Malipo
(Elekezwa kutoka Aina ya malipo)
Malipo ni pesa au kitu atoacho mtu kulipia kitu alichonunua au kazi au huduma aliyofanyiwa. Malipo pia yanaweza kuwa ya shukrani kwa mazuri aliyofanyiwa mtu
Msamiati wa malipo mbalimbali
hariri- Arbuni/Rubuni/Advansi/Chambele/Kishanzu - malipo ya kwanza ya kuzuia kitu kisiuzwe.
- Risimu - bei ya kwanza ya kukinunua kitu mnadani.
- Fidia - malipo yalipwayo na shirika la bima kwa ajili ya hasara au maumivu yaliyompata mtu.
- Zawadi/Tuzo/Takrima/Hidaya - atunukiwacho mtu kama ni ishara ya mapenzi, wema, ushindi au kwa utendaji mzuri wa shughuli.
- Karo - malipo ya masomo shuleni.
- Ushuru - malipo yanayotozwa bidhaa forodhani.
- Mshahara - malipo ya mfanyakazi mwishoni mwa kila mwezi.
- Mahari - malipo ya kuoa ua kuolewa.
- Dhamana - malipo kwa niaba ya mtu ili ahudumiwe au aachiliwe huru kwa muda maalumu kesi au daawa inpoendelea mahakamani.
- Kivusho - malipo ya kuvuka daraja, mto au kivuko chochote.
- Nauli - malipo ya kusafiria.
- Faini - malipo anayotozwa mhalifu mahakamani.
- Kibarua - malipo ya kufanya kazi kutwa au malipo ya usiku.
- Mtaji - pesa za kuanzishia biashara.
- Riba - faida inayotozwwa na mkopeshaji au ziada ya benkini.
- Arshi / Dia - malipo kwa ajili ya kumtoa mtu damu.
- Rushwa/Kadhongo/Chirimiri/Chauchau/Kilemba/Mvugulio - malipo au zawadi anayotoa mtu ili kupata haki asiyostahili.
- Kilemba - ada ya harusi wanayopewa wajomba wa bibiharusi; pia malipo anayotoa mwanagenzi kwa mhunzi wake baada ya kuhitimu mafunzo yake.
- Kiingilio - malipo ya kuingia mahali kwa mfano mchezoni au densi.
- Kombozi - malipo ya kukombolea kitu au mtu.
- Koto/Ufito - ada anayotoa mzazi kwa mwalimu anapomwingiza mtoto wake chuoni.
- Ridhaa - malipo apewayo mtu aliyevunjiwa hadhi au heshima yake.
- Fichuo - malipo anayopewa kijana anapotoka jandoni.
- Kiinuamgongo/Pensheni/Bonasi - malipo baada ya kustaafu.
- Kodi - mapato au malipo kwa serikali kutokana na mishahara ya wafanyakazi au mapato mengine.
- Karadha - mkopo bila riba au malipo ambayo ni sehemu ya mshahara apewayo mtu katikati ya mwezi.
- Bahashishi - malipo ya kuonesha shukrani.
- Masurufu - pesa za matumizi ya safarini, matumizi ya nyumbani, njiani au mfukoni (pocket money).
- Thawabu - malipo anayopata mtu kutoka kwa Mwenyezi Mungu ajili ya kutii amri zake.
- Rada - malipo yanayotoka kwa Mwenyezi Mungu kurudi mtu aliyefanya jambo ovu.
- Advansi /Karadha - malipo yanayotolewa kabla kabla ya wakati wake kuwadia au kazi kumalizika.
- Urithi/Urathi - malipo anayopewa mtu kutokana na mali ya marehemu.
- Ujira - malipo ya kazi yoyote ya mkono.
- Mchango - malipo ya hiari kwa ajili ya kujenga au kutoa hisani au msaada kwa yule anayehitaji.
- Mapoza - malipo unayomlipa uliyemwudhi ili kuondoa hasira zake.
- Faida/Natija/Tija - pesa za ziada azipatazo mfanyabiashara.
- Marupurupu/Posho - malipo anayopata mtu zaidi ya malipo yake ya kawaida.
- Karisaji - malipo ya pesa ya muda uliopita.
- Utotole/Kiangazamacho/Machorombozi/Chorombozi Kiokozi - zawadi ya ugunduzi wa kitu au kushuhudia jambo linapofanyika mahali wakati fuluani.
- Mrabaha - faida au pato linalotokana na biashara; pia malipo anayopewa mwandishi au msanii na kampuni iliyotoa kazi yake kila baada ya kipindi fulani cha mauzo.
- Fola - malipo ya kumshika mtoto mchanga kwa mara ya kwanza.
- Kipkasa/Kipamkono/Jazua/Ukonavi - malipo anayopewa biharusi aonwapo mara ya kwanza.
- Kikunjajamvi - ada idaiwayo kwa wafanyabiashara au wakazi wa mabaraza ya kiasili na ya kizamani ambayo hujumuisha fedha au mali, kwa mfano: kondoo, mbuzi, kuku n.k.
- Bakora - zawadi ambayo baba humpa fundi akitaka mwanawe afundishwe ufundi.
- Haka - malipo ya kufidia kosa fulani katika mambo ya familia.
- Mukafaa - malipo ya mshahara kwa mfanyakazi kutokana na faida iliyopatikana.
- Honoraria - malipo apewayo mtu kama bahashishi kwa kazi maalumu aliyoifanya.
- Kudu - malipo alipayo mwari kwa nyakanga kama adhabu kwa kukosa adabu alipokuwa unyagoni.
- Mwago - malipo kwa mke wa kwanza mume anapooa mke wa pili.
- Mbiru - malipo kwa serikali kutokana na mishahara ya wafanyakazi wake.
- Zaka - moja ya kumi ya mapato ambayo waumini wa dini humtolea Mwenyezi Mungu kama shukrani.
- Fungule/Kanda - malipo ya kwanza kwa mganga.
- Tapisho - malipo kwa ngariba kwa ajili ya utahirishaji.
- Pango - kodi ya nyumba alipwayo mwenye nyumba baada ya kipindi fulani kulingana na makubaliano.
- Rehani - malipo ya kitu kilichowekwa dhamana ili kukombolewa baadaye.
Makala hii kuhusu mambo ya uchumi bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Malipo kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |