Historia ya Zanzibar inahusu historia ya eneo ambalo leo linaunda Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ambayo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais Amani Abeid Karume akishiriki sherehe ya miaka 40 tangu mapinduzi kufanyika.
Historia ya Tanzania
Coat of Arms of Tanzania
This article is part of a series
Uendo
Historia ya Zanzibar
Afrika Mashariki 1800-1845
Ukoloni
Afrika ya Mashariki ya Kijerumani
Mkataba wa Zanzibar-Helgoland
Mkwawa
Vita vya Maji Maji
Vita vikuu vya kwanza Afrika Mashariki
Tanganyika
Mapambano ya uhuru Tanganyika
Uhuru
Uhuru wa Tanganyika
Mapinduzi ya Zanzibar
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
Julius Nyerere
Ujamaa
Tamko la Arusha
Vita vya Kagera
Ali Hassan Mwinyi
Benjamin Mkapa
Jakaya Kikwete
John Magufuli
Samia Suluhu Hassan

Tanzania Portal

Historia ya awali

Mabaki ya vifaa vya mawe inaonyesha kwamba kwa kiasi cha miaka 20,000 kumekuwepo makazi ya binadamu katika visiwa vya Zanzibar.

Visiwa hivyo ni sehemu ya kumbukumbu ya kihistoria ya ulimwengu wakati Waajemi wafanyabiashara walivigundua na kuvifanya ndiyo makao makuu kwa safari kati ya Mashariki ya Kati, India na Afrika.

Katika karne ya mwanzo BK Zanzibar pamoja na mwambao wa Afrika ya Mashariki vilikuwa katika ufalme wa Saba.

Katika kipindi cha karne ya 3 na ya 4, Wabantu walianza biashara na Waarabu waliokuja Afrika ya Mashariki.

Katika karne ya 7, Waarabu walikuja Zanzibar kibiashara pamoja na kusambaza dini ya Uislamu, Waarabu ndio waliyoipa jina ZANZIBAR kutokana na maneno ya Kiajemi ZINJI BAR yaani sehemu ya Watu Weusi.

Lugha ya Kiswahili imeanza kutumika kiasi cha karne ya 13 ikitokana na mchanganyiko wa lugha ya Kiarabu na lugha za Kiafrika.

Katika karne ya 16 Wareno walikuja Zanzibar lakini utawala wao ulifuatiwa na kutokuwepo utulivu, lakini biashara ya utumwa iliwaweka watu pamoja.

Chini ya Waarabu

Waarabu kutoka Oman walichukua utawala Zanzibar katika karne ya 17 na Zanzibar ilikuwa makao makuu ya utawala wa Waomani.

Miaka 1820-1870 Zanzibar ilifaidi matunda mazuri ya kiuchumi na maendeleo yaliyosababishwa na utawala wa kisultani na hivyo kupelekea Zanzibar kuwa na mwakilishi nchini Marekani na kupelekea kuenea kwa Dini ya Kiislamu.

Katika karne ya 19 Zanzibar ilikuwa chini ya utawala wa Oman, mwaka 1830 Zanzibar ilikuwa inaongoza kwa kilimo cha karafuu, na hiyo kupelekea haja ya watumwa kuongezeka kutumika katika kilimo. Hatimaye watumwa walikuwa 90% za wakazi wote.

Sayyid Said kuhamia Unguja

Usultani wa Zanzibar ulianzishwa mwaka 1856 wakati Sultani Sayyid Said alipoamua kuhamisha makao makuu yake kutoka Maskat (Omani) kwenda Unguja.

Sayyid Said alikuwa Sultani wa Omani tangu mwaka 1804. Aliimarisha utawala wa Omani juu ya pwani ya Afrika ya Mashariki.

Mwaka 1829 alifaulu kuteka Mombasa iliyokuwa mji pekee wa kujitegemea kati ya miji yote ya Uswahilini.

Visiwa vya Unguja na Pemba vilikuwa chini ya Omani tangu mwaka 1689, Wareno walipofukuzwa katika pwani za Uswahilini.

Biashara ya karafuu na watumwa

Sayyid Said aliona nafasi kubwa ya biashara ya karafuu kwa ajili ya soko la Uhindi na kwingineko. Mwaka 1829 akaanzisha mashamba ya mikarafuu kwa kutumia kazi ya watumwa kutoka bara.

Biashara hiyo ikabadilisha uso wa mji wa Zanzibar wa karne ya 19 uliowahi kuwa kijiji kikubwa tu cha vibanda kando ya boma lililojengwa na Omani kama kizuizi dhidi ya Wareno.

Baada ya azimio la mwaka 1832 la kuhamisha mji mkuu wa Omani kwenda Unguja, idadi ya wakazi wa mji ilikua haraka.

Nchi za nje zikatambua mji mkuu mpya na kujenga uhusiano. Ubalozi wa Marekani ulijengwa mwaka 1837, Uingereza ukafuata mwaka 1841 na Ufaransa mwaka 1844.

Sultani mwenyewe aliondoka kabisa Maskat mwaka 1840. Kukua kwa Zanzibar kulisababisha kukonda kwa mji wa Maskat

 
Bendera ya Usultani wa Zanzibar

Kugawiwa kwa Omani kulikuwa mwanzo wa Zanzibar

Baada ya kifo cha Sayyid Sultan mwaka 1856, usultani wa Oman uligawiwa kati ya wanawe. Sayyid Majid bin Said Al-Busaid (1834/18351870) akawa Sultani wa kwanza wa Zanzibar na kaka yake Sayyid Thuwaini bin Said al-Said akawa Sultani wa Oman akitawala nchi hiyo bila maeneo ya Afrika ya Mashariki.

Usultani mpya ulikuwa nchi yenye nguvu kati ya Rasi Delgado (mpakani na koloni la Kireno ya Msumbiji) hadi Mogadishu (Somalia). Athira yake ilienea kupitia njia za misafara ya pembe za ndovu na watumwa hadi mto Kongo.

Wafanyabiashara kama Tippu Tip waliokuwa raia wa Usultani wakapita Tabora na Ujiji kwenda ziwa Tanganyika na kuingia ndani ya eneo la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ya leo. Wapagazi wao walibeba bidhaa kutoka Zanzibar zilizobadilishwa kwa pembe za ndovu hasa. Watumwa walikamatwa au kununuliwa wakabeba pembe hadi pwani.

 
Jumba la Sultani Zanzibar

Pamoja na hayo, sultani alipokea kwa moyo wamisionari Wakristo.

Mapadri Wakatoliki wa kwanza pamoja na masista walitokea Reunion wakakaa Unguja tangu tarehe 12 Desemba 1860 hadi mwaka 1863, walipokabidhi misheni kwa shirika la mapadri wa Roho Mtakatifu.

Waanglikana wa chama cha Misheni ya Vyuo Vikuu kwa Afrika ya Kati U.M.C.A. (Universities` Mission to Central Africa) ambacho kiliundwa ili kutekeleza wito kutoka David Livingstone kuhubiri Injili na kukomesha utumwa katika Afrika, waliingia Zanzibar mwaka 1864.

Baadaye wakajenga kanisa kuu mahali pa soko la watumwa lililofungwa, altari ikiwa imejengwa juu ya nafasi ya mti wa kuwafunga watumwa walioadhibiwa kwa viboko, na batizio kuwa mahali walipotupwa watoto watumwa ambao hawakuuzwa pamoja na mama zao.

Sayyid Bargash

Sultani wa pili wa Zanzibar yenyewe, Sayyid Bargash, alijitahidi kujenga uhusiano na nchi za nje. Alifunga soko la watumwa Zanzibar mjini kulingana na mapatano ya kimataifa, lakini akavumilia biashara ya watumwa kuendelea chinichini. Wakati wa Bargash majengo mengi ya Mji Mkongwe yakajengwa.

Mwishowe mwa utawala wake aliona kupungukiwa kwa eneo lake kutokana na mashindano ya nchi za Ulaya ya kuenea katika Afrika baada ya mkutano wa Berlin.

Mwaka 1885 Karl Peters alifanya mikataba ya ulinzi na watawala wadogo waliokuwa chini ya Sultani barani Tanganyika. Upingamizi wa Sultani ulishindikana kwa sababu Wajerumani walituma manowari Unguja akapaswa kukubali maeneo mapya ya Wajerumani.

Kuenea kwa ukoloni

Mwaka 1886 mkataba kati ya Uingereza na Ujerumani ulibana eneo la sultani barani katika kanda yenye upana wa maili kumi tu kati ya Rasi Delgado na Mogadishu. Bargash na mfuasi wake Khalifa bin Said waliamua kuuza maeneo hayo au kuyakodisha.

  • 1887/1888 pwani ya Kenya ilikodishwa kwa Waingereza. Wakati wa uhuru wa Kenya sehemu hii ikaingizwa katika Jamhuri ya Kenya.
  • Pwani ya Tanganyika ikakodishwa kwa Wajerumani mwaka 1888 na hatimaye kuuzwa mwaka 1890.
  • Miji kwenye pwani ya Somalia ikakodishwa kwa Italia mwaka 1892 ikauzwa mwaka 1906, ila Mogadishu mwaka 1924.

Hali halisi usultani ukabaki na visiwa viwili vya Unguja na Pemba tu.

Waingereza walikuwa walisita kuhusu Zanzibar lakini baada ya jaribio la Karl Peters la kufanya mkataba na Sultani ili kuingiza visiwa hivyo katika Afrika ya Mashariki ya Kijerumani, Uingereza uliamua kutafuta utawala wa visiwa.

Mkataba wa Zanzibar-Heligoland na mwisho wa uhuru

Mkataba wa Zanzibar-Helgoland kati ya Ujerumani na Uingereza ulileta patano la kuwa Zanzibar itakuwa chini ya Uingereza.

Tangu mwaka 1890 waziri mkuu wa Sultani alikuwa Mwingereza aliyepokea amri kutoka London.

Tangu mwaka 1913 nafasi ilichukuliwa na afisa mkazi mkuu.

Kwa muda wa miaka 26 usultani ulikuwa na fedha yake ya pekee iliyoitwa Riali ya Zanzibar.

Tangu mwaka 1890 Zanzibar ilikuwa chini ya uangalizi wa Waingereza rasmi, lakini uchaguzi wa mwanzo ulifanyika mwaka 1957, na miaka iliyofuata kukawepo fujo na machafuko kutoka kwa Waafrika wanaodai uhuru dhidi ya utawala wa Kiarabu.

Baada ya uhuru na mapinduzi

Tarehe 10 Desemba 1963 Waingereza waliipa uhuru Zanzibar chini ya jumuiya ya madola.

Uhuru wa usultani ukadumu muda mdogo tu.

Tarehe 12 Januari 1964 yalitokea mapinduzi ya Zanzibar ili kumuondoa madarakani Sultani wa Zanzibar na serikali yake, iliyoundwa hasa na Waarabu, na hatimaye kuweka uongozi mikononi mwa Waafrika, ambao ndio wengi visiwani humo (230,000 hivi), kwenye bahari ya Hindi, karibu na pwani ya Tanganyika.

Usultani wa Zanzibar ulikuwa umepewa na Uingereza uhuru wake mwaka 1963. Kabla ya hapo, Waarabu walikuwa wamefaulu kudumisha katika mfululizo wa chaguzi utawala waliokuwa nao tangu zamani za Zanzibar kuwa chini ya Usultani wa Omani.

Chama cha Afro-Shirazi Party (ASP), kilichowakilisha hasa Waafrika, kilipoona kwamba bungeni kina viti vichache ingawa kilipata 54% za kura katika uchaguzi wa Julai 1963, kilipatana na chama cha mrengo wa kushoto Umma Party.

Tarehe 12 Januari 1964 asubuhi na mapema, mwanachama wa ASP John Okello (1937-1971 ?) kutoka Uganda aliongoza wanamapinduzi 600–800 wa kisiwa kikuu cha Unguja kushinda polisi wa nchi na kuteka silaha zao. Halafu walielekea Zanzibar Town walipompindua Sultani Jamshid bin Abdullah na serikali yake. Waliokufa katika mapigano wamekadiriwa kuwa 80 hivi tu.

Kumbe yalifuata kwa siku kadhaa (labda hadi tarehe 20 Januari) maangamizi ya kimbari dhidi ya Waarabu (waliokuwa 50,000 hivi) na Waasia wa Asia Kusini (waliokuwa 20,000 hivi); hakuna hakika kuhusu idadi ya waliouawa: makadirio yanataja kuanzia mamia kadhaa hadi 20,000.

Kiongozi wa ASP Abeid Karume, asiyekuwa na msimamo mkali akawa rais wa kwanza wa nchi, na wanachama wa Umma party walipewa nafasi serikalini. Kufikia Machi Okello alikuwa ameshawekwa pembeni na kufikia Aprili kikosi chake kimeshanyang'anywa silaha[1].

Mwelekeo wa Kikomunisti wa baadhi katika serikali mpya uliogopesha nchi za Magharibi. Kwa kuwa Zanzibar ilikuwa chini ya athari ya Uingereza, serikali yake iliandaa mipango kadhaa. Hata hivyo, hofu ya kuundwa serikali ya Kikomunisti haikutimia kamwe, na kwa kuwa wananchi wa Uingereza na Marekani waliweza kuhama bila shida, mipango hiyo haikutekelezwa.

Wakati huo nchi za Kikomunisti za China, Ujerumani Mashariki na Umoja wa Kisovyeti zilianzisha mahusiano ya kirafiki na serikali mpya ya Zanzibar kwa kuitambua rasmi na kwa kutuma washauri.

Karume alifanikisha majadiliano ya kuunganisha Zanzibar na Tanganyika ili kuunda hatimaye muungano wa Tanzania; vyombo vya habari vilitafsiri muungano huo kuwa juhudi za kuzuia Ukomunisti kugeuza Zanzibar.

Mapinduzi yalikomesha miaka 200 ya utawala wa Waarabu Zanzibar, na yanaadhimishwa kila mwaka kama sikukuu ya taifa zima la Tanzania.

Muda mchache baadaye, tarehe 26 Aprili 1964, iliungana na Tanganyika kuunda Jamhuri ya Muungano wa TANZANIA.

Tanbihi

Viungo vya nje

  • Excerpt from: Race, Revolution and the Struggle for Human Rights in Zanzibar by Thomas Burgess
  • Steere, Edward (1869). Some account of the town of Zanzibar . London: Charles Cull.
  Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Historia ya Zanzibar kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.