Ad Gentes
Siku ya mwisho kabla ya kufunga Mtaguso wa pili wa Vatikano (7 Desemba 1965) zilitolewa bado hati tatu, mojawapo kuhusu umisionari wa Kanisa, aina ile ya utume inayowaelekea watu wengi zaidi (thuluthi mbili za watu wote) yaani wasio Wakristo.
Kazi hiyo ni tofauti na uchungaji (unaowaelekea Wakatoliki) na ekumeni (inayowalenga Wakristo wengine).
Jina la hati hiyo kwa lugha asili ya Kilatini ni "Ad Gentes", maana yake "Kwa Mataifa". Ilitolewa na Papa Paulo VI baada ya kupata kura 2394 dhidi ya 5 tu za washiriki wa mtaguso huo.
Sura ya kwanza
haririSura ya kwanza inafafanua misingi ya umisionari: kwanza upendo wa Baba uliomfanya amtume Mwana halafu kwa jina lake amtume Roho Mtakatifu kwa Kanisa lililotumwa na Yesu kuendeleza kazi yake.
Basi, umisionari unatokana moja kwa moja na umbile la Kanisa, pamoja na kudaiwa na azimio la Mungu la kutaka watu wote waokoke na kujua ukweli.
Kwa umisionari tunawakusanya pia watu katika umoja na kuharakisha ujio wa ufalme wa Mungu.
Sura ya pili
haririSura ya pili inaeleza utendaji wenyewe kwanzia ushuhuda wa maisha ya Kikristo na wa matendo yaliyojaa upendo. Kwa ajili hiyo waamini wahusiane na kujadiliana vema na watu wengine.
Juu ya msingi huo inaweza kufanyika kazi ya kuwahubiria Injili na kuwakusanya katika taifa la Mungu. Hati hii inakataza katakata hao wasilazimishwe wala kuvutwa kwa udanganyifu wakubali imani, kama inavyodaiwa wasizuiwe kufuata imani.
Baada ya kuchunguza na kunyosha sababu za uongofu wao, waliojaliwa mwanzo wa imani wapokewe kwa ibada maalumu katika ukatekumeni ambao ufuate maagizo mbalimbali ya mtaguso mkuu.
Waliobatizwa wanatakiwa kuishi kijumuia kama familia ya Mungu, ambayo itie mizizi kweli katika makabila ya mahali, hasa kwa njia ya walei.
Pamoja nao Kanisa, likilenga mara kujitegemea iwezekanavyo katika miundo yote, linahitaji zaidi na zaidi wahudumu wanaotokana na makabila hayo mpaka liundwe jimbo lenye askofu, mapadri, mashemasi, watawa na makatekista wenyeji.
Sura ya tatu
haririSura ya tatu inajadili Makanisa maalumu ikionyesha jinsi yale machanga yanavyoendelea na kukomaa hata kuanza kuwatuma mapadri, watawa na walei walio tayari kwenda kwa wasio Wakristo, ndani ya jimbo na nje pia.
Hivyo Kanisa lililokomaa katika mazingira yake linashirikisha utajiri wa nchi yake, badala ya kuishia kukidhi mahitaji yake tu.
Sura ya nne
haririSura ya nne inazungumzia wamisionari wenyewe, malezi yao na maisha ya kiroho yanayopaswa kulingana na wito wao maalumu. Ili kurahisisha malezi hayo na kazi hiyo Mungu alitokeza pia mashirika yenye umisionari kama lengo kuu.
Sura ya tano
haririSura ya tano inatoa maagizo ili umisionari uwe na umoja na kufanikiwa. Kimataifa papa aratibu umisionari kwa njia ya idara ya uenezaji imani, isipokuwa Makanisa ya Mashariki yanafuata idara yao. Vilevile kijimbo na kitaifa kuwe na miundo na ushirikiano kati ya mashirika.
Sura ya sita
haririSura ya sita inapanua mtazamo kwa kuonyesha kuwa umisionari unahusu Kanisa lote kama wajibu wake mkuu.
Kwa hiyo ni lazima kila mwamini ajirekebishe na kuchangia wokovu wa wasio Wakristo.
Vilevile kila jumuia iwashughulikie walio mbali kwa bidii ileile inayowashughulikia walio jirani.
Kwa namna ya pekee wanapaswa kuwajibika maaskofu kama waandamizi wa mitume waliowekwa wakfu kwa wokovu wa ulimwengu mzima. Baada yao mapadri waeneze moyo wa kimisionari ili miito ya namna hiyo ipatikane na michango ifanikiwe.
Tena mashirika yote ya kitawa, yawe ya sala tu au ya utume, yafikirie upya yanavyowajibika katika umisionari.
Mwishoni walei pia wana nafasi kubwa katika kazi hiyo nchini kwao na kwenye misheni za mbali.