Kongo ya Kibelgiji

(Elekezwa kutoka Kongo ya Belgiji)

Kongo ya Kibelgiji ni jina la koloni la Ubelgiji katika Afrika ya Kati hasa katika beseni ya mto Kongo kati ya mwaka 1908 hadi 1960.

Bendera ya Kongo ya Kibelgiji

Leo hii ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Katika miaka 1925 hadi 1946 maeneo ya Rwanda na Burundi yalitawaliwa kama sehemu za Kongo ya Kibelgiji.

Koloni binafsi la mfalme kuwa koloni la Ubelgiji hariri

Kongo ya Kibelgiji ilianzishwa wakati wa kuhamishwa kwa Dola huru la Kongo kutoka mali binafsi ya mfalme Leopold II wa Ubelgiji kwenda mikononi mwa serikali ya Ubelgiji mwaka 1908.

Utawala wa mfalme ulionekana kuwa wa kinyama na upinzani dhidi yake ulikua katika nchi nyingi za dunia. Alipaswa kukabidhi koloni lake binafsi mikononi mwa serikali ya Ubelgiji iliyomlipa fidia kwa mali aliyoacha.

 
Picha za watoto waliokatwa mikono kama adhabu chini ya Leopold II zilienea na kusababisha madai ya kumwondolea utawala wa Kongo

Siasa ya wakoloni hariri

Wabelgiji walijitahidi kuboresha hali ya maisha ya wenyeji baada ya miaka mibaya ya Leopold II. Nia ilichelewa kuonekana hali halisi kwa sababu utaratibu wa kulazimisha Waafrika kufanyia kazi kampuni na shirika kubwa iliendelea hata bila idhini ya serikali mpya ukadai vifo vingi.

Kwenye uwanja wa elimu, matibabu na mawasiliano jitihada za siasa mpya zilionekana zaidi. Kongo ilikuwa kati ya nchi chache ambako lugha za kienyeji zilifundishwa shuleni kwa sababu shule nyingi ziliendshwa na wamisionari.

Kwa upande mwingine ubaguzi wa rangi uliwaruhusu Waafrika wachache sana kufikia ngazi za juu za elimu.

Makampuni makubwa ya migodi kama vile "Société Générale" na "Union Minière du Haut Katanga" yalichimba madini hasa katika jimbo la Katanga. Makampuni haya yalikuwa na athira kubwa.

Katanga ilikuwa maarufu kwa shaba iliyochimbwa huko. halafu pia kwa uranium iliyotumiwa kwa mabomu ya kwanza ya kinyuklia ya Marekani mwaka 1945.

Upinzani hariri

Baada ya unyama wa miaka ya Leopold II upinzani dhidi ya utawala wa kikoloni ulikuwa hafifu. Kuanzia miaka ya 1920 Wakongo wengi walionyesha upinzani huo katika mahudhurio katika madhehebu mapya ya wafuasi wa Simon Kimbangu yaliyopigwa marufuku na Wabelgiji kuanzia mwaka 1926.

Tangu mwaka 1950 upinzani uliongezeka na kuonyesha pia uso wa kisiasa.

Wabelgiji ambao hawakujiandaa kwa madai hayo yalipaswa kukubali uchaguzi wa halmashauri za vijiji na miji mwaka 1957.

Mwaka 1958 vyama vya kisiasa vilikubaliwa. Harakati mbili muhimu kati ya hivi zilikuwa Abako (Alliance de Bakongo) chini ya Joseph Kasavubu na MNC (Mouvement National Congolais) chini ya Patrice Lumumba.

Mwaka 1959 mkutano wa wanasiasa Wakongo ulidai uhuru wa nchi.

Mwisho wa koloni na uhuru hariri

Wabelgiji walijaribu kuchelewesha harakati hizo lakini baada ya kutambua matatizo serikali ya Ubelgiji ilitangaza mnamo Januari 1960 kuwa uchaguzi utaendeshwa haraka na baada ya miezi sita Wabelgiji watakabidhi nchi kwa wenyeji.

Chama cha Patrice Lumumba kilishinda kwa kura nyingi naye akawa kiongozi wa kwanza wa nchi huru kama waziri mkuu.

Tovuti za nje hariri

  Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Kongo ya Kibelgiji kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.