Kuchanyika Michirizi

Kuchanyika michirizi
Kuchanyika michirizi
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Chordata (Wanyama wenye ugwe wa neva mgongoni)
Nusufaila: Vertebrata (Wanyama wenye uti wa mgongo)
Ngeli: Aves (Ndege)
Oda: Passeriformes (Ndege kama shomoro)
Familia ya juu: Sylvioidea (Ndege kama kucha)
Familia: Scotocercidae (Ndege walio na mnasaba na kuchanyika michirizi)
Fregin, Haase, Olsson & Alström, 2012
Jenasi: Scotocerca
Sundevall, 1872
Spishi: S. Inquieta
(Cretzschmar, 1830)

Kuchanyika michirizi (Scotocerca inquieta; kwa Kiing. Streaked Scrub Warbler) ni ndege mdogo na spishi pekee ya familia Scotocercidae. Hupatikana Afrika na kusini-magharibi mwa Asia. Ni ndege wa pindo za majangwa, ambapo hutembelea maeneo ya vichaka, mabonde na makorongo, na anakaa mahali pamoja kwa kawaida, ijapokuwa mahamiaji ndani ya eneo lao yanaweza kutokea nje ya msimu wa kuzaliana.

Mayai ya kuchanyika michirizi.

Maelezo

hariri

Kuchanyika michirizi ni kucha mdogo wa jangwani anayejificha na kupinda mkia wake juu ya mgongo wake. Wapevu ni kijivu juu na wana michirizi ya rangi ya kahawa. Wana nyusi nyeupe pana na mstari mweusi mwembamba kupitia macho. Sehemu za chini ni nyeupe na mbavu na tako ni nyekundu. Kidari kina michirizi myembamba. Manyoya ya mkia yanakuwa marefu zaidi kutoka kingo mpaka kati na yana rangi ya kahawa na ncha nyeupe. Wachanga wana rangi zisizoiva.

Makazi

hariri

Huyu ni ndege wa jangwa wazi lenye tandiko la vichaka vichache, haswa sakafu za makorongo zenye tandiko zito kuliko jangwa la karibu, na pia maeneo ya mawe yenye vichaka katika mabonde na makorongo.

Kuchanyika michirizi huunda tago lake kwenye vichaka vya chini hadi m 1.5 juu ya ardhi. Kiota ni muundo wenye kuba uliojengwa kwa nyasi na vijiti na kutandikwa ndani yake kwa manyoya ya ndege na wanyama na nyuzi za mimea. Kina miingilio 1-2 kwa upande, lakini ikiwa kuna wa pili hutumiwa tu ili kuondoka. Ukubwa wa wastani wa klachi ni 3-4 lakini inaenda kutoka 2 hadi 5. Uatamia ni takriban wiki mbili na wiki mbili tena kabla ya kupata manyoya ya tama.

Chakula chake kikuu ni wadudu lakini atakula mbegu pia ambayo inaweza kuwa muhimu sana wakati wa baridi. Hutafuta chakula ardhini, ikipitia takataka za majani na uchafu mwingine chini ya vichaka. Huingia vishimo pia lakini anajilisha pia juu kwenye mimea wakati mwingine.