Mashambulio ya kigaidi ya 7 Agosti 1998 katika Afrika ya Mashariki
Mashambulio ya kigaidi ya 7 Agosti 1998 katika Afrika ya Mashariki yalitokea katika miji ya Daressalam na Nairobi kwa kulipusha malori yaliyojaa baruti mbele ya balozi za Marekani kila mahali. Angalau watu 224 waliuawa na maelfu kujeruhiwa.
Watendaji walikuwa raia wa nchi za Kenya na Tanzania pamoja na nchi za Kiarabu mbalimbali. Walitekeleza mashambulio kwa maagizo ya kundi la Jihadi ya Kiislamu ya Misri ambalo ni sehemu ya mtandao wa Al Qaida iliyoongozwa na Osama bin Laden.
Shambulio la Nairobi
haririMnamo saa nne na nusu asubuhi ya siku ya Ijumaa 7 Agosti watu wawili walioendesha lori dogo kilogramu 700 za baruti walifika mbele ya ubalozi wa Marekani iliyokuwepo njiapanda ya barabara za Moi na Haile Selassie karibu na kituo cha reli. Dereva Azzam aliingia kwenye njia ya kutoka katika maegesho ya magari akajaribu kufikia gereji chini ya ubalozi. Hapa alizuiliwa na mlinzi Benson Okuku Bwaku aliyekataa kufungua geti ya gereji. Gaidi wa pili Mohamed Rashed Daoud Al-Owhali alimtupia kombora ya mkononi lakini alimkosea. Bwaku alifaulu kukimbia na kufikia kona ya jengo akajiokoa. Hapo Azzam alianza kufyatua risasi hovyo. Hapo Al-Owhali alikimbia kuelekea mtaa wa Haile Selassie akajiokoa wakati Azzam akajilipusha kwa baruti kwenye lori. Mlipuko mkubwa ulitikisisha ubalozi na jengo jirani la Ufundi Building. Mshtuko wa mlipuko uliharibu pia vyoo vya madirisha katika kipenyo cha kilomita 1 na sauti yake ilisikika kwa umbali wa kilomita 16.
Jengo la ubalozi liliharibiwa kiasi tu kwa jumla likasimama kwa sababu lilijengwa imara. Ndani ya ubalozi walikufa watu 44, Wamarekani 12 na wafanyakazi wengine 32, wengi wao Wakenya hasa waliothiriwa na mshtuko ulioingia madirishani na kuangusha kuta za ndani.
Vifo vingi vilitokea kwa sababu jengo dogo jirani la Ufundi building lilibomolewa kabisa na kuanguka. Wahanga wengi walikuwa vijana wanafunzi waliosoma kwenye chuo cha ukarani ndani ya jengo hili pamoja na walimu na wafanyakazi wake.
Pamoja na watu waliojeruhiwa katika majengo ya karibu kuna wengi waliouawa na kujeruhiwa kwenye barabara ya Haile Selassie kwa sababu moto na mshtuko wa bomu zilielekezwa kati ya kuta za ubalozi na Ufundi Building. Basi lililokwama kwenye msongamano wa magari mbele ya kiingilio cha ubalozi lilichomwa kabisa pamoja na abiria wake.
Watu wengi walijeruhiwa macho kwa vipande vya kioo; walisikia mlipuko wa kwanza wa kombora la mkononi na risasi zilizofyatuliwa a Azzam wakaenda madirishani kuangalia kuna nini wakapigwa vipande vya kioo cha madirisha usoni wakati bomu ililipuka.
Shambulio la Dar es Salaam
haririKaribu kwenye dakika ya mlipuko wa Nairobi shambulio la pili lilitokea kwenye ubalozi wa Marekani mjini Dar es Salaam. Hata hapa dereva alijaribu kuingia kwenye eneo la ubalozi kwa lori lakini alikataliwa getini akalipusha mzigo wake. Hapa ni watu 11 waliokufa na 85 waliojeruhiwa. Idadi ya wahenga ilikuwa ndogo kuliko Nairobi kwa sababu ubalozi ulikuwepo nje ya kitovu cha jiji kando la mtaa wa Bagamoyo na nafasi likuwa kubwa hadi majengo ya jirani.
Mwaka uleule washiriki wa kwanza wa mashambulio haya walikamatwa na kukabidhiwa kwa Marekani. Hadi mwaka 2010 watu 5 walihukumiwa jela ya maisha kwa kushiriki katika ugaidi wa 7 Agosti.