Milki ya Uingereza

(Elekezwa kutoka Dola la Uingereza)

Milki ya Uingereza (pia: Milki ya Britania, ing. British Empire) ilikuwa milki kubwa ambayo ilijumlisha maeneo yaliyomilikiwa na Ufalme wa Maungano. Milki hii ilikuwa himaya kubwa ya kisiasa katika historia nzima, na iliweza kumiliki wakati wa kilele chake robo ya uso wa dunia.

Ramani ya nchi ambazo zilikuwa sehemu ya Milki ya Uingereza mnamo mwaka 1921.

Zaidi ya watu milioni 458 walikuwa chini ya udhibiti wa seikali ya London. Leo hii, maeneo yake mengi yamekuwa nchi huru zilizo wanachama wa Jumuiya ya Madola.

Kiini cha milki hii kilikuwa utawala wa Uingereza juu ya Uhindi uliotajirisha nchi tawala. Mwanzoni ilikuwa kampuni ya binafsi iliyofanya biashara huko, baadaye kutwaa maeneo hadi Uhindi yote kuwa mchanganyiko wa makoloni na "maeneo lindwa" zilizosimamiwa na washauri Waingereza kando ya watawala wenyeji.

Katika maeneo mengine Uingereza haukutafuta utawala wa moja kwa moja lakini ilitandaza nyavu za vituo vya kijeshi na kibiashara juu ya sehemu zote za dunia. Pale ambako wafanyabiashara wa Uingereza walikuwa na maslahi jeshi liliingia kati kuhakikisha ya kwamba wapate faida jinsi ilivyokuwa katika China ambayo haikufanywa kuwa koloni lakini ililazimishwa kuruhusu biashara ya madawa ya kulevya kwa njia ya vita mbili.

Katika karne ya 19 Uingereza ilichukua pia utawala juu ya sehemu kubwa ya Afrika; ingawa serikali ya London ilisita mara nyingi kuchukua maeneo mapya, maslahi ya wafanyabiashara na walowezi yalisababisha uenezaji wa himaya yake.

Katika robo ya mwisho wa karne ya 19 mashindano kati ya mataifa ya Ulaya yalisababisha kutwaliwa kwa maeneo mengine hasa kwa shabaha ya kwamba nchi nyingine isienee; kwa njia hii Kenya ikawa koloni la Uingereza.

Mwisho wa karne ya 19 Uingereza ilianza kuyapa makoloni kadhaa viwango tofauti vya kujitawala kama "dominion" kama idadi ya wakazi Waingereza ilikuwa kubwa; kwa njia hii nchi kama Kanada, Australia, New Zealand na Maungano ya Afrika Kusini zilipata serikali na katiba zao na kiwango cha kujitawala kiliongezeka polepole hadi mfalme au malkia wa Uingereza alikuwa mkuu wa dola wa heshima bila athira juu ya siasa tena.

Baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia Uingereza ilikosa nguvu ya kuendelea na utawala juu ya maeneo haya makubwa. Ilipaswa kuyapa uhuru, kuanzia Uhindi na Pakistan mwaka 1947 hadi nchi za Afrika tangu mwaka 1960.

Makoloni kadhaa, hasa nchi za visiwa vidogo, yaliamua kutotafuta uhuru yakaendelea kama Maeneo ya ng'ambo ya Uingereza hadi leo. Koloni la mwisho lililorudishwa kwa nchi mama ilikuwa Hongkong mwaka 1997.

Visiwa vya Falkland vilisababisha vita kati ya Uingereza na Argentina mwaka 1982 kwa sababu Argentina inadai visiwa kama mali yake ikapeleka wanajeshi visiwani, lakini Uingereza ulidai wakazi wa Falkland wanataka kuendelea kama raia wa Uingereza, wakaondoa Waargentina kwa nguvu ya kijeshi.

Viungo vya nje

hariri
  Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Milki ya Uingereza kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.