Pesa ni chombo cha kubadilishana bidhaa na huduma kati ya watu. Pesa yenyewe haina faida, haitoshelezi mahitaji ya binadamu ila imekubalika katika jamii kama njia ya kujipatia mahitaji mengine.

Pesa za Afrika ya Mashariki
Pesa ya Euro

Kuna maneno mengine ya Kiswahili kwa pesa kama vile hela, fedha au sarafu.

Mfumo wa sarafu unamaanisha utaratibu wa kutoa na kusimamia pesa katika uchumi wa kisasa.

Historia ya pesa

 
Sarafu ya mwaka 640 KK kutoka Lydia

Kiasili watu walibadilishana vitu kwa mfano ng'ombe mmoja kwa mbuzi kadhaa au mazao kwa samaki n.k.

Baadaye imeonekana ya kwamba itasaidia zaidi kama kiwango fulani inapatikana kwa vitu vyote.

Metali zilizokuwa haba zilitumiwa kama kipimo hiki, kwa mfano dhahabu, fedha au shaba. Vilipimwa kufuatana na uzito.

Hatua iliyofuata ilikuwa kutumia vipande vya metali hizi vilivyogongwa mihuri halafu hapakuwa na lazima ya kuvipima kimoja-kimoja. Inavyojulikana Wachina walikuwa watu wa kwanza waliochukua hatua hii katika milenia ya 2 KK. Hii ilikuwa mwanzo wa sarafu.

Pesa hutolewa na serikali ya nchi au na taasisi kama benki kuu inayofanya kazi hii kwa niaba ya serikali. Mwanzoni sarafu ilikuwa sawa na kiasi fulani cha dhahabu au fedha.

Hatua nyingine ilikuwa kutolewa kwa pesa ya karatasi au benknoti zilizoahidi kumpatia mtu yeyote kiasi kilichoandikwa kwa dhahabu au fedha yenyewe. Kwa muda mrefu benki kuu zilikuwa na hazina ya dhahabu iliyolingana na kiasi cha benknoti zilizochapishwa.

Tangu mwisho wa karne ya 20 nchi kadhaa zilianza kutoa benknoti za plastiki kwa sababu zinadumu kushinda noti za karatasi, tena ni vigumu zaidi kwa wajanja kutengeneza pesa bandia.

Katika karne ya 20 nchi zote zilifanya hatua ya kuacha makadirio ya dhahabu kwa sababu thamani ya bidhaa katika jamii ilipita kiasi cha dhahabu iliyopatikana. Siku hizi jumla ya pesa inayotolewa inatakiwa kulingana na thamani ya rasilmali ya taifa fulani.

Pale ambako serikali inachapisha benknoti kushinda kiwango hicho, thamani ya pesa inashuka na mfumko wa bei unatokea.

 
Pesa 1 ya Afrika ya Mashariki ya Kijerumani (hadi 1904) - nyuma; maandishi yasema: "Deutsch-Ostafrikanische Gesellschaft 1892"
 
Pesa 1 ya Afrika ya Mashariki ya Kijerumani (hadi 1904) - mbele; maandishi yasema: "sharaka almaniya 1309"

Asili ya neno "Pesa" katika sarufi ya Kihindi

Asili ya neno "pesa" katika lugha ya Kiswahili ni sarufi ndogo ya Kihindi iliyokuwa kitengo cha rupia. Rupia 1 ilikuwa na "paisa" 64 ikawa sarufi ya kawaida katika Afrika ya Mashariki kabla ya kipindi cha ukoloni. Neno la kiasili "paisa" likanyoshwa kuwa "pesa".

"Pesa" ya Afrika ya Mashariki ya Kijerumani

Wajerumani walipoanzisha koloni la Afrika ya Mashariki ya Kijerumani waliendelea kutoa sarafu kwa jina la rupia na pesa hadi 1904. Pesa 64 zilifanya rupie 1. Mwaka 1904 walibadilisha muundo na sarafu ya pesa ilipotea, badala yake heller ilianzishwa. Lakini neno lilibaki katika lugha.

Sarafi za pesa zilitolewa na Kampuni ya Kijerumani kwa Afrika ya Mashariki. Zilikuwa na maandishi ya Kiarabu upande mmoja na maandishi ya Kijerumani nyuma yake. Upande wa Kiarabu ulionyesha mwaka wa kutolewa kama tarehe baada ya hijra na upande wa Kijerumani ulionyesha mwaka BK. Maandishi yalikuwa jina la kampuni tu kwa Kiarabu na Kijerumani; upande wa Kijerumani ulikuwa na tai mwenye taji kama nembo la Milki ya Ujerumani.

Pesa za dunia

Pesa za dunia zinazotumiwa zaidi kimataifa
Pesa za nchi mbalimbali zinazotumiwa katika biashara ya kimataifa na asilimia yao katika biashara ya pesa
 
utengezaji wa pesa mjini Perm
Pesa Kifupi
(alama)
% ya biashara
(Aprili 2013)
 Dollar ya Marekani USD ($) 87.0%
 Euro EUR (€) 33.4%
 Yen ya Japani JPY (¥) 23.0%
 Pauni ya Uingereza GBP (£) 11.8%
 Dollar ya Australia AUD ($) 8.6%
 Frank ya Uswisi CHF (Fr) 5.2%
 Dollar ya Kanada CAD ($) 4.6%
 Peso ya Mexiko MXN ($) 2.5%
 Renminbi (Yuan) ya China CNY (¥) 2.2%
 Dollar ya New Zealand NZD ($) 2.0%
 Krona ya Uswidi SEK (kr) 1.8%
 Rubel ya Urusi RUB (₽) 1.6%
 Dollar ya Hong Kong HKD ($) 1.4%
 Dollar ya Singapur SGD ($) 1.4%
 Lira ya Uturuki TRY (₺) 1.3%
Pesa za nchi nyingine 12.2%
Jumla (jumla imekadiriwa kuwa 200% kwa sababu biashara ya pesa za kimataifa inahusu aina mbili tofauti) 200%

Tazama pia

Tanbihi

Viungo vya Nje

  Makala hii kuhusu mambo ya uchumi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Pesa kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.