Mwezi
Mwezi (alama: ) ni gimba la angani linalozunguka sayari, sayari kibete au asteroidi fulani. Kuna miezi mingi katika anga-nje. Vipindi vya kuonekana kwa mwezi wa Dunia vilisababisha matumizi ya "mwezi" kama majira ya wakati.
Mabadiliko ya kuonekana kwake yalisababisha katika Kiswahili neno "mwezi" litumike kama kipindi cha wakati. Awamu zake nne pengine ndizo chanzo cha majuma ya siku sabasaba.
Miezi ya sayari na sayari kibete
haririSayari inaweza kukosa mwezi au kuwa na miezi mingi. Mshtarii na Zohali ina miezi zaidi ya 80, mingine mikubwa kama sayari ndogo, mingine midogo yenye kipenyo cha km 1 tu. Dunia yetu ina mwezi mmoja tu. Utaridi haina mwezi.
Mwezi hauna nuru ya kwake yenyewe bali unang'aa kutokana na nuru ya jua inayoakisiwa usoni mwake kama kwenye kioo.
Sayari na sayari kibete zenye miezi katika mfumo wa jua:
- Dunia: mwezi 1
- Mirihi: miezi 2
- Mshtarii: miezi 95
- Zohali: miezi 146
- Uranus: miezi 28
- Neptun: miezi 16
- Orkus: mwezi 1
- Pluto: miezi 5
- Haumea: miezi 2
- Kwaoar: mwezi 1
- Makemake: mwezi 1
- Gongong': mwezi 1
- Eris: mwezi 1
Sayari na sayari kibete zisizo na miezi katika mfumo wa jua:
Mwezi wa Dunia yetu
haririMwezi wa dunia yetu ni kati ya miezi mikubwa kwenye mfumo wa Jua. Hakuna jina tofauti kuliko "Mwezi" isipokuwa watu wametumia pia jina la Kilatini "Luna" wakitaja Mwezi wetu ili kuutofautisha na miezi ya sayari nyingine. Katika Wikipedia hi tunajitahidi kuandika "Mwezi" kwa gimba linalozunguka Dunia na "mwezi" kama habari inahusu sayari nyingine.
Mwezi wetu huwa na umbo la tufe lakini si tufe kamili. Kipenyo cha wastani ni kilomita 3,476 ambacho ni takribani robo ya kipenyo cha Dunia. Mwezi unazunguka dunia yetu kwenye obiti chenye umbo la duaradufu. Umbali wake na Dunia ni baina ya kilomita 363,300 hadi 405,500 kutoka Dunia.
Huwa tunaangalia uso wake upande mmoja, tena uleule tu. Sababu yake ni ya kwamba mzunguko wa Mwezi kwenye mhimili wake ni sawa na kipindi cha obiti ya kuzunguka Dunia mara moja. Kipindi cha obiti yake ni siku 27 , masaa 7, dakika 43 na sekunde 11.5. Upande wa nyuma wa Mwezi uko gizani wakati sisi tunaona mwezi mpevu. Wakati wa mwezi mwandamo kwetu upande wa nyuma unapokea nuru ya Jua. .
Nuru ya Mwezi hautoki kwake bali ni nuru ya jua inayoakisiwa na uso wake.
Uso wa Mwezi unajaa mashimo ya kasoko yaliyosababishwa kwa kugongwa na meteoridi. Mwezi hauna angahewa inayozuia mapigo ya meteoridi ndogo au kupunguzu nguvu yao jinsi ilivyo duniani.
Mwezi kama kipimo cha wakati
haririUso wa mwezi jinsi unavyoonekana duniani hubadilikabadilika. Mwezi mpevu unaonekana kama duara kamili la kung'aa lakini baada ya kuonekana hivi umbo linapungua kila siku hadi kutoonekana kabisa na hali hii huitwa mwezi mwandamo. Baadaye mwezi unaonekana tena kama hilali nyembamba na kuongezeka hadi kuwa duara tena. Muda wa mabadiliko yote kupita mara moja ni siku 29 na robo.
Muda wa mabadiliko kati ya mwezi mwandamo hadi kupotea na kuwa mwezi mwandamo tena ni kati ya siku 28 hadi 29. Kipindi hiki kinakumbukwa kirahisi kinaonekana kwa watu wote.Hivyo muda wa kurudi kwa Mwezi ulikuwa kati ya vipimo vya kwanza vya wakati kwa binadamu pamoja na kipindi cha siku.
Inawezekana kipimo cha siku saba katika juma kilianza kwa kuzingatia robo 4 za mwezi wenye siku 28.
Awamu za mwezi zilikuwa vipindi vya kuhesabu wakati tangu mwanzo wa kalenda. Hadi leo kuna kalenda ya mwezi ambayo ni kalenda ya Kiislamu. Inapanga wakati kutokana na hali halisi ya awamu za mwezi.
Safari kwenda mwezini
haririMwezi wetu ni gimba la angani la kwanza ambako wanadamu wamefika. Tarehe 21 Julai 1969 mwanaanga Mmarekani Neil Armstrong alikuwa mtu wa kwanza wa kukanyaga uso wa mwezi. Wanaanga wengine 11 kutoka Marekani waliendelea kufika mwezini hadi mwaka 1972.Baadaye safari za kwenda mwezini hazikufanywa tena kutokana na gharama kubwa.
Mwezi mali ya watu?
haririHata kama Warusi na Wamarekani walifikisha bendera zao mwezini, hawadai kuwa na mali huko. Katika mkataba kuhusu anga-nje nchi 192 za Dunia zimekubaliana kuwa Mwezi utaangaliwa sawa na maeneo ya kimataifa ya bahari. Walikubaliana kuwa ni marufuku kupeleka silaha kali kama za nyuklia angani. Mataifa mengi ya Dunia yametia sahihi mkataba huo, isipokuwa nchi chache hususan za Afrika ikiwemo Tanzania.
Lakini kuna watu binafsi wanaodai kuwa na mali kwenye Mwezi. Tangu mwaka 1980 yupo Mwamerika mmoja aliyefaulu kuandikisha Mwezi kwa jina lake kwenye ofisi ya msajili wa viwanda mjini San Francisco akiendelea kuuza hati za kumiliki maeneo mwezini. Kuna pia familia moja pale Ujerumani iliyorithi hati ambako mfalme wa Prussia kwenye mwaka 1756 alitoa zawadi ya Mwezi kwa mzee wao. Taasisi ya Sheria ya Anga-Nje (International Institute of Space Law) ilitoa tamko kuwa madai haya hayana msingi wa kisheria [2].
Vyanzo
hariri- ↑ ["http://solarsystem.nasa.gov/planets/profile.cfm?Object=Moon" ""NASA Solar System Exploration: Planets""]. NASA. Iliwekwa mnamo 2010-10-01.
{{cite web}}
: Check|url=
value (help) - ↑ Statement by the Board of Directors of the International Institute of Space Law (IISL) on Claims to Property Rights Regarding the Moon and Other Celestial Bodies Ilihifadhiwa 22 Desemba 2009 kwenye Wayback Machine., International Institute of Space Law. 2004
Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Mwezi kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |