Chai

Kinywaji kinachotengenezwa kwa kuchanganya maji na majani ya mmea wa chai

Chai ni kinywaji kinachotengenezwa kwa kulowesha majani ya mchai (Camellia sinensis) katika maji ya moto. Wakati mwingine hata vinywaji vinavyopatikana kwa kutumia majani ya mimea mingine vinaitwa "chai".

Chai ya maziwa.
Mavuno ya chai duniani 2003 nchi kwa nchi.

Watu hunywa chai kwa sababu inatoa uchovu. Athari hii inatokana na dawa ya kafeini iliyopo ndani ya chai sawa na kahawa. Hapo awali, chai ilitumika kama bidhaa ya dawa. Matumizi yake kama kinywaji yalienea sana wakati wa Nasaba ya Tang ya China.

Aina za chai

hariri

Majani ya chai huandaliwa kwa njia mbili: kama chai nyeusi na chai ya kijani.

Chai nyeusi hupatikana kwa kukausha majani yake kwanza. Baadaye zinavunjwa na kuachwa ziumuke. Hapa kunatokea mmenyuko wa kikemia unaobadilisha rangi na ladha ya majani. Majani hushika joto kutokana na mmenyuko na joto hili halitakiwi kuzidi sentigredi 29. Chai nyeusi hutokea hasa Uhindi, Sri Lanka na Afrika pamoja na Kenya.

Chai ya kijani hutengenezwa kwa kukausha majani mabichi mara moja bila kuyapa nafasi ya kuumuka. Chai hii utokea hasa China na Japani.

Namna za kunywa chai

hariri

Kwa kawaida chai hunywewa ikiwa moto. Katika Afrika ya Mashariki huungwa maziwa ndani yake pamoja na sukari na viungo vingine. Aina hii ya chai imeenea kutoka Uhindi. Pasipo maziwa huitwa "chai ya mkandaa", pia "chai ya rangi".

Nchi nyingi zina utamaduni wa pekee jinsi ya kutengeneza chai. Wengine hunywa chai bila kitu kingine, wengi hupenda kuongeza sukari tu.

Ladha na rangi ya chai zinabadilika kadiri majani yanavyokaa ndani ya maji ya moto. Dawa la kafeini linatoka mapema, kwa hiyo kama mtu anataka hasa athari ya kuamsha anaweza kunywa chai iliyokaa dakika 1-2 mbili pekee. Kama majani yanakaa muda mrefu zaidi, dawa nyingine zilizomo mwenye majani zinayeyuka na dawa hizi zinaweza kubatilisha athari ya kafeini hata kuleta athari ya kutuliza. Kiasi cha rangi ya chai si dalili kwa kiasi chake cha kafeini na athari ya kuamsha.

Katika nchi za Mashariki ya Kati majani ya chai mara nyingi huwekwa ndani ya maji baridi na kuchemshwa pamoja naye.

Huko Urusi na Uajemi birika ndogo ya chai kali huwekwa juu ya chombo kikubwa cha maji ya moto kinachoitwa samowar. Kiasi kidogo cha chai kali huwekwa katika kikombe au bilauri halafu hujazwa kwa maji ya moto.

Katika Ulaya watu huweka majani katika maji ya moto kwa dakika chache tu. Waingereza na Wafrisia huongeza maziwa au krimu, wengine kidogo maji ya limau, halafu sukari.

Chai kama chakula

hariri

Neno "chai" hutumiwa pia kwa mlo mdogo. "Karibu chai" humaanisha mara nyingi kumwalika mgeni ale kitafunio hata pasipo kinywaji chenyewe.

Chai kama hongo

hariri

Katika Afrika ya mashariki neno "chai" limetumiwa mara nyingi kudai hongo. Asili yake ilikuwa ombi: "Naomba pesa kidogo ili nipate kununua chai". Hii imeshafupishwa mara nyingi kwa matamko mbalimbali kama "naomba chai", "toa chai" n.k. Kwa kawaida mwomba chai atashangaa akipewa kile anachosema kwa sababu anategemea pesa.

Tazama pia

hariri

Tanbihi

hariri


Viungo vya nje

hariri
 
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
  Makala hii kuhusu mambo ya utamaduni bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Chai kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.