Wagogo (mmojawao anaitwa Mgogo) ni kabila kubwa la Tanzania ya kati, wenyeji wa mikoa ya Dodoma na Singida. Wanakadiriwa kuwa zaidi ya 1,500,000.

Wagogo (1906)

Lugha yao ni Cigogo (kwa Kiswahili hutamkika Kigogo).

Dini ya wengi wao ni Ukristo, hasa wa madhehebu ya Anglikana, halafu wa Kanisa Katoliki.

Historia na maendeleo ya Wagogo viliathiriwa sana na ukame na biashara ya watumwa, kiasi kwamba hata leo ni kati ya makabila fukara zaidi nchini Tanzania.

Muziki wao umepata sifa ya kimataifa.

Utawala wa jadi

Wagogo walikuwa wakiongozwa na mtu aliyeitwa Mtemi. Watemi kadhaa waliongoza kabila hilo kabla ya mfumo wa uongozi kuvurugwa na ukoloni.

Mtemi wa mwisho aliitwa Mazengo ambaye alitokea katika kijiji cha Mvumi, wilaya ya Dodoma vijijini.

Nyumba za asili

Wagogo wamekuwa wakijenga nyumba ambazo kwa Kigogo huitwa "itembe". Tangu zamani kuta za tembe zilijengwa kwa fito (kwa Kigogo hutamkwa sito) zilizosukwa kwa kupisha kuzuia mwanga na maji. Vipande vya kuta vilivyosukwa kwa sito vinaitwa "izizi".

Tembe huezekwa kwa udongo ambao hushikiliwa na miti midogomidogo iitwayo "walo". Walo huwa inashikiliwa na miti mikubwa kidogo iitwayo "mahapa" na mahapa hushikiliwa na miti mikubwa iitwayo "michichi". Michichi ambayo ndiyo hubeba uzito wote hushikiliwa na nguzo kubwa za miti imara na migumu. Nguzo hizo hutiwa "masumbilili".

Kwa miaka ya karibuni kuta za tembe hujengwa pia kwa matofali yanayotengenezwa kwa udongo

Shughuli za uchumi

Wagogo ni miongoni mwa makabila ya wakulima na wafugaji kwa asili na hufuga mifugo kama ng'ombe, mbuzi na kondoo. Kwa Kigogo wanyama hao huitwa "ng'ombe, mhene na ngholo" pamoja na punda "ndogowe" kwa ajili ya ubebaji mizigo na wakati mwingine kulimia wakitumika kukokota majembe ya kukokotwa, kama watumikavyo ng'ombe pia.

Sambamba na shughuli hiyo, kilimo ndiyo shughuli kubwa na ya wengi, ijapokuwa kwa miaka mingi imekuwa ikiathiriwa na kiwango kidogo cha mvua zinazonyesha kutokana na jiografia ya mikoa hiyo miwili, yaani Dodoma na Singida.

Mazao yanayolimwa kwa wingi ni mahindi, mtama, uwele, na lugugu. Siku za hivi karibuni umeingia mtama unaokomaa kwa muda mfupi kama vile serena, lulu, tegemeo, masia, okoa, n.k., muhogo kiasi na katika maeneo machache mpunga na mzabibu, zao ambalo ni mahususi kwa biashara.

Chakula kikuu

Wagogo hula ugali wa uwele kama chakula kikuu na huchukulia ugali wa mahindi na mtama kama chakula laini na chepesi kisicho na nguvu.

Miaka ya zamani mlo wa kawaida wa Mgogo mwenye uwezo (yaani mwenye ng'ombe) ulihusisha ugali, maziwa, mafuta ya ng'ombe, kwa kigogo samuli na mboga kama mlenda ("ilende"), safwe, cidingulilu, nyakifwega, muhilile, sanghala, munzimwa, cipali, ihaji, sagulasagula, ikuwi, fwene, nghalabwajila (hasa wakati masika inapoanza) n.k.

Kwa sasa Wagogo wamekuwa wakila chakula cha kawaida kama makabila mengine nchini Tanzania.

Lafudhi ya lugha

Kabila la Wagogo lina lahaja ndani yake ambazo hutofautiana kutoka moja hadi nyingine kwa jinsi ambavyo hutamka maneno, yaani huongeza na kupunguza baadhi ya matamshi kwenye neno, na pia katika msamiati. Kwa ujumla kuna lahaja zipatazo 4, ambapo lahaja za Cinyambwa na Cinyaugogo ndizo hujulikana zaidi.

1. Wanyambwa - Hili ni kundi linaloonekana wazi kwenye kabila hili ambao huongea lafudhi ya Kinyambwa. Wanyambwa hutokea vijiji vya magharibi kwa mji wa Dodoma na sehemu ya wilaya ya Manyoni mkoani Singida.

Mifano - matamshi - vipi? = ntaule?

-msamiati - panda darini = ukwine kitembe

2. Wanyaugogo - hawa huongea lafudhi iitwayo Chinyaugogo. Wanyaugogo ambao ndio wanaowakilisha kundi kubwa sana hutokea vijiji vya mashariki na kusini kwa mji wa Dodoma na pia wilaya ya Mpwapwa. Kwa sababu mtemi Mazengo alikuwa Mnyaugogo kutoka Mvumi, mahali ambapo palijengwa kijiji kinachoitwa Mvumi Makulu (kwa maana kwamba ndipo ilipokuwepo Ikulu ya Mtemi), inaaminika kuwa lafudhi hii ndicho Kigogo cha asili isiyoathiriwa na lugha za nje.

Mifano - matamshi: - vipi? = nhaule?

-msamiati - panda darini = unanuce kitembe

3. Wetumba - Hawa ni Wagogo walioathiriwa Kigogo chao na Kikaguru. Hupatikana katika wilaya za Kongwa na Mpwapwa

Mfano - matamshi - jua limekuchwa - dizuwa diswa. Wanyaugogo hapa husema "lizuwa laswa/liswa"

4. Wetiliko - Hawa ni Wagogo wenye asili au mchanganyiko na Wahehe pamoja na Wabena, na hupatikana maeneo ya Kibakwe wilayani Mpwapwa.

Mfano - matamshi - twende = tibite. Wanyaugogo hapa husema "cibite"

Majina ya ukoo ya Cigogo

Majina hayo ni kama Mazengo, Cidosa, Cilongani, Malecela, Mwaluko, Mavunde, Ndejembi, Manyesela, Mbogambi, Mdachi, Kapaya, Matonya, Mtunya, Kusila, Nhonya, Mhalanyuka, Mbenaa, Chibile, Mdoli, Lusinde, Njamasi, Majenda, Chiwamba, Chiwaligo, Mazoya, Ufinyu, Chilyawanhu, Mahujilo, Magaya, Ngoli, Chiwanga,Lenjima, Lubeleje, Makupila, Fukunyi, Mondigwa, Ndasimi, Nhukuwala, Muhembano, Masinga, Ndahani, Chedego, Chenda, Chonya, Chimbwi, Cibehe, Mabwe, Malejehe, Madole (endeleza)

  Makala hii kuhusu utamaduni wa Tanzania bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Wagogo kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.