Jangwa ni eneo kavu lenye mvua au usimbishaji kidogo tu. Kutokana na ukavu kuna mimea michache tu, pia wanyama wachache. Wanyama walioko hufanya shughuli zao hasa wakati wa usiku. Kipimo cha usimbishaji kinachotambulika kimataifa ni kiwango cha chini ya mm 250 kwa mwaka[1]. Uoto wa mimea hufunika chini ya asilimia 5 za eneo lake.

Matuta ya mchanga katika Sahara ya Libya
Nguzo za mwamba katika Jangwa la Australia
Jangwa la Atacama

Wakati mwingine huitwa jangwa hata maeneo ambayo ni makavu kutokana na baridi kali.

Aina za maeneo makavu: jangwa na mibuga

hariri

Maeneo makavu yanaweza kutofautishwa kuwa yabisi sana (en: extremely arid) pasipo usimbishaji kwa muda wa miezi 12 mfululizo (maana yake hakuna mvua kila mwaka), yabisi (en: arid) pasipo usimbishaji zaidi ya mm 250 kwa mwaka, nusu yabisi (en:semiarid) penye usimbishaji kati ya mm 250 and 500 kwa mwaka. Maeneo yabisi sana na maeneo yabisi ni jangwa. Maeneo nusu yabisi yenye nyasi huitwa mbuga.

Takriban theluthi moja ya uso wa nchi kavu duniani ni yabisi sana, yabisi au nusu yabisi.

Athari ya uvukizaji

hariri

Kiasi cha usimbishaji peke yake hakitoshi kila mahali kutofautisha maeneo makavu. Mm 200 za mvua katika eneo la joto zitasababisha eneo kuonekana kama jangwa kabisa kwa sababu kiasi kikubwa cha maji yale kidogo yanayoneshewa hupotea kutokana na uvukizaji. Kuna mifano ya kwamba eneo penye kiasi kilekile cha 200 mm halionekani kuwa jangwa tayari kwa sababu kutokana na halijoto na mawingu (hata yasiponyesha mvua) kiasi kidogo cha maji yanavukiza.

Kama uvukizaji unapita kiasi cha mvua hata eneo penye mvua zaidi ya 250 mm inaonekana kama jangwa.

Aina za jangwa

hariri

Mara nyingi majangwa hutofautishwa kutokana na uso wake:

 
Jangwa baridi la mawe la Ladakh kwenye milima ya Himalaya
  • Jangwa la changarawe — uso lake huonyesha hasa changarawe. Changarawe imetokea kutokana na mmomonyoko wa mawe au miamba - punje ndogo zaidi zimeshapulizwa mbali na upepo. Hii ni sababu ya majangwa mengi kuwa na maeneo ya mchanga na changarawe yanayobadilishana. Changarawe hupatikana pia pale ambako zamani barafuto zilisaga mawe na kuzisukuma mbele ya barafu zao pale zilizobaki. Ni ajabu kutafakari ya kwamba sehemu fulani ilikuwa ya barafuto tukisimama leo mahali penye joto kali lakini mabadiliko ya hali ya hewa yalileta baridi au joto kila sehemu ya dunia yetu katika mamilioni ya miaka iliyopita.
  • Jangwa la mawe — uso lake huonyesha miamba na mawe makubwa. Maana yake hapo udongo wote mwenye rutba na mchanga vimeshapulizwa mbali na mwamba umebaki. Athira za joto na baridi zinaweza kupasua mwamba. Mmomonyoko wa upepo hutokea.
  • Jangwa la chumvi — mara nyingi penye beseni yabisi za mashapo bila njia ambako maji ya mvua (au mto) yanaweza kutoka. Maji yote huvukiza na kuacha chumvi yake katika udongo. Kiasi cha chumvi kinaendelea kuongezeka polepole katika udongo wa beseni hizi.

Jangwa ni eneo kavu lakini maji hutokea.

Maji ya chini

hariri

Mara nyingi kuna maji chini ya ardhi. Pale ambako maji haya si chini mno mimea inaweza kuyafikia kwa mizizi yao. Mahali kadhaa chemchemi hutokea. Sehemu kama hizi zinaonekana kama oasisi penye miti, wakati mwingine hata na bwawa. Mahali pengine wakazi wa jangwa wamechimba kisima kirefu pasipo na mimea kinachosaidia maji ya watu na wanyama hasa wa misafara.

Maji ya mvua

hariri

Mvua ikionyesha unaweza kutokea kwa wingi. Maji yake hukusanyika katika mabonde na kutokea kama mto wa muda. Kuna mifano mingi ya wasafiri jangwani waliokufa kwa sababu walipiga kambi katika bonde penye kivuli lakini walizama kwa sababu mto mkali ulijitokeza kwa ghafla kutokana na mvua ulionyesha katika umbali mkubwa.

Sehemu nyingine mvua husababisha kutokea kwa mbwawa hata maziwa kwa muda.

 
Jangwa la Sahari jinsi lafunika Afrika ya Kaskazini yote (picha kutoka angani)

Mito inayopita jangwa

hariri

Mito kadhaa kama Nile ina maji ya kutosha ili ivuke neo la jangwa. Inawezesha maisha ya mimea, wanyama na watu katika mabonde yao.

Mito mingine inakwisha jangwani kwa sababu maji yote hupotea na kuvukiza. Mfano wake ni delta ya mto wa Okavango unaokwisha katika jangwa la Kalahari huko Botswana. Delta hii ni eneo la mimea na wanyama wengi katikati ya jangwa.

Mto wa Ewaso Nyiro katika Kenya ya kaskazini kwa kawaida hukwisha katika nchi yabisi za Usamburu. Lakini kila baada ya miaka makumi kadhaa baada ya mvua kubwa sana inaendelea kuvuka jangwa la Somalia ya kusini na kufikia Bahari Hindi jinsi ilvyotokea wakati wa El-Nino 1998.


Majangwa makubwa duniani

hariri
Majangwa makubwa 10 ya dunia ni:[2]
Nambari Jina la jangwa Eneo (km²) Eneo (mi²)
1 Bara la Antaktiki 14,200,000 5,500,000
2 Aktiki 13,900,000 5,400,000
3 Sahara (Afrika) 9,100,000 3,500,000
4 Jangwa la Uarabuni (Mashariki ya Kati (Middle East)) 2,600,000 1,000,000
5 Jangwa la Gobi (Asia) 1,300,000 500,000
6 Jangwa la Patagonia (Amerika ya Kusini) 670,000 260,000
7 Jangwa kuu la Victoria (Australia) 647,000 250,000
8 Jangwa la Kalahari (Afrika) 570,000 220,000
9 Great Basin Desert (Amerika ya Kaskazini) 490,000 190,000
10 Jangwa la Syria (Mashariki ya Kati (Middle East)) 490,000 190,000

Marejeo

hariri
  1. Marshak (2009). Essentials of Geology, 3rd ed. W. W. Norton & Co. p. 452. ISBN 978-0-393-19656-6.
  2. "The World's Largest Deserts". Geology.com. Iliwekwa mnamo 2015-06-01.