Gofu (michezo)
Kuhusu mabaki ya majengo angalia Gofu
Gofu (kwa Kiingereza: golf) ni mchezo ambako mchezaji anapiga mpira mdogo kwenye uwanja mkubwa kwa kutumia vingoe (fimbo za pekee) akilenga kufikisha mpira katika mashimo yanayofuatana. Analenga kuupiga mpira mara chache iwezekanavyo.
Sheria ya msingi inasema: "Mchezaji anafikisha mpira kutoka chanzo hadi kufikia shimoni kwa pigo moja au mapigo yanayofuatana."
Uwanja
haririUwanja wa gofu kwa kawaida ni eneo kubwa linaloweza kufikia hektari 60 hadi 80. Sehemu kubwa ya eneo linafunikwa na nyasi na miti. Uwanja kamili huwa na mashimo 18, uwanja mdogo una mashimo 9.
Kucheza
haririKuanzia chanzo kinachoitwa "tee" mchezaji anaelekea mashimo ya uwanja kwa utaratibu wake; maana anahitaji kufika kwanza shimo namba 1, halafu namba 2 na kadhalika. Lengo ni kufikisha mpira shimoni kwa mapigo machache iwezekanavyo. Idadi ya mapigo inaandikwa na kulinganishwa baadaye kwa kusudi la kumpata mshindi kati ya wachezaji wanaomaliza mashimo yote.
Gofu huchezwa na mtu peke yake kwa mazoezi, na wachezaji wawili kati yao au na timu za wachezaji. Wachezaji wawili au timu mbili huanza mahali pamoja na kupita kwenye mashimo kwa ufuatano uliopangwa.
Shimo linafikiwa kwa kupiga mara moja au mbili kwa nguvu yaani kuvukia umbali mkubwa na baadaye kwa nguvu kidogo ambako ni muhimu kulenga mpira vizuri mpaka ikaanguka katika shimo dogo.
Vingoe au fimbo
haririWachezaji huwa na chaguo la aina tofauti za vingoe au "klabu" yaani fimbo za kupiga. Kingoe kizito kinamwezesha mchezaji kupiga kwa nguvu kubwa na kurusha mpira mbali. Kwa kazi ngumu ya kuulenga shimo kuna vingoe vyepesi zaidi.
Wachezaji huchagua seti ya vingoe vyake kabla ya mchezo; anaruhusiwa kubeba hadi jumla ya vingoe 14 tofauti. Wanatofautisha "ubao", "chuma" na "putter".
Historia
haririMichezo inayofanana na gofu ilijulikana katika nchi na tamaduni mbalimbali lakini chanzo cha gofu cha kisasa kinaaminiwa kilikuwa Uskoti. Tangu karne ya 18 wachezaji waliungana katika shirika (golf club) na polepole wakaanza kupatana kanuni za mchezo kwa kusudi la mashindano. Mwaka 1900 na 1904 gofu ilianza kuwa sehemu ya michezo ya Olimpiki. Mwaka 1971 mwanaanga Alan Shepard alibeba mpira na kingoe hadi mwezi alipopiga mpira huu mara mbili.
Kwa muda mrefu gofu ilikuwa mchezo wa watu wenye pesa kwa sababu kukodi na kutunza uwanja kuna gharama kubwa kiasi. Uwanja wa gofu huwa na hektari 50 au zaidi, yaani kama ekari 120. Kwa mashindano eneo hili linahitaji kutunzwa vema hata kwa mashine za pekee, hivyo linahitaji wafanyakazi. Pia vifaa kama mipira na vingoe vilikuwa na gharama kubwa. Siku hizi mchezo umeenea zaidi na gharama zimeshuka katika nchi nyingi.
Mashindano makuu
haririKuna mashindano kadhaa maarufu na hapo hushiriki hasa wachezaji wanaocheza kikazi. Mashindano haya huitwa "majors".
- Wanaume
- The Masters
- U.S. Open
- The Open Championship (British Open)
- PGA Championship
- Wanawake
- Kraft Nabisco Championship
- LPGA Championship
- U.S. Womens Open
- Womens British Open
Marejeo
hariri[1] GDO
Tovuti za nje
hariri- Gofu nchini Kenya Ilihifadhiwa 25 Septemba 2020 kwenye Wayback Machine.
- Best Players
- Rules of Golf Ilihifadhiwa 8 Oktoba 2003 kwenye Wayback Machine.
- Golf Equipment Reviews Ilihifadhiwa 23 Julai 2008 kwenye Wayback Machine.
- Golf ball aerodynamics
- Golfers' Dictionary Ilihifadhiwa 4 Julai 2008 kwenye Wayback Machine.
- Golf news Ilihifadhiwa 15 Desemba 2018 kwenye Wayback Machine.
- Golf history Ilihifadhiwa 1 Februari 2003 kwenye Wayback Machine.
- Golf trivia Ilihifadhiwa 19 Julai 2008 kwenye Wayback Machine.
- Titleist Golf Clubs Ilihifadhiwa 21 Juni 2021 kwenye Wayback Machine.
Makala hii kuhusu mambo ya michezo bado ni mbegu. Je, unajua kitu zaidi kuhusu Gofu (michezo) kama historia yake, uenezi au kanuni zake? Labda unaona katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine habari zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |