Zaka (kutoka neno la Kiarabu زكاة, zakat, lenye maana ya "kinachotakasa") ni toleo la sehemu ya mapato ambalo muumini wa dini fulani anapaswa kutoa. maana ya zaka katika dini ya uislamu ina maana nyingi Zaka kilugha:Ni kukua kwa kitu na kuzidi. Zaka kisheria ni kiwango maalumu cha mali kinachotolewa wakati maalumu ili kupewa watu maalumu.

Katika Biblia

Desturi ya Mashariki ya Kati ya kutoa sehemu moja ya kumi kwa makuhani iliingia katika Uyahudi kuanzia Abrahamu aliyempa Melkisedek mfalme wa Salem aliyekuwa pia kuhani wa El Elyon (Mungu Mkuu).

Habari hiyo inasimuliwa katika Kitabu cha Mwanzo 14:18-20 na kusisitizwa na Waraka kwa Waebrania 7:5.

Zaka (kwa Kiebrania מעשׂר, ma‛ăśêr, kwa Kigiriki δεκάτη, dekatē) inaagizwa na vitabu vingine vya Biblia ya Kiebrania, kama vile Mambo ya Walawi, Hesabu na Kumbukumbu la Sheria katika Torati.

Baadaye wajibu huo ulisisitizwa na Kitabu cha Malaki 3:8-12 na Kitabu cha Tobiti 1:6–8.

Katika Agano Jipya, mtume Paulo alifundisha kuwa anayetumikia kwenye altare anastahili kupata riziki zake kwa njia hiyo (Waraka wa kwanza kwa Wakorintho 9:13).

Katika Ukristo

 
Stoo ya zaka huko Kronenburg, Ujerumani.

Mwanzoni mwa Kanisa waamini walikuwa wanawajibika, lakini baadaye zilianza kutolewa sheria ili kuwahimiza, kwa mfano huko Ufaransa katika mtaguso wa Tours (567) na ule wa Mâcon (585).

Hatimaye Papa Adrian I alipitisha maagizo hayo mwaka 787.

Baadaye njia za kuwategemeza viongozi wa Kanisa zilitofautiana kadiri ya nchi na madhehebu.

Katika Uislamu

Umuhimu wa sadaka katika uislamu

Zaka[1] ni faradhi katika faradhi za Dini ya Kislamu, na ni nguzo ya tatu katika nguzo za Uislamu, Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na simamisheni swala na toeni zaka} (Suratu An-Nur: 56),

Na akasema Mtume: (Umejengwa Uislamu kwa mambo matano: Kushuhudia ya kwamba hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu na kwamba Muhammad ni mja wake na ni Mtume wake, na kusimamisha Swala (tano za kila siku), na kutoa Zaka, na kuhiji nyumba tukufu (Al-ka’abah – ilioko Makkah), na kufunga Mwezi wa Ramadhani) [Imepokewa na Bukhari na Muslim.].

Zakat ni mojawapo ya Nguzo Tano za Kiislamu, ambayo inadai muumini atoe sehemu fulani ya mapato yake kwa maskini. Masharti ya mtu kulazimika kutoa Zaka ni:

  • 1. Uislamu. Haikubaliwi Zaka kwa kafiri, kwa sababu Mwenyezi Mungu hakubali matendo yake.
  • 2. Kuwa huru (muungwana). Haikubaliwi kwa mtumwa kutoa Zaka, kwasababu mali yake ni milki ya bwana wake.
  • 3. Kumiliki Nisabu. (kiwango) Maana ya Nisabu ni kiwango maalumu cha mali ambacho kwamba kikifikiwa basi inalazimika mali hayo kutolewa Zaka.

Masharti ya Nisabu

1. Iwe Nisabu ni ziada ya mahitaji ya dharura ambayo kwamba mtu hatosheki kwa kuyapata mahitaji hayo, kama chakula, mavazi na makazi, kwasababu Zaka ni wajibu kwa lengo la kuwaliwaza mafukara. Hivyo basi inatakiwa mwenye kutoa hiyo mali asiwe ni mtu muhitaji.

2. Iwe Nisabu inamilikiwa na mtu maalumu umiliki wa kiukamilifu, basi haiwajibiki Zaka kwa mali ambayo haimilikiwi na mtu maalumu, kwa mfano: mali iliyokusanywa kwa lengo la kujenga msikiti, au mali iliyowekwa wakfu kwa maslahi ya ummah, au mali iliyoko kwenye hazina za jumuia za mambo ya kheri.

4. Mali kupitiwa na Mwaka: Ni mwaka wa kiislamu uliokamilika.

Na hii ni kwamba ipite miezi kumi na mbili ya kalenda ya mtizamo wa mwezi hali ya kuwa Nisabu iko kwenye miliki ya mwenye mali. Na sharti hili ni peke yake kwa pesa (dhahabu na fedha), na mapato ya biashara, na wanyama wa mifugo. Ama mazao ya kilimo na matunda, na madini, hazina iliyozikwa ardhini sio sharti kwa vitu hivi kupitiwa na mwaka.

Tendo hilo muhimu la kutoa msaada linatazamwa na Waislamu kama njia ya kujipatia utakaso wa uroho na ubinafsi na ya kubarikiwa katika riziki zao.

Hukumu ya anayekataa kutoa Zaka

Anayekataa kutoa Zaka, ima amekataa kwa kupinga kwamba si lazima kutoa [Juhuud: Ni kukataa kuwajibishwa kwake.], au kwa ubakhili.[2]

Mwenye kukataa kutoa Zaka kwa kupinga

Anayepinga wajibu wa Zaka basi amekufuru kwa makubaliano ya umma wote – ikiwa mtu huyu anajua vizuri wajibu wa Zaka; kwa sababu atakuwa amemzulia uwongo Mwenyezi Mungu na Mtume wake.

Anayekataa kutoa Zaka kwa ubakhili

Atakayekataa kutoa Zaka kwa ubakhili wake basi huchukuliwa kutoka kwake Zakaa kwa nguvu na wala hawi kafiri kwa kufanya hivyo kukataa kutowa Zaka kwa ubakhili.

Na atakuwa ametenda dhambi kubwa miongoni mwa madhambi makubwa na ni uovu mkubwa sana.

Kwa kauli ya Mtume kuhusu wanaokataa kutoa Zaka: “Mtu yeyote aliye na hazina ya dhahabu na fedha na wala haitolei Zaka basi atachomwa nayo katika moto wa Jahannam na itajaaliwa kama vinoo ambavyo atapigwa navyo kwenye migongo na vipaji kila akipata ubaridi (yakipoa makali ya moto) anaregelewa tena (kupigwa navyo), mpaka Allaah Amalize kuhukumu waja wake siku ambayo ni sawa na miaka elfu khamsini. Kisha ndio ataoneshwa njia yake ikiwa ni ya peponi au motoni” [ Imepokewa na Bukhari.]

Na lau atapigana na kukataa kutekeleza amri ya zaka basi mpigeni vita mpaka arudi katika kutekeleza amri ya Mwenyezi Mungu, na atoe zaka, kwa kauli ya Mwenyezi Mungu: {Lakini wakitubu na wakasimamisha swala na wakatoa zaka, basi iacheni njia yao (waacheni} (Suratu At-tawbah: 5).

Na kwa kauli ya Mtume: (Nimeamrishwa niwapige watu vita mpaka washuhudiye ya kwamba hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu na kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na wasimamishe Swala, na watoe Zaka, watakapofanya hivyo basi imeharamishwa kwangu damu yao na mali yao isipokuwa kwa haki ya Uislamu, na malipo yao yako kwa Mwenyezi Mungu) [Imepokewa na Muslim.]

Na Abubakar alipiga vita mtu yoyote ambaye alipinga wajibu wa zaka, na akasema: (Naapa kwa Mungu ya kwamba nitampiga vita yoyote aliyetenganisha kati ya Swala na Zaka, kwa hakika hiyo Zaka ni haki ya mali, Wallaahi kama wakinizuilia hata kwa (kamba ya) kutiwa shemere (anayofungwa mnyama kwenye pua zake) nitapambana nao madamu walikuwa wakiitoa kwa Mtume) [Imepokewa na Bukhari.].

Katika Usingasinga

Katika dini ya Sikh muumini anadaiwa kutoa dasvand (ਦਸਵੰਦ) maana yake moja kwa kumi. Inaonekana sheria hiyo ilitokana na Uislamu.

Tanbihi

Viungo vya nje

Wikimedia Commons ina media kuhusu:
  Makala hii kuhusu mambo ya dini bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Zaka kama historia yake au uenezi wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.