Barua pepe ni ujumbe unaotumwa kwa njia ya intaneti au mtandao mwingine wa kielektroniki.

Njia ya baruapepe kutoka Anna kwenda kwa Hamed kupitia seva za intaneti

Barua pepe ni huduma ya intaneti, tena kati ya huduma za intaneti hii ndiyo inayotumiwa zaidi na watu kote duniani. Inapeleka habari mahali popote penye intaneti katika muda mfupi sana, mara nyingi katika sekunde chache hadi upande mwingine wa dunia.

Ujumbe unaweza kupelekwa ndani ya barua pepe yenyewe au kama nyongeza ya barua pepe. Nyongeza za aina hii ni kama faili za programu mbalimbali, picha au muziki zinazopatikana kwa umbo la digitali.

Gharama za kutuma barua pepe ni ndogo, karibu bure. Swala ni lile la upatikanaji wa tarakilishi/kompyuta iliyounganishwa na intaneti tu. Kwa hiyo tangu kutokea kwa barua pepe idadi ya barua za kawaida zinazotumwa na watu wanaoandika kwenye karatasi imepungua.

Mawasiliano ya barua pepe hutegemea utaratibu uliokubaliwa na kupatikana kote.

Muundo wa barua pepe

hariri

Kila barua pepe huwa na sehemu mbili:

  • kichwa ("header") chenye mistari ya kuonyesha anwani ya mwandishi, ya mpokeaji, tarehe na saa ya kupelekwa, fomati ya ujumbe na vituo vilivyopitiwa njiani katika intaneti.
  • sehemu kuu ("body") yenye habari ya ujumbe.
  • nyongeza ("attachment") zinaweza kuongeza faili za maandishi, picha au sauti.

Hasara na hatari

hariri

Hasara ya barua pepe ni ujao na wingi wa habari zisizorasmi ambazo hujulikana kama jumbe taka (kwa Kiingereza: "spam", yaani takataka). Watu, vikundi na makampuni mengi hutumia kompyuta kwa kusambaza matangazo ya kila namna na kwa kila anwani wanayojua. Mifumo mingi inafanya kazi usiku na mchana kukusanya taarifa na anwani za akaunti za watu wanaotumia barua pepe.

Kutokana na gharama nafuu ya matumizi ya barua pepe ni rahisi kutuma matangazo kwa mamilioni ya anwani kwa matumaini ya kwamba walau wachache wataisoma au labda hata kununua bidhaa zinazotangazwa. Mara nyingi matangazo haya yanalenga kuvuta watumiaji kwenda kurasa za intaneti ambako wanapaswa kulipa kiasi fulani kwa kuingia, kwa mfano kurasa za ngono.

Kati ya barua pepe za spam mara nyingi kuna ile mifumo inafuata mbinu kompyuta zisizotambulika kwakukusanya pia habari mbalimbali za watumiaji.

Kuna makadirio ya kwamba zaidi ya 80% za barua pepe zote zinazopita katika intaneti ni za aina za spam. Kwa watumiaji wa intaneti ni muhimu kuwa na programu zinazotambua hizi spam na kuzihamisha katika orodha ya pekee nje ya barua pepe zinazotakiwa.

  Makala hii kuhusu mambo ya teknolojia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu mada hiyo kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.