Kitabu cha Ezra
Kitabu cha Ezra kinapatikana katika Biblia ya Kikristo katika Agano la Kale.
Kiasili kiliandikwa kwa lugha ya Kiebrania lakini kuna pia sehemu fupi za Kiaramu.
Andiko la Ezra lilitunzwa katika Biblia ya Kiebrania pamoja na Nehemia kama kitabu kimoja lakini kimegawiwa baadaye kuwa vitabu viwili ambavyo Vulgata inavitaja kama "Esdras I" na "Esdras II".
Kitabu kinasimulia habari za Wayahudi chini ya utawala wa Waajemi.
Mwaka 587 KK mfalme wa Babeli alikuwa amevamia mji wa Yerusalemu, kubomoa hekalu la Sulemani na kumaliza ufalme wa Yuda. Wakazi walipelekwa Mesopotamia kwa uhamisho wa Babeli. Tangu wakati huo Waisraeli kwa kawaida walijulikana kuwa Wayahudi. Lakini, kwa kuwa utengano wa Israeli haukuendelea, majina hayo mawili, pamoja na jina la Waebrania, yaliweza kutumiwa kwa watu walewale (Yer 34:9; Yn 1:19, 47; 2 Kor 11:22; Gal 2:14).
Mwaka 539 KK Waajemi chini ya mfalme Koreshi walivamia Babeli ambayo ikawa jimbo la milki ya Uajemi. Koreshi aliwaruhusu Wayahudi kadhaa warudi Yerusalemu na kujenga upya hekalu.
Habari hizi na zilizofuata zinasimuliwa katika vitabu vya Ezra na Nehemia.
Kama vitabu vingine vyote vya Biblia, hiki pia kinatakiwa kisomwe katika mfululizo wa historia ya wokovu ili kukielewa kadiri ya maendeleo ya ufunuo wa Mungu kwa binadamu.
Mazingira ya Ezra na Nehemia
haririInaonekana vitabu vya Mambo ya Nyakati, Ezra na Nehemia viliandikwa kama mfululizo wa habari. Ndiyo sababu habari za Ezra zinaanzia wakati uleule ambapo habari za Mambo ya Nyakati zinamalizika.
Wakati huo ulikuwa mwaka 538 KK Waajemi walipokuwa wameshinda Babeli muda mfupi uliopita, na mfalme wao Koreshi, alikuwa ametangaza amri iliyowapa Wayahudi uhuru wa kurudi katika nchi yao (2 Nya 36:22-23; Ezra 1:1-4).
Wakati uliofuata unajulikana kuwa wakati wa baada ya uhamisho wa Babeli. Vitabu kadhaa vya Biblia (vya historia na vya manabii), vinahusika na wakati huo. Muhtasari wa matukio unaotolewa hapa chini unataka kusaidia kuelewa vitabu hivyo zaidi.
Kurudi kwa watu wa kwanza kutoka kifungoni
haririMiaka kama 200 hivi ya nyuma watu wa ufalme wa kaskazini walipelekwa kifungoni katika mataifa mbalimbali, wengi wao wakapoteza utambulisho wa taifa lao. Lakini watu wa ufalme wa kusini, yaani wa Yuda, walipopelekwa Babeli baadaye, walihifadhi utambulisho huo.
Kufuatana na amri ya Koreshi ya mwaka wa 538 KK, Wayahudi walirudi Yerusalemu kwa maelfu. Walikuwa na viongozi wao wa Kiyahudi, yaani Zerubabeli aliyekuwa kiongozi tangu wakati wa kifungoni, na kuhani mkuu Yoshua, lakini wote waliendelea kuwa chini ya himaya ya Uajemi, hivyo walikuwa chini ya wafalme wake. Mji wa Yerusalemu ulikuwa katika mkoa uliojulikana kuwa "Ng'ambo ya Mto" (au "Magharibi ya Frati"), ulioanza katika Mto Frati na kuendelea mpaka Bahari ya Kati (Ezra 4:10, 16; 7:21, 25).
Muda mfupi baada ya kufika Yerusalemu, Wayahudi walianza kazi ya kujenga hekalu upya. Madhabahu iliwekwa mahali pake tena, na katika mwaka wa pili misingi ya hekalu ikawekwa (Ezra 3:1-3, 8-10). Lakini wakati huo maadui walianza kuwapinga wajenzi wakasababisha kazi yote iahirishwe kwanza (Ezra 4:1-5, 24).
Manabii Hagai na Zekaria
haririKwa muda wa miaka 16 hivi haikufanyika kazi yoyote katika ujenzi wa hekalu (Ezra 4:24). Kisha, mwaka 520 KK, Mungu aliwaita watu wawili miongoni mwa Wayahudi walioishi Yerusalemu ili wawaamshe na kuwahamasisha waendelee na kazi ya hekalu, wala wasilegee tena mpaka waimalize. Watu hao wawili walikuwa manabii Hagai na Zekaria (Ezra 5:1-2; Hag 1:1; Zek 1:1).
Mara watu walipoanza tena kazi ya ujenzi, upinzani mpya ulitokea (Ezra 5:3). Jambo hilo likawekwa mbele ya mfalme mpya wa Uajemi aliyeitwa Dario (Koreshi alikuwa amekufa tangu miaka michache). Baada ya kuchunguza jambo hilo vizuri, Dario aligundua kwamba Koreshi alikuwa ametoa ruhusa ya kujenga hekalu. Kwa hiyo Dario akaandika amri mpya iliyothibitisha ile ya kwanza ya Koreshi, ambayo iliruhusu kazi ya kujenga hekalu iendelee (Ezra 6:6-12).
Mahubiri ya Hagai ya kuamsha watu yalileta matokeo ya haraka, na baada ya wiki tatu Wayahudi walikuwa katika kazi yao tena ya kujenga hekalu.
Nabii Zekaria akamwunga mkono Hagai, akitoa mafundisho marefu zaidi yaliyokusudiwa kuleta mabadiliko ya kiroho katika maisha na matumaini ya watu.
Miaka minne baada ya kuanza tena kazi hiyo, hekalu lilimalizika (mwaka 516 KK; taz. Ezra 6:14-15; 4:24).
Kitabu cha Esta
haririMfalme aliyetawala baada ya Dario alikuwa Ahasuero, ambaye alijulikana pia kama Xerxes I. Alitawala tangu 486 hadi 465 KK Yeye ndiye mfalme aliyetajwa kuhusika na habari za kitabu cha Esta.
Kurudi chini ya uongozi wa Ezra
haririKatika mwaka 465 KK Artashasta (au Artaxerxes) alikuwa mfalme wa Uajemi badala ya Ahasuero (au Xerxes I). Katika mwaka wa saba wa utawala wake (yaani 458 KK), aliandika amri iliyompa Ezra mamlaka na fedha arudi Yerusalemu na kutekeleza matengenezo ya huko (Ezra 7:1, 7, 13).
Kutokana na uchunguzi wa tarehe zinazohusika, inaonekana kwamba matukio yaliyoandikwa katika mafungu ya kwanza ya kitabu cha Ezra (k.mf. matukio yaliyohusika na Zerubabeli, Yoshua na kujengwa upya kwa hekalu), kwa kweli yalikuwa kabla ya kuzaliwa kwake Ezra. Bila shaka mwandishi wa kitabu cha Ezra alichunguza barua, hati na ripoti za historia nyingi ili kuandaa mambo mengi ya sehemu ya kwanza ya kitabu chake. Inatupasa kusoma zaidi ya nusu ya kitabu mpaka tunapopata habari za wakati wa Ezra mwenyewe. Kurudi kwa Ezra kulikuwa kama miaka 80 baada ya Zerubabeli. Watu wa Yerusalemu walikuwa kizazi kingine kuliko wale waliorudi pamoja na Zerubabeli.
Ezra alikuwa kuhani na mwandishi aliyejua sana sheria ya Mungu (Ezra 7:6, 12). Zamani za kale "mwandishi" alikuwa mtu aliyenakili sheria ya Mungu kwa watu waliotaka kuisoma, lakini baada ya uhamisho wa Babeli alikuwa mtu wa maana au mtaalamu ambaye uamuzi wake katika mambo ya dini uliheshimiwa sana. Katika miaka ya baadaye waandishi walizidi kupata nguvu na ushawishi katika Israeli, ambapo manabii walipungua kwa idadi na umuhimu.
Hata hivyo, Ezra alikuwa ametumwa na Mungu. Hakusoma sheria tu, bali pia alieleza maana yake, ili kitabu cha sheria kiwafundishe watu jinsi ya kuishi kila siku (Ezra 7:10; Neh 8:8). Hapa tunaweza kuona asili ya mipango ya dini ya Kiyahudi iliyoendelezwa na waandishi wa baadaye. Lakini mifano ya dini hiyo ya wakati wa Yesu ilitofautiana sana na aina ya maisha iliyofundishwa na Ezra.
Kurudi chini ya uongozi wa Nehemia
haririKatika mwaka wa 20 wa utawala wake, Artashasta alitoa amri ya pili iliyowaruhusu Wayahudi wengine warudi Yerusalemu kwa msaada wa fedha nyingi za serikali, wakati huo wakiongozwa na Nehemia (445 KK). Hekalu la Yerusalemu lilikuwa limemalizika zaidi ya miaka 70 iliyopita, lakini mji wenyewe ulikuwa bado na hali ya kusikitisha, na kuta za kuuzunguka zilikuwa hazijajengwa upya. Ilikuwa kwa kusudi la kujenga kuta hizo kwamba Nehemia alipata amri na msaada kutoka kwa Artashasta (Neh 2:1-8).
Labda Ezra alikuwa amerudi Yerusalemu miaka 13 kabla ya Nehemia. Marekebisho yake yalikuwa na matokeo madogo tu, wala haikuwa mpaka baada ya Nehemia kufika na kuwa liwali mkuu wa Yerusalemu, kwamba marekebisho yale yalileta matunda kwa wenyeji kwa jumla. Watu hao wawili walifanya kazi moja, wakiwaongoza watu wamrudie Mungu (Neh 8:9). Nehemia aliishi Yerusalemu kwa muda wa miaka 12 kabla ya kurudi tena Uajemi (Neh 2:1; 13:6). Baada ya muda akarudi tena Yerusalemu (Neh 13:6-7). Kitabu cha Nehemia katika Biblia kinaeleza matendo makuu ya Nehemia mjini Yerusalemu.
Manabii wa mwisho
haririInafikiriwa kwamba ulikuwa wakati uleule wa marekebisho ya Ezra na Nehemia baada ya kifungo cha Babeli ambapo nabii Malaki alitoa ujumbe wake. Tarehe za unabii wake haziwezi kupangwa kwa uhakika, lakini dhambi alizozilaumu zinafanana na zile ambazo Ezra na Nehemia walipaswa kushughulika nazo. Watu walikuwa wametazamia kwamba, kwa sababu walirudi katika nchi yao na kumaliza ujenzi wa hekalu (515 KK), wangefurahia baraka za Mungu zisizokuwa na mwisho. Mategemeo hayo hayakutimizwa, hivyo watu walianza kutia shaka kama Mungu aliwaangalia kweli.
Ni kwamba, taratibu za ibada ziliendelea moja kwa moja, lakini tarajio la wengi la kuona mapema taifa la Mungu lina hali tukufu halikutimia. Hivyo ilitokea tena hali ya kukata tamaa iliyowafanya makuhani na Wayahudi kwa jumla wamtumikie Mungu kwa uzembe. Ndipo alipotumwa nabii Malaki kukaripia makosa yao katika kumuabudu, akijibu hoja zao na kutabiri ujio wa mjumbe wa Agano na wa mjumbe mwingine atakayemuandalia njia; hapo maadili na ibada vitaratibishwa tena (3:1-5) na kila mahali itatolewa sadaka safi kwa Mungu (1:11). Katika wajumbe hao wawili Wakristo waliwatambua kwa urahisi Yesu na Yohane Mbatizaji.
Baada yake Obadia akatangaza adhabu ya Mungu kwa Waedomu, kielelezo cha maadui wa taifa la Mungu, siku yake itakapofika.
Muhimu zaidi ni unabii wa Yoeli aliyetangaza vivyo hivyo siku ya Bwana akichukua mfano hai wa uvamizi wa nzige wengi uliolazimisha Wayahudi wote kufanya toba, lakini alitabiri pia mmiminiko wa Roho wa Bwana juu ya watu wake wa kila aina (2:28-32) alivyoomba Musa na utakavyowatokea wanafunzi wa Yesu siku ya Pentekoste (Mdo 2:16-21). Hivyo tapo la unabii kabla halijakoma lilitabiri kipindi kingine cha unabii chenye kustawi kuliko cha awali.
Kweli katika karne mbili za utawala wa Waajemi unabii ulizidi kufifia ukiacha nafasi kwa aina nyingine za uongozi wa kiroho: wataalamu wa Torati na watu wenye hekima waliotunga vitabu kwa uvuvio wa Mungu bila ya kupatwa na hali za pekee kama manabii.
Maandiko mengine
haririPengine ni wakati huo kwamba, baada ya muda mrefu wa mapokeo ya sauti, vilianza kuandikwa vitabu vya hekima (Kitabu cha Mithali, Kitabu cha Ayubu) na vinginevyo (Wimbo Ulio Bora, Zaburi nyingi). Ingawa vinafanana na vile vya makabila ya jirani, vinafikiria maisha kwa mwanga wa imani katika Mungu aliye mmoja, hasa kwa kuzingatia uzima na kifo, uchungu, mwenendo, heri n.k.
Mithali ndicho kitabu kinachotuletea mawazo ya zamani zaidi na ya kwamba Mungu anamtuza mwadilifu na kumuadhibu mwovu hapa duniani.
Kitabu cha Ayubu kinakataa mtazamo huo kwa kuonyesha hali halisi, yaani kuwa duniani mara nyingi mwadilifu ndiye anayeteseka; hata hivyo binadamu hawezi kujua ni kwa nini: basi amuachie Mungu na kumuabudu katika fumbo lake (42:1-6).
Wimbo ulio Bora haumtaji Mungu wala dini: ulihusu mapenzi ya wachumba, lakini ukaja kufafanuliwa kama mapenzi ya Mungu na Israeli wanaotafutana ili kuungana kabisa.
Zaburi, ambazo zilitungwa na kurekebishwa polepole kwa muda unaokaribia miaka elfu, yaani muda ule wote uliotumika kutunga vitabu vingine vyote vya Agano la Kale, ndizo sala za kishairi au nyimbo ambazo katika hali ya sifa, ibada, shukrani na dua zinajumlisha Biblia nzima.
Muhtasari wa matukio
haririTarehe zilizotajwa katika jedwali lifuatalo zinajadiliwa sana na wataalamu bila ya kufikia mwafaka.
Miaka ya KK | Wafalme wa Uajemi | Matukio |
---|---|---|
539 | Koreshi | Koreshi ashinda Babeli (Dan 5:30-31), Amri ya Koreshi: Kurudi kwa Serubabeli (Ezra 1:1; 2:2) |
538 | Kuanza ujenzi wa hekalu (Ezra 3:1-3, 8-10) | |
537 | Kuahirisha ujenzi wa hekalu (Ezra 4:1-5:24) | |
530 | Kambyses | atawazwa |
521 | Dario I | atawazwa |
520 | Unabii wa Hagai na Zekaria (Ezra 5:1-2; Hag 1:1; Zek 1:1) Amri ya Dario kujenga hekalu (Ezra 4:24; 6:6-12) | |
516 | Kumalizika kwa hekalu (Ezra 6:14-15) | |
486 | Xerxes I | Atawazwa (Esta 1:1) |
465 | Artashasta I (Artaxerxes I) | atawazwa |
458 | Amri ya kwanza ya Artashasta: Ezra arudi (Ezra 7:1, 7, 13) | |
445 | Amri ya 2 ya Artashasta: Nehemia arudi (Neh 2:1-8) | |
424 | Mwisho wa utawala wa Artashasta |
Viungo vya nje
hariri- Blenkinsopp, Joseph, "Ezra-Nehemiah: A Commentary" (Eerdmans, 1988)
- Blenkinsopp, Joseph, "Judaism, the first phase" (Eerdmans, 2009)
- Coggins, R.J., "The Books of Ezra and Nehemiah" (Cambridge University Press, 1976)
- Fensham, F. Charles, "The books of Ezra and Nehemiah" (Eerdmans, 1982)
- Grabbe, L.L., "Ezra-Nehemiah" (Routledge, 1998)
- Grabbe, L.L., "A history of the Jews and Judaism in the Second Temple Period, Volume 1" (T&T Clark, 2004)
- Pakkala, Juha, "Ezra the scribe: the development of Ezra 7–10 and Nehemiah 8" (Walter de Gryter, 2004)
- Throntveit, Mark A., "Ezra-Nehemiah" (John Knox Press, 1992)
Mwanzo * Kutoka * Walawi * Hesabu * Kumbukumbu * Yoshua * Waamuzi * Ruthu * Samueli I * Samueli II * Wafalme I * Wafalme II * Mambo ya Nyakati I * Mambo ya Nyakati II * Ezra * Nehemia * TobitiDK * YudithiDK * Esta * Wamakabayo IDK * Wamakabayo IIDK * Yobu * Zaburi * Methali * Mhubiri * Hekima DK * SiraDK * Wimbo Bora * Isaya * Yeremia * Maombolezo * BarukuDK * Ezekieli * Danieli * Hosea * Yoeli * Amosi * Obadia * Yona * Mika * Nahumu * Habakuki * Sefania * Hagai * Zekaria * Malaki
Alama ya DK inaonyesha vitabu vya deuterokanoni visivyopatikana katika matoleo yote ya Biblia.