Sota

(Elekezwa kutoka Klugeana)
Sota
Nondo wa sota-mboga (Agrotis segetum)
Nondo wa sota-mboga (Agrotis segetum)
Sota-mboga (Agrotis segetum)
Sota-mboga (Agrotis segetum)
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Arthropoda (Wanyama wenye miguu yenye viungo)
Ngeli: Insecta (Wadudu)
Ngeli ya chini: Pterygota (Wadudu wenye mabawa)
Oda: Lepidoptera (Wadudu walio na mabawa yenye vigamba)
Nusuoda: Glossata {Lepidoptera wenye ulimi unaoweza kuviringwa)
Familia ya juu: Noctuoidea (Nondo kama nondo wa nyanya)
Latreille, 1809
Ngazi za chini

Jenasi na spishi kadhaa za Afrika:

Sota ni aina za viwavi vya nondo wa jenasi mbalimbali za familia ya juu Noctuoidea ambao ni wasumbufu mara nyingi kwenye mashamba ambapo wanakata mashina ya miche. Kwa sababu ya hii huitwa “cutworms” kwa Kiingereza.

Maelezo

hariri

Sota haswa ni viwavi wa spishi fulani za familia kubwa ya nondo Noctuidae na spishi kadhaa za familia nyingine za Noctuoidea. Walakini, spishi nyingi sana za familia hii ya juu si sota na viwavi wenye mwenendo sawa, ambayo ni sababu nzuri kuwaita sota, wako ndani ya familia nyingine. Kwa kawaida sota ni wanene kiasi na wakikutwa huviringanika katika umbo la O ama C. Rangi yao ni nyeusi, kijivu, kahawia au kwa madoa. Nondo wao wana rangi hizo hizo kwa kawaida, ingawa mabawa ya nyuma ni meupe au rangi ya fedha mara nyingi. Wana mabaka kwenye mabawa ya mbele yaliyo bainifu kwa spishi.

Uharibifu

hariri

Sota mweusi, sota-mboga na sota madoadoa ni lava maarufu wa Noctuoidea walio wasumbufu sana. Hujulikana sana kwa kuwa wadudu waharibifu wa mashamba na bustani ambao ni walafi wabaya wa majani, matumba na mashina na wanaweza kuharibu mimea mizima. Wengi wanajulikana kwa tabia yao ya kukata miche kwenye kiwango cha ardhi kwa kutafuna kupitia shina. Spishi nyingine huishi chini ya ardhi na hula mizizi, pamoja na viazi. Mmojawapo wa wadudu wasumbufu wa bustani ni sota madoadoa (Peridroma saucia), ambaye anaweza kuondoa majani yote kwenye bustani na migunda kwa muda wa siku chache.

Chakula

hariri

Sota hutofautiana katika mwenendo wao wa kujilisha, ingawa wote hujificha kwenye ardhi au chini ya takataka wakati wa mchana na hujilisha usiku. Wengine hukaa na mmea waliokata na kujilisha nao na wengine huendelea baada ya kula kiasi kidogo kutoka kwa mche uliokatwa. Njia hii mbaya ya kujilisha husababisha uharibifu mkubwa wa mazao. Kwa hivyo sota ni wadudu wasumbufu kwa wenye bustani kwa ujumla, lakini kwa wakulima wa mboga na nafaka haswa. Kwa mfano, imependekezwa kuwa huko Afrika Kusini sota-mboga, Agrotis segetum, ndiye msumbufu mbaya wa pili wa mahindi[1].

Siyo spishi zote zinazokata miche. Nyingine hujilisha kwa mimea iliyokomaa na hata miti. Spishi fulani, kwa mfano Klugeana philoxalis, hushambulia mimea yenye majani mapana isiyo mirefu, kama vile Oxalis, gizani na huanguka chini mara tu taa ikiwaka juu yao. Anachukuliwa hata kama spishi ya udhibiti wa kibiolojia kwa Oxalis pes-caprae uliovamia nchi nyingi kutoka Afrika Kusini. Wengine hupanda miti, kama spishi za migunga, usiku wakiacha njia za hariri, lakini huacha njia za kibinafsi, sio njia zilizounganika kama viwavi-mwandamano. Sota anayetoboa matunda, Serrodes partita, vile vile huishi chini ya takataka chini ya mti wake wa chakula, Pappea capensis (mbambangoma)[2].

Spishi za Afrika Kusini kwa Sahara

hariri

Marejeo

hariri
  1. Smit, Bernard, "Insects in South Africa: How to Control them", Pub: Oxford University Press, Cape Town, 1964.
  2. Annecke, D. R.; Moran, V. C. (1982). Insects and mites of cultivated plants in South Africa. London: Butterworths. ISBN 978-0-409-08398-9.