Charles Darwin
Charles Robert Darwin (12 Februari 1809 - 19 Aprili 1882) alikuwa mwanasayansi Mwingereza katika karne ya 19.
Amekuwa mashuhuri kutokana na nadharia yake ya maendeleo ya uhai (mageuko ya spishi).
Nadharia hii yasema kuwa spishi zote za viumbehai vimetokana na spishi asilia zilizogeuka baada ya muda. Mageuko haya hufuata uteuzi asilia yaani viumbehai wanaolingana vizuri zaidi na mazingira wanaishi na kuzaa kushinda viumbehai wasiolingana nayo.
Kwa njia hiyo tabia za viumbehai wanaofaa vizuri zaidi zinazidi kuendelezwa kwa sababu watoto wao hurithi tabia hizi. Lakini tabia za viumbehai wasiofaa sana zinaweza kutoweka kwa sababu wanakufa mapema na hawana watoto wengi wanaoendeleza tabia zao.
Utoto na masomo
haririAlizaliwa mjini Shrewsbury (Uingereza) kama mtoto wa tano wa daktari Robert Darwin na Susannah Darwin (née Wedgwood).
Baada ya kumaliza shule alijiunga na chuo kikuu] cha Edinburgh (Uskoti) 1825 akajiandikisha katika idara ya tiba lakini hakupenda upasuaji. Alitumia muda mwingi kufuata kozi za biolojia, jiografia na jiolojia nje ya masomo ya tiba. Alifuatana mara nyingi na wataalamu walipofanya uchunguzi wa wanyama, mimea au mawe.
Baba baada ya kuona hafai kuwa daktari alimwandikisha katika masomo ya teolojia kwa shabaha ya kuwa mchungaji wa kanisa la Anglikana aliyomaliza mwaka 1831.
Baada ya kumaliza masomo haya Darwin alipata nafasi ya kujiunga kama mshiriki na safari ya kisayansi ya jahazi MS Beagle iliyotakiwa kuzunguka dunia yote kwa kusudi la kuboresha ramani hasa za pwani la Amerika Kusini. Darwin alipewa nafasi ya mwanaviumbe bila malipo ya kuongozana na kushauriana na nahodha na kiongozi wa safari kuhusu wanyama na mimea visivyojulikana na vitakavyopatikana safarini.
Katika safari hii Darwin aliona Amerika Kusini na visiwa vya Pasifiki. Akaona mengi na kushika kumbukumbu yake akakusanya mimea na miili ya wanyama na kuibeba naye kwa ajili ya maonyesho katika jumba la makumbusho la historia ya viumbe.
Kwenye visiwa vya Galapagos aliona ya kwamba kila kisiwa kilikuwa na spishi za ndege pia kobe zilivyotofautiana kidogo kati ya kisiwa na kisiwa.
Mapinduzi ya kisayansi
haririBaada ya kurudi Uingereza mwaka 1836 Darwin alianza kuchunguza sampuli zote alizokusanya. Alipata kazi kama katibu wa shirika la jiolojia.
Alipochungulia sampuli za Galapagos hasa alipata dhana ya kwamba spishi hizi zote za karibu zilitokana na aina moja tu iliyowahi kufika kwenye visiwa hivyo lakini baadaye zilianza kuwa tofauti katika kila kisiwa na kuwa spishi ya pekee. Kama hiyo ilikuwa kweli spishi hizi hazikuumbwa hivyo tangu mwanzo.
Darwin aliendelea na utafiti wa sampuli zake na kutoa masomo mbalimbali na kuyatafakari. 1859 alitoa kitabu kuhusu mageuko ya spishi kwa njia ya uteuzi asilia (On the Origin of Species by Means of Natural Selection, or the Preservation of Favoured Races in the Struggle for Life) alimoeleza nadharia yake.
Kitabu kilikuwa kama bomu kati ya watu wa sayansi na wa dini.
Darwin alishambuliwa mara nyingi ya kuwa mafundisho yake yanapinga taarifa ya uumbaji katika Biblia. Lakini hiyo inategemea jinsi masimulizi yake yanavyosomwa: si lazima mwamini achukue kila kitu kama ilivyoandikwa, kwa sababu Biblia hailengi kutufundisha sayansi, bali njia ya wokovu.
Leo hii nadharia yake inakubaliwa na wanasayansi karibu wote hata kama bado kuna kiasi cha upingamizi dhidi yake kwa sababu za kisayansi na za kidini.