Hekalu la Yerusalemu

(Elekezwa kutoka Hekalu la Solomoni)

Hekalu la Yerusalemu lilikuwa kitovu cha ibada za dini ya Uyahudi wakati wa Israeli ya Kale.

Uchoraji wa Hekalu ya Kwanza

Kwa jumla kulikuwa na majengo mawili yaliyofuatana kwenye mlima wa hekalu mjini Yerusalemu.

Imani ya Kiyahudi inategemea kujengwa kwa hekalu la tatu pamoja na kuja kwa Masiya wakati ujao.

Katika imani hiyo sehemu ya Patakatifu pa Patakatifu ndani ya hekalu ilikuwa mahali ambapo Mungu mwenyewe aligusa dunia.

Hekalu la kwanza

hariri

Hekalu la kwanza lilijengwa na mfalme Suleimani kuanzia mwaka 957 KK. Hekalu hilo lilichukua nafasi ya hema ya kukutania iliyotunza vifaa vya ibada za Kiyahudi tangu siku za kale (iliaminiwa tangu Musa).

Hasa wakati wa urekebisho (622 KK - 609 KK) wa mfalme Yosia hekalu hilo lilifikia hatua ya kuhesabiwa mahali halali pekee pa ibada za sadaka.

Hata hivyo kuna taarifa, hasa katika sehemu za zamani za Biblia, kuhusu ibada kwenye "mahali pa juu" (yaani juu ya milima na vilima) zilizolaumiwa baadaye kama ishara ya imani potofu.

Hekalu hilo la Suleimani lilibomolewa mwaka 587 KK wakati mfalme Nebukadreza II wa Babeli alipovamia Yerusalemu na kuharibu mji mzima.

Hekalu la pili

hariri

Baada ya ushindi wa Waajemi juu ya Babeli (mwaka 539 KK) mfalme Koreshi Mkuu aliwaruhusu Wayahudi kujenga upya hekalu.

Katika Biblia, kitabu cha Ezra, pamoja na vile vya nabii Hagai na nabii Zekaria, vinasimulia habari hizi.

Ujenzi ulifuata mpango wa hekalu la kwanza na ulifanyika mahali palepale Yerusalemu kwenye "mlima wa hekalu".

Katika hekalu hilo la pili sehemu ya Patakatifu pa Patakatifu ilikaa bila ya kitu ndani yake, kwa sababu Sanduku la Agano lilipotea tangu kubomolewa kwa hekalu la kwanza.

Hekalu liliharamishwa na mfalme Antioko IV mwaka 169 KK alipoweka hapa sanamu ya mungu wa Kigiriki Zeus.

Hatua hiyo ilisababisha upinzani wa Wamakabayo waliorudisha ibada ya Kiyahudi hekaluni na hadi leo sherehe ya Hanuka inakumbusha kutakaswa kwa hekalu mwaka 167 KK.

Matengenezo chini ya Herode

hariri

Mnamo mwaka 21 KK mfalme Herode Mkuu aliamuru matengenezo ya hekalu.

Wataalamu wengi huona ya kwamba matengenezo yalifanana na ujenzi mpya wa hekalu kwa jinsi lililopambwa na kuongezeka.

Kwa kawaida hekalu linalotajwa katika Agano Jipya ni hilo la Herode.

 
Wanajeshi Waroma wakibeba kinara cha mishumaa na vifaa vingine kutoka Hekalu la Yerusalemu baada ya huliharibu mwaka 70

Mwisho wa hekalu

hariri

Mwaka 70 jeshi la Dola la Roma lilivamia Yerusalemu na kubomoa hekalu, tarehe ileile lilipobomolewa mara ya kwanza.

Kuta za msingi tu zilibaki na ukuta mkubwa wa magharibi unasimama hadi leo, ukijulikana kama Ukuta wa Maombolezo na ni patakatifu pa Wayahudi.

Baada ya kuharibika kwa hekalu

hariri

Waroma walijenga hapohapo hekalu kubwa kwa mungu wao Jupiter lililobomolewa baada ya ushindi wa Ukristo katika Dola la Roma.

Mara mbili kulitokea majaribio ya kujenga tena hekalu la Kiyahudi: mara ya kwanza chini ya Kaisari Julian Apostata, na mara ya pili wakati wa uvamizi wa Uajemi kwenye vita dhidi ya Bizanti mnamo 614 lakini majaribio yote yalishindikana.

Waislamu walipovamia Yerusalemu walikuta mlima wa hekalu kama mahali pa maghofu tu wakajenga hapo misikiti miwili: msikiti wa Al Aqsa pamoja na Kubba ya Mwamba.