Wanilamba

(Elekezwa kutoka Wanyiramba)

Wanilamba (au Wanyiramba) ni kabila la watu wa Tanzania wanaoishi mpakani mwa mikoa ya Singida na Shinyanga. Vijiji vya mpakani mwa Tabora wanapopatikana ni: Shelui, Mgongo, Nkonkilangi, Nsunsui, Mingela na Dolomoni.

Lugha yao ni Kinilamba.

Asili hariri

Kama ilivyo kwa jamii zingine za Kibantu barani Afrika ambao walihamia Mashariki na Kusini mwa Afrika wakitokea Afrika Magharibi, hususani nchi za Kameruni, Naijeria na Ghana wakipita misitu ya Kongo, Wanyiramba na Wanyisanzu walikuwa katika kundi mojawapo lililoelekea mashariki hadi maeneo ya Ziwa Nyanza (Victoria) hadi katika kisiwa cha Ukerewe kilichopo katika ziwa hilo kubwa zaidi barani Afrika.

Japo haijulikani sababu hasa, kundi moja liliondoka katika kisiwa cha Ukerewe hadi kisiwa cha Uzinza na kutoka huko wakahama hadi maeneo ya Tabora ambako waligawanyika, kundi moja likielekea kusini na inasemekana ndio waliokuja kuwa Wagogo na baadhi ya Wanyaturu (Wanyaturu wa Kibantu, yaani wasio na asili ya Kikushi, maana kuna Wanyaturu wa Kibantu na wale wa asili ya Kikushi wa kutoka Ethiopia), huku kundi lingine likiendelea kuelekea mashariki kupitia mlima Sekenke hadi Kisiriri.

Walipoanza kuitwa Wanyiramba na Wanyisanzu/Waihanzu hariri

Wakaishi hapo Kisiriri kwa muda mrefu kabla ya kutokea ukame mkubwa sana uliosababisha njaa katika eneo hilo. Ili kukabiliana na tatizo hilo la njaa, watu hao walitumia mboga za majani zaaina ya mlenda uliokaushwa zijulikanazo kama "ndalu" kama chakula kikuu. Kutokana na kula "ndalu" kwa mtindo wa kulamba, watu wa makabila mengine ya kibantu walivyowaona wakawaita "wenye kulamba" na baadaye likabadilika hadi kuwa "wenyilamba" hadi "Wanyiramba". Ikumbukwe kuwa hadi hapo Wanyisanzu na Wanyiramba walikuwa kabila moja na wote walifahamika kama Wanyiramba baada ya njaa hiyo.

Wanyisanzu/Waihanzu wahamia pori la Mkalama hariri

Kundi moja likaamua kuondoka hapo Kisiriri hadi pori la Mkalama wakiwa na mifugo yao na familia zao na walipofika katika pori hilo ili kujilinda na wanyama wakali wakajenga nyumba na kuzungushia maboma ya miba maarufu kama "masanzu/mahanzu". Baadaye baadhi ya Wanyiramba waliobaki Kisiriri nao waliamua kuondoka hapo na walipofika Mkalama wakawakuta wenzao wamezungushia nyumba zao kwa Maboma ya "masanzu/mahanzu" ndipo walipoanza kuwaita hawa ni wanyisanzu au waihanzu.

Wanyiramba na Wanyisanzu japo wana historia inayofanana na kwa mtu mgeni anaweza kudhani kuwa hakuna tofauti baina yao, lakini ukweli ni kuwa kuna tofauti kubwa sana baina yao.

Koo zao na wanapopatikana hariri

Wanyiramba: Hizi ni koo tano za Wanyiramba na wanapopatikana

 • Kinampanda: Wanaishi sehemu za milimani hasa huko Kinampanda
 • Anagimbu: Wapo Iramba Mashariki
 • Waiambi/waiyambi: Wanaishi Nkungi na Iambi
 • Anishai: Wanapatikana Kinandili na
 • Akimbu: Hawa wapo mpakani mwa Iramba na Tabora

Kwa upande wa Wanyisanzu, wao wana koo nne tu

 • Mnyakilumi: Wapo maeneo ya Kilumi/Kirumi
 • Mnyatumbili: Wanaishi Ikolo
 • Mnyadintima: Hawa wanapatikana Mwangeza na
 • Mnyasoha: Waishio Mkalama

Vyakula wanavyopenda Wanyiramba hariri

 1. Ugali wa uwele, mahindi ya kupikwa na kuchoma, maboga
 2. Mboga (ndalu/nswalu, muzuo, nsonga, matembele, mung'ang'i, kinsagi, ulyoze, mrenda/kyuluga, nyama/nama, majokolo)
 3. Vinywaji (togwaa, pombe/magai mantulu)
  Makala hii kuhusu utamaduni wa Tanzania bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Wanilamba kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.