9.58 |
Uranus | 19.23 |
Neptuni | 30 |
Ukanda wa Kuiper | kuanzia 30 |
Pluto | 39 |
Chombo cha angani kilichofika mbali hadi sasa ni "Voyager 1". Mwaka 2019 kilipita vizio astronomia 145 kutoka Jua, nje ya obiti ya Pluto na ukanda wa Kuiper.
Tanbihi
- ↑ Resolution B2 on the re-definition of the astronomical unit of length, mkutano mkuu wa UKIA 2012
- ↑ Resolution B2 on the re-definition of the astronomical unit of length, mkutano mkuu wa UKIA 2012
Viungo vya Nje
- Measuring the universe, tovuti ya UKIA, iliangaliwa Novemba 2017