Mdudu Mabawa-nusu
Mdudu mabawa-nusu | ||||||||||||
---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|
Kisulisuli mraba-mweusi (Dysdercus nigrofasciatus)
| ||||||||||||
Uainishaji wa kisayansi | ||||||||||||
| ||||||||||||
Ngazi za chini | ||||||||||||
Nusuoda 4:
|
Wadudu mabawa-nusu ni wadudu wadogo sana hadi wakubwa kiasi wa oda Hemiptera katika nusungeli Pterygota (wenye mabawa). Jina ni tafsiri ya jina la kisayansi. Wadudu hawa wanajulikana sana kama kunguni, kunguni-mgunda, vidukari, vidung'ata, nzi weupe, wadudu-gamba na nyenje-miti k.m. Familia kadhaa zina spishi zinazoishi majini, kama nge-maji, waogeleaji-juuchini na wendamaji. Spishi za Halobates huenda juu ya maji ya bahari na hizi ni wadudu pekee wanaoishi baharini.
Katika spishi nyingi sehemu ya mbele ya mabawa ya mbele ya wadudu hawa ni ngumu na sehemu ya nyuma ni kiwambo. Mabawa yakiwa yamekunjwa yanalala bapa na kufunika fumbatio. Mabawa ya nyuma ni kama viwambo. Katika spishi nyingine jozi zote mbili za mabawa ni kama viwambo na mara nyingi yakiwa yamekunjwa yanakaa kama paa la nyumba. Pengine mabawa yana manyoya (k.m. nzi weupe).
Sehemu za kinywa zinafaa kufyonza na zimeunda kwa mrija. Hufyonza utomvi wa mimea au damu ya wadudu wengine na hata ya mamalia katika spishi kadhaa. Spishi fulani za nusufamilia Triatominae zinaambukiza watu kwa ugonjwa wa Chagas, jamaa ya ugonjwa wa malale.
Wadudu hawa hutaga mayai juu ya majani au mashina ya mimea, lakini kuna spishi zinazozaa lava badala ya mayai, k.m. spishi nyingi za vidukari.
Spishi kadhaa za Afrika ya Mashariki
hariri- Acyrthosiphon pisum, Kidukari wa Njegere
- Aulacaspis tubercularis, Mdudu-gamba wa Mwembe
- Bemisia tabaci, Nzi Mweupe wa Kiazi Kitamu
- Dysdercus nigrofasciatus, Kisulisuli Mraba-mweusi
- Oxypleura polydorus, Nyenje-miti
- Phenacoccus manihoti, Kidung'ata wa Muhogo
- Ptyelus flavescens, Mdudu-mate Ngano
Picha
hariri-
Auchenorrhyncha (Nyenje-miti)
-
Auchenorrhyncha (Mdudu-mate ngano)
-
Coleorrhyncha (Kunguni-kigoga)
-
Heteroptera (Kunguni)
-
Heteroptera (Kunguni-mgunda)
-
Sternorrhyncha (Kidukari wa Njegere)
-
Sternorrhyncha (Nzi mweupe wa kiazi kitamu)
-
Sternorrhyncha (Kidung'ata wa Solanum)
-
Sternorrhyncha (Mdudu-gamba wa Muhogo)