Wamakabayo
Wamakabayo (kwa Kiebrania מכבים au מקבים, Makabim au Maqabim; kwa Kigiriki Μακκαβαῖοι) walikuwa familia ya mashujaa wa Israeli walioongoza mapigano dhidi ya dola la Waseleuki ili kupata uhuru wa dini na hatimaye uhuru wa taifa upande wa siasa pia.
Mashujaa hao walikuwa kuhani Matatia na wanae watano waliopokezana kushika uongozi kuanzia Yuda Mmakabayo
Habari zao zinasimuliwa katika kitabu cha kwanza cha Wamakabayo na kitabu cha pili cha Wamakabayo vilivyoandikwa na watu tofauti katika karne II KK na ambavyo vyote viwili ni kati ya vile vya Deuterokanoni vinavyokubaliwa na Wakristo wengi kama sehemu ya Biblia. Ushujaa wao unasifiwa pia na waraka kwa Waebrania kama kielelezo cha imani.
Pia kuna vitabu vingine viwili juu yao (Wamakabayo III na Wamakabayo IV) ambavyo havimo katika toleo la Septuaginta wala katika Biblia ya Kikristo.
Ukoo wao (Wahasmonei) ulitawala Yudea tangu mwaka 164 KK hadi 63 KK, wakisisitiza dini ya Uyahudi na kupunguza athari ya ustaarabu wa Ugiriki wa kale kati ya Wayahudi.
Mazingira yao: uenezi wa utamaduni wa Kiyunani (333-63 K.K.)
haririKwa muda mfupi sana Aleksanda Mkuu wa Makedonia (Ulaya Kusini Mashariki) aliteka Asia (mpaka India) na Misri. Kuanzia hapo utamaduni na lugha ya Kiyunani vikaenea pote, hata kwa Wayahudi wengi, hasa walioishi nje ya nchi yao.
Chini ya utawala wa Kiyunani unabii ukaja kwisha (1Mak 9:27): badala yake yalitolewa maandiko ya kiapokaliptiko (hasa kitabu cha Danieli ambacho ni kama Ufunuo wa Agano la Kale), hadithi (Yona, Tobiti, Esta, Yudithi) na vitabu vya hekima (Mhubiri, Yoshua bin Sira, Hekima).
Humo tunaona maendeleo ya ufunuo, hasa kwa sababu Wayahudi wengi walianza kusadiki ufufuko wa wafu na mengineyo.
Nguvu ya imani hiyo iliwasaidia kukabili dhuluma na kifo (2Mak 7:1-41) chini ya Antioko Epifane (175 KK - 164 KK) aliyetaka kuwalazimisha waache kufuata Torati ili wajilinganishe na watu wengine. Tena akijidai kuwa tokeo la Mungu Mkuu alijenga altare kwa mungu wake ndani ya hekalu la Yerusalemu.
Hapo Wayahudi wakaanza kupigania uhuru wao wa kidini na wa kisiasa chini ya ukoo wa Wamakabayo, ambao kwa imani na ushujaa mkubwa wakafaulu kushinda majeshi ya kutisha (1Mak 3:18-22), kutakasa hekalu (1Mak 4:36-61) na kurudisha ufalme wa Israeli mpaka baada ya Warumi kuweka Uyahudi chini ya himaya yao (63 K.K.).
Ndiyo asili ya kundi la Mafarisayo (yaani “waliojitenga”), walioshika kwa bidii Torati kadiri ya mapokeo ya walimu wa sheria, wengi wao wakiwa walei. Kwa jumla walileta uamsho wa kiroho kati ya Wayahudi, lakini walidharau wenzao wasiojua Maandiko Matakatifu. Pia walishindana sana na Masadukayo kuhusu masuala ya dini na ya siasa hata kusababisha mauaji; kwa kuwa Masadukayo (waliokuwa na nguvu kati ya makuhani) walikataa mafundisho hayo mapya huku wakishika Torati tu.
Viungo vya nje
hariri- Jewish Encyclopedia: Maccabees, The
- Catholic Encyclopedia: Jerusalem (Before A.D. 71)
- 1911 Encyclopedia Britannica: Maccabees
Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Wamakabayo kama enzi zake au matokeo yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |